Wednesday, September 2, 2015

NSSF, YAJIKITA KWA WACHEZAJI

Tangakumekuchablog

Tanga, MFUKO wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Tanga, imeanzisha kampeni ya kutoa elimu ya Ustawi wa  jamii kwa wachezaji wa mpira wa miguu kujiunga na mfuko huo kunufaika na mafao ya muda mrefu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja wa Mfuko huo Mkoa wa Tanga, Frenk Maduga, alisema NSSF itatoa elimu kwa wachezaji na viongozi kwa timu za mipira zinazoshiriki ligi mbalimbali ikiwemo Coastal Uniona na African Sports za Tanga zinazoshiriki ligi kuu Tanzania Bara.

Alisema NSSF imeona ni vyema wachezaji wa mpira kupata elimu ya kujiunga na mfuko huo na kuweza kunufaika na huduma zinazopatikana ikiwemo ajali kazini pamoja na mafao ya muda mrefu.

“Kwa kutambua changamoto za wachezaji wanazokumbana nazo viwanjani sisi kama mfuko wa hifadhi ya jamii tumeona kuwapa elimu ya ustawi wa jamii ili kuweza kujiunga na kupata matibabu pindi wapatapo ajali” alisema Mduga na kuongeza

Alisema wachezaji hukumbana na changamoto nyingi viwanjani ikiwemo kuumia na kuvunjika hivyo kuona ni vyema kuwapa elimu ya ustawi wa jamii na kuweza kunufaika na huduma za NSSF pamoja na mafao ya muda mrefu.

Alisema kwa sasa wanakamilisha taratibu za usajili kwa wachezaji wa timu ya Coastal Union na African Sports na kusema kuwa mfumo huo utawajenga na kujiamini wakati wakiwa uwanjani kwa kujituma kwa moyo mmoja.

Akizungumza kupata huduma hiyo, katibu wa timu ya Kisosora United, Nyala Msei, aliushukuru mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kuliona jambo hilo kwani litawajengea uwezo wachezaji wa mpira uwanjani.

Alisema wachezaji wengi wamekuwa hawajitumi ipasavyo uwanjani kuogopa kuumia au kuvunjika na hivyo kujiunga kwao na mfuko wa NSSF wataweza kujituma na  kuipa heshima Mkoa wa Tanga kisoka.

“Tunaishukuru NSSF kwani imetambua na kuona umuhimu wa kutupa elimu ya ustawi wa jamii----kwa moyo huu tutashirikiana nao kwa maendeleo ya Tanga na Taifa kwa ujumla” alisema Msei

Aliitaka mifuko mengine kuiga NSSF kwani kutoa elimu ya ustawi wa jamii kutawawezesha vijana kuwajibika wakiwa uwanjani kwa kutambua mfuko unaweza kuwatibu matibabu bure.

                                               Mwisho

No comments:

Post a Comment