HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 14
ILIPOISHIA
Jaji aliinua tena uso wake
akamtazama Mwendesha Mashitaka ambaye uso wake ulikuwa umepatwa na fadhaa.
Akaendelea kusoma muhutasari huo.
“Katika kesi ya mauaji kama
hii ambayo hukumu yake inaweza kuwa kifo ni lazima kuwepo ushahidi mzito na
usio na shaka. Kwa hiyo narudia kusema kuwa mshitakiwa hana kosa la kujibu na
namuachia huru”
Alipofika hapo alimtazama
mshitakiwa na kumwambia.
“Uko huru, nenda zako”
Simon Puto alikuwa amepatwa
na kiwewe cha kuachiwa. Alikuwa amemkodolea macho jaji kabla ya kuzinduka na
kushuka kizimbani haraka. Alipongezana na wakili wake ambaye alikuwa akimsubiri
mbele ya kizimba mara tu jaji alipomwambia, nimekuachia huru”
Mwendesha Mashitaka na
Inspekta Amour walikuwa wakiwatazama huku wakitikisa vichwa kwa uchungu.
SASA ENDELEA
Baada ya kupongezana na
wakili wake, Simon alitoka nje ya mahakama na kukutana na James aliyekuwa
akimsubiri mbele ya lango la mahakama.
James alimpa mkono na
kumpongeza kutokana na kuachiwa huru. Akampigapiga kwenye bega na kumwambia.
“Kupotea njia ndiyo kujua
njia, usijali”
“Asante sana” Simon alimjibu
uso wake ukiwa umejaa aibu.
“Okey gari ile pale,
twendezetu”
James alimuonesha gari lake
alilokuwa ameliegesha mbele ya viwanja vya mahakama.
James na Simon walifuatana
kuelekea kwenye gari hilo. Wakajipakia. James akaliwasha na kuondoka na Simon.
Miaka miwili iliyopita mtu
mmoja ambaye aliwahi kufanya kazi wizara ya afya akiwa na taaluma ya udaktari
aliwahi kusuhubiana na Maria kabla ya kifo chake.
Dokta Kweka alifahamiana na
Maria kwa sababu ya kufika mahakamani mara kwa mara akiwa na shughuli zake
binafsi zilizohitaji vibali vya mahakama.
Wakati huo Maria akiwa karani
wa mahakama ndiye aliyekuwa akimhudumia Dokta Kweka, kupokea nyaraka zake na
kuzifikisha kwa hakimu na kisha kuzichukua tena kwa hakimu na kumpa Dokta
Kweka.
Alikuwa akimrahisishia sana
kazi. Badala ya Kweka kusota kwenye mabenchi ya mahakama kumsubiri hakimu au
kuelekezwa kwenda huku na huko, alikuwa akizikabidhi kazi zake kwa Maria ambaye
huzishughulikia na kisha huja kuzichukua tena kwa Maria.
Maria alikuwa akimtumikia
Kweka kwa sababu Kweka alikuwa akimpa bahashishi nono. Kuna siku Kweka
alikwenda mahakamani hapo asubuhi akampa nyaraka zake Maria. Maria akamwambia
azipitie mchana.
Saa sita mchana Kweka alifika
mahakamani. Maria alikuwa ameshazishughulikia. Akampa.
“Naomba tuonane saa saba kwa
ajili ya chakula cha mchana” Kweka akamwambia Maria.
“Unataka kunipa ofa?” Maria
akamuuliza.
“Au hupendi?”
“Kwanini…tukutane hoteli
gani?’
“Nitakuwa pale Afrique”
“Nitahitaji usafifiri”
“Usijali”
Dokta Kweka alitia mkono
kwenye mfuko wa ndani wa koti lake akatoa noti mbili za shilingi elfu kumi kumi
akampa.
“Usafiri wako ndio huo”
“Asante”
“Usikose”
“Sitakosa”
Kweka akaondoka.
Saa saba mchana Maria akafika
Afrique. Ulikuwa mkahawa uliokuwa juu ya ghorofa. Watu waliokuwa wakiingia
katika mkahawa huo walikuwa watu wanaojiweza kwani bei yake ya vyakula ilikuwa
kubwa.
Maria alimkuta Kweka
akimsubiri. Alipomuona alimfuata kwenye meza aliyokuwa ameketi na yeye akaketi.
Mhudumu alipowaendea, Kweka alimwambia Maria.
“Agiza chakula unachotaka”
Kweka mwenyewe aliagiza ugali
na kuku. Maria akaagiza chips kuku. Wote wawili walitaka waletewe pia juisi ya
nanasi.
Mhudumu alipoondoka. Kweka
aliendelea kusoma gazti alilokuwa amelishika mkononi.
Vyakula walivyoagiza
vilipoletwa, Kweka alilikunaja gazeti wakaanza kula.
“Kuna kitu nilikuwa nataka
kukwambia Maria, umekuwa ukinisaidia sana.
Nashukuru kwa hilo.
Nilikuwa nikijiuliza ni kwanini tusisuhubiane mimi na wewe?” Kweka alimwambia
Maria.
Maria alinyamaza kimya.
“Nadhani nitatafuta muda
mwingine mzuri zaidi ili tuliongelee hilo
kwa kirefu au unasemaje?”
Maria akabetua mabega.
“Ni sawa tu”
“Unadhani lini utakuwa na
nafasi nzuri, siku ambayo si ya kazi?”
“Jumapili mchana nikitoka
kanisani”
“Nitakupata wapi?”
“Hapa hapa”
“Naomba unipatie namba yako
ya simu”
Maria hakuwa na uchoyo na
namba yake, akampa. Kweka naye akampa namba yake. Baada ya kumaliza chakula
Kweka alimpa Maria shilingi laki moja.
“Zitakusaidia kununulia vocha
ya simu”
“Asante
sana,
nashukuru”
Wakaagana. Siku ya jumapili
Maria alitimiza ahadi. Alipotoka kanisani alipanda teksi hadi mkahawa wa
Afrique. Alipofika akakutana na Kweka.
Siku ile ndio Kweka alimtolea
undani wake. Alimwambia wazi kuwa alikuwa akimuhitaji katika maisha yake. Kule
kutoa kauli ya kukubali tu, Kweka alimpeleka ‘shopping’ siku ile ile. Alimfanyia
shoping ya shilingi laki tano.
Kutoka hapo Kweka na Maria
wakawa wapenzi. Siku zote walikuwa wakikutana kwenye mahoteli tu. Maria aliwahi
kumfikisha nyumbani kwake mara kadhaa lakini Kweka hakumuonesha Maria alikuwa
anaishi wapi zaidi ya kumwambia kuwa alikuwa akiishi Masaki.
Mapenzi yalipowakolea
walifunga uchumba. Uchumba huo ulidumu kwa mwezi mmoja tu kabla ya Maria kupata
balaa la kukamatwa na kuwekwa ndani.
Kweka alikuwa ameshitakiwa
kwa kugushi nyaraka za wizara kwa ajili ya shughuli zake binafsi. Alipotolewa
kwa dhamana alimtuma Maria kulitafuta faili la kesi yake hapo mahakamani na
kuchomoa nyaraka muhimu za ushahidi ili kuharibu kesi.
Maria kwa sababu ya kutaka
mpenzi wake asifungwe alifanya hivyo. Uchunguzi ulipofanyika ilibainika kuwa
baadhi ya nyaraka za ushahidi hazikuwemo kwenye faili la Kweka. Shuku ikaenda
kwa Maria. Maria akashukiwa kuzichomoa nyaraka hizo.
Polisi walimkamata
akafunguliwa mashitaka. Wakati yeye akiendelea na kesi, Kweka alikuja kuachiwa
kutokana na kukosekana kwa ushahidi. Uamuzi huo ulikuja baada ya kesi yake
kuchukua muda mrefu.
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment