Wednesday, June 24, 2015

VIJANA WATAKIWA KUTUMIA RASILIMALI KUJIKWAMUA NA UMASIKINI



Tangakumekuchablog
Tanga, DIWANI kata ya Kiomoni halmashauri ya jiji la Tanga, Kauli Makame, amewataka vijana kijiji cha Kivuleni kuitumia rasilimali ya ardhi kwa kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji lengo likiwa ni kuondosha umasikini miongoni mwao.
Akizungumza katika mkutano wa wananchi jana, Makame alisema kata hiyo iko na fursa nyingi za kimaendeleo kikiwemo kilimo cha kisasa na cha umwagiliaji pamoja na mifugo hasa ikiwa na eneo kubwa la kufanya shughuli hizo.
Alisema kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha vijana wanaweza kuzitumia nguvu zao kwa kulima kilimo cha kisasa na kuweza kupata mavuno mengi baada ya ardhi hiyo kuwa na rutba nzuri kuendesha   kilimo.
“Ndugu zangu na vijana ambao tumekusanyika hapa tumekuwa tukishuhudia mvua zinavyonyesha mfululizo----hii ni baraka ambayo tunatakiwa kuitumilia vyema kwa kulima na ufugaji” alisema Makame na kuongeza
“Binafsi nashawishika kushinda shambani kwani mvua zitakapokata kunyesha hapa itakuwa ni kutafutana kwani kutazuka kila aina ya balaa likiwemo la njaa----kwanza hatuna ada ya kuhifadhi chakula ndani” alisema
Aliwataka wakazi hao wake kwa waume kuyatumia mashamba yao kwa kazi za kilimo na kuacha kuuza kwani baada ya kukamilika mradi wa barabara wageni wengi watamiminika kufuata mazao ya chakula.
Kwa upande wake mkazi wa Kivuleni, Salama Mikidadi, alimtaka Diwani huyo kuwasemea katika vikao vya mabaraza ya  Madiwani juu ya kupata asilimia tano zilizotengwa halmashauri kwa wanawake.
Alisema vikundi vyao vimekuwa  vikiomba kupatiwa asilimia tano iliyotengwa lakini hadi muda huo wamekuwa wakipewa ahadi jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma jitihada za kujiletea maendeleo.
“Mheshimiwa diwani sisi wajasiriamali wanawake kazi zetu zimekuwa haziendelei na kila siku umasikini umekuwa ukituandama----hii ni kwa sababu fursa za mikopo hatuzipati” alisema Mikidadi
Alimtaka Diwani huyo kuwatafutia masoko ya kuuzia bidhaa zao za mikono ndani na nje ya nchi likiwemo soko la pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)  ambalo wajsiriamali wengi nchini hawana uelewa nalo.
                                                      Mwisho

No comments:

Post a Comment