Thursday, April 14, 2016

HADITHI , MWANAMKE ALIENICHUNUKE SEHEMU YA 13

HADITHI hii imeletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, Candle ni mabingwa wa kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu, Candle ni kituo maarufu cha kuzalisha vipaji katika fani mbalimbali ikiwemo ya QT, Candle wapo na hosteli na wanafunzi hupelekwa shuleni kw akutumia gari la shule, Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
 
MWANAMKE ALIYENICHUNUKA 13
 
ILIPOISHIA
 
“Tunapokuwa kwenye mwanga, mboni zetu za macho zinakuwa
 Ndogo lakini tukiwa kwenye kiza mboni zinakuwa kubwa na kutuwezesha kuona”
 
“Kwa hiyo mimi sitaweza kuona”
 
“Tutatokea kwenye mwanga muda si mrefu”
 
“Kiza hiki kinatisha sana bora mngeweka taa”
 
“Usijali, utazoea tu”
 
Mara nikasikia Banuna akisemeshana na mwenzake mwenye sauti ya kiume ambaye sikuweza kumuona kutokana na kiza. Lugha waliyozungumza haikuwa ya Kiswahili.
 
Hapo hapo nikaona mlango unafunguliwa. Nikaona mwanga mzuri mweupe umetokea.
 
“Tuingie” Banuna akaniambia.
 
SASA ENDELEA
 
Tukaingia mle ndani. Kwa vile sasa kulikuwa na mwanga niliondoa mkono wangu kwenye bega la Banuna. Licha ya kuuona ule mwanga sikuweza kujua ni kitu gani kilichokuwa kinatoa mwanaga huo.
 
Tulikuwa tumetokea katika ukumbi mpana uliokuwa umetandikwa mazulia mazuri na wenye hewa safi lakini ulikuwa mtupu usio na kitu chochote.
 
Ulikuwa na milango mitatu iliyoingia ndani ambayo ilikuwa imezibwa kwa mapazia mazito ya hariri. Banuna alinipeleka katika mlango uliokuwa katikati, tukaingia.
 
Tulitokea katika ukumbi mwingine mdogo uliokuwa na ngazi za kupanda. Tukapanda ngazi hadi juu kidogo, tukaingia kwenye mlango mwingine ambao pia ulizibwa kwa pazia. Tulipoingia katika mlango huo tulitokea katika ukumbi mwingine uliokuwa kama sebule iliyokuwa ina meremeta.
 
Ulikuwa na fanicha zilizotengezwa kwa madini. Fanicha hizo zilikuwa zikitoa rangi mbalimbali za kupendeza. Muundo wa fanicha hizo sikuwahi kuuona popote. Nikabaki ninakikodolea macho kila kitu ninachokiona kwani kilikuwa  cha ajabu kwangu. Mbali na vitu hivyo, harufu iliyokuwa inasikika humo ndani ilikuwa ni ya marashi na udi wa Ajemi.
 
“Kaa hapo chini” Banuna akaniambia.
 
“Nikae chini wapi?” nikamuuliza.
 
“Kaa popote tu, sisi huku tunakaa chini”
 
Nikakaa chini huku nikiendelea kuikodolea macho ile sebule. Kila kitu nilichokiona kilikuwa kigeni kwangu.
 
“Sasa nisubiri nikamuite mama yangu, aje muonane” Banuna akaniambia na kupotea kwenye pazia lililokuwa mbele yake.
 
Baada ya muda kidogo niliona pazia likipenuliwa akatokea tena Banuna na mwanamke mmoja mzee. Alikuwa mfupi aliyevaa shuka nyeupe. Alikuwa na nywele ndefu nyeupe zizilizomteremka kwenye mabega. Hata hivyo alikuwa amefunga kilemba cheupe kichwani. Licha ya kumtazama kwa makini bibi huyo, sikuweza kutambua alikuwa muarabu au muhindi.
 
Bibi huyo wa kijini alikuja hadi pale nilipokuwa nimeketi. Nikayaona macho yake ya kijivu, yalikuwa na mboni zilizosimama kama mboni za paka. Hata Banuna anapokasirika mboni zake hubadilika na kuwa hivyo..
 
Jambo la ajabu ni kuwa sikutishika kukaa na viumbe hao waliokuwa na maumbile tofauti na mimi.
 
Yule bibi aliketi karibu yangu akakunja miguu yake kisha akaniambia.
 
“Asalaam alaykum”
 
“Alaykumu salaam” nikamjibu.
 
Banuna naye akaketi palepale.
 
“Alfred, huyu ni mama yangu. Anaitwa Ummi Mariam” Banuna akaniambia.
 
“Nimefurahi kumuona” nikamwambia Banuna.
 
Banuna akamtazama mama yake na kumwambia.
 
“Maa, huyu ndiye yule kijana niliyekuwa ninakwambia. Leo nimekuja naye umuone”
 
Yule bibi akanitazama na kuniuliza.
 
“Mmekubaliana nini na Banuna?”
 
Swali hilo lilinishitua kidogo. Hata hivyo nilibetua mabega yangu na kumjibu.
 
“Hatukukubaliana chochote!”
 
“Alipokwambia mje huku alikwambia manakuja kufanya nini?”
 
“Hakuniambia kitu”
 
“Amekuleta tu!”
 
“Aliniambia twende kwetu”
 
Yule mama akamtazama Banuna.
 
“Mbona mwenyewe hajui amekuja kufanya nini huku?”
 
“Anajua” Banuna akasema kisha akabadili lugha na kusema kwa kiarabu, lakini sikuelewa alisema nini.
 
Mama yake akanitazama mimi tena.
 
“Eti mmekubaliana kuwa mnakuja huku kuoana?” akaniuliza.
 
“Hatukukubaliana kuwa tunakuja kuoana” nikamjibu.
 
“Na wala hakuwahi kukueleza jambo hilo?”
 
“Aliwahi kunieleza”
 
“Je ulikubali kwa hiyari yako?”
 
“Hapana, sikukubali”
 
“Alikuwa anakutisha?”
 
Hapo nikanyamaza. Sikutaka kusema ukweli kuwa alikuwa ananitishia maisha.
 
Yule mama alitambua mawazo yangu, akaniambia.
 
“Sema usifiche”
 
“Ndiyo alikuwa ananitisha” nikamwambia.
 
Banuna akanitazama kwa uso wa tadhaa.
 
“Alfred sema ukweli, nimekutisha mimi? Si tumekubaliana tuoane, uliniambia kuwa umenipenda?” Banuna akaniambia lakini sauti yake haikuwa na nguvu kwa vile maneno aliyosema yalikuwa ya uongo.
 
ITAENDELEA KESHO hapahapa Tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment