HADITHI na Faki A Faki 0713 340572
MWANAMKE ALIYENICHUNUKA 7
Nikasubiri. Baada ya kupita kama dakika tatu hivi, Juma alifungua mlango akatoka.
Alipoona nimejifunga shuka alishituka.
“Vipi tena Alfred?”
akaniuliza.
“Tuingie ndani nikueleze”
nikamwambia.
“Karibu”
Tukaingia ndani. Alinikaribisha
chumbani kwake. Yeye aliketi kitandani, mimi nikakaa kwenye kiti.
Nikamueleza mkasa wa yule
msichana wa kijini, tangu nilivyoanza kukutana naye hadi alivyoniingilia
chumbani usiku ule.
Juma nilipomueleza
alishituka.
“Unasema kweli?” akaniuliza
huku amenikazia macho.
Nakueleza ukweli, huyo
msichana nimemuacha chumbani mwangu na kukimbilia hapa kwako. Hata nguo
sikuwahi kuvaa”
“Amekwambia mwenyewe kwamba
yeye ni jini?” Juma akaniuliza.
“Ndiyo ameniambia. Mlango
niliufunga kwa ndani lakini ulifunguka wenyewe, akaingia”
“Dah! Sasa utafanyaje rafiki
yangu?”
“Jana nilikwenda kwa
Mchungaji akaniambia atanifanyia maombi hii leo”
“Unadhani atakapokufanyia
maombi, huyo jini hatakufuata tena?”
“Hatanifuata”
“Basi ni vizuri ufanyiwe hayo
maombi haraka kwani inaonekana huyo msichana atakusumbua. Anataka uwe mume
wake. Utaishije naye wakati yeye ni jini?”
“Hapo sasa!”
“Pole sana Alfred. Ni matatizo makubwa
yaliyokukuta! Sasa utalala wapi?”
“Nakuomba unisindikize
nyumbani nikavae nguo na nifunge milango. Mlango wa chumbani mwangu na wa nje
ipo wazi”
‘Umesema yule msichana yuko
chumbani mwako?”
“Atakuwa ameshaondoka baada
ya mimi kukimbia”
“Ngoja nivae twende” Juma
akaniambia.
Baada ya dakika kumi hivi,
mimi na Juma tukawa tunakwenda katika nyumba niliyokuwa ninaishi. Kwa vile
nilikuwa na mwenzangu. Hofu ilinipungua.
Tulipofika nyumbani
nilisukuma malango tukaingia ndani. Tulikwenda kwenye mlango wa chumba changu
nikamwambia Juma aufungue yeye.
Juma akaufungua mlango na
kuchungulia ndani.
“Yumo?” nikamuuliza kwa sauti
ya kunonong’ona.
“Sioni mtu” Juma alinijibu
huku akitumbukiza mguu wake ndani. Aliangalia pande zote za chumba kabla ya
kuingia kabisa.
“Ingia, hayumo”akaniambia.
Nikaingia.
Chumba changu bado kilikuwa
kina harufu ya manukato yake. Juma aliyasikia.
“Mbona kunanukia hivi?
Unatumia manukato gani?”
“Ni yule msichana
aliyeingia….”
“Ananukia manukato namna
hii!....ni jini kweli!”
“Tena hii harufu imepungua.
Naona ameondoka muda mrefu”
“Viumbe hawa wanapenda sana manukato!”
Wakati tunazungumza na Juma
nilikuwa nikivaa suruali yangu na shati. Juma aliketi kwenye kiti.
“Sasa unavaa uende wapi?”
“Navaa turudi kwako”
“Kwanini tujisumbue? Huyo
msichana si ameshaondoka?”
“Hata kama!. Ile imani ya
kubaki humu sina kabisa”
“Tutabaki sote mpaka
kutakapokucha. Kule nimeshawambia wafunge mlango. Siwezi kwenda kuwasumbua
tena.”
“Basi tutabaki hapa hapa sote.
Tukiwa wawili si neno”
Tukakaa mle chumbani na Juma
mpaka asubuhi. Juma aliondoka saa kumi na mbili asubuhi akaniacha ninakwenda
kuoga. Niliporudi nilivaa nikawa nasubiri muda wa kwenda kanisani. Siku ile
sikukumbuka kunywa chai kabisa
Muda wa kwenda kanisani
ulipowadia nilitoka nikaenda kanisani. Baada ya ibada waumini wenye matatizo
mbalimbali waliitwa ili waombewe. Na mimi nikawemo.
Wenye mapepo yalitolewa na
wenye magonjwa mengine walipata nafuu. Mimi niliombewa mpaka machozi yakanitoka.
Niliamini kabisa yule jini ametokomezwa mbali au ameshateketezwa kwa moto.
Baada ya kipindi hicho cha
maombi kilichochukua karibu saa mbili, tulitoka kanisani nikiwa na furaha.
Furaha yangu ilinifanya nisalimiane na kila ninayemuona ingawa haikuwa kawaida
yangu.
Nilipotoka kwenye lango la
kanisa, nilimuona Juma amesimama kando ya lango hilo. Nikamfuata.
“Mbona uko hapa?”
nikamuuliza.
“Nimekufuata wewe.
Umeshafanyiwa maombi?”
“Tayari. Nashukuru nimeombewa
sana”
“Sasa hivi hofu yako
imekwisha kabisa?”
“Imekwisha. Leo najiona kama nimezaliwa upya”
“Kwanini Alfred?”
“Nimeepushwa na yule shetani
aliyekuwa ananisumbua na nimeambiwa na Mchungaji nisiache ibada. Kwa vile
nimeshampokea Yesu sitaacha kabisa”
“Ni vizuri kama
matatizo yale yamekwisha. Kwa sasa utaweza kulala peke yako?”
“Bila shaka yoyote. Yule jini
hawezi kunifuata tena
“Na mimi nimefurahi Alfred.
Twenzetu”
Tukaondoka na Juma.
“Juma umeshakunywa chai?”
nikamuuliza wakati tukienda. Sasa nilikuwa nasikia njaa.
“Mimi nimeshakunywa, sijui
wewe?”
“Mimi bado. Asubuhi nilikuwa
na kihoro, sikukumbuka kunywa chai”
“Sasa utakwenda kunywa wapi?”
“Mimi nakunywa chai kwa kina
mama lishe”
“Tena kibanda cha mama lishe
kile pale”
Juma alinionesha kibanda cha
mama lishe kilichokuwa kwenye uchochoro. Tukaenda.
Nilikunywa chai. Baada ya
hapo Juma alinisindikiza hadi nyumbani. Tukaagana.
ITAENDELEA KESHO
| |||||||||||||||||
Thursday, April 7, 2016
HADITHI SEHEMU YA ( 7 )
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment