HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 14
ILIPOISHIA
“Ni kitu gani ambacho wewe
hukubaliani nacho?’ Mwendesha mashitaka aliendelea kumuuliza.
“Sikubaliani
kwamba mshitakiwa aliye mbele yangu ni muuaji”
“Ni
nani?”
“Simtambui”
“Una maana kwamba yule
uliyekwenda kumtambua kituo cha polisi mara tu alipokamatwa si yeye?”
“Si
yeye”
“Utakuwa
umemsahau?’
“Nina
kumbukumbu timamu, si yeye!”
“Lakini unakubaliana kwamba
aliyeuawa alikuwa mchumba wako?”
“Ndiyo
alikuwa mchumba wangu”
“Sasa nikikwambia kwamba
mshitakiwa aliye hapo ndiye yule uliyemthibitisha wewe mwenyewe mbele ya polisi
kuwa alimuua mchumba wako, bado utakataa?’
James
akatikisa kichwa.
“Nitakataa. Na ninasema
kwamba mshitakiwa huyu simtambui, ni bora aachiwe tu”
“Unasema
kweli James?”
“Kweli
tupu. Hapa niliapishwa niseme ukweli”
“Sawa”
Mwendesha
mashitaka akamtazama jaji.
“Mheshimiwa
shahidi wangu amenikana” alimwambia.
SASA ENDELEA
“Amesema kwamba mshitakiwa
aliyeko kwenye kizimba, siye aliyemuua mchumba wake” Jaji alimwambia na
kuongeza “Nyinyi mnatakiwa mumlete muuaji halisi”
“Nimekuelewa mheshimiwa”
Mwendesha Mashitaka alimjibu na kuketi kinyonge.
“Wakili wa mshitakiwa una
maswali yoyote ya kumuuliza shahidi?”
Jaji akamuuliza wakili aliyewekwa na serikali kumtetea mshitakiwa.
Kwa mujibu wa sheria, mtu
anayeshitakiwa kwa kosa la mauaji huwekewa wakili na serikali kama hana uwezo
wa kuweka wakili.
“Ninayo
maswali” Wakili huyo alijibu huku akiinuka.
“Uliza
maswali yako”
Wakili
alisimama na kumtazama James.
“Aliyeuawa
alikuwa ni nani wako?” alimuuliza.
“Alikuwa
mchumba wangu”
“Wewe
ulishuhudia wakati marehemu anauawa?”
James
akaeleza jinsi tukio zima lilivyotokea.
“Kwa
hiyo ulimuona muuaji?’
“Ndiyo
nilimuona”
“Wakati
mshitakiwa anakamatwa uliitwa kwenda kumtambua?”
“Ndiyo
niliitwa”
“Ulikwenda
kumtambua?”
“Ndiyo
nilikwenda”
“Alikuwa
ndiye aliyemuua mchumba wako?”
“Alikuwa
ndiye”
“Sasa
hebu mtazame mshitakiwa aliyeko kizimbani”
James
akamgeuzia macho mshitakiwa huyo.
“Ndiyo
ninamtazama” akasema.
“Ndiye
yeye aliyemuua mchumba wako?”
James
akatikisa kichwa.
“Hapana,
siye”
“Je
ndiye yeye uliyekwenda kumtambua kituo cha polisi?”
“Siye”
“Nini
maoni yako, unadhani polisi wameleta mtu mwingine?”
“Naweza
kusema hivyo”
“Kwa
maoni yako mshitakiwa anastahili kuendelea kushitakiwa?’
“Hastahili,
ni bora aachiwe tu”
“Sawa.
Asante sana” Wakili alisema na kumtazama jaji.
“Mheshimiwa
nimemaliza maswali yangu”
Aliposema hivyo alivuta kiti
na kukaa huku akiona kazi yake imekuwa ndogo kuliko alivyotarajia.
Mwendesha mashitaka alikuwa
amefadhaika. Hakujua jaji angekuwa na uamuzi gani kuhusu shahidi wao kuwakana
na kuwa shahidi wa upande wa utetezi wakati ushahidi wake ndio uliokuwa
ukitegemewa kumtia hatiani mshitakiwa.
Jaji baada ya kumaliza
kuandika alimwambia James ashuke kizimbani, akamuuliza Mwendesha Mashitaka.
“Mna
mashahidi wengine?”
Mwendesha
Mashitaka akasimama.
“Tuna ushahidi wa vielelezo
vya alama za vidole na picha zilizokutwa katika simu ya mshitakiwa zinazomuhusu
marehemu”
“Shahidi
wenu yuko tayari?’
“Yuko
tayari”
“Aitwe”
Shahidi
aliyeitwa alikuwa mpelelezaji wa ile kesi, Inspekta Amour.
Amour alianza kuukosoa
ushahidi wa James kwamba haukuwa na ukweli kwani mshitakiwa aliyekuwa
kizimabani alimtambua na kumthibitisha yeye kabla ya kufunguliwa mashitaka.
Wakili wa utetezi akasimama
na kupinga maelezo ya Inspekta Amour.
“Inspekta wewe si mwendesha
mashitaka, umekuja hapa kutoa ushahidi wa vielelezo. Toa ushahidi uliotakiwa
kuutoa na si vinginevyo” alimwambia.
“Nilikuwa naeleza kuhusu
shahidi aliyepita. Ushahidi wake haukuwa wa kweli” Amour alijitetea.
“Unaeleza kama nani?”
Wakili alimtolea macho.
“Kama
shahidi wa upande wa serikali”
“Hapa tuko kisheria, hatuko
kinyemela. Wewe hukupaswa kutoa maelezo hayo bali ni muendesha mashitaka wako”
“Sawa. Nimekuelewa”
Wakili akakaa.
Amour akaielezea mahakama
kwamba alama za vidole za mshitakiwa zilikutwa kwenye kitasa cha mlango wa
nyumba ya marehemu mara tu baada ya tukio hilo
la mauaji. Kadhalika zilikutwa kwenye simu ya marehemu ambayo aliishika kabla
ya kufanya mauaji.
Aliendelea kueleza kuwa
mshitakiwa pia alikuwa amejirushia picha za marehemu zinazomuonesha akiwa na
mchumba wake bila ridhaa ya marehemu. Akaeleza kuwa picha hizo zilizokutwa
kwenye simu ya mshitakiwa zilitoka kwenye simu ya marehemu.
“Wewe kama mpelelezi wa hii
kesi, kukuta picha za marehemu kwenye simu ya mshitakiwa na kupatikana kwa
alama za vidole vya mshitakiwa kwenye simu ya marehemu na kwenye kitasa cha
mlango wa nyumba yake kulikupa picha gani?” Mwendesha mashitaka alimuuliza
Inspekta Amour.
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment