Sunday, June 28, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO, JUNE 28 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746

sunMWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete, ameelezea kushangazwa na ongezeko la uhalifu nchini kwamba kila anapotoa msamaha kwa wafungwa 4,000 katika sherehe za Muungano, lakini inapofika siku ya Uhuru, Desemba 9, anapewa taarifa kuna ongezeko la wafungwa 3,000.
Rais Kikwete, aliyasema hayo jana wakati akifunga mafunzo ya ngazi ya juu ya uongozi wa askari magereza, yaliyofanyika katika Chuo cha Magereza Ukonga wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.
Alisema: “Kila tunapofanya sherehe mbalimbali za kitaifa, najitahidi kutafuta sababu za kuwapunguza…lakini mambo yanakuwa tofauti,” alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa na mamia ya walioudhuria halfa hiyo.
Aliongeza kuwa “magereza 126, yaliyopo hivi sasa, hayatoshelezi kukidhi mahitaji ya kukabiliana na wimbi hilo la msongamano wa wafungwa kutokana na kasi ya uhalifu kuongezeka.
Alisema kutokana na hali ya misongamano ikitokea ikafanyika sensa ya kimataifa juu ya wafungwa magerezani, Tanzania inakuwa ya mwisho katika kukabiliana na ongezeko la wafungwa kwenye magereza.
“Hivi sasa kuna haja ya kurekebisha na kujenga magereza mapya, ili kukabiliana na changamoto hiyo sanjari na kuboreshwa huduma za wafungwa, kwani nao ni binadamu.Hivyo kuwataka askari wa jeshi hilo kufuata taratibu na kutenda haki kwa wafungwa.
“Tendeni haki kwa wafungwa hawa ili kuondoa malalamiko na maneno toka kwa ndugu zao, kwani wapo gerezani kwa ajili ya kujifunza kutokana na makosa yao,”Rais Kikwete.
Pia, aliliagiza jeshi hilo kuandaa mpango mkakati kama wanavyofanya polisi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ili kujua namna za kukabilina na changamoto zinazowakabili.
“Mpango wenu ukikamilika msipite njia ndefu… nileteeni mimi moja kwa moja nijiue namna ya kuufanyia kazi, kabla ya kuondoka madarakani, Rais Kikwete.
Kamishna Jenerali wa Magereza, John Minja, alisema jumla ya askari 104 walihitimu na kupewa vyeti, kati yao 10 wanatoka katika vyuo vya mafunzo Zanzibar.
MWANANCHI
Mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM, Kingunge Ngombare Mwiru amesema anahisi kuna mchezo mchafu unapangwa kwenye mchakato wa kupata mgombea wa urais wa chama hicho tawala, akitaja idadi kubwa ya waliojitokeza kuwa ni ishara mbaya.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliyefanya kazi na marais wa awamu zote nne, pia, bila kumtaja jina, alitumia muda mwingi kwenye hotuba yake kujibu kauli ya makamu mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula aliyekaririwa akisema kuwa mgombea wa chama hicho hatakiwi kujinadi.
Kingunge, ambaye amejitokeza hadharani kumpigia debe Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alionyesha hofu hiyo jana wakati mbunge huyo wa Monduli alipokuwa akihitimisha kazi ya kusaka wadhamini mkoani Dar es Salaam kwenye ofisi za CCM Mkwajuni wilayani Kinondoni.
Hadi sasa, makada waliochukua fomu kuwania urais kwa tiketi ya CCM ni 41 baada ya mwanachama mmoja kuchukua fomu jana akisema atamudu kupata wadhamini kwa njia ya mtandao katika siku tano zilizosalia.
Kingunge alipingana na kauli ya Mangula kuwa mgombea wa CCM atanadiwa na chama, si kujinadi mwenyewe akisema chama hicho kinataka mgombea anayekubalika ndani na nje.
Siku tatu zilizopita, Mangula alihojiwa na kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC) na kusema mgombea wa chama hicho hatakiwi kujinadi mwenyewe, kusisitiza kuwa anatakiwa kunadiwa na chama.
Lakini Kingunge aliikosoa kauli hiyo jana akisema chama hicho kimeweka utaratibu na hakuna sababu ya kuuacha na kuanza kuwahukumu wagombea kabla ya vikao na kusisitiza kuwa CCM haikuwahi kuwahukumu wagombea kabla katika chaguzi zilizopita.
“Mchakato ufuate taratibu zilizowekwa,” alisema Kingunge ambaye aliibuka Kinondoni ambako Lowassa alimalizia shughuli zake jijini Dar es Salaam.
“Nimemsikia kiongozi wetu mmoja tena juzi juzi hapa, nikamuona kwenye televisheni anasema mtu hawezi kwenda kujinadi yeye binafsi, ananadiwa na chama.
“Nikasema eh! hilo hilo. Lakini nataka nimweleze yeye na wenye fikra kama hizo kuwa kuna ngazi mbili katika utaratibu wetu; kwanza, mwanachama anayetaka kuwania ubunge, udiwani, urais lazima ajinadi ndani ya chama, ndivyo tulivyofanya miaka yote kwa mujibu wa katiba na taratibu zetu. Ndivyo wanavyofanya sasa wakina Lowassa.”
Alisema pili, wagombea wakishajinadi chama kitamteua mmoja ambaye kitamnadi na yeye ataendelea kujinadi.
“Si vizuri watu ambao tumewapa vyeo katika chama wakaanza ama wakaendelea kukitumia chama chetu kwa mambo yao binafsi. Kama wana mashaka tupo tunaojua mambo ya chama,” alisema Kingunge huku akishangiliwa na mamia ya watu.
Kingunge alisema mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiwa Dodoma alisema chama kinatafuta mgombea anayekubalika ndani na nje ya chama hicho ili kuweza kushindana na vyama vingine.
MWANANCHI
Antony Chalamila amekuwa mgombe wa 41 kuchukua fomu ya kuomba kupitishwa na CCM kuwania urais, lakini kivutio kilikuwa ni jinsi alivyochapa mguu kutoka ofisi za chama hicho hadi stendi ya mabasi kurudi mkoani Morogoro.
Wakati kada huyo akijitokeza tano kabla ya muda wa kuchukua na kurejesha fomu kuisha, makada wengine wawili walirejesha fomu, huku Balozi Amina Salum Ali akilalamikia kukithiri kwa rushwa katika mchakato.
Chalamila, ambaye aliongozana na msaidizi wake Benjamin Ruvunduka kwenda kuchukua fomu ofisi za makao makuu ya CCM, hakuwa na usafiri wowote wakati wa kuondoka na hivyo kutembea umbali wa takriban kilomita 1.2 kwenda kituo cha mabasi kurejea mkoani kwake Morogoro.
“Naelekea Morogoro hivi sasa wananisubiri huko,” alisema Chalamila alipokuwa akiondoka maeneo ya ofisi hizo huku akisema anashangazwa na kitendo cha waandishi wa habari kumuuliza sababu za kutotoa taarifa za tukio lake.
Chalamila alifika ofisi hizo saa 4:15 asubuhi, akiwa amevalia shati la kijani na suruali nyeusi huku akiwa ameshikilia kifimbo cheusi mithili ya kile cha Hayati Mwalimu Nyerere.
Tofauti na wengine, Chalamila alikuwa akizungumza mithili ya  Mwalimu Nyerere kwa kuzungusha midomo na kuitembeza mikono usoni akiwa na kifimbo hicho ambacho alisema alikinunua Rufiji.
Chalamila aliwaambia waandishi wa habari kuwa anaomba nafasi hiyo kwa sababu yeye ni mwanachama wa CCM na miongoni mwa haki zake kikatiba ni kuchagua na kuchaguliwa.
Alipoulizwa iwapo muda wa siku tano kuanzia jana utatosha wa kutafuta wadhamini, Chalamila alisema unamtosha na kwamba atatumia teknolojia ya mawasiliano ya kompyuta kupata wadhamini na maeneo mengine atatembea.
Siku zilizobaki siyo chache wala nyingi sana. Sasa hivi vijana tunajifunza IT (teknolojia ya mawasiliano ya kompyuta). Nitatumia IT na vilevile nitatembea,”alisema.
“Suala la kwanini nimekuwa wa mwisho, si tatizo kwa sababu aliyetangulia anaweza kuwa wa mwisho na wa mwisho akawa wa kwanza,”alisema kada huyo huku akikicheza kifimbo chake.
NIPASHE
Watu watatu, wakiwamo wawili wenye Asili ya kiasia wanadaiwa kufariki dunia wakati wakipambana na polisi waliokuwa wakilishambulia kundi linalodhaniwa kuwa ni la vijana wa Al -Shaabab lililokuwa limejificha kwenye msitu wa Kibindu, mpakani mwa Morogoro na Tanga.
Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Kamishna Msaidizi, Musa Marambo, alikanusha kuwa kundi hilo kuwa ni la Al Shabaab.
Alisema taarifa walizonazo ni kuwa kulikuwa na kundi la vijana 50 katika eneo hilo likiwa na sare za majeshi mbalimbali, silaha na mabegi ambayo haijulikani yalikuwa na nini ndani.
Kamanda Marambo alisema baada ya jeshi la polisi kupata taarifa za kuwapo kwa kundi hilo, juzi wakishirikiana na polisi mkoa wa Tanga walianza msako ambao umefanikisha kukamata vijana sita.
Kamanda Marambo alikanusha kutokea kwa vifaa hivyo na alikataa kueleza watu wanaowashikilia walikutwa na nini zaidi ya kusisitiza kuwa msako wa wenzao waliokimbia unaendelea kufanyika.
Alisema juzi usiku walifanikiwa kumkamata kijana mmoja ambapo hadi jana walikuwa wanawashikilia wengine watano.
Marambo alisema kuwa, taarifa za kuwa kundi hilo ni Al-Shabaab sio za kweli na kwamba walichojua ni kwamba walikuwa na mabegi, silaha aina ya Shotgun na sare za majeshi mbalimbali.
“Hatujathibitisha kama kundi hili ni Al-Shaabab nani amekwambia hivyo, hawa ni wahalifu na tunaendelea kuwasaka wenzao na hapakuwa na majibizano ya risasi,” alisema.
Aliongeza kuwa, wajibu wa jeshi la polisi mkoani humo ni kujipanga na mikoa ya jirani kuhakikisha wanazuia uhalifu wa aina yoyote usitokee.
Wakati kamanda huyo akikanusha baadhi ya mambo kwenye tukio hilo, Muuguzi wa zamu wa hospitali ya Misheni ya Turiani, alithibitisha hospitali hiyo kuhifadhi maiti tatu.
Alisema kuwa, kati ya maiti hizo, mbili ni za watu wenye asili ya Kiasia na moja Mwafrika ambaye aliletwa akiwa majeruhi na kufariki wakati akipatiwa matibabu.
Kadhalika, alisema  askari mmoja amejeruhiwa na yupo hospitalini hapo kwa matibabu. Kufuatia tukio hilo, inasemekana wananchi wa eneo ambalo mapigano hayo yametokea wameanza kuyakimbia kwa kuhofia maisha yao.
Mwezi Aprili mwaka huu, jumla ya watu kumi walikamatwa na polisi Morogoro baada ya kukutwa msikitini wakiwa na milipuko 30, sare za jeshi na bendera nyeusi inayodaiwa kutumiwa na kundi la wapiganaji wa Al-Shabaab wa nchi ya Somalia.
Watu hao walikamatwa katika kitongoji cha Nyandero, tarafa ya Kidatu wilayani  Kilombero, mkoani humo wakiwa katika msikiti wa Suni uliopo Kidatu.
Wakati kukiwa na uvumi wa makundi hayo, mapema mwaka huu Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya kilishambuliwa na kundi hilo na kusababisha watu 147 kupoteza maisha.
NIPASHE
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema kipindi hiki cha uchaguzi mkuu siyo muda muafaka kwa wagombea ambao ni sehemu ya serikali kutoa ahadi.
Alisema Watanzania wamechoka na ahadi bali kinachotakiwa ni kuelezea mambo yaliyofanywa na Serikali ya CCM.
Alisema hayo jana wakati akizungumza na wanachama 45 wa CCM wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam waliojitokeza kumdhamini katika harakati za kuwania urais kupitia chama hicho.
“Watanzania wamechoshwa na ahadi inakuwaje hata sisi tuliopo ndani ya serikali tunatoa ahadi, tutaambiwa unatoa ahadi ulikuwa wapi wakati na wewe ni sehemu ya serikali, tunachotakiwa tueleze serikali ya CCM imefanya nini na wana CCM tutembee kifua mbele siyo kujikunyata sababu serikali imefanya mambo mengi ya maendeleo,” alisema.
Dk. Mwakyembe alisema uchaguzi wa mwaka huu siyo wa kutoa ahadi waachwe wapinzani ndio watoe ahadi kwani kutokana na mambo makubwa ya maendeleo yaliyofanywa na serikali ya awamu ya nne ni wazi kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu CCM itaibuka na ushindi wa kishindo.
Alisema serikali ya CCM imefanya mambo mengi lakini bahati mbaya baadhi ya watu hawayaoni na kutoa mfano Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2010 kulikuwa na shule za sekondari 1700 lakini hivi sasa zipo zaidi ya 4,000, vyuo vikuu vilikuwa 17 sasa vipo 52.
Alijivunia rekodi yake akiwa Waziri wa Uchukuzi kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambapo aliweza kudhibiti wizi wa makontena katika Bandari ya Dar es Salaam ambayo iligeuzwa kama kichaka cha wezi na majambazi kufanya mambo watakavyo.
Dk. Mwakyembe alisema Serikali ya Awamu ya Tano inatakiwa kuimarisha mambo ya maendeleo yaliyofanywa na serikali ya awamu ya nne mfano ni kuongeza thamani ya mazao ili mkulima aweze kupata bei nzuri katika soko.
Dk. Mwakyembe akizungumzia suala la kujitokeza makada wengi kuwania urais, alisema hii inaonyesha kuwa CCM imeonyesha ukomavu wa kisiasa wa kuwa na Demokrasia pana ndani ya chama japo wapo wanaotafsiri kama ni utitiri lakini hata wakifika 100 ndio afya ya chama.
Alisema wagombea wote waliojitokeza ni wazuri lakini chama kitampata mmoja tu ambaye ana sifa zaidi na wote waliojitokeza watamuunga mkono ili kukifanya chama kipate ushindi.
NIPASHE
Wakati waandikishaji wa vitambulisho vya kupigia kura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa kielektroniki (BVR) kata ya Mabatini jijini Mwanza waligoma kwa zaidi ya saa tatu, mashine moja kati ya 14 iliibwa katika kata ya Kayenze wilayani Magu juzi.
Awali Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, alisema watu wasiojulikana usiku wa kuamkia juzi, waliiba mashine moja kati ya 14 zilizokuwa zikichajiwa katika nyumba ya wageni ya BM iliyopo wilayani humo.
Kamanda Mkumbo alisema mashine hiyo pamoja na nyingine zilipelekwa katika nyumba hiyo ya kulala wageni, lakini asubuhi zilipofuatwa haikuweza kupatikana.
Alisema baada ya kupata taarifa ya kuibiwa mashine hiyo, msako mkali ulifanyika ukiwamo wa kuwahoji wasimamizi wa mashine hizo, na baada ya kuweka vizuizi sehemu mbalimbali walifanikiwa kuikuta ikiwa imetelekezwa njiani.
Hata hivyo, alisema polisi walifanikiwa kuwakamata watu wawili wa nyumba hiyo ya kulala wageni kwa mahojiano ili kufahamu mashine hiyo jinsi ilivyoweza kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.
Katika hatua nyingine waandikishaji wa kata ya Mabatini na Mbugani wilayani Nyamagana, jana walifanya mgomo kutokana na kugomea Sh. 3,000 badala ya 5,000 za usafirishaji wa mashine hizo.
Waandikishaji hao waligoma baada ya kuelezwa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza, mashine hizo hazitosafirishwa kwa kutumia pikipiki zaidi ya magari, hivyo pesa walizokuwa wakilipwa Sh. 5,000 kwa ajili ya matumizi hayo kupunguzwa hadi 3,000.
Mwananchi aliyefika kujiandikisha katika kituo cha Shule ya Sekondari Mbugani, James Chacha, alisema waandikishaji walifika kituoni hapo zinapohifadhiwa mashine za kata zote mbili, huku wakidai hawatafanya kazi mpaka kieleweke.
“Wananchi walifika vituoni na kukuta waandikishaji wakiwa wamegoma kwa madai ya kutaka kulipwa posho zao, ni kutosha kabisa kwani iwapo walifahamu hivyo wangedai jana (juzi) jioni baada ya zoezi hilo kufunga,”Chacha.
Naye mwenyekiti wa mtaa wa Mabatini Kaskazini, Hamisi Nassoro, alisema juzi jioni kulitokea mjadala wa kusafirisha mashine na kuonekana zinavyochukuliwa katika pikipiki zinaharibika na uongozi unaohusika na suala la uandikishaji uliwaeleza waandikishaji na kukatwa Sh. 3,000 na watabakiziwa 2,000 na wakakubaliana lakini cha kushangaza waandikishaji wameamka wakidai hawajashirikishwa na wafanyikazi mpaka mkurugenzi abadilishe uamuzi wake.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Halifa Hida, alisema Sh. 5,000 katika makubaliano kati yao na waandikishaji wa zoezi la vitambulisho hivyo zilikuwa ni kwa ajili ya usafiri wa mashine na sio vinginevyo.
Fedha hizo zitaendelea kufanya kazi hiyo na sio vinginevyo kila mwandikishaji analipwa posho halali, chakushangaza wanataka waende kinyume na makubaliano na kusababisha watu kuchelewa kujiandikisha, pesa hiyo itabaki palepale katika kazi yake na sio vinginevyo,Hida.
NIPASHE
Wakati Tanzania ikianza kutumia sheria mpya kwa washukiwa wa dawa za kulevya inayomhukumu mshtakiwa kifungo cha maisha jela, wafanyabiashara wa madawa hayo wamebuni mbinu mpya ya kusafirisha dawa hizo kwa kutumia taulo lililolowekwa kwenye dawa hizo.
Wafanyabiashara hao wanaposafirisha dawa hizo kama heroine au cocaine huziweka kwenye mfumo wa kimiminika kisha taulo wanalidumbukiza kwenye maji ya dawa na kuanika kwenye jua.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzoa, alisema hayo katika mahojiano maalum na NIPASHE Jumapili.
Alisema taulo husafirishwa kama nguo nyingine na wanapofika nchi husika huliloweka kwenye maji na kulikamua ili kutoa dawa hizo.
Alisema mbinu hiyo ilibainika kupitia mkutano uliofanyika nchi ya Seychelles wiki iliyopita ambapo moja ya washirika kwenye mapambano hayo aliielezea kama changamoto mpya.
Alisema ingawa hakuna mtu aliyekamatwa kwa kutumia mbinu  hiyo Tanzania, imebainika kwenye moja ya nchi wanazoshirikiana nazo dhidi ya mapambano hayo hutumika.
Kamanda Nzoa alisema wamekuwa na ushirikiano na nchi nyingine kwenye mapambano ya dawa za kulevya ambayo sasa yamezaa matunda baada ya usafirishaji kupungua.
Alisema mkutano huo ni mwendelezo wa mikutano mingine inayofanyika kila mara yenye lengo la kubadilishana mikakati ya mapambano ambayo mafanikio yake yalionekana toka mwaka uliopita.
Alitaja mbinu nyingine inayoendelea kutumiwa kuwa ni usafirishaji wa vibashirifu ambavyo ukamataji wake huhitaji kutumia mbwa.
Alisema baada ya Mtanzania kukabilia na kesi za namna hiyo, walizungumza na Afrika Kusini ambapo wengi huvipeleka huko ili nao wabadili njia za ukamataji.
Alisema mbinu nyingine ni kubadili uelekeo wa usafirishaji ambapo kama alikuwa anaenda Afrika Kusini atapita nchi nyingine kupoteza ushahidi na kwenda alikokusudia.
Kuhusu sheria mpya, Kamanda Nzoa alisema, itaanza kutumika wakati wowote ambapo mshitakiwa atakapokutwa na hatia atahukumiwa kifungo cha maisha.
Kamanda Nzoa alisema Rais Jakaya Kikwete, ameshaisaini sheria hiyo na itawahusu wenye tabia ya kuwakodishia nyumba wafanyabiashara wa dawa za kulevya, ambao mara baada ya kukamatwa hudai hawajui chochote.
Alisema baada ya changamoto nyingi kujitokeza dhidi ya vita hiyo, wameamua kubadilisha sheria.
“Sheria ya sasa tofauti na mwanzo, itakuwa haionyeshi thamani ya mzigo aliokutwa nao mhusika, mzigo uwe mdogo au mkubwa wote kifungo ni cha maisha jela,” alisema.
Alifafanua, tofauti nyingine ya sheria ya sasa na ya zamani, hii mpya imeongezwa vibashirifu vya kutengenezea dawa hizo ambavyo ni  moja ya mbinu za wasafirishaji zinazotumika kusafirisha dawa hizo.
Alisema kwa ujumla hali ya dawa za kulevya kidunia ikiwamo Tanzania, ni nzuri kutokana na mtandao mpana waliokuwa nao dhidi ya mapambano.
Kuhusu takwimu za ukamataji, Kamanda Nzoa, alisema mwaka jana katika ukanda wa bahari walikamata kilo 241 za dawa hizo na mwaka huu jumla ya kilo 48 za heroine zimekamatwa ndani ya nchi.
Alisema wamekamata kilo 981 za dawa za kulevya aina ya Heroine Bahari Kuu ambazo ziliteketezwa huko huko.
“Kiwango hiki kilichokamatwa mwaka huu maana yake ni kwamba wale wanaotumia Heroine kwa sasa Tanzania hali zao ni mbaya kwa maana kuna upungufu mkubwa,” alisema.
Alisema ushirikiano walionao na nchi nyingine umesaidia, idadi ya majahazi yaliyokuwa yakitumika kusafirishia dawa hizo kupungua.
Kuhusu bajeti iliyotengwa kwenye eneo hilo Kamanda Nzoa alisema ofisi yake haiingalii sana kwa sababu, mapambano kati ya nchi na nchi yanahitaji mawasiliano ya simu ambayo gharama zake sio kubwa.
NIPASHE
Ufisadi wa `kutupwa’ umeikumba Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara, ambapo pamoja na mambo mengine, kiasi cha zaidi ya Sh. milioni 932 zilizotengwa katika miradi ya maji na shule za msingi zinadaiwa kutumiwa isivyo.
Tayari malalamiko kuhusu matumizi mabaya ya fedha hizo zinazotokana na ufadhili wa Benki ya Dunia na Serikali Kuu, yameainishwa na wajumbe wa Baraza la Madiwani na kuwasilishwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Tuhuma hizo zinaelekezwa kwa uongozi wa halmashauri hiyo iliyo chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake, Felix Mabula, kwamba zilitumiwa kinyume na utaratibu katika kipindi cha Novemba 2014 na mwanzoni mwa mwaka huu.
Wakati fedha hizo zikipangwa kwa matumizi ya sekta za elimu na maji, hali inayozikabili huduma zilizopaswa kugharamiwa ni duni huku wananchi hususan wanafunzi wakiendelea kukabiliwa na mazingira duni yanayohatarisha afya na kuwaathiri kisaikolojia.
Kwa upande wa maji, imedaiwa kuwa katika kipindi cha mwaka 2013/14, halmashauri hiyo ilipokea Sh. 1,171,984,031 kwa ajili ya miradi ya maji na hadi mwaka wa fedha ulipomalizika, Juni 2014, fedha zilizotumika ni Sh. 631,834,500 tu.
Taarifa za malalamiko ya madiwani, zinathibitisha kuwa fedha zilizobaki baada ya gharama hizo ni Sh. 540,149,451 na ilipofikia Novemba 2014, Sh. 622,174,849 ziliongezwa kwenye fungu hilo kufikia Sh. 1,162,624,298.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa katika `kipindi kifupi’ taarifa ya akaunti hiyo ilionyesha  kuwa na Sh. 513,812,4119  wakati matumizi ya Sh. 648,811,879 hayakujulikana.
Matumizi ya ruzuku kwa shule za msingi katika halmashauri hiyo pia yanatajwa kukabiliwa na ‘harufu’ ya ufisadi unaoelekezwa zaidi katika Sh. 225,585,000 zilizotengwa katika kikao cha madiwani cha Novemba 17, mwaka jana. Fedha hizo zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya chakula cha shule za msingi za bweni.
Hata hivyo, kiasi hicho kiliongezeka baada ya Serikali Kuu kupeleka wilayani humo Sh. 508,779,500, ikiwa ni ongezeko la Sh. milioni 283,194, 500.
“Kutokana na fedha zilizotumwa kuwa nyingi tofauti na tulivyoomba, kikao cha madiwani kiliamua kuomba kibali cha matumizi ya fedha ili zitumike katika ukarabati wa mabweni, mabwalo na ununuzi wa vifaa vingine kwa shule nne zenye matatizo,” kilisema chetu katika uchunguzi huo.
HABARILEO
Watu watatu, wakiwamo wawili wenye Asili ya kiasia wanadaiwa kufariki dunia wakati wakipambana na polisi waliokuwa wakilishambulia kundi linalodhaniwa kuwa ni la vijana wa Al -Shaabab lililokuwa limejificha kwenye msitu wa Kibindu, mpakani mwa Morogoro na Tanga.
Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Kamishna Msaidizi, Musa Marambo, alikanusha kuwa kundi hilo kuwa ni la Al Shabaab.
Alisema taarifa walizonazo ni kuwa kulikuwa na kundi la vijana 50 katika eneo hilo likiwa na sare za majeshi mbalimbali, silaha na mabegi ambayo haijulikani yalikuwa na nini ndani.
Kamanda Marambo alisema baada ya jeshi la polisi kupata taarifa za kuwapo kwa kundi hilo, juzi wakishirikiana na polisi mkoa wa Tanga walianza msako ambao umefanikisha kukamata vijana sita.
Kamanda Marambo alikanusha kutokea kwa vifaa hivyo.
Aidha,  alikataa kueleza watu wanaowashikilia walikutwa na nini zaidi ya kusisitiza kuwa msako wa wenzao waliokimbia unaendelea kufanyika.
Alisema juzi usiku walifanikiwa kumkamata kijana mmoja ambapo hadi jana walikuwa wanawashikilia wengine watano.
Marambo alisema kuwa, taarifa za kuwa kundi hilo ni Al-Shabaab sio za kweli na kwamba walichojua ni kwamba walikuwa na mabegi, silaha aina ya Shotgun na sare za majeshi mbalimbali.
“Hatujathibitisha kama kundi hili ni Al-Shaabab nani amekwambia hivyo, hawa ni wahalifu na tunaendelea kuwasaka wenzao na hapakuwa na majibizano ya risasi,” alisema.
Aliongeza kuwa, wajibu wa jeshi la polisi mkoani humo ni kujipanga na mikoa ya jirani kuhakikisha wanazuia uhalifu wa aina yoyote usitokee.
Wakati kamanda huyo akikanusha baadhi ya mambo kwenye tukio hilo, Muuguzi wa zamu wa hospitali ya Misheni ya Turiani, alithibitisha hospitali hiyo kuhifadhi maiti tatu.
Alisema kuwa, kati ya maiti hizo, mbili ni za watu wenye asili ya Kiasia na moja Mwafrika ambaye aliletwa akiwa majeruhi na kufariki wakati akipatiwa matibabu.
Kadhalika, alisema  askari mmoja amejeruhiwa na yupo hospitalini hapo kwa matibabu. Kufuatia tukio hilo, inasemekana wananchi wa eneo ambalo mapigano hayo yametokea wameanza kuyakimbia kwa kuhofia maisha yao.
Mwezi Aprili mwaka huu, jumla ya watu kumi walikamatwa na polisi Morogoro baada ya kukutwa msikitini wakiwa na milipuko 30, sare za jeshi na bendera nyeusi inayodaiwa kutumiwa na kundi la wapiganaji wa Al-Shabaab wa nchi ya Somalia.
Watu hao walikamatwa katika kitongoji cha Nyandero, tarafa ya Kidatu wilayani  Kilombero, mkoani humo wakiwa katika msikiti wa Suni uliopo Kidatu.
Wakati kukiwa na uvumi wa makundi hayo, mapema mwaka huu Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya kilishambuliwa na kundi hilo na kusababisha watu 147 kupoteza maisha.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment