HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 21
ILIPOISHIA
James lipopokea simu
alimuuliza.
“James uko kazini au uko
nyumbani?”
“Niko kazini” James alimjibu
kwenye simu.
“Ukitoka mchana kwenda kula
tukutane”
“Si unapafahamu pale
ninapokula?”
“Ndiyo”
“Nikukute hapo”
“Sawa”
Wakati Simon anakata simu
alipata wazo jingine. Upande mmoja wa akili yake ulimwambia arudi pale hoteli
ili aone nini kitatokea. Akageuza gari na kurudi. Alipofika hapo hoteli
aliliegesha gari pembeni.
Tayari alishaona gari la
polisi na gari la hospitali yaliyokuwa yamesimama mbele ya mlango wa hoteli.
Wakati anasimamisha gari aliona polisi waliobeba machela iliyokuwa na mwili wa
Dokta Kweka wakitoka kwenye mlango wa hoteli.
Mwili huo ulipakiwa kwenye
gari la hospitali. Simon alimuona msichana wa Kweka aliyekuwa mke wake
akitolewa na polisi akiwa analia huku mikono yake imefungwa pingu.
Alipakiwa kwenye gari la
polisi. Gari hilo
likaondoka pamoja na gari la hospitali.
Ndipo Simon alipoondoka.
Hakujua ni kwanini mke wake wa zamani alikamatwa, wakati alipofika hapo hoteli
Kweka alikuwa ameshauawa.
SASA ENDELEA
Simon akafikiria kwamba aende Kimara. Kwa vile kile
alichokuwa anakitaka kimetimia aliona aende akajipongeze kwa kinywaji kwenye
baa ya ABC.
Alipofika alilisimamisha gari
kwenye eneo la kuegesha la ABC akashuka na kuingia ndani. Akiwa kwenye ukumbi
wa baa, Simon alizungusha macho kumtafuta kimanzi wake, lakini hakumuona.
Alikwenda kaunta akaketi
kwenye kigoda na kumuuliza msichana aliyemkuta.
“Kimanzi wangu yuko wapi?”
“Anaingia usiku” msichana
huyo alimjibu.
“Oh! Sikufurahi kutomkuta,
nipatie kinywaji”
“Unaweza kumfuata nyumbani
kwake kama unamuhitaji”
“Muda huo wa kufuatana
majumbani ndio sina”
“Basi njoo usiku”
“Nipatie kinywaji”
“Kinywaji gani?”
“Ndiyo tatizo la kutomkuta
Kimanzi, yeye ndiye anayejua kila kitu. Nipatie toti mbili za kunyagi na
kibonge cha barafu”
“Ukija tena kesho nitakuwa
ninajua sasa”
Msichana alimpatia kinywaji hicho.
Simon aliinua bilauli akaipiga funda konyagi iliyopozwa kwa barafu kisha
akaimeza huku akikunja uso.
Aliondoka hapo baa majira ya
saa sita. Ingawa alikunywa konyagi ya kutosha, hakuonesha dalili yoyote ya
kulewa. Alikwenda katika hoteli aliyopanga kukutana na James.
Alipofika alimkuta James
ameshafika.
“Nina habari njema, nataka
kukwambia” Simon aliwambia James huku akiketi.
“Niambie”
“Nimeshamuua Dokta Kweka”
“Sipendi utani Simonai!
“Si utani, tayari nimemuua”
“Umempata
wapi?”
“Nilimuandama na gari hadi
Suzy Hotel, alikwenda kupangisha chumba pale sijui ni kwa ajili gani.
Nikamuingilia chumbani na kumpiga risasi mbili”
James alikuwa akimsikiliza
kwa makini.
“Ilikuwa
saa ngapi?”
“Wakati ule ninakupigia simu
ndiyo ninatoka kumuua”
“Simon una hakika kuwa
umemuua?”
“Amini usiamini. Maiti yake
imechukuliwa na polisi na yule mke wangu alijitokeza pale naye alikamwatwa”
“Alikamatwa kwa sababu gani?”
“Sijajua bado lakini nadhani
ni kwa sababu alikutwa katika eneo la tukio akashukiwa yeye”
“Wakati huo wewe ulikuwa
wapi?”
“Mimi baada ya kumpiga
risasi, nilitoka haraka mle chumbani nikashuka chini na kuingia garini. Nilikaa
kwenye gari kwa muda mrefu, nikamuona yule mwanamke. Alifika pale kwa teksi,
sijui alifuata nini. Akaingia ndani ya hoteli. Baadaye nikaona polisi wamefika”
“Nitakwenda hapo hoteli
kuhakikisha”
“Itakuwa vyema sana, nenda sasa hivi”
“Chakula pia nitasamehe, acha
niende kwanza. Nitakupigia simu nikueleze tukutane wapi. Sawa?”
James alikuwa ameshanyanyuka kwenye
kiti.
“Sawa”
James akatoka na kumuacha
Simon akimtazama.
Dakika chache baadaye
alilisimamisha gari mbele ya hoteli ya Suzy. Mandhari aliyoiona hapo nje ya
hoteli, peke yake ilimuashiria kuwa palikuwa na tukio ambalo halikuwa la
kawaida.
Mbali ya polisi kuendelea kuonekana
katika eneo hilo
kulikuwa na watu waliokuwa wamezagaa mbele ya hoteli.
James alishuka kwenye gari
akaelekea kwenye mlango wa hoteli. Aliwasikia watu wakizungumza kuhusu mtu
aliyeuawa kwa kupigwa risasi ndani ya chumba cha hoteli hiyo.
Aliingia ndani ya hoteli
akaelekea upande wa mkahawa. Kulikuwa na watu wawili watatu wakila chakula
lakini wafanyakazi wa hotelini hapo walionekakana kuwa kwenye taharuki.
James aliketi kwenye meza
iliyokuwa na mtu mmoja.
“Kaka habari ya saa hizi?”
akamsalimia.
“Nzuri. Karibu”
“Asante”
Mhudumu alipomfuata
alimuagiza chakula alichohitaji. Mhudumu alipoondoka alimuuliza yule mtu
aliyemkuta akila chakula.
“Pametokea nini hapa hoteli,
naona watu wengi na polisi?’
“Nilisikia kuna mtu ameuawa
humu ndani” Mtu huyo alimjibu.
James akajifanya anashangaa.
“Kuna mtu ameuawa humu ndani
ya hoteli?”
“Nimesikia aliuawa chumbani, alipigwa risasi
na mtu asiyefahamika”
“Huyo mtu amekamatwa?”
“Hakufahamika”
“Loh! Dar
es Salaam imeharibika sana
siku hizi. Watu wanauana kama nzige!”
“Kwa kweli inatisha sana”
“Na sidhani kama
atapatikana”
“Nimesikia
kuna mwanaamke aliyekamatwa aliyehusishwa na hayo mauaji”
“Mwanamke? Alikamatwa wapi?”
“Hapa hapa hoteli”
Pakapita kimya hadi chakula
alichoagiza James kilipoletwa.
“Eti huyo mtu aliyeuawa hapa
hoteli ni nani?” James akamuuliza mhudumu huyo.
“Alikuwa ni mteja wetu.
Alichukua chumba tangu jana. Leo mchana ndio amekutwa amepigwa risasi chumbani”
Mhudumu huyo akamueleza.
“Alichukua chumba tangu
jana?”
“Ndiyo alikuja jana, hatujui
ni nani aliyemuua na kwa sababu gani”
“Eti kuna mwanamke
aliyekamatwa?”
“Huyo mwanamke ndiye
aliyesababisha tujue kuwa huyo mtu ameuawa. Aliingia mle chumbani kisha akatoka na kupiga
kelele”
“Kwa hiyo siye aliyemuua?’
“Hatujui. Yeye anadai yule
mtu ni mume wake lakini yule bwana alikuja peke yake hapa hoteli”
“Polisi
wamemkamata kwa kumtilia mashaka?” Yule mtu mwingine alisema.
Baada ya hapo mhudumu
aliondoka. James alipomaliza kula alilipa pesa naye akaondoka. Sasa aliamini
kuwa Dokta Kweka alikuwa ameuawa.
“Nitapata mengi kwenye
taarifa ya habari ya usiku” James alijiambia wakati akiendesha gari kurudi
kazini kwake.
**************
Alikuwa mfanyakazi mmoja wa
hoteli ya Suzy aliyeitwa Mage ambaye alimpigia simu Vicky na kumjulisha kuwa
mwanaume wake alikuwa amepangisha chumba hapo hoteli.
Vicky ambaye alikuwa mke wa
Simon kabla ya kuchukuliwa na Dokta Kweka alikuwa akifahamiana na Mage na
ulikuwa umbea tu wa kike uliomfanya Mage ampigie simu.
ITAENDELEA kesho usikose uhondo huu
No comments:
Post a Comment