Thursday, April 14, 2016

KAYA 10 WAZIKIMBIA MAJUMBA YAO BAADA YA MAJI KUINGIA NDANI



Tangakumekuchablog
Tanga, KUFUATIA Mvua kubwa iliyonyesha  kwa siku mbili mfululizo mjini Tanga, familia zaidi ya 10 wameyahama makazi yao na kuiomba Serikali kujenga miundombinu ya maji baada iliyopo kufukiwa na mchanga na maji kupotea njia.
Mvua hiyo ambayo ilionyesha mfululizo ilisababisha maji kuingia mitaani na kuathiri kaya maeneo mbalimbali kata ya  Makorora, Mikanjuni  Sahare na Magaoni.
Wakizungumza na Tangakumekuchablog leo  baadhi ya familia ambazo wameyakimbia makazi yao, wamesema toka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanga ilipotoa tahadhari ya uwepo wa mvua kubwa waliiambia halmashauri ya jiji la Tanga  juu ya mifereji hiyo kujaa mchanga na kuota majani.
“Tuliona kwenye vyombo vya habari juu ya kuwepo kwa mvua kubwa na upepo mkali, nyumba zetu haziko mabondeni lakini tunaishi kandokando ya mifereji ipitishayo maji mengi” alisema Said Ally na kuongeza
“Mfereji huu ulioanzia gofu viwandani na kupitia mabawa na mikanjuni hupitisha maji mengi, yapata mida mrefu haufanyiwa usafi na badala yake umejaa michanga na majani na mvua ikinyesha yote huja mitaani” alisema
Ally alisema  mvua hiyo imeacha njia na kuingia majumbani na kuharibu samani nyingi za ndani hivyo ili kuepusha kutokea  maafa zaidi wamefikia maamuzi ya kuyahama makazi yao.
Wameitaka halmashauri ya jiji kuchukua hatua za haraka kabla mvua hizo hazijafikia hatua ya kunyesha masaa 24 na kufikia hatua ya kuishi kwa hofu.
Kwa upande wake mkazi wa Sahare, Khamis Mdoe, alisema  hakunamafuriko badala yake ni maji hayana muelekeo wa kupitia na hulazimika kuingia kwenye makazi ya watu.
Alisema kama halmashauri ya jiji la Tanga itaifanyia usafi mifereji yake na kuongeza mengine kutokana na mji kuongeza Tanga hakutakuwa na mafuriko mitaani.
“Nashangaa kusikia katikati ya jiji kuna mafuriko tena familia kuyahama majumba yao, yale siyo mafuriko bali ni maji hayana mwelekeo wa kwenda” alisema Mdoe
Ameiomba halmashauri ya jiji hilo kuboresha mifumo yake ya upitishaji maji hasa nyakati za mvua ikiwa na pamoja na ubireshaji wa mfumo wa maji taka ambayo hufurika mvua ikinyesha.
                                                           Mwisho

No comments:

Post a Comment