HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 22
ILIPOISHIA
Alimuita kwa kumpigia simu ya
mkononi.
“Rose unaitwa hapa kaunta”
“Naitwa na nani?” Sauti ya
Rose ikauliza kwenye simu.
“Kuna askari anakuulizia”
“Anataka nini?”
“Sijui, we njoo umsikilize.
Si unajua kuna tukio limetokea hapa hoteli”
“Mimi bado nina kazi”
“Njoo mara moja”
Fatuma akakata simu. Dakika
chache baadaye Rose akafika hapo mapokezi. Alimsalimia Inspekta Temba kisha akamuuliza Fatuma.
“Nani
ananiita?”
“Nimekuita mimi” Inspekta
Temba alimwambia na kuongeza.
“Naitwa Inpekta Temba,
natokea makao ya polisi. Wewe ndiye Rose?”
“Ndiye mimi”
“Unamfahamu Vicky?”
“Namfahamu?”
“Ni kweli kwama mtu aliyeuawa
hapa hoteli ni mume wake?”
“Ndio, ni mume wake”
“Wewe ndio ulimpigia simu
kumjulisha kuwa mume wake amekodi chumba hapa hoteli”
Rose akagwaya.
“Nataka jibu”
SASA ENDELEA
“Nilimpigia lakini tulikuwa
na maongezi mengine, hilo nililiingiza tu baada ya kumuona mume wake yuko hapa”
“Sawa. Hebu nieleze ukweli, huyo
mume wake alikuwa na msichana?”
“Sikumwambia kama mume wake
alikuwa na msichana…”
“Najua hukumwambia isipokuwa
nakuuliza mimi, je mume wake alikuwa na msichana”
“Sikumuona na msichana”
“Nina maana kwamba kama alikuwa na msichana ndiye atakuwa muuaji”
“Kusema kweli hakuwa na
msichana”
“Au alikuwa naye lakini
hamkumuona, pengine alikuja baadaye”
“Inawezekana”
“Sawa, asanteni sana.
Nitakuja kuwaona wakati mwingine”
Dakika chache baadaye wakati
Temba akiwa kwenye gari alipigiwa simu na kamanda
wa polisi.
Ingawa hakupenda kuzungumza
kwenye simu wakati anaendesha lakini alipoona namba ya kamanda
wake aliipokea simu haraka.
“Afande, nakusikiliza”
“Uchunguzi wako juu ya mauaji yaliyotokea katika
hoteli ya Suzy umefikia wapi?” Sauti nzito ya kamanda
wa polisi ikamuuliza kutoka simu ya upande wa pili.
“Bado ninaendelea na
uchunguzi huo”
“Waandishi wa habari wameanza
kufika ofisini kwangu kutaka kujua nini kilitokea hadi mtu huyo akauawa. Lakini
mpaka sasa sijakuwa na taarifa kamili”
“Yule mtu alikutwa akiwa ameshakufa katika chumba
alichokuwa amepangisha tangu jana. Aliyegundua maiti yake ni msichana mmoja
aliyedai ni mke wa marehemu, alifika pale hoteli na kugundua kuwa mume wake
alikuwa ameuawa”
“Huyo msichana aliyedai ni
mke wa marehemu alitokea wapi?”
“Alifika pale hoteli baada ya
kupigiwa simu na mfanyakazi mmoja wa hapo hoteli ambaye ni rafiki yake,
alimwambia kwamba mume wake alikuwa amechukua chumba hapo hoteli. Nadhali
alikuwa amekuja kumfumania akidhani mume wake alikuwa na msichana”
“Sasa uchunguzi wenu wa awali
umeonesha kwamba marehemu aliuawa kwa sababu gani na labda aliuawa na nani?”
“Ndio tunaendelea na
uchunguzi afande”
“Kuna mtu yeyote ambaye
mnamshikilia kufuatia tukio hilo”
“Tunamshikilia yule msichana
ambaye alidai ni mke wa marehemu”
“Ningependa hadi kesho mchana
nipate taarifa iliyo kamili”
“Sawa afande nitajitahidi”
Simu ikakatwa.
Saa mbili usiku James akiwa
mbele ya televisheni yake aliisikia taarifa ya kuuawa kwa Stiphano Kweka na mwili wake
ulioneshwa ukipakiwa kwenye gari la polisi.
Taarifa ya polisi ikaeleza
kuwa mtu huyo aliuawa kwenye chumba cha hoteli ya Suzy ambacho alikuwa
amepangisha.
Taarifa hiyo iliendelea
kueleza kuwa Kweka aliuawa kwa kupigwa risasi mbili za bastola kifuani akiwa
katika chumba hicho na kwamba polisi walikuwa wanamshikilia msichana mmoja
aliyedai kuwa ni mke wa marehemu kwa uchunguzi wa tukio hilo.
Baada ya kuiona taarifa hiyo
James alimpigia simu Simon.
“Kesho ni jumamosi siendi
kazini, njoo nyumbani kwangu saa nne asubuhi nikupe chako” alimwambia.
“Lakini umeshathibitisha”
“Ndiyo nimethibitisha”
“Sawa. Basi ni hapo kesho
asubuhi”
James akakata simu.
Alifarijika sana
kupata uhakika kuwa Kweka alikuwa ameuawa.
“Sasa nimetimiza kisasi
changu, hata Maria huko aliko atafurahi” akajiambia kimoyo moyo.
Akiwa amelala katika chumba
cha mahabusi usiku, Vicky alipata wazo ambalo hapo mapema hakuwa amelitia
maanani. Pengine ilikuwa sakafu ya mahabusi iliyokuwa ikizizima ndiyo
iliyomfanya amkumbuke Simon.
Alikumbuka kwamba wakati
nafika katika hoteli ya Suzy alimuona Simion. Alimuona wakati anashuka kutoka
kwenye teksi iliyokuwa imempeleka hotelini hapo. Alipomuona aliugeuza uso wake
haraka akajifanya kama hakumuona.
Akajiuliza Simon alifuata
nini pale hoteli? Na licha ya kuwa na hakika kuwa alionekana na Simon,
alijiuliza ni kwanini Simon hakumuulia kitu wakati anajua kuwa alimtoroka na
kuchukuliwa na mwanume mwingine?
Hapo ndipo shaka ilipoingia
kwa Viky, kwamba huenda Simon ndiye aliyemuua Dokta Kweka kwa chuki ya
kuchukuliwa mke wake.
“Wazo hilo halikunijia mapema lakini inawezekana
kuwa Simon ndiye aliyemuua Dokta Kweka kwa sababu alishawahi kukamatwa kwa
tuhuma za mauaji” Vick alijiambia huku akiinuka.
Aliketi kwenye sakafu na
kuendelea kujiambia.
“Kama
ningewambia polisi mapema, Simon angelikwishakamatwa na pengine wangeniachia
mimi”
Asubuhi kulipokucha Vicky
aliwambia polisi kuwa alitaka kuzungumza na Inspekta Temba. Polisi walidhani
kuwa Vicky alikuwa ameamua kulikiri kosa la mauaji.
Inspekta Temba alipofika
alijulishwa kuwa Vicky alikuwa anataka kuzungumza naye.
“Mleteni” akawambia.
Polisi mmoja mwanamke alikwenda kumtoa mahabusi na
kumpeleka ofisini kwa Temba.
“Kaa kwenye kiti” Temba
alimwambia. Ilikuwa nadra sana
kwa polisi kumkaribisha mtuhumiwa kwenye kiti.
Vicky akaketi.
“Unasemaje?” akamuuliza.
“Kuna kitu ambacho jana
nilisahau kukizungumza” Vicky akaanza.
“Kitu gani? Kizungumze hivi
sasa”
“Mimi kabla ya kuolewa na
marehemu nilikuwa na mume mwingine anayeitwa Simon. Tulitenganishwa na Padre
baada ya mume wangu huyo kukabiliwa na kesi ya mauaji….”
“Ndiyo, endelea”
“Mwanzo nilijua kuwa atanyongwa lakini baadaye
mahakama ilimuachia huru kwa kumuona hakuwa na hatia”
“Ndiyo”
“Mimi sikutaka tena kurudi
kwa yule mwanaume, ninahisi kuwa yeye ndiye amemuua Dokta Kweka”
“Unahisi tu au unayo maelezo
zaidi ya kutuambia?”
“Ninahisi na pia nilimuona
jana pale hoteli?”
Inspekta Temba akagutuka.
“Ulimuona wakati gani na
alikuwa wapi?”
“Wakati nashuka kwenye teksi
nilimuona”
“Ulimuona wapi?”
“Nilimuona akitoka kwenye
mlango wa hoteli”
“Halafu akaenda wapi?”
“Sikumpatiliza tena, mimi
nilijifanya kama sikumuona nikaingia hoteli.
Na ndio nikaenda kumkuta Kweka ameuawa kule chumbani”
“Yeye alikuona?”
“Nina hakika kuwa aliniona”
“Alikusemesha chochote?”
“Hakunisemesha”
“Je aliwahi kukwambia au
kumwambia marehemu kuwa atafanya kitu?’
“Hakuwahi kuniambia wala
kumwambia marehemu kuwa atafanya kitu lakini nina shaka naye”
“Ungetuambia tangu jana
tungelikwisha mkamata. Anaweza kuwa mtuhumiwa namba mbili. Anapatikana wapi?”
“Kwa sasa sijui anapatikana
wapi?”
“Unadhani tutampataje”
“Hapo siwezi kujua”
“Una namba yake ya simu?”
ITAENDELEA kesho hapahapa tangakumekuchablog, Usikose uhondo huu
No comments:
Post a Comment