HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 16
ILIPOISHIA
Dokta Kweka akampa mkono
Simon kabla ya kunyanyuka.
“Nadhani tumemaliza, nione
matokeo baada ya siku tatu”
“Utayaona”
Simon naye akanyanyuka.
Siku iliyofuatia Simon
aliingia baa ya ABC ya Kimara saa kumi na moja jioni, akanywa bia hadi saa moja
usiku ambako aliondoka kuelekea Kinondoni. Alisimamisha gari mbele ya nyumba ya
Maria akatulia kwenye siti kama ambaye alikuwa akimsubiri mtu.
Baada ya kupita dakika tano
hivi alifungua mlango akashuka alikwenda kwenye mlango wa nyumba ya Maria
akaujaribu na kuona haukuwa umefungwa kwa ndani, Akaufungua na kuingia ndani.
Alitupa macho sebuleni, hapakuwa na mtu.
Maria alikuwa chumbani akivaa
baada ya kuoga. Simon aligonga mlango wa chumba cha Maria. Maria alifungua
mlango. Alipomuona Simon alishituka akaufunga. Alichukua simu akamtumia ujumbe
James.
“James njoo haraka, yule mtu
amekuja!”
Alipotuma ujumbe huo
alifungua mlango. Hakutambua dhamiri ya mtu huyo ilikuwa nini.
“Unasemaje?” akamuuliza bila
kutoka sebulani.
Ndipo Simon alipojipenyeza
mle chumbani kwa nguvu.
SASA ENDELEA
“Unataka nini?” Maria
alimuuliza huku akimpigia simu James.
“Nataka roho yako. Nilikuwa
nakutafuta sana na nimethibitisha kuwa ni wewe ninayekutaka”
Simon akatoa bastola
aliyokuwa ameificha ndani ya koti. James alikuwa ameshapokea simu ya Maria.
Lakini Maria hakuweza kumueleza lolote kwani Simon alimnyang’anya ile simu
kisha akampiga risasi ya kifua, mahali ambapo Simon alikuwa na hakika kuwa
Maria asingeweza kupona.
Akatoka. Wakati anatoka James
alikuwa anawasili na gari akamuona.
James alishuka na kumfuata.
Simon akawahi kuliondoa gari na kuondoka kwa kasi. James akakimbilia kwenye
mlango wa nyumba ya Maria ambao aliukuta uko wazi. Akaingia ndani.
Kwenye sebule hakukuwa na
mtu. James akasimama na kuita.
“Maria!
Hakukuwa na jibu, nyumba
ilikuwa kimya. James alikwenda kwenye mlango wa chumba cha Maria akausukuma na
kuingia ndani.
Alichokutana nacho kilimfanya
atoe macho na kuacha mdomo wazi. Maria alikuwa amelala chini, damu nyembamba
ilikuwa ikimtoka kifuani na kuchirizika hadi sakafuni. James alichutama na
kumuinua upande wa kichwani.
Maria alikuwa akipumua kwa
taabu.
“Maria umepatwa na nini?”
James akamuuliza kwa sauti iliyotaharuki.
Maria alijitahidi kuinua
mdomo akatamka kwa taabu.
“Pascal…Pascal…amenipiga
risasi…ameniambia alikuwa akinitafuta sana na amethibitisha kuwa ni mimi…”
“Amekupiga risasi kwa kosa
gani lakini…?”
Nguvu zilikuwa zimemuishia
Maria. Hakuweza kutamka tena. Akaguna na kufumba macho.
“Maria…Maria…!” James
akamuita huku machozi yakimtoka.
Maria alikuwa kimya.
“Maria!” James alimuita kwa
sauti ya juu huku akimtikisa.
Maria alikuwa kama hakuwepo
tena. Uliokuwepo pale ulikuwa ni mwili mtupu usio na uhai….
************
Simon alilikimbiza gari
kutoka nyumbani kwa Maria hadi kwenye mkahawa wa Afrique ambako Dokta kweka
kila saa mbili usiku hufika kupata chakula.
Alilisimmisha gari mbele ya
jengo hilo lililokuwa na mkahawa, akapanda ghorofa ya kwanza ulikokuwa mkahawa
huo. Kwa vile Dokta Kweka mwenyewe alimthibitishia kuwa atakuwa hapo, alimkuta
amemaliza kula chakula. Alikuwa akinywa juisi.
Simon alikaa kwenye kiti.
Dokta Kweka aliinua macho
yake akamtazama Simon na kumuuliza “Je?”
“Tayari” Simon akamjibu.
“Tayari nini?”
“Nimekamilisha kazi”
“Unaniambia ukweli Simon?”
“Kesho utapata habari yote
kwenye vyombo vya habari”
“Umemuuaje”
“Nimempiga risasi”
“Akiwa wapi?”
“Nyumbani kwake”
“Umehakikisha kuwa amekufa
sawa sawa?”
“Nimempiga risasi ya kifua,
hawezi kupona”
“Vizuri. Tukutane hapa hapa
kesho saa tatu asubuhi tumalizane. Na nitakuwa nimeshathibitisha ukweli wako.
Sawa?”
“Sawa”
Simon aliondoka na kwenda
nyumbani kwake Temeke. Aliliingiza gari lake ndani ya banda, akaenda kuketi
sebuleni.
“Unaonekana umechoka unatoka
wapi?” mke wake akamuuliza huku akiketi kando yake.
“Ni kweli mke wangu, natoka
Kibaha nilikuwa na mipango ya kazi” Simon alimdanganya mke wake.
“Nikuwekee chakula au
utakwenda kuoga kwanza?”
“Niwekee. Nahitaji kula na
kupumzika”
Vicky, mke wa Simon
alinyanyuka na kuelekea jikoni. Simon alikuwa akimtazama kwa nyuma wakati
anaondoka.
Alijivunia sana kufanikiwa
kumuoa msichana huyo ambaye alimsumbua kwa muda mrefu. Ingawa ndoa yao ilikuwa
na miezi michache tu, alishagundua kuwa msichana huyo aliyemtoa shamba alikuwa
ni mmoja wa wasichana wachache duniani wenye vipaji vya kuzaliwa katika mapenzi
na kumuenzi mume.
Mwenyewe alikiri kimoyomoyo
kuwa hakuwahi kupata kusuhubiana na msichana mrembo na mwelevu kama alivyokuwa
Vicky.
Siku zote Simon alikuwa akijisifu kumuoa Vicky
kwa kujiambia kuwa chaguo lake lilikuwa la maana. Alijiambia Vick ndiye mke wa
maisha yake na kama atamuacha Vicky asingepata tena msichana wa aina hiyo.
Baaada ya dakika tano Vicky
alirudi na kumwambia.
“Karibu mezani mume wangu”
“Asante mke wangu”
Simon alinyanyuka na kwenda
mezani. Alikaa kwenye kiti na kujisogezea sahani. Vicky alikuwa amesimama kando
ya meza akamtengea wali na vitakataka vingine kisha akamnawisha mikono.
“Karibu” Vicky akamwambia
huku akiketi.
“Wewe umeshakula?”
“Mimi tayari”
Vicky alimzungumzisha Simon
hadi alipomaliza kula akamnawisha mikono.
Saa tatu asubuhi ya siku
iliyofuata, Simon alifika katika mkahawa wa Afrique. Alimkuta Dokta Kweka akinywa
chai.
“Karibu” alimwambia.
Simon aliketi. Mhudumu
alipomfuata, Dokta Kweka alimwambia.
“Msikilize”
“Naweza kukuhudumia” Mhudumu
alimwambia Simon.
“Nipatie supu ya ng’ombe na
chapatti mbili”
Mhudumu aliondoka. Simon
akamtazama Kweka.
“Ndiyo Dokta, umepata habari
gani?”
Dokta Kweka akatabasamu.
“Umefanya kazi nzuri,
nimeshapata taarifa zote. Asante sana”
Simon akacheka.
“Jana nilipokwambia ulidhani
ni mzaha”
“Nilijua haikuwa mzaha,
nitakupatia pesa yako iliyobaki”
Supu ilipoletwa Simon alianza
kula huku akiendelea kuzungumza na Kweka. Walipomaliza kula Dokta Kweka
alifungua mkoba wake akampa Simon shilingi milioni mbili na nusu.
Simon alizitia mifukoni kisha
akamuaga Kweka na kunyanyuka.
“Subiri” Kweka alimwambia.
Simon akainamia meza ili
kumsikiliza Kweka.
“Ndiyo”
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment