Ndege isiyotumia mafuta yatua Misri
Ndege inayotumia
nishati ya jua imetua mjini Cairo, Misri na kupokelewa na waziri na
maafisa wengine wa ngazi ya juu wa maswala ya usafiri wa anga wa nchi
hiyo.
Ndege hiyo ilikuwa imefanya safari ya saa 48 kutoka mji wa Seville, Uhispania hapo Jumatatu.Haikutumia mafuta ya ndege ya kawaida hata chembe bali nguvu za kawi zinazotokana na miali ya jua.
Marubani wawili wa Uswizi ndio wanaoiongoza ndege hiyo, huku kituo cha mwisho cha safari hiyo ya majaribio kikiwa Abu Dhabi.
Rubani Andre Borschberg amenukuliwa akisema safari ya saa chache kabla ya kutua mjini Cairo ndiyo ilikuwa na changamoto zaidi kwani kwa mara ya kwanza betri ya ndege hiyo ilikuwa imeshuka hadi asilimia 30 pekee.
Sasa rubani Bertrand Piccard ndiye atachukua usukani wa mkondo wa mwisho wa safari hadi Umoja wa Milki za Kiarabu lakini haijajulikana mkondo huo utachukua muda gani kwani itategemea zaidi hali ya hewa.
Huko ndiko mpango huo wa majaribio wa ndege hiyo ya sola ulianza hapo 2015.
Marubani hao Piccard na Borschberg awali walikuwa wakifanyakazi katika mradi wa sola uitwao Solar Impulse kwa muda wa zaidi ya miaka 10.
Japo ni safari ya polepole ndege hiyo imeweza kuvuka anga zaidi ya nchi 7 nyinginezo zikiwa ni zile zilizo na shughuli nyingi za ndege za usafiri wa umma.
Ni mradi ambao kufikia sasa umegharimu $100 millioni, tangu 2002 lakini lengo la utafiti huu ni kuwa huenda hatimaye gharama kama hiyo itakuwa ndogo ikilinganishwa na gharama ya harakati za kukabiliana na changamoto za kuongezeka kwa hali ya uchafuzi wa hewa kutokana na usafiri wa ndege nyingi unaotumia kawi ya mafuta.
No comments:
Post a Comment