HADITHI
MWANAMKE ALIYENICHUNUKA 2
ILIPOISHIA
Msichana hakunijibu mpaka
nilipomuuliza mara ya pili.
“Natoka hukoo!” akaniambia.
“Wapi?”
“Kazini”
“Ni wapi?”
Akanitajia klabu moja ya
usiku ilikokuwa karibu na Posta.
“Na unakwenda wapi?”
“Ninaenda nyumbani”
“Unaishi wapi?”
“Hukoo”
Akanionesha kwa kidole kule
alikokuwa anakwenda.
“Kwani kule kunaishi watu?”
nikamuuliza.
Akanikubalia kwa kichwa.
SASA ENDELEA
Pakapita kimya kifupi huku
mvua ikiendelea kunyesha. Nikamsikia akisema.
“Hii mvua haiachi, nakwenda
nayo hivyo hivyo”
“Subiri kidogo, inaweza
kuacha”
Msichana akatikisa kichwa.
“Hii haitaacha, sitaki
alfajiri inikute hapa”
“Jinsi unavyotetemeka
ukiendelea kunyeshewa unaweza kupata homa”
“Si kitu, acha niende”
“Ngoja basi nikupe koti langu
uendenalo, utanirudishia kesho”
Nikavua koti langu na
kumvalisha yeye.
“Asante kaka, nitakurudishia kesho”
akaniambia kisha akaingia kwenye mvua na kwenda zake.
Nilimsindikiza kwa macho hadi
alipopotea kwenye macho yangu.
Nikabaki kujiuliza kama kule alikokuwa anakwenda kulikuwa na nyumba za watu.
Kwa jinsi nilivyokuwa nafahamu mimi upande ule haukuwa na nyumba isipokuwa
maghala ya zamani yaliyokuwa hayatumiki tena na viwanda vidogo vidogo
vilivyokufa.
Msichana huyo alipoondoka
ndipo nilianza kujilaumu kwa kutomuuliza jina lake. Hata hivyo niliona hata
kama ningemuuliza asingenitajia jina lake
kwa vile ilikuwa ndio
kwanza tunakutana. Baadhi ya wanawake wa pwani huwa hawapendi kutaja majina yao kwa watu ambao
hawawafahamu vyema.
Siku iliyofuata ambayo
haikuwa na mvua, yule msichana alipita tena saa nane usiku. Nilikuwa nimemsubiri
kwa hamu ili nizungumze naye.
Alikuja mpaka pale kwenye
ghala nilipokuwa nimesimama akanisalimia.
“Asalaam alaykum”
“Waalayka salaam. Hujambo?”
nikamjibu.
“Sijambo. Habari ya tangu
jana?”
“Nzuri”
“Samahani kaka, nilisahau
kukuchukulia koti lako asubuhi lakini kesho nitakupitishia” akaniambia kwa
sauti ya kubembeleza.
Na kweli nilibembelezeka.
Hata sikujali kuwa koti hilo
lilikuwa muhimu kwangu.
“Usijali, utaniletea kesho”
“Asante kaka”
“Mimi naitwa Alfredy, wewe
unaitwa nani?” nikamuuliza ghafla.
Msichna aliguna kisha
akanitazama machoni mwangu.
“Nitakutajia jina langu
kesho, kwaheri”
Msichana huyo alikuwa
ameshageuka ili aende zake.
“Unakwenda zako?”
nikamuuliza.
“Ndiyo. Usiku mwema”
Msichana akawa anachanganya
mwendo kuelekea kule alikodai anaishi.
Udadisi ukanipata. Alipofika
mbali nikaamua kumfuata ili niweze kujua anakwenda wapi.
Nilimfuata kwa kumnyemelea
huku nikijificha ficha kwenye miti ili asinione au kugundua kuwa namfuata.
Nilisahau kuwa niliacha lindo
langu likiwa halina mlinzi. Tulikwenda mbali kidogo. Nilijiambia kama ni kukosa
uoga msichana huyo alikuwa namba moja. Huko mahali alikokuwa anakwenda kulikuwa
kimya na kulikuwa kunatisha.
Binafsi kama nisingekuwa na
bunduki nisingethubutu kufika katika eneo hilo
usiku huo lakini yule msichana alikuwa haogopi kabisa.
Baada ya mwendo wa nusu saa
hivi nilimuona akiingia katika jumba moja la zamani ambalo upande wake mmoja
ulibomoka na kuwa kama gofu.
Jumba hilo
kama sikosei lilijengwa enzi za wajerumani na
sikuweza kujua lilikuwa likitumika kwa shughuli gani.
Kulikuwa na msufi mrefu
uliokuwa umeota mbele ya jumba hilo
na kusababisha kivuli kipana.
Msichana huyo alipoingia ndani
ya jumba hilo nilishituka, nikajiuliza kama alikuwa akiishi mle ndani.
Udadisi wa kutaka kumchunguza
ukanipata. Nikatembea haraka haraka na kufika katika mlango wa jumba hilo ambao ulikuwa wazi,
nikaingia ndani.
Nilipoingia ndani nilisimama
kando ya mlango kwani kiza kilinifanya nisiweze kuona chochote. Nilitaka macho
yangu yazoee kiza ili niingie ndani zaidi. Sikujua yule msichana aliingiaje
wakati kulikuwa na kiza kiasi kile.
Macho yangu yalipozoea kiza
nilijikuta nimeingia katika chumba kipana kilichokuwa na vichuguu vya mawe
baada ya sakafu iliyokuwapo kuvunjika. Pia kulikuwa na mimea iliyoota mle
ndani.
Kitu cha kwanza
kilichonishitua ni kwamba nilikuta lile koti langu nililomuazima yule msichana
limetundikwa kwenye moja ya kuta za chumba hicho
Nilikuwa sitaki kutoa tochi
yangu ndogo lakini nililazimika kuitoa na kulimulika lile koti, nikahakikisha
kuwa ni langu.
Hapo nikajiuliza yule
msichana anaishi katika gofu lile?. Halikuelekea kuwa ni makazi ya binaadamu
kwani licha ya kuwa linatisha, mazingira ya gofu hilo
yalikuwa ni ya kuishi wadudu kama nyoka.
Dukuduku likanifanya
niharakishe kuingia ndani zaidi. Nilizima ile tochi ili mwanga usionekane.
Nikapita kwenye sehemu iliyokaa kama ukumbi
ambayo pia ilikuwa na mawe na mimea iliyoota.
Upande mmoja wa ukuta
palikuwa na tundu ambalo nilihisi zamani lilikuwa ni dirisha lililong’oka.
Tundu hilo
lilikuwa likiingiza mwanga wa mwezi ulionifanya nione uwazi mwingine mbele
yangu. Nikaenda mbele zaidi.
ITAENDELEA KESHO
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa Tangakumekuchablog
|
Friday, April 1, 2016
MWANAMKE ALIENICHUNUKU SEHEMU YA ( 2 )
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment