Monday, September 7, 2015

NUNDU AWATIA MOYO VIJANA AKIREJEA UBUNGE



Tangakumekuchablog
Tanga, MGOMBEA Ubunge jimbo la Tanga mjini kupitia (CCM), Omari Nundu, amesema akichaguliwa kuwa Mbunge ataongeza ajira kwa vijana na kuviwezesha vikundi vya akinamama wajasiriamali  mikopo na kuwatafutia soko la kuuzia bidhaa zao.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni wa kujinadi jana kijiji cha Ngome kata ya Chumbageni Tanga, Nundu alisema vikundi vingi vimekufa kutokana na kushindwa kupata mikopo na kuyafikia masoko.
Alisema jambo ambalo atalipa kipaumbele wakati wa Ubunge wake ni kuhakikisha fursa za vijana zinapatikana ikiwemo kupata mikopo katika taasisi za fedha kuendeleza kazi zao na kulifikia soko la pamoja la Afrika Mashariki (EAC).
“Ndugu zangu wa kijiji cha ngome ambapo kuna wazee wangu na wajomba pamoja na mashangazi----nipeni tena ridhaa nikamilishe yale ambayo niliyabakisha kiporo” alisema Nundu
Alisema akichaguliwa kuongoza jimbo hilo atahakikisha anaisaidia Serikali katika upatikanaji wa huduma za jamii ikiwemo kukarabati majengo ya shule na kusaidia kuongeza vyumba vya madarasa na madawati.
Alisema shule ambazo ziko na upungufu wa madawati atashirikiana na marafiki wa elimu kuhakikisha shule zote ambazo zinakabiliwa na kero mbalimbali zinatatuliwa na kupatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wake mgombea nafasi ya Udiwani kata ya Chumbageni, Saida Ghadafi (CCM), alisema akichaguliwa kuwa Diwani, atajenga soko maalumu la Wajasiriamali wa kazi za mikono.
Alisema wanawake wengi wameacha kujishughulisha na kazi za mikono kutokana na kukosa soko la uhakika la kuuzia bidhaa zao na kusababisha kuongezeka kwa umasikini majumbani.
“Nawaomba ndugu zangu munipe mimi kura nyingi za ndio pamoja na mgombea ubunge kupitia chama hiki hiki chama cha mapinduzi----tuko na mipango kemkemu ya kuhakikisha jimbo la Tanga linabadilika kimaendeleo” alisema Ghadafi
Alisema kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali na mashirika yasiyo ya Kiserikali pamoja na Mbunge wako na mipango mizuri ya kuenua maendeleo ya watu wa Tanga na hivyo kuwataka kuwachagua kwa kura nyingi.
                                                    Mwisho

No comments:

Post a Comment