HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 17
ILIPOISHIA
Mhudumu aliondoka. Simon
akamtazama Kweka.
“Ndiyo Dokta, umepata habari
gani?”
Dokta Kweka akatabasamu.
“Umefanya kazi nzuri,
nimeshapata taarifa zote. Asante sana”
Simon akacheka.
“Jana nilipokwambia ulidhani
ni mzaha”
“Nilijua haikuwa mzaha,
nitakupatia pesa yako iliyobaki”
Supu ilipoletwa Simon alianza
kula huku akiendelea kuzungumza na Kweka. Walipomaliza kula Dokta Kweka
alifungua mkoba wake akampa Simon shilingi milioni mbili na nusu.
Simon alizitia mifukoni kisha
akamuaga Kweka na kunyanyuka.
“Subiri” Kweka alimwambia.
Simon akainamia meza ili
kumsikiliza Kweka.
“Ndiyo”
SASA ENDELEA
“Usifurahie pesa tu, kumbuka
kwamba Inspekta Amour wa jeshi la polisi ameshingia kazini kumtafuta muuaji.
Kwa hiyo jihadhari”
“Ninafahamu”
“Kama una fahamu, sawa”
Simon akaondoka.
Kwa kawaida kila ifikapo saa
mbili usiku Simon alikuwa na tabia ya kufika katika klabu ya usiku ya ABC
iliyopo Kimara. Pale ABC alikuwa na msichana wake ambaye alikwishaachana naye
baada ya kuoana na Vicky.
Siku chache baada ya mauaji
ya Maria, Inspekta Amour aliipata namba ya msichana huyo kutoka kampuni ya simu
na kumpigia. Baada ya kumpigia alimfuatilia hapo klabu na kukutana naye uso kwa
uso.
Simon alipofika klabuni hapo
saa mbili usiku, msichana huyo alikwenda kumuita lakini Simon alipomuona
aliyemuita aliamua kukimbia. Alikuwa akimjua Inspekta Amour na alijua kuwa
alikwenda pale kumkamata yeye kufuatia mauaji ya Maria.
Baada ya Simon kukimbia Amour
alimuandama. Ndipo yalipotokea yaliyotokea ambapo Simon alikamatwa na hatimaye
kufikishwa mahakamani kabla ya kuachiwa huru na mahakama baada ya James kutoa
ushahidi ulioonesha kuwa Simon hakumuua Maria na kwamba alikuwa hamtambui.
Tangu Simon alipokamatwa hadi
kuachiwa huru ilikuwa imeshapita miezi sita.
***** **********
James alipoondoka na Simon
nje ya mahakama, alikwenda naye nyumbani kwake Msasani. Alishuka kwenye gari
akamkaribisha ndani.
“Karibuni ndani Mr Simon”
alimwambia.
Waliingia ndani na kutokea
kwenye sebule pana iliyopangwa vizuri.
“Karibu ukae tafadhali”
Simon alikaa kwenye kochi
mojawapo.
“Umepata kifungua kinywa?”
“Uji tu”
“Subiri nikutayarishie
kikombe cha chai ya maziwa”
James alimwambia na kwenda
jikoni alichukua chupa ya chai, bisikuti na vikombe viwili. Alirudi sebuleni
akamimina chai kwenye vikombe viwili. Kimoja alimpa Simon akamsogezea sahani ya
bisikuti.
“Karibu” alimwambia mgeni
wake huku akichukua biskuti moja na kuipeleka midomoni. Alitafuna na kuisukumia
na kikombe cha chai.
Simon naye aliinua kikombe
akapiga funda la chai ya maziwa kisha akaokota bisikuti na kuitia midomoni.
“Umekaa ndani miezi mingapi?”
James alimuuliza huku akiuweka mguu mmoja juu ya mwingine.
“Huu ni mwezi wa sita” Simon
alimjibu.
“Pole sana, yote ni maisha”
James alimwambia baada ya kumeza funda la chai.
Pakapita kimya cha sekunde
kadhaa kabla ya james kumtazama Simon.
“Najua umeshangaa sana
kutokana na ushahidi wangu dhidi yako. Nadhani hukuutegemea kabisa”
“Ni kweli”
“Katika kipindi ambacho wewe
uko mikononi mwa polisi niligundua mambo mengi ambayo sikuyatarajia” James
aliendelea kumueleza.
Alimeza funda la chai kisha
akaongeza.
“Niligundua kwamba marehemu
Maria alikuwa na mchumba mwingine kabla yangu. Kuna visa walifanyiana na Maria
akaamua kuvunja uchumba. Kitendo kile cha Maria kuvunja uchumba kilimpa yule
mtu chuki akaamua kukutuma wewe umuue…”
Muda wote Simon alikuwa kimya
akinywa chai huku akimsikiliza James kwa makini.
“Baada ya wewe kukamatwa, mtu
huyo alimfuata mke wako akamchukua. Alimwambia mume aliyemuoa ni jambazi na
atanyongwa kutokana na kukabiliwa na kesi ya mauaji. Hivi sasa mke wako si wako
tena amechukuliwa na mtu huyo na anaishi naye nyumbani kwake”
Maneno ya kuchukuliwa mke
wake na Dokta Kweka yalipiga kwenye moyo wa Simon kama mkuki uliotiwa sumu.
Akashituka na kumkazia macho James.
James alitoa simu yake
akaingia katika eneo la kuhifadhi picha na kumuonesha Simon picha
zinazomuonesha Dokta Kweka akiwa na Vicky. Kulikuwa na picha tatu, mojawapo
iliyomchoma zaidi Simon ilimuonesha Vicky akipigana busu na Dokta Kweka huku
Dokta Kweka amekishika kiuno cha Vicky.
“Nilitaka utoke ili
nikuoneshe hizi picha. Hivi sasa mke wako anatembea na gari alilopewa na huyo
mtu” James alizidi kumuumiza Simon aliyekuwa ameduwaa.
James alikuwa amemuachia simu
Simon, akainuka na kuanza kuranda.
“Mimi ninajua kuwa wewe
ulimuua mchumba wangu lakini usingemuua kama usingetumwa. Huyo aliyekutuma si
tu amenifanyia ubaya mimi, amekufanyia ubaya na wewe kwa kukuchukulia mke wako.
Pengine alikuwa akimtamani siku zote”
Simon aliweka simu kwenye
kochi akamtazama James. Uso wake sasa ulikuwa umetaharuki.
James aliendelea kuranda.
“Sikutaka unyongwe na huyo
mtu abaki akitanua” alisema na kuongeza.
“Nilikutoa kwa makusudi ili
nikutume uende ukamuue kama alivyomuua Maria”
Jame alisita akamtazama
Simon.
“Ukimuua mtu huyo nitakuwa
nimekusamehe”
Simion alikuwa ameduwaa kwa
sekunde kadhaa akiwaza. Sebule ikawa kimya. James alikwenda kuketi kando ya
Simon.
“Unafikiri nini?” akamuuliza.
“Nanifikiri kwamba Dokta
Kweka amenitoa muhanga” Simon alimjibu huku macho yake yakimkwepa James.
“Kwanini?”
“Ni kweli alinituma nimuue
Maria. Sikujua ni kwanini alitaka Maria afe lakini mbali na hilo bila shaka
alijua kuwa nitakamatwa na alishapanga kumchukua mke wangu. Mtu yule ni mshenzi
sana”
“Nataka uende ukamuue!” James
alirudia kumwambia kwa mkazo.
“Ameniweka katika wakati
mgumu hivi sasa. Miezi sita niliyokaa ndani nimepoteza kila kitu, nyumba, mke
na pesa…”
“Kwa tatizo la pesa
nitakusaidia. Unahitaji kiasi gani cha kuanzia maisha?”
“Kama milioni moja hivi”
“Nitakupatia laki tano,
ukimuua huyo mtu aliyekutuma umuue Maria, nitakumalizia laki tano hapo hapo”
“Utanipatia sasa hivi?”
“Kama tumekubaliana
nitakupatia”
“Bado nitkuwa na tatizo la
usafiri”
“Nitakukodia gari”
“Sawa. Nipatie hizo pesa na
usafiri. Nitakwenda kumuua”
“Unadhani utaweza kumpata kwa
leo?”
“Kwa leo si rahisi, nipe siku
tatu”
“Sawa. Sasa twende kwenye ATM
nikatoe pesa”
James akanyanyuka. Simon naye
akainuka. Walitoka nje wakajipakia kwenye gari la James na kuondoka.
“Ulifahamianaje na Dokta
Kweka?” James alimuuliza Simon wakati gari likiwa kwenye mwendo.
“Alinitafuta”
ITAENDELEA kesho hapahapa usikose uhondo huu
No comments:
Post a Comment