HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU19
ILIPOISHIA
Simon aliichukua ile bastola
akaikagua.
“Lakini unaziwekea mafuta
hizi bastola, usitukodishie vimeo vinavyokwama wakati wa hatari”
“Simon umekuja kufanya mzaha
au unataka bastola. Hicho ni kimeo? Si unaona bastola mpya, unasema kibeo!”
Simon aliipindisha akaikagua
kwa ndani.
“Hii mpya wapi, acha ujanja
wako Samson! Tena hukuweka risasi!”
“Risasi utaweka mwenyewe”
“Sasa ziko wapi?”
“Umesema unataka risasi
ngapi?”
“Nimekwambia risasi kumi”
SASA ENDELEA
“Nipatie hizo pesa kwanza
nikupe risasi”
“Nitakupa laki mbili,
nikikurudishia kesho kutwa nitakumalizia laki yako” Simon alimwambia huku
akijipekua mifukoni.
Alitoa shilingi laki mbili
akampa.
Mtu huyo alizihesabu pesa
hizo kisha akazitia kwenye mfuko wa bukta aliyokuwa amevaa.
“Risasi hizi hapa”
alimwambvia huku akimpa risasi hizo alizozitoa mfukoni.
“Hii inakaa risasi ngapi?’
Simon akamuuliza wakati akizipokea risasi hizo.
“Inakaa risasi kumi na mbili,
hiyo ni mashine kubwa”
Simon alizitia zile risasi
kisha akaiunga ile bastola. Alinyanyuka kutoka kwenye sofa akaipachika bastola
ndani ya koti alilokuwa amevaa kisha akamuaga mwenyeji wake.
“Mimi nakwenda, makutano ni
kesho kutwa” alimwambia na kuelekea kwenye mlango.
Mtu huyo hakumjibu kitu,
alimtazama tu. Simon alifungua mlango akatoka na kujipakia kwenye gari,
akaliwasha na kuondoka. Alirudi jijini.
Alikuwa ameshapanga mahali pa
kwanza pa kumtega Dokta Kweka ni kwenye mkahawa wa Afrique ambapo Dokta Kweka
huenda kupata chai kila asubuhi.
Wakati anafika alimuona Kweka
akiondoka na gari lake
baada kumaliza kunywa
chai. Simon akaamua kumfuata nyuma. Alimfuata hadi kwenye kituo cha mafuta
ambapo Dokta Kweka alilitia mafuta gari lake.
Wakati Kweka analitia mafuta
gari hilo,
Simon aliliegesha gari pembeni mwa barabara kumsubiri. Dokta Kweka alipoondoka
na gari, Simon aliendelea kumfuata nyuma.
Kweka alikwenda kusimamisha
gari mbele ya hoteli moja maarufu jijini Dar akashuka na kuingia ndani ya
hoteli hiyo. Simon naye alilisimamisha gari kwa pembeni.
Alisubiri kwa karibu nusu
saa. Alipoona Kweka hatokei alishuka na kumfuata ndani ya hoteli. Alimtafuta
sehemu mbalimbali bila kumuona, akahisi pengine alikuwa amechukua chumba.
Akaenda mapokezi kumuulizia.
“Unasema nani?” msichana aliyekuwa
mapokezi alimuuliza.
“Dokta Kweka”
Msichana alitazama kwenye
kitabu cha wageni na kumwambia.
“Hapa tuna Alphonce Kweka
aliyetoka Mwanza, si Dokta Kweka”
Simon kwa kujua huenda Dokta
Kweka alikuwa akitumia majina ya bandia na kujifanya anatoka Mwanza
alimkubalia.
“Ndiye yeye, yuko chumba
namba ngapi?”
“Nenda chumba namba 45”
Chumba namba 45 kilikuwa
ghorofa ya kwanza. Simon alipanda ngazi hadi ghorofa ya kwanza akakitafuta
chumba namba 45. Alipokiona alifungua mlango akaingia ndani bila kubisha akiwa
na hakika kwamba atakutana Dokta Kweka.
Lakini alipoingia alikutana
na kitu cha kushangaza sana.
Alimkuta Dokta Kweka amelala chini huku damu ikimvuja kwenye kifua. Simon
alishuhudia tundu mbili za risasi zilizokuwa zikivuja damu kwenye kifua cha Kweka.
Ingawa macho ya Kweka
yalikuwa wazi yakilitazama dari jeupe la chumba cha hoteli lakini hayakuwa na
uhai wowote. Simon hakuhitaji mtaalamu wa kumuuliza kama
mtu huyo alikuwa hai au alikuwa amekufa. Alithibitisha yeye mwenyewe kuwa Kweka
hakuwa hai.
Kutokana na uthibitisho wa
tundu mbili za risasi zilizokuwa zikivuja damu kifuani mwa Kweka ilitosha
kumuonesha Simon kuwa Kweka alipigwa risasi mbili sekunde chache tu zilizopita.
Simon aliyazungusha macho
yake ndani ya chumba hicho na kujiuliza ni nani aliyempiga risasi Kweka katika
muda mfupi ule. Alikosa jibu akaona ageuke na kutoka ndani ya kile chumba.
Alifunga mlango akatoa kitambaa cha mkononi na kukisafisha kitasa kufuta alama
zake za vidole kisha akaondoka.
Alipotoka nje ya hoteli
hakuliona lile gari la Kweka. Wakati anaelekea lilipokuwa gari lake alimuona
mke ake aliyekuwa amechukuliwa na Dokta Kweka akishuka kwenye teksi. Akajifanya
hakumuona, alikwenda alipoliacha gari akafungua mlango na kujipakia.
Kabla ya kuliwasha gari hilo alimuona mke wake
akiingia ndani ya hoteli. Aliwaza kwamba huenda Kweka alikuwa amepangana na
msichana huyo wakutane hapo. Lakini atakachokwenda kukiona mle chumbani
kitamshangaza, Simon alijiambia.
Aliliwasha gari na kuondoka
mahali hapo. Akili yake ilikuwa ikijaribu kutafuta ni nani aliyemuua Dokta
Kweka. Alijiambia kama alivyokuwa akimuinda yeye kulikuwa na mtyu mwingine
aliyekuwa akimuinda ili amuue.
Atakuwa ni mtu mwepesi na wa
ajabu sana,
Simon alijiambia akiamini kuwa muuaji huyo alikuwa pale hoteli wakati Kweka
anafika.
Simon aliamini kuwa baada ya
mtu huyo kumuua Kweka, ndiye aliyeondoka na gari lake sekunde
chache tu zilizopita. Simon alijiambia kama angewahi kutoka tu angemfuma
akiondoka na gari hilo
na angemtambua.
Simon aliendelea kujiambia
kuwa japokuwa Kweka ameuawa na mtu mwingine aende akamwambie James kuwa amemuua
yeye ili aweze kumpa pesa aliyomuahidi.
Asante sana
muuaji, umenirahisishia kazi. Sasa nitaona ujanja wa yule mwanamke
aliyenitoroka mimi, Simon alijiambia kwa faraja.
Alitoa simu akampigia James.
James lipopokea simu
alimuuliza.
“James uko kazini au uko
nyumbani?”
“Niko kazini” James alimjibu
kwenye simu.
“Ukitoka mchana kwenda kula
tukutane”
“Si unapafahamu pale
ninapokula?”
“Ndiyo”
“Nikukute hapo”
“Sawa”
Wakati Simon anakata simu
alipata wazo jingine. Upande mmoja wa akili yake ulimwambia arudi pale hoteli
ili aone nini kitatokea. Akageuza gari na kurudi. Alipofika hapo hoteli
aliliegesha gari pembeni.
Tayari alishaona gari la
polisi na gari la hospitali yaliyokuwa yamesimama mbele ya mlango wa hoteli.
Wakati anasimamisha gari aliona polisi waliobeba machela iliyokuwa na mwili wa
Dokta Kweka wakitoka kwenye mlango wa hoteli.
Mwili huo ulipakiwa kwenye
gari la hospitali. Simon alimuona msichana wa Kweka aliyekuwa mke wake akitolewa
na polisi akiwa analia huku mikono yake imefungwa pingu.
Alipakiwa kwenye gari la
polisi. Gari hilo
likaondoka pamoja na gari la hospitali.
Ndipo Simon alipoondoka.
Hakujua ni kwanini mke wake wa zamani alikamatwa, wakati alipofika hapo hoteli
Kweka alikuwa ameshauawa.
ITAENDELEA kesho usikose hapahapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment