Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772736
JamboLEO
Madereva wa kiume wa pikipiki maarufu
kama bodaboda na wengine wanaotumia usafiri huo kwa muda mrefu wapo
katika hatari ya kuwa wagumba.
Tafiti nyingine zilizofanywa
zinazonyesha kuwa huenda wakakabiliwa na uhaba wa mbegu za kiume na
hatimaye kushindwa kutoa mbegu za kiume zenye uwezo wa kutunga mimba.
Hali hiyo inatokana na sehemu za siri
zinazozalisha mbegu muda mwingi kuwa katika hali ya joto kitu ambacho
kitaalamu kimebainisha kuwa kinafanya mishipa ya damu kutofanya vyema na
kuchochea uzalishaji mbegu hizo.
Maelfu ya vijana nchini wamejiajiri
kupitia usafiri wa bodaboda huku wengi wakiwa katika umri mdogo wa kati
ya miaka 18 hadi 50, kutokana na tafiti hizo huenda Tanzania ikaathirika
zaidi kwa kuwa na vijana wengi wanaoweza kuwa wagumba.
Utafiti unaonyesha kuwa vijana wengi
wanaokaa katika kiti cha pikipiki hupambana na joto kutokana na ngozi
laini iliyopo katika korodani,mirija ya damu hushindwa kupitisha
virutubisho kutokana na msuguano mkali uliopo.
MWANANCHI
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
na watu wengine 24 juzi walijikuta wakiwekwa mikononi mwa polisi kwa
saa nne kutokana na purukushani za uandikishaji wa wapigakura katika
mfumo wa BVR.
Tukio hilo lilitokea juzi jioni kwenye
kituo cha uandikishaji kituo cha Osunyai, Kata ya Sombetini ambako watu
hao akiwamo mbunge walitiwa mbaroni.
Diwani wa Kata ya Sombetini, Ally Bananga alisema mbunge huyo na watu wengine walikamatwa huku wengine 13 wakijeruhiwa katika tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema juzi kuwa tukio hilo alikuwa amelisikia juujuu lakini hakuwa amepata taarifa zaidi.
Mmoja wa washuhuda wa tukio hilo, Amiri
Ally alisema juzi saa 12.20 jioni Lema alifika katika kituo hicho na
kuuliza kinachoendelea na kuhamasisha waandikishaji kufanya haraka
katika kuandikisha lakini walitokea vijana kadhaa waliodhaniwa ni
wanachama wa CCM na kuanza kumzuia mbunge huyo asiingie ndani.
“Kila
jioni Lema huwa anazungukia vituo kuangalia maendeleo lakini hakuna
jambo linalotokea ila leo (juzi) kuna vijana ambao huwa tunawaona kwenye
misafara ya CCM kama walinzi, walianza kumzuia Lema asiingie ndani,
walianza kusukumana na wananchi nao waliingilia kati, ndio vurugu
zikaanza,” alisema.
“Vurugu
zilipopamba moto polisi walikuja na kuwakamata baadhi ya watu na
kuondoka nao akiwamo Lema na watu wengine wakaanza kukimbia ovyo,”Amiri.
Mmoja wa watu waliojeruhiwa, Abduli Adam
alisema baada ya kuona mbunge anasukumwa hovyo na vijana walioonekana
kama ni kutoka kwa walinzi wa CCM aliingilia kati kutaka kumsaidia
lakini alichomwa kisu cha kichwa na kuvuja damu nyingi.
“Mimi
nilikuwa kwenye foleni nikashangaa kelele upande wa pili kuangalia
nikamuona Mbunge Lema katikati, hivyo nikajitosa kumsaidia nikachomwa
kisu cha kichwa sijui aliyenichoma na sasa niko njiani naelekea
hospitali ya Mkoa Mount Meru kutibiwa,” alisema.
Wengine waliokamatwa ni pamoja na
mwanasheria wa Chadema, mwenyekiti wa Mtaa wa Osunyai, viongozi
mbalimbali wa chama na wananchi waliokuwa wanajiandikisha kituoni hapo.
Kukamatwa kwa watu hao kulisababisha
shughuli ya uandikishaji kusitishwa kutokana na vurugu kuzuka kwenye
kituo hicho saa 12 jioni badala ya saa 2:00 usiku kama ilivyopangwa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Akizungumzia tukio hilo, Lema alisema, “Nimeshindwa
kuelewa kukamatwa kwangu baada ya kutoa taarifa polisi, inawezekana
vipi mlalamikaji akakamatwa na wahalifu wakawa huru.”
MWANANCHI
Waziri Mkuu Mizengo Pinda
amewashukuru wanachama waliojitokeza kumdhamini, huku akieleza kuwa
anaondoka mkoani Iringa na msemo mpya; “Yeye anatosha na chenji
inabaki.”
Pinda alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wanachama wa CCM waliofika kwenye ofisi za chama hicho kumdhamini.
Akiongoza wanachama hao wakati wa
utambulisho wa watu waliohudhuria hafla hiyo, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa
wa Iringa Dk Yahya Msigwa alisema: “CCM oyee, wanachama wakajibu oyeee, Pinda oyeee wanachama wakajibu oyeee. Pinda anatosha hatoshi? wanachama wakajibu anatosha, Dk Msigwa akaongeza: “Pinda anatosha na chenji inabaki.”
Katika shukrani zake, Pinda alisema: “Niwashukuru
wanachama wa CCM mkoani hapa mliofika kunidhamini, lakini pia katika
mkoa huu nimepata neno jipya na ninaondoka nalo. ‘Mimi natosha na chenji
inabaki…sijui chenji inayobaki ndiyo nani.”
Katika hafla hiyo, Waziri Pinda aliitaka
CCM kupitisha majina ya wagombea wa nafasi ya urais, ubunge na udiwani
kwa kuzingatia matakwa ya wananchi ili kuepuka chama kupoteza nafasi kwa
jamii.
Alionya kama chama kitapuuza matakwa
wananchi, kinaweza kupata pigo kama ilivyotokea katika Uchaguzi Mkuu
mwaka 2010 katika Jimbo la Iringa na majimbo mengine kadhaa nchini.
“Mimi
ni mlezi wa Mkoa wa Iringa kichama, nawaombeni wekeni masilahi ya chama
mbele badala ya masilahi ya mtu binafsi na mnapokwenda kutafuta viongozi
wa ngazi ya kata, jimbo na urais. Hakikisheni wagombea mnaowaleta ni
wale wanaokubalika na jamii ya eneo husika,” Pinda.
Akiwa mjini Morogoro jana, Pinda
alizungumzia kauli yake aliyotoa bungeni akilitaka Jeshi la Polisi
kuwapiga wanaokiuka amri halali kuwa ilikuzwa sana na vyombo vya habari.
Pinda alisema,
“Niwashukuru waandishi wa habari kwa kujitokeza kwa wingi kuliko mikoa
yote niliyopita kuomba wadhamini lakini na nyinyi mkisikia jambo
mnalikuza.”
Alitolea mfano kauli hiyo kisha akasema,
“baadhi ya vituo vya redio vimefikia hatua ya kuitengeneza sauti ile
kama naulizwa swali na kusikika nikitoa amri ya kumpiga mhusika
aliyefanya kosa.”
Pinda alisema yeye ni muumini mkubwa wa kudumisha amani na utulivu.
NIPASHE
Baadhi ya wabunge wa Viti Maalum, wamelalamika kwamba wamekuwa wakidharauliwa na jamii kutokana na uteuzi wao.
Waliyatoa malalamiko hayo walipokuwa wakiingia kwenye semina ya uelewa wa mchakato wa uchaguzi mjini hapa jana.
Semina hiyo ipo chini ya uwezeshaji
wabunge ambayo iliandaliwa na Bunge kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa
Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP).
Mbunge wa Viti Maalum (Cuf), Zahara Ali Hamad, alisema Katiba imetoa viti maalum kwa mkono mmoja, lakini imekataa kwa upande mwingine.
Alitoa mfano kwa sheria inayotaka waziri
mkuu atokane na jimbo la uchaguzi wakati mawaziri wengine wanaweza
kutokana na jimbo ama viti maalum.
Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Taulida Nyimbo, alisema wanawake wa viti maalum wanadharauliwa na kutopendana.
“Siamini kuwa wanawake hatupendani, ukiweka mtu hauziki hawezi kupata hata kura za wanawake wenzake,” alisema.
Aidha, alisema viti maalum vimekuwa vikisumbua kwa sababu watu hawafahamu jinsi gani vinapatikana.
Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Suleiman Bundara, alisema taabu kubwa ni wanawake wenyewe kutopendana.
Mwenyekiti wa semina hiyo, Anna Abdallah, alitaka vyama vikubwa vya siasa kuonyesha mfano kwa kuwapa wanawake vyeo katika vyama.
Hata hivyo, Mbunge wa Manyovu (CCM), Albert Ntabaliba, alisema ni vyema wanawake wakaanzisha vyama vyao vya siasa ili nafasi ya juu ziwe zao.
“Sijaona wanawake walioanzisha vyama vya siasa na sheria inaruhusu kufanya hivyo. Waanzishe ili wachukue nafasi zote za juu,” alisema.
Akijibu hoja za wabunge hao, Mkurugenzi wa Utetezi wa Kituo cha Haki za Binadamu Nchini (LHRC), Harold Sungusia,
alisema ili kuondoa dharau kwa viti maalum, mambo ya msingi ya
kuyafanya ni kuweka utaratibu muafaka utakaowekwa katika sheria wa jinsi
ya kuwapata wabunge.
“Pia majukumu ya wabunge yajulikane kisheria ili wawajibike katika eneo hilo walilopangiwa,” alisema.
Aidha, alitaka elimu itolewe kwa umma ili waelewe upatikanaji wa wabunge hao na majukumu yao.
NIPASHE
Umoja wa Madereva Tanzania (UMT), umesema umepanga kwenda bungeni kuonana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
pamoja na Wabunge kwa madai kuwa Kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu
inaonekana kushindwa kutatua madai yao ya muda mrefu dhidi ya waajiri
wao.
Aidha wamesema kuwa katika kikao cha
kamati hiyo kitakachokaa Juni 23, mwaka huu, wanataka kiwe cha mwisho na
kupata majibu na kuwa kama Serikali haitatoa majibu yanayoridhisha,
Ijumaa wiki hii watasimamisha usafiri nchi nzima ili mazungumzo
yaendelee.
Wamefikia uamuzi huo baada ya kikao cha
Ijumaa iliyopita cha kamati hiyo kushindwa kutoa majibu huku wamiliki
wa vyombo vya usafirishaji wakishindwa kuudhuria bila taarifa.
Katibu Mkuu wa UMT, Rashid Salehe,
alisema Serikali na wamiliki wanawachezea mchezo mchafu, huku madereva
wakiendelea kuteseka na kufanya kazi katika mazingira magumu bila
mikataba wala bima za matibabu.
“Tumepanga
kuwa madereva wote tutakodi basi kwenda bungeni Dodomaili kuonana na
Waziri Mkuu pamoja na wabunge watusaidie kwani kila siku hii kamati
inatuzungusha bila kuta majibu yanayoeleweka, hivyo in wazi wameshindwa
kazi,” alisema.
Alisema kuwa awali walitaka kikao cha
Ijumaa iliyopita kuwa cha mwisho na kutoa majibu ya matatizo yao, lakini
haikuwa hivyo kwani inaonekana wazi kuwa Serikali inawasikiliza
wamiliki kuliko madereva.
MTANZANIA
Waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa
amesema hana wasiwasi wa kukatwa jina lake ndani ya vikao vya CCM
vitakavyochuja majina ya makada wa chama hicho wanaoteuliwa kuwa
wagombea Urais kwa kuwa na hakuna mgombea aliyefikia rekodi yake ya
utendaji.
Lowassa aliwataka wanachama wake kutokuwa na wasiwasi wowote wa jina lake kukatwa na vikao vya chama.
“Nikitazama
majina ya wagombea, hakuna anayenifikia rekodi yangu, nimeanza kazi
mwaka 1977, sijafanya kazi nyingine zaidi ya CCM, Sasa leo anayekata
jina langu anatoka wapi?, ngoja niulize anakata kwa sababu gani? sioni
kosa la kukatwa jina langu na Watanzanai hawaoni, kwa hiyo msiwe na
wasiwasi” Lowassa.
Lowassa alisema anapata ujasiri kwa
sababu kuna Watanzania wengi wanamuunga mkono na kwamba CCM itatenda
haki katika uteuzi wa majina.
HABARILEO
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imetoa
makadirio ya idadi ya watu wanaotarajiwa kupiga kura katika uchaguzi
mkuu wa Oktoba 2015 ambao wanakisiwa kuwa watafikia milioni 24.2 nchi
nzima.
Taarifa hizo ni makadirio ya idadi ya watu wanaostahili kupiga kura katika majimbo ya uchaguzi Tanzania kwa mwaka 2015.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010,
idadi ya wapigakura waliojiandikisha ilikuwa 20,137,303, lakini
waliopiga kura Oktoba 31 mwaka huo walikuwa 8,626,283 sawa na asilimia
42.84 ya wapiga kura wote waliojiandikisha.
Takwimu hizi zimetolewa katika ngazi ya
Mkoa, Wilaya, Jimbo la Uchaguzi na Kata au Shehia kama yalivyokuwa mwaka
2010. Makadirio ya idadi ya wapigakura yametokana na Sensa ya Watu na
Makazi ya Mwaka 2012.
Kwa mujibu wa ripoti iliyo kwenye kitabu
maalumu cha takwimu za wapiga kura mwaka huu, ambayo nakala yake
imepatikana kupitia Ofisi ya Takwimu ya Mkoa wa Arusha, idadi hiyo
imepatikana kwa kutumia mbinu za kidemografia zinazohusisha mabadiliko
katika viwango vya uzazi, vifo, uhamaji na uhamiaji katika ngazi ya
Taifa, Mkoa, Wilaya, Majimbo ya Uchaguzi na Kata au Shehia husika.
Inakadiriwa kuwa ifikapo siku ya
uchaguzi, Tanzania itakuwa na watu wapatao 48,522,229 ambapo watakaokuwa
na umri wa kupiga kura watakuwa ni watu 24,252,927 iwapo wote
watafanikiwa kuandikishwa upya.
Mkoa wa Dar es Salaam wenye majimbo nane
unatarajiwa kuwa na wapiga kura wengi zaidi watakaofikia milioni 3,
ukifuatiwa na Mbeya itakayokuwa na wapiga kura milioni 1.5, Mwanza
milioni 1.4 na Morogoro itakayokuwa na wapigakura milioni 1.3 katika
nafasi ya nne.
Mikoa mingine inayotarajiwa kuwa na
wapiga kura wengi ni pamoja na Kagera itakayokuwa na wapigakura milioni
1.2, Tabora inayokadiriwa kuwa na idadi ya wapiga kura milioni 1.1,
Tanga nayo kwa idadi kama hiyo ya milioni 1.1 pamoja na Dodoma
itakayokuwa na wastani wa wapigakura milioni moja.
Maandalizi ya kitabu cha idadi tarajiwa
ya wapigakura yameshirikisha maofisa kutoka Wizara, Idara na Taasisi za
Serikali ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa
Serikali Zanzibar, pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Tume ya Uchaguzi Zanzibar na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC).
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment