HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 16
ILIPOISHIA
Akaendelea “ Nimeupitia
ushahidi uliotolewa na mashahidi wawili wa upande wa mashitaka. Shahidi wa
kwanza amejitoa kuwa shahidi wa upande wa utetezi kutokana na maelezo yake
kumnufaisha mshitakiwa. Yeye ndiye aliyekuwa shahidi muhimu wa upande wa
mashitaka na amekuwa shahidi muhimu wa upande wa utetezi.
“Kwa vile shahidi muhimu
aliyetegemewa na upande wa mashitaka kueleza mahakama jinsi mshitakiwa
alivyofanya mauaji amedai kuwa mshitakiwa aliyeletwa mahakamani siye aliyeua na
hakukuwa na shahidi mwingine aliyesema kuwa mshitakiwa ndiye aliyeua, tayari
ushahidi huo umeshakuwa ni faida kwa mshitakiwa”
Jaji aliinua uso wake
akamtazama Mwendesha Mashitaka kisha akaendelea.
“Shahidi wa pili ambaye ni
mpelelezaji wa kesi hii ameshindwa kuielezea mahakama kinaganaga uhusiano wa
alama za vidole za mshitakiwa zilizokuwa kwenye simu ya marehemu na kwenye
kitasa cha mlango wa marehemu zinahusiana vipi na mauaji yaliyotokea.
“Kwa hivyo mahakama hii
inamuona mshitakiwa hana kosa la kujibu kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa
kutosha amabao ungeweza kumtia hatiani mshitakiwa. Mshitakiwa hutiwa hatiani
kwa kukiri kosa yeye mwenyewe au kwa ushahidi unaodhihirisha kosa bila kuacha
shaka”
SASA ENDELEA
Jaji aliinua tena uso wake
akamtazama Mwendesha Mashitaka ambaye uso wake ulikuwa umepatwa na fadhaa.
Akaendelea kusoma muhutasari huo.
“Katika kesi ya mauaji kama
hii ambayo hukumu yake inaweza kuwa kifo ni lazima kuwepo ushahidi mzito na
usio na shaka. Kwa hiyo narudia kusema kuwa mshitakiwa hana kosa la kujibu na
namuachia huru”
Alipofika hapo alimtazama
mshitakiwa na kumwambia.
“Uko huru, nenda zako”
Simon Puto alikuwa amepatwa
na kiwewe cha kuachiwa. Alikuwa amemkodolea macho jaji kabla ya kuzinduka na
kushuka kizimbani haraka. Alipongezana na wakili wake ambaye alikuwa akimsubiri
mbele ya kizimba mara tu jaji alipomwambia, nimukuachia huru”
Mwendesha Mashitaka na
Inspekta Amour walikuwa wakiwatazama huku wakitikisa vichwa kwa uchungu.
Baada ya kupongezana na
wakili wake, Simon alitoka nje ya mahakama na kukutana na James aliyekuwa
akimsubiri mbele ya lango la mahakama.
James alimpa mkono na
kumpongeza kutokana na kuachiwa huru. Akampigapiga kwenye bega na kumwambia.
“Kupotea njia ndiyo kujua
njia, usijali”
“Asante sana” Simon alimjibu
uso wake ukiwa umejaa aibu.
“Okey gari ile pale,
twendezetu”
James alimuonesha gari lake
alilokuwa ameliegesha mbele ya viwanja vya mahakama.
James na Simon walifuatana
kuelekea kwenye gari hilo. Wakajipakia. James akaliwasha na kuondoka na Simon.
Miaka miwili iliyopita mtu mmoja
ambaye aliwahi kufanya kazi wizara ya afya akiwa na taaluma ya udaktari aliwahi
kusuhubiana na Maria kabla ya kifo chake.
Dokta Kweka alifahamiana na
Maria kwa sababu ya kufika mahakamani mara kwa mara akiwa na shughuli zake
binafsi zilizohitaji vibali vya mahakama.
Wakati huo Maria akiwa karani
wa mahakama ndiye aliyekuwa akimhudumia Dokta Kweka, kupokea nyaraka zake na
kuzifikisha kwa hakimu na kisha kuzichukua tena kwa hakimu na kumpa Dokta
Kweka.
Alikuwa akimrahisishia sana
kazi. Badala ya Kweka kusota kwenye mabenchi ya mahakama kumsubiri hakimu au
kuelekezwa kwenda huku na huko, alikuwa akizikabidhi kazi zake kwa Maria ambaye
huzishughulikia na kisha huja kuzichukua tena kwa Maria.
Maria alikuwa akimtumikia
Kweka kwa sababu Kweka alikuwa akimpa bahashishi nono. Kuna siku Kweka
alikwenda mahakamani hapo asubuhi akampa nyaraka zake Maria. Maria akamwambia
azipitie mchana.
Saa sita mchana Kweka alifika
mahakamani. Maria alikuwa ameshazishughulikia. Akampa.
“Naomba tuonane saa saba kwa
ajili ya chakula cha mchana” Kweka akamwambia Maria.
“Unataka kunipa ofa?” Maria
akamuuliza.
“Au hupendi?”
“Kwanini…tukutane hoteli
gani?’
“Nitakuwa pale Afrique”
“Nitahitaji usafifiri”
“Usijali”
Dokta Kweka alitia mkono
kwenye mfuko wa ndani wa koti lake akatoa noti mbili za shilingi elfu kumi kumi
akampa.
“Usafiri wako ndio huo”
“Asante”
“Usikose”
“Sitakosa”
Kweka akaondoka.
Saa saba mchana Maria akafika
Afrique. Ulikuwa mkahawa uliokuwa juu ya ghorofa. Watu waliokuwa wakiingia
katika mkahawa huo walikuwa watu wanaojiweza kwani bei yake ya vyakula ilikuwa
kubwa.
Maria alimkuta Kweka
akimsubiri. Alipomuona alimfuata kwenye meza aliyokuwa ameketi na yeye akaketi.
Mhudumu alipowaendea, Kweka alimwambia Maria.
“Agiza chakula unachotaka”
Kweka mwenyewe aliagiza ugali
na kuku. Maria akaagiza chips kuku. Wote wawili walitaka waletewe pia juisi ya
nanasi.
Mhudumu alipoondoka. Kweka
aliendelea kusoma gazti alilokuwa amelishika mkononi.
Vyakula walivyoagiza
vilipoletwa, Kweka alilikunaja gazeti wakaanza kula.
“Kuna kitu nilikuwa nataka
kukwambia Maria, umekuwa ukinisaidia sana.
Nashukuru kwa hilo.
Nilikuwa nikijiuliza ni kwanini tusisuhubiane mimi na wewe?” Kweka alimwambia
Maria.
Maria alinyamaza kimya.
“Nadhani nitatafuta muda
mwingine mzuri zaidi ili tuliongelee hilo
kwa kirefu au unasemaje?”
Maria akabetua mabega.
“Ni sawa tu”
“Unadhani lini utakuwa na
nafasi nzuri, siku ambayo si ya kazi?”
“Jumapili mchana nikitoka
kanisani”
“Nitakupata wapi?”
“Hapa hapa”
“Naomba unipatie namba yako
ya simu”
Maria hakuwa na uchoyo na
namba yake, akampa. Kweka naye akampa namba yake. Baada ya kumaliza chakula
Kweka alimpa Maria shilingi laki moja.
“Zitakusaidia kununulia vocha
ya simu”
“Asante
sana,
nashukuru”
Wakaagana. Siku ya jumapili
Maria alitimiza ahadi. Alipotoka kanisani alipanda teksi hadi mkahawa wa
Afrique. Alipofika akakutana na Kweka.
Siku ile ndio Kweka alimtolea
undani wake. Alimwambia wazi kuwa alikuwa akimuhitaji katika maisha yake. Kule
kutoa kauli ya kukubali tu, Kweka alimpeleka ‘shopping’ siku ile ile.
Alimfanyia shoping ya shilingi laki tano.
ITAENDELEA kesho hapahapa tangakumekuchablog, usikose uhondo huu
No comments:
Post a Comment