Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha elimu cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongozakufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kiko na Hostel pamoja na kutoa kozi ya Kiingereza na Computer. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
Harusi ya mshambuliaji wa Simba, Mganda Emmanuel Okwi
imeacha historia nchini Uganda akitumia dola 80,000 ( Sh 160,000 Mil )
kwa ajiri ya kuifanikisha iliyofanyika Jumamosi jijini Kampala.
Kiasi hicho kinatosha kabisa kukamilisha
usajili wa timu zisizopungua tatu za Ligi Kuu Bara, lakini yeye
alitumia fedha hizo kwa ajili ya sherehe, huku Gazeti hili lilikuwa
Uganda na kushuhudia kila kitu kilivyokuwa kinaendelea wakati Okwi
akimuoa Florence Nakalega.
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Hamis Kiiza na Nabisubi Julian ndiyo walikuwa wasimamizi wao wa harusi hiyo, ilifungwa katika kanisa la Miracle Centre Cathedral lililopo Lubaga, Kampala.
Baada ya hapo shughuli ya kupiga picha
za ukumbusho kwa maharusi, ilifanyika katika hoteli kubwa ya kifahali ya
Munyonyo Lesort Beach na kumaliziwa na sherehe kamili kwenye Ukumbi wa Main Exbition Hall uliopo ndani ya jengo la UMA maeneo ya Lugogo.
Okwi alitumia magari saba yalikuwa maalumu kuwabeba maharusi, kati ya hayo matano ni aina ya Jaguar na mawili Brevis.
Hata hivyo, msafara wa harusi hiyo
ulipata matatizo baada ya magari mawili yaliyowabeba wasimamizi akiwemo
Hamis Kiiza kupata ajali, lakini hakuna aliyeumia zaidi ya mishtuko ya
kawaida.
Maharusi wabadili nguo mara mbili
Hapa ndipo kulikuwa na utamu kamili,
maharusi waliingia ukumbini majira ya saa 11 jioni, mwanaume walivaa
suti za bluu na mwanamke gauni na shela nyeupe kabla ya kwenda kubalisha
na kuvaa suti za kaki kwa wanaume na bibi harusi alivaa gauni lenye
rangi ya kijivu.
Okwi alipokelewa na wachezaji wenzake
waliokuwa wameshika mipira kwa juu yeye akapita katikati yao huku
wakicheza na baada ya hapo walikabidhiwa mpira na makocha Sam Simbwa na
Moses Basena.
Katika hali isiyo ya kawaida, Okwi
alijikuta akidondosha chozi alipokuwa anazungumzia wasifu wa mkewe,
Florence na alilia baada ya kuona chozi la mkewe ambaye ndiye alianza
kuelezea wasifu wa mumewe.
Okwi alipoulizwa alisema: “Nililia kutokana na furaha kwani tumepita katika mazingira ya kila namna, magumu na raha.
“Nimefurahi sana kukamilisha shughuli hii na sasa nina mke ambaye tutatengeneza familia moja na atakuwa mshauri wangu,” Okwi.
MWANANCHI
Zikiwa zimesalia siku nne, kabla ya
kumalizika kwa uchukuaji na urudishaji fomu za kuwania urais CCM, kada
wa chama hicho Banda Sonoko (46) amechukua fomu akijigamba kwamba yeye
ni greda linalokuja kusawazisha nchi.
Wagombea wote wanatakiwa kumaliza
michakato yao ndani ya wiki hii na hadi kufikia Ijumaa, kila mmoja awe
amewasilisha vielelezo vyake ikiwamo majina ya wadhamini 450 kutoka
mikoa 15, kati ya hiyo mitatu ya Zanzibar kupisha vikao vya kujadili na
kuchuja wagombea vitakavyofanyika kuanzia mwishoni mwa wiki ijayo.
Sonoko ambaye anakuwa kada wa 42 wa CCM
kuchukua fomu alisema ameamua kufanya hivyo kwa sababu anazo sifa,
vigezo na uwezo kwamba ndiye anayeweza kuvaa viatu vya Mwalimu Julius
Nyerere… “na hivi viatu sina haja
ya kuvifuata Mwitongo (Kijiji alichozaliwa Mwalimu), hivi viatu anavyo
mchezaji mmoja, aliwahi kucheza aliwahi kucheza nchini hapa. Huyo
mchezaji alipocheza alifunga magoli mengi sana na kama Taifa,
tukafaidika.
Hivi
viatu havijakwenda Mwitongo, sihitaji kwenda Butiama, anavyo mtu fulani
ni kiasi tu cha kwenda na kumwambia naomba viatu hivi nivivae. Kilicho
kizuri ni kwamba navifahamu mpaka na namba na alama zake. Kiatu cha
kulia cha Mwalimu Nyerere kina alama mbili ya kwanza ni nchi kujiendesha
kwa kodi zetu. Kodi hizi zitathiminiwe, zidaiwe kwa muda na hilo liwe
jambo la msingi, misaada iwe suala la mjadala,” alisema.
Alisema nchi ina raslimali nyingi za kutosha na kinachotakiwa ni usimamizi katika eneo hilo.
Alisema CCM imefanya mambo makubwa
katika uongozi wake ikiwamo kutengeneza miundombinu ya kutosha na sasa
kinachotakiwa kuisawazisha… “Miji yetu imeshakaa vizuri sasa nchi yetu
inahitaji greda liweze kusawazisha… na greda ni mimi, nitaweza
kusawazisha matatizo yaliyobaki na kuweza kuhakikisha lindi la umaskini
linaondolewa.”
Sonoko alisema rais anayehitajika kwa wakati huu ni yule anayejali muda na kuwa na uamuzi, mambo ambayo yote anayo.
Alisema kaulimbiu yake ni kutokomeza umaskini na kwamba anaamini katika usimamizi jambo hilo mkazo endapo atafanikiwa kuwa rais.
Vipaumbele vingine ni kufufua uchumi wa
viwanda, kuwekeza katika uchumi wa kilimo na kwamba tangu alipoondoka,
Mwalimu Nyerere hakuna kiongozi ambaye amekuwa tayari kuimba wimbo wa
kuboresha kilimo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
amesema CCM na Serikali yake, haviwezi kutishwa na mtu yeyote katika
kutekeleza uamuzi wowote kutokana na kuwa na historia, msimamo usioyumba
na uongozi thabiti.
Membe aliwataka Watanzania wakatae vitisho na ulaghai kutoka kwa mtu yeyote katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
MWANANCHI
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe
amesema kama angekuwa ni msaliti na kibaraka wa Chama cha Mapinduzi
(CCM), asingeweza kuongoza mapambano ya kuwang’oa mawaziri 13 kwa miaka
mitatu katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
Aliyasema hayo jana alipokuwa akihutubia
mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mabawa uliolenga
kukitangaza rasmi chama chake kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga na vitongoji
vyake.
Zitto alisema mwaka 2012 aliongoza
mapambano ya kuwang’oa mawaziri wanane wakati mwaka 2013 walijiuzulu
mawaziri wanne kwa kashfa ya Oparesheni Tokomeza, wakati mwaka jana,
mawaziri watatu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali walilazimika kuachia
ngazi kutokana na kashfa ya Akaunti ya Tegeta escrow.
“Wananchi wa Tanga jiulizeni, hivi msaliti anawezaje kuwang’oa mawaziri wote hao ndani ya kipindi cha miaka mitatu?” alihoji Zitto na kusisitiza kuwa kuna watu wamelenga kutumia hoja hiyo kwa lengo la kumchafua.
Zitto alisema ni kutokana na kunyanyaswa
na kuonewa na viongozi wa ngazi ya juu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), hivyo aliona njia mbadala ni kutafuta jukwaa
lingine la siasa ili aweze kuwatumikia Watanzania.
“Kuanzisha
chama kipya siyo kazi nyepesi, lakini kwa sababu tulikuwa na dhamira ya
dhati tumeweza kufyeka mapori na sasa tumefanikiwa na leo hii
tunakileta kwenu ili mkipokee kwa sababu ACT ni yenu,” Zitto.
Alisema chama hicho kina mpango wa
kuhamasisha ufufuaji wa zao la mkonge mkoani hapa ili lilimwe na
wakulima wadogo badala ya wakubwa kwa sababu katika nchi zilizofanikiwa
kuleta mapinduzi ya mkonge zimesaidiwa na wakulima wadogo.
Alisema kupitia ACT atahakikisha hoja
yake aliyoiwasilisha bungeni na kupingwa na wabunge wa majimbo ya Mkoa
wa Tanga ya kulifufua zao la mkonge inatekelezwa.
Mjumbe wa ACT, Seleman Msindi maarufu
‘Afande Sele’ alisema hajajiunga na ACT – Wazalendo kwa sababu ya
urafiki wake na Zitto, bali amebaini kuwa ndiyo chama chenye mlengo
makini wa kuipeleka nchi kunakostahili mara kitakapofanikiwa kushika
dola.
HABARILEO
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
ambaye anawania kuchaguliwa kuwania nafasi ya urais kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM) amemwagia sifa Rais, Dk Jakaya Kikwete kwa kuliongoza
Taifa vizuri huku likiwa bado na amani na utulivu mkubwa wakati
akielekea kumaliza muda wake wa kuliongoza Taifa kwa vipindi viwili.
Aliyasema hayo jana mjini Kibaha wakati
wa kuomba wanachama wa CCM mkoani Pwani wamdhamini ikiwa ni taratibu kwa
wanachama wanaowania Urais kupitia chama hicho kudhaminiwa.
Lowassa alisema kuwa anampongeza Rais
Kikwete kwa kuongoza nchi vyema na kuendeleza sifa ya nchi ya Tanzania
kuwa na amani ambayo baadhi ya nchi zimeifanya kama mfano wa kuigwa kwa
utawala bora.
“Rais Dk Kikwete kafanya kazi kubwa ya kupongezwa kwani anaicha nchi ikiwa kwenye hali nzuri kwa umoja na mshikamano mkubwa,” Lowassa.
Aidha alisema kuwa mkoa wa Pwani ndipo
Rais Dk Kikwete alipoanzia safari yake ya kuwa Rais na yeye anaamini
Mungu akimjalia atapata nafasi hiyo.
Alisema kuwa endapo atachaguliwa
atahakikisha matatizo ya hospitali ya Tumbi anayatatua ndani ya mwaka
mmoja pamoja na changamoto za miundombinu na barabara Naye Mwenyekiti wa
CCM Kibaha Mjini Maulid Bundala alisema kuwa anaomba vikao
vinavyohusika vimpitishe ili aweze kuwania nafasi hiyo na wasiangalie
mtu bali waangalie maslahi ya chama.
Jumla ya wanachama wa CCM mkoa wa Pwani
wapatao 78,500 walimdhamini kwenye nafasi hiyo kutoka wilaya sita za
mkoa huo ikiwa ni pamoja na Kibaha Mjini 25,500, Bagamoyo 16,000,
Mkuranga 11,200, Kibaha Vijijini 10,200, Rufiji 7,800 na Kisarawe 7,000.
HABARILEO
Zaidi ya wahamiaji haramu 50 wanaoishi
katika kijiji cha Tamau wilayani Bunda, mkoani Mara, akiwemo mwenyekiti
wa kijiji hicho wamezuiwa kujiandikisha kwenye daftari hilo.
Ofisa uhamiaji wa Mkoa wa Mara, Ally Dady
jana amethibitisha kuzuiwa kwa watu hao wanaodaiwa kuwa ni raia wa nchi
jirani Kenya. Dady alisema taratibu za kuwafikisha kwenye vyombo vya
sheria watuhumiwa hao zinafanyika na kuongeza kuwa baadhi yao, wapo
ambao walikamatwa wakiwa tayari wamekwishajiandikisha katika daftari
hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waliobainika
kuwa ni wahamiaji haramu ni pamoja na mwenyekiti wa kijiji hicho, John
Seda, ambaye anatafutwa baada ya kutoroka.
Aidha, ilielezwa kuwa wale ambao tayari
walikuwa wamekwishajiandikisha katika daftari hilo, wameamriwa kurudisha
vitambulisho hivyo kwa ofisa mtendaji wa kijiji na wa kata hiyo ya
Kunzugu.
Ilidaiwa kuwa tayari watu hao wamepewa
fomu maalumu ya kujieleza na ofisi ya uhamiaji wilayani hapa, ambapo
vyanzo vya habari vinasema kuwa wahamiaji hao wamo askari polisi kutoka
nchini Kenya ambao wanaishi kijijini hapo kinyume cha sheria.
Aidha, vyanzo hivyo vya habari vimedai
kuwa watu hao wanaishi kijijini hapo kinyemela na kwamba mwenyekiti huyo
aliyechaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita alitumia
mbinu nyingi ya kupata uongozi huo ikiwa ni pamoja na kutoa rushwa.
Pia vyanzo hivyo vinasema kuishi
kijijini hapo kwa wahamiaji hao kwa kipindi chote hicho ni kutokana na
viongozi wa serikali kuwahalalisha watu hao kuishi hapo baada ya kupewa
kitu kidogo, yaani pesa, mbuzi na ng’ombe.
Hata hivyo, Kaimu Ofisa Mtendaji Bernard
Methew alipotafutwa na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu,
alisema kuwa hana taarifa yoyote juu ya jambo hilo na wala hakuna
wahamiaji haramu kijijni hapo.
“Hizo habari umezipata wapi wewe, mbona
mimi sijui….. kama ni uhamiaji nenda uwaulize huko huko” alisema Ofisa
mtendaji huyo na kukata simu.
Gazeti hili lilimtafuta msimamizi
msaidizi wa uchaguzi katika Wilaya ya Bunda, ambaye pia ni mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Lucy Msoffe, ambaye alisema kuwa
hana taarifa zozote kuhusu wahamiaji hao haramu.
Aidha, Lucy aliahidi kufuatilia zaidi
suala hilo, ambapo baadaye alipiga simu na kusema kuwa ni kweli
wahamiaji haramu zaidi ya hamsini wamezuiwa kujiandikisha katika daftari
hilo kijijini hapo na kwamba taratibu za kisheria zinafanywa na watu wa
uhamiaji.
Hivi karibuni wahamiaji haramu watatu
walikamatwa wakiwa wamejiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga
kura, huku baadhi yao wakiwa wamejiandikisha zaidi ya mara moja katika
vituo tofauti wilayani hapa.
Wakati huo huo, Ofisa uhamiaji huyo wa
Mkoa wa Mara, alisema kuwa wahamiaji haramu wengi wako katika vijiji vya
Nyaburundu, Karukekere na Tamau, katika Wilaya ya Bunda, na katika
vijiji vya Bugwema na Masinono katika Wilaya ya Butiama, katika
halmashauri ya wilaya ya Musoma vijijini.
HABARILEO
Taasisi ya Utafiti wa Maendeleo ya Elimu Tanzania (TEDRO) imetoa matokeo ya utafiti kuhusu wagombea ambao hotuba zao ziligusa mahitaji wa wananchi kuwa Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ndiye aliyeibuka kidedea.
Mkurugenzi wa TEDRO, Jacob Kateri
alisema lengo la utafiti huo ilikuwa kujua ni kwa kiasi gani Watanzania
wanafuatilia mchakato mzima wa kuelekea uchaguzi mkuu, hususani kipindi
hiki cha watu kutangaza nia na kutambua mchango wa vyombo vya habari
kufikisha elimu ya uraia kwa umma tunapoelekea uchaguzi mkuu.
Alisema utafiti huo umefanywa katika za
Njombe Mjini na Vijijini, Mbeya Mjini, Rombo, Arumeru, Kinondoni,
Kilombero na Kibaha vijijini. Wakati wilaya walizohojiwa kwa simu ni
zingine zilizosalia kwa kuzingatia kwamba kumbukumbu za wahojiwa za simu
zinapatikana katika ofisi yetu.
Mkurugenzi huyo alisema uchambuzi wa
kujua nani anayewafaa wananchi kupitia vipaumbele vilivyoainishwa na
watangaza nia, kutathmini hotuba iliyo bora kwa kuzingatia yaliyomo na
mahitaji ya Watanzania na nini yaweza kuwa agenda ya msingi
tunapotarajia kumpata Rais wa awamu ya tano.
Alisema katika sehemu ya uadilifu
usiotiliwa shaka, matokeo yanaonesha kuwa Naibu Waziri wa Fedha Mwigulu
Nchemba anaongoza kwa kupata asilimia 15. Aliyefuata ni Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe 13 na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais Kazi Maalumu, Mark Mwandosya 13.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda asilimia nane,
Naibu Waziri Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba nane,
Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani saba, Waziri Mkuu wa
aliyejiuzulu, Edward Lowasa 10, Makongoro Nyerere tano na waliosema
hakuna msafi ni wananchi 12.
Pia kuhusu kipengele cha hotuba bora
Mwigulu aliongoza kwa kupata alama A, akifuatiwa na Januari, Wasira,
Profesa Mwandosya, Profesa Muhongo , Wasira na Membe walifungana kwa
kupata alama B+, Lowasa, Mbunge wa Sengerena William Ngeleja walifungana
kwa kupata alaba B.
“Tathmini ya hotuba imezingatia utulivu
katika uwasilishaji, mkusanyiko wa mambo yanayohusu wananchi wa makundi
yote ya jamii katika hotuba, uwezo wa kujibu maswali na ufafanuzi wa
mambo mtambuka ya kiuchumi ikiwamo kushuka kwa thamani ya shilingi, na
njia za utatuzi kwa nchi kama Tanzania,” alisema.
Kuhusu kipengele cha mtangaza nia wenye
uwezo wa kupambana na vita ya rushwa na kuboresha utawala bora, matokeo
yalionesha kuwa Mwigulu anaongoza asilimia 17, Dk Magufuli 14, Membe 11,
Lowasa 6.10, Jaji Ramadhani sita.
Profesa Mwandosya, Pinda na Mwakyembe
walifungana kwa kupata asilimia nane, Januari saba, Waziri wa Uchukuzi
Samuel Sitta sita, Kigwangala tatu, na wengine nne.
NIPASHE
Mtoto wa Rais Jakaya Kikwete anayesoma shule ya kimataifa ya Feza, Khalfan Jakaya Kikwete ameiwakilisha vema Tanzania katika shindano la kusaka wanafunzi wenye akili nyingi ‘Genius Olympiad’ lililofanyika Oswego, Marekani mwaka huu.
Shindano hilo huandaliwa na Idara ya
Sayansi na Elimu ya Chuo Kikuu cha New York likishirikisha shule za
kimataifa duniani likihusisha kazi za masuala ya sayansi, sanaa,
biashara na mazingira.
Kwa mujibu wa mtandao wa
www.geniusolympiad.org, mwaka huu nchi 69 zilishiriki kwa kupeleka kazi
1,171. Kazi 401 zilikidhi vigezo na kupokewa. Shule za kimataifa za Feza
ziliwasilisha kazi nne na kushinda medali moja ya dhahabu na tatu za
shaba.
Kazi iliyoshinda medali ya dhahabu
iliitwa ‘Vcardin’ iliyoandaliwa na kuwasilishwa na Khalfan na Seif Yahya
Mhata ambao wote ni wanafunzi wa shule za Feza.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Khalfan alisema kazi
yao imelenga kurahisisha mawasiliano ya kimataifa kwa kuwa na njia ya
uhakika ya kuwasiliana.
“Mradi huu unahusu kubadilishana kadi za
mawasiliano kwa njia ya mtandao. Ni muhimu sana kwa mawasiliano hasa ya
wafanya biashara, lakini inahitaji uwe na simu ya kisasa yenye intaneti
au kifaa kingine chenye intaneti,” alisema Khalfan aliyekuwa amefuatana
na Mhata.
Kazi nyingine kutoka Feza zilizoshinda
medali za shaba ni ‘The Fault of Humanity’ iliyoandaliwa na Prince
Mwemezi ambaye alipiga picha ya moto ukiunguza miti eneo la Tanganyika
Packers, Kawe jijini Dar es Salaam na kuonyesha athari za mazingira
zitokanazo na uchomaji misitu.
Medali nyingine ya shaba imeletwa katika
shule ya Feza na wanafunzi wawili Goodluck Komba na Sajjad El-Amin
ambao walianza kazi inayoonyesha namna mkaa unavyoweza kupatikana
kupitia karatasi na takataka badala ya kukata miti.
Veronica Ndomba, mhitimu wa kidato cha
sita mwaka huu katika shule ya Feza Girls, aliandaa kazi ya kuzuia
uchafuzi wa mazingira ya bahari kwa kuelimisha watu kuhusu kutotupa
taka, mafuta na uvuvi haramu baharini na kushinda medali ya tatu ya
shaba.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete
ameomba radhi kwa Watanzania aliowakosea wakati wa utumishi wake wa
miaka kumi Ikulu huku akisisitiza hakuna binadamu aliyemkamilifu.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki
iliyopita, wakati akizungumza kwenye sherehe ya kuadhimisha miaka miwili
ya Upapa wa Baba Mtakatifu Francis iliyofanyika nyumbani kwa Balozi wa
Vatican nchini, Oysterbay jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na
viongozi mbalimbali.
Rais Kikwete alitumia pia nafasi hiyo
kuwaaga viongozi hao wakuu wa Kanisa Katoliki akiwasisitizia kuwa
anaacha nyuma nchi yenye amani na utulivu huku akiwataka viongozi hao
kufanyakazi vizuri na kiongozi mpya na kudumisha amani na utulivu wa
kijamii kama walivyofanya kwake.
Alisema anaamini kuwa hakuna asiyekosea
katika maisha kwani yeye alijaribu alivyoweza na kwa kadri ya uwezo wake
lakini inawezekana kukawa na watu ambao aliwakosea hivyo wamsamehe na
waelewe ukomo wa uwezo wa binadamu.
“Napenda
pia kusisitiza kuwa hakuna binadamu aliyekamilifu na kwa wale ambao
niliwakosea naomba waelewe ukomo wa uwezo wa binadamu naacha nyuma nchi
yenye amani na utulivu, nchi ambayo inapitia katika kipindi cha ustawi
wa kiuchumi na kijamii ambao haujapata kutokea katika historia ya
Tanzania,” alisema na kuongeza kuwa:
“Nina
hakika kuwa mrithi wangu ataendeleza kazi nzuri ambayo nimeifanya
katika miaka 10 iliyopita hasa ile ya kujenga na kuimarisha uhusiano
kati ya Dola na Kanisa.”
Aidha, aliwaomba viongozi wa dini nchini
kusaidia kuendeleza jadi nzuri ya Tanzania kwa kuhakikisha nchi
inabaki na amani, kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, 2015.
Alilishukuru Kanisa Katoliki nchini kwa
kuendeleza ushirikiano wake na serikali wa kutoa huduma za jamii katika
maendeleo mbali mbali likiwamo la elimu na afya.
Kikwete pia alisema kuwa kwa sababu Dola
na Kanisa ni taasisi zinazoendeshwa na binadamu, inatokea wakati
mwingine uhusiano kati ya taasisi hizo mbili ukapitia katika mawimbi
lakini ni uhusiano unaoendelea kuwapo na kuimarishwa.
Wengine waliohudhuria sherehe hiyo
iliyoandaliwa na Balozi Askofu Mkuu Francisco Padalli, ni Askofu Mkuu
wa Jimbo Kuu la Katoliki Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na maskofu wa karibu majimbo yote ya kanisa hilo nchini.
“Kila
miaka mitano, Tanzania hupiga kura kupata ridhaa ya wananchi ya
kuongoza. Makabidhiano ya madaraka katika Tanzania limekuwa suala la
amani na tunabakia mfano wenye kung’ara katika Afrika kwa kuruhusu
makabidhiano ya amani,” alisema.
“Kwa
utaratibu huu mzuri, nitamaliza muda wangu wa uongozi na kukabidhi
madaraka kwa rais mpya. Naamini kuwa Kanisa Katoliki litasaidia sana
kuhakikisha mchakato wetu wa uchaguzi na makabidhiano ya uongozi
vinakuwa vya amani.”
Kuhusu miaka miwili ya uongozi wa Papa
Francis, Kikwete, alisema kiongozi huyo ameleta matumaini mapya
duniani, ujumbe mpya wa amani, heshima kwa utawala wa sheria amani na
utulivu.
“Ujumbe
wake kuhusu changamoto nyingi duniani, likiwamo lile la tabianchi,
umeongeza sauti yenye nguvu sana kwa namna dunia yetu inavyoendeshwa.”
NIPASHE
Hatimaye kile kikao cha Baraza la Ushauri la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachowahusisha pia marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa,
kinatarajiwa kufanyika wakati wowote wiki hii kujadili mwenendo wa
mchakato wa kumpata mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho.
Taarifa kutoka chanzo kimoja ndani ya
CCM kimeeleza kuwa Mwinyi, Mkapa na wazee wengine wanaounda Baraza la
Wazee la Ushauri, watapasua kichwa wiki hii kujadili mwenendo wa urais
ikiwa ni siku chache kabla ya kufikia Julai 2, mwaka huu, inayoonyeshwa
katika ratiba ya uchaguzi ya CCM kuwa ndiyo siku ya mwisho ya kurejesha
fomu kwa wanaowania urais.
Lengo la kikao cha Wazee ni kujadili kwa
kina mwenendo wa mchakato wa kumpata mgombea urais na mwishowe kutoa
mapendekezo yao juu ya namna bora ya kumpata mgombea kwa Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya CCM (CC)
“Kikao
hiki ni muhimu kwa hatma ya mchakato wa uchaguzi… baada ya kutofanyika
wiki iliyopita, sasa kitafanyika wiki hii, tena wakati wowote kuanzia
kesho (leo),” chanzo kilieleza.
Awali, kikao hicho kilitarajiwa
kufanyika Jumatano iliyopita jijini Dar es Salaam lakini kikaahirishwa
na Katibu wa Baraza la Ushauri la Wazee, Pius Msekwa, kutokana na kile
kilichoelezwa kuwa ni baadhi ya viongozi wakuu wa CCM kuwa safarini.
Kikao cha Baraza la Ushauri la Wazee ni
mahususi kwa ajili ya ushauri juu ya watia nia 42 wa urais waliojitokeza
kutaka kuteuliwa na CCM kupeperusha bendera yake katika Uchaguzi Mkuu
wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Wanaounda Baraza la Ushauri la Wazee kwa
mujibu wa mabadiliko yaliyofanywa na CCM mwaka 2012 katika katiba yake
ni marais wastaafu Mwinyi (Mwenyekiti), Mkapa (Mjumbe), Amani Abeid Karume (Mjumbe) na Dk. Salmin Amour (Mjumbe).
Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais, John Malecela (mjumbe) na Pius Msekwa (Katibu).
Mkutano huo wa Baraza la Wazee CCM ni utangulizi wa mfululizo wa vikao vingine vya chama hicho vitakavyoanza Julai 5, mwaka huu.
Vikao vingine ambavyo viko katika
maandalizi ya kukutana ni Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa
itakayokutana Julai 7 na Kamati Kuu (CC) itakayokutana Julai 8, chini ya
Rais Kikwete, ikifuatiwa na kikao cha NEC Julai 9, mwaka huu.
Jina la mgombea urais atakayepeperusha
bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu litajulikana Julai 12
baada ya kupigiwa kura na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM, ambao ni maalum
kwa ajili kuchagua jina la mgombea mmoja kati ya watatu.
Hatimaye kile kikao cha Baraza la
Ushauri la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachowahusisha pia
marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, kinatarajiwa
kufanyika wakati wowote wiki hii kujadili mwenendo wa mchakato wa
kumpata mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho.
No comments:
Post a Comment