Friday, June 26, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO, JUNE 28 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746


ROUNDMWANANCHI
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wamemzuia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kuhudhuria shughuli ya kuvunja Baraza hilo itakayoongozwa na Rais Dk Ali Mohamed Shein leo.
Uamuzi huo ulitolewa baada ya Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho kutoa utangulizi kwa wajumbe akiwataka watengue kanuni ili viongozi wa kitaifa watakaohudhuria shughuli hiyo waweze kuingia ukumbini badala ya kukaa sehemu ya kawaida ya wageni waalikwa.
Baada ya kutoa utangulizi, Spika Kificho alianza kuwahoji wajumbe wanaokubali viongozi wa kitaifa waruhusiwe kuingia ndani ya Ukumbi wa Baraza kwa kuwataja wakiwamo Rais wa Zanzibar, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, mpambe wa Rais na kuungwa mkono kwa kupigiwa makofi na sauti za ndiyo.
Hata hivyo, alipomtaja Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad wajumbe wote waliokuwapo katika Baraza hilo, ambao wote ni wa CCM, walikataa wakisema kwa sauti “hapana,” kitendo ambacho kilimfanya Spika kurudia kutamka jina hilo kwa zaidi ya mara tatu na majibu yalikuwa hapana.
Hatua ya wawakilishi kumkataa Maalim Seif, imekuja siku moja baada ya mawaziri na wajumbe wa CUF kutoka nje ya Baraza wakisusa kujadili na kupitisha muswada wa sheria wa bajeti kuu ya matumizi ya Serikali ya mwaka wa fedha 2015/16 wakipinga pamoja na mambo mengine, mchakato unaoendelea sasa wa uandikishaji wapigakura katika Daftari la Kudumu.
“Mnakubali kutengua kanuni kuruhusu viongozi wa kitaifa kuhudhuria katika shughuli yetu ndani ya ukumbi? Wageni wetu ni Rais wa Zanzibar, mpambe wake, Jaji Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais,” alihoji Spika Kificho lakini alipingwa baada ya kulitaja jina la Makamu wa Kwanza wa Rais.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed aliwasilisha hati ya Serikali kuhusu marekebisho ya kanuni za Baraza.
Waziri Aboud alisema, Rais wa Zanzibar atakagua gwaride maalumu la Polisi kabla ya kuhutubia Baraza hilo saa 9.30 alasiri na kuwataka wajumbe wote kufika kabla ya kuwasili kwa Rais.
Kuhusu uamuzi wa kumkataa Maalim Seif, Aboud alisema upo katika mamlaka ya wajumbe kwa mujibu wa kanuni za Baraza hilo na kwamba hatua itakayofuata ni Spika kumwandikia barua Maalim Seif ya kutohudhuria shughuli hiyo ili kulinda uamuzi wa baraza hilo.
MWANANCHI
Mtafiti binafsi na kada wa CCM, Helena Elinawinga, amejitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama chake kuwania urais na kusema amefikia uamuzi huo ili kupunguza kujirudiarudia kwa adhabu za vifo kwa viongozi.
Helena anakuwa kada wa 40 wa CCM kuomba ridhaa ya chama hicho kuteuliwa kupeperusha bendera yake katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Kada huyo ni mwanamke wa sita kuchukua fomu za kuomba kuwania nafasi hiyo katika chama hicho akitanguliwa na Balozi Amina Salum Ali, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Mwele Malecela, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro, Monica Mbega na Ritta Ngowi.
Helena alifika katika ofisi za Makao Makuu ya CCM saa saba mchana akiwa ndani ya bajaji lakini tofauti na wenzake, akiwa amevalia shati la rangi ya zambarau, suruali nyeusi na kofia yenye rangi za Taifa.
Akiwa na Katibu wa Oganaizesheni, Muhammed Seif Khatib, kada huyo ambaye pia hakuwa na wapambe kama ilivyo kwa wagombea wengine, alikataa ombi la wapigapicha kuvua kofia. “…nitawaambia kitu kizuri baadaye kwa nini sitaki kuvua hii kofia,” alisema huku Khatib akiwasihi waandishi kutoendelea kumtaka avue au asogeze kofia hadi atakapomaliza kuchukua fomu.
Aidha, wakati akichukua fomu hiyo, kada huyo ambaye mkononi alikuwa amebeba begi lililotengenezwa kwa kitambaa cha nguo aina ya batiki, alilazimisha kupigwa picha pamoja na bango lake huku akisisitiza umuhimu wa picha hiyo kupigwa hata kabla ya kumaliza shughuli ya kukabidhiwa fomu.
Bango hilo, licha ya kuwa na maneno ambayo yalikuwa hayaeleweki vizuri na michoro ya watu waliovalia mavazi ya kifalme, moja lilionyesha akiwa amebeba mizani inayotumiwa na mahakama kuonyesha usawa wa sheria na mkono mwingine akiwa amebeba jambia.
Bango hilo pia lilikuwa na gari aina ya shangingi, picha za marais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor, Mohammed Morsi wa Misri na wanawake wengine wawili ambao hawakufahamika.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu hiyo, huku akicheka, Helena alisema: “Nilikataa kuvua kofia kwa sababu sikuchana nywele.”
Kuhusu kutovaa sare za CCM, Helena alisema aliwaambia viongozi wa chama chake kuwa wanatakiwa kufanya mafunzo ya pamoja ya wagombea wote ili kuelewa hadhi ya sare. Alipoulizwa kama siku saba zitamtosha kukusanya wadhamini katika mikoa 15 alisema; “Huwezi kujua nini kitatokea kama utakuwa hai au utakufa.”
MWANANCHI
Watoto wawili wenye umri wa kati ya miaka miwili na mitano wameuawa na fisi katika Kijiji cha Mnkola, Kata ya Ibihwa wilayani Bahi Mkoa wa Dodoma katika matukio mawili tofauti.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Teya Kata ya Ilindi wilayani hapa, Paul Mwaja alisema kuwa watoto hao wameuawa katika matukio mawili ndani ya kipindi cha wiki moja.
Mwaja alisema tukio la kwanza lilitokea juzi ambapo mtoto mmoja wa kiume mwenye aliuawa na fisi wakati akiwa na wenzie wawili wamelala. “Alikwenda fisi katika eneo hilo na kumvuta (mtoto mmoja) na kumtafuna hadi akamuua,”Mwaja.
Alisema usiku wa kuamkia jana, fisi huyo alirudi tena katika kijiji hicho na kumnyang’anya mama mmoja mtoto wake mdogo mwenye umri wa miaka miwili.
Mwaja alisema fisi huyo alimla mtoto huyo na kumbakisha kichwa na utumbo tu, hali iliyozua taharuki katika kijiji hicho.
Hata hivyo, alisema baada ya tukio hilo wananchi waliamua kufanya msako na kumkamata fisi huyo na kumuua.
Baba mzazi wa mtoto aliyeuawa usiku wa kuamkia jana aliyejitambulisha kwa jina moja la Mchamingi, alisema hawana imani kama fisi huyo kama ni wa kawaida kwani katika tukio la kwanza kabla ya kuuawa, alikimbilia katika kijiji jirani cha Bahi Makulu na kupotelea kwenye nyumba za watu.
MWANANCHI
Wakati Muswaada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2015 ukipitishwa jana bungeni, Spika, Anne Makinda ameitaka Serikali na wabunge kuwa na nidhamu kwenye matumizi ya fedha za umma, kwani itawajengea heshima.
Akihitimisha mjadala huo uliopitishwa kwa kifungu kwa kifungu, Makinda alisema: “Mkiwa na nidhamu ya matumizi ya fedha mtaheshimika na mkionyesha njaa, mtajishushia heshima.”
Hata hivyo, Makinda aliipongeza Kamati ya Bajeti kwa kazi waliyoifanya, huku akisisitizia kuwa Spika ajaye atakuta tayari kuna sheria ya fedha ambayo inasisitizia nidhamu ya matumizi yake.
Awali, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya aliwasilisha Muswada huo ili Bunge liliruhusu matumizi ya fedha za bajeti zilizopitishwa hivi karibuni pamoja na tozo za kodi zilizopendekezwa.
Katika michango yao, wabunge wengi walionyesha hofu kuwa hata kama Serikali itajitahidi kukusanya fedha, bado matumizi yake hayaridhishi hali inayoifanya ionekane kama ‘inatwanga maji kwenye kinu’.
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCS Mageuzi), David Kafulila alisema tatizo kubwa linaloikabili Tanzania ni Serikali kushindwa kudhibiti matumizi ya rasilimali zake.
Kafulila alilalamikia pia suala la matumizi ya bidhaa feki ambazo alidai zinaipunguzia hadhi Serikali, kwa madai kuwa haina ubavu wa kuwadhibiti watu wanaozingiza nchini.
“Pamoja na hayo, nimelalamikia na kuomba miongozo mara kadhaa hapa lakini sijapata majibu ya kutosha kuhusu kiasi cha Sh238 bilioni ambazo zinahusishwa na kuagizwa kwa mabehewa hewa na bando 1,000 za mabati bandia lakini hakua anayejali,” alilalamika na kuongeza:
“Mimi naamini hakuna uthubutu ndani ya Serikali, mnaishia kuwaogopa watu na hasa kampuni kubwa mnaziogopa sana, igeni mfano wa Mkurugenzi wa Bahati Nasibu (Abbas Tarimba) ambaye akikamata mashine bandia, anazichomwa moto hadharani,”  Kafulila.
Kwa upande wake, Rajabu Mohamed Mbarouk (CUF), alisema kuna mianya mingi inayotumika katika ukwepaji wa kodi inayowapa nafuu wafanyabiashara wakubwa wakati wadogo wakiendelea kubanwa.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), aliiambia Serikali iache kigugumizi kwani wafanyabiashara wanaokwepa kodi inawajua na ndiyo maana imekuwa ikipiga kelele kuwa wako wakwepa kodi wakubwa.
Godbless Blandes (Karagwe – CCM), aliitaka Serikali kuondoa ushuru na kodi katika maji. Mbunge huyo alisema binadamu yeyote lazima anywe maji na hiyo siyo starehe, hivyo kuyawekea kodi ni sawa na kutaka kuwaumiza wananchi wake.
NIPASHE
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na Waziri aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, Prof. Sospeter Muhongo, jana aliumbuka  baada ya Chama chake kukataa kupokea lundo la makasha ya CD (santuri) zenye picha za wadhamini wake 675.
Badala yake, alielezwa kwamba, hakuna kipengele kinachoruhusu kuwa na kumbukumbu hiyo.
Profesa Muhongo, alirejesha fomu yake ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, saa 9:57 asubuhi na kumkabidhi Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) na Oganaizesheni, Mohamed Seif Khatibu kwenye makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma.
Baada ya kukabidhi fomu za wadhamini wake katika mikoa 15 aliyopita, Profesa Muhongo alitoa pia makasha 15 yenye CD za picha ambazo alidai amefanya hivyo ili kuonyesha hajapita njia ya mkato akidai anaamini mtu sahihi atakayeweza kuwavusha watanzania kwa sasa, ni yeye na si mgombea mwingine kati ya makada wote waliojitokeza kutaka kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Alipomaliza kuzungumza na kisha kukabidhi CD hizo, Khatibu alisema:”Bahati mbaya katika Daftari la kurejesha fomu za CCM za kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 2015 hakuna mahala panapoonyesha kwamba utapaswa kukabidhi CD ulizonipa…wanaangua (vicheko).”
Baada ya kuelezwa hivyo, aliondoka na kuziacha CD hizo kwa Khatibu.
Profesa Muhongo alijiuzulu uwaziri wa Nishati na Madini, baada ya kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na baadaye kutangaza nia ya kugombea urais.
Kwa upande wake, Leonce Mulenda ambaye naye alirejesha fomu yake ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais, aliiga mfumo uliotumiwa na watangulizi wake, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, kugoma kuzungumzia safari yake ya kusaka wadhamini mikoani na kurejesha fomu kimya kimya.
Mulenda alirejesha fomu hiyo saa 5:35 asubuhi na kumkabidhi Khatibu na kumweleza kwamba amepata wadhamini katika mikoa 15 ikiwamo mitatu ya Zanzibar na baadaye kuagana na kuondoka huku akikwepa kuzungumzia safari yake.
NIPASHE
Wanafunzi wawili wa mafunzo ya awali wa Jeshi la Kujenga Taifa Kambi ya Chita mkoani Morogoro, wamefariki dunia na wengine 14 kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka eneo la mto Wami Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Wanafunzi hao walikuwa wakienda kambi ya Oldjoro mkoani Arusha kwa ajili ya kumalizia mafunzo yao  ya awali.
Marehemu hao wametajwa kuwa ni Edgar Kapunga na Adam Nassoro.
Kwa mujibu wa taarifa ilitolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani jana, Jafar Ibrahim, ajali hiyo ilitokea juzi saa 12:00 jioni katika tarafa na kata ya Msata barabara ya Chalinze – Segera.
Kamanda Ibrahim alisema katika taarifa yake hiyo kuwa  wanafunzi hao walikuwa katika gari la kukodi lenye namba za usajili T510 Alu aina ya Scania likitokea Chita kwenda Oldjoro kumalizia mafunzo yao.
Alifafanua kuwa gari lililokuwa limewabeba askari hao wanafunzi, liliacha njia baada ya breki zake kufeli katika mteremko na kona za mto Wami na hivyo kupinduka.
Kamanda Ibrahim alisema majeruhi hao 14 wanaendelea kupatwa matibabu katika Hospitali Kuu nya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo jijini Dar es Salaam.
Aidha, alisema dereva wa gari hilo alikimbia baada ya ajali hiyo na polisi wanaendelea kumtafuta huku miili ya marehemu ikiwa imehifadhiwa katika Hosipitali ya Lugalo.
NIPASHE
Mbunge wa Songea Mjini (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, amewaacha njia panda wapiga kura wa jimbo hilo kutokana na kushindwa kuweka wazi atagombea katika jimbo gani kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Dk. Nchimbi amekuwa akitajwa kuwa huenda atagombea katika Jimbo la Mbinga Magharibi lililopo wilayani Nyasa ambalo lilikuwa likishikiliwa na marehemu Kapten John Komba ambaye alifariki dunia mapema mwaka huu.
Dk. Nchimbi alisema uchaguzi mkuu wa mwaka huu huenda asigombee ubunge katika Jimbo la Songea Mjini.
“Nawashukru viongozi wenzangu wa chama na serikali mliopo hapa na wale ambao wamepita ndani ya miaka hii 10 ya uongozi wangu kwani walikuwa chachu ya maendeleo, hivyo natamani kutogombea tena jimbo hili ingawa wananchi wa Jimbo la Nyasa nao wanataka nikagombee ubunge  baada ya mbunge wao mpendwa Kapteni John Komba kufariki dunia,” alisema.
Dk. Nchimbi alisema katika kipindi cha miaka 10 ya ubunge wake amefanikisha kuleta maendeleo kwenye sekta ya elimu, maji, afya, barabara, kilimo, ushirika, mifugo, uvuvi, ardhi, maliasili, umeme, mawasiliano, biashara, masoko, utawala bora na michezo.
Alisema anapata wakati mgumu kueleza kwamba hatagombea Jimbo la Songea Mjini, lakini jambo la msingi ni kwamba ametekeleza kwa ukamilifu ahadi alizoahidi.
Mbunge huyo alimshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kumuamini wakati wa kipindi chake cha ubunge na kumteua kuwa naibu waziri na baadaye kuwa waziri kamili.
Dk. Nchimbi aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na baadaye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Aliondolewa katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mwishoni mwa mwaka juzi kwa sababu za uwajibikaji kufuatia sakata la operesheni Tokomeza sambamba na mawaziri wengine watatu.
Kwa upande wao, viongozi waliohudhuria mkutano huo  walionyesha masikitiko kwa hatua ya Dk.  Nchimbi kuwaaga na pia kutoweka wazi atakwenda kugombea jimbo gani la uchaguzi.
Mmoja wa viongozi hao, Alfonce Haule alisema hatua hiyo imewachanganya na imewaacha njia panda wapigakura wa Jimbo la Songea Mjini na kwamba wazee wamejipanga kwenda kuzungumza naye ili abaki kugombea tena katika jimbo hilo kwani mchango wake kwa maendeleo ya jimbo hilo bado unahitajika.
“Dk. Nchimbi tumezoea na hata alipokosea tulimuonya na alijirekebisha sasa leo ghafla anatuacha,” alisema.
Haule alisema kuwa timu ya wazee iliyoundwa kwenda kumshauri Dk. Nchimbi agombee tena jimbo hilo imepewa hadi Juni 28, mwaka huu iwe imerudisha jibu.
Kada wa CCM kutoka wilaya ya Nyasa, Anuciata Ngatunga, alisema Dk. Nchimbi Juni 19 na 20  mwaka huu alikuwa wilayani humo na alikutana na makundi mbalimbali na kuwakaribisha kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa nyumba yake ambayo ameijenga kijijini kwao Mbaha.
Ngatunga alisema kitendo hicho kimewashtua viongozi mbalimbali wa chama na wananchi kwani hawaelewi nia yake kwasababu amewaita na kuwashukuru kwa kwenda kwao kujumuika nae kwenye hafla hiyo bila kueleza nia yake hasa.
 Hata hivyo, Dk. Nchimbi alipotafutwa jana kutoa ufafanuzi kuhusiana na suala hilo hakupatikana.
HABARILEO
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR Mageuzi) ameitaka Serikali kuwasilisha bungeni taarifa ya kashfa ya ununuzi wa mabehewa feki katika Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kusababisha hasara ya Sh bilioni 230.
Baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni jana, mbunge huyo alisimama kuomba muongoza wa Spika kwamba kutokana na unyeti wa jambo hilo, ikiwa ni pamoja na madai kwamba Kampuni iliyopewa zabuni ya kuagiza mabehewa hayo haikuwa na uwezo huo, kwa nini suala hilo lisipelekwe bungeni kujadiliwa.
Mbunge huyo alihoji kwamba si vyema suala hilo likazungumzwa na kuishia nje ya Bunge badala ya kujadiliwa na kupata ufumbuzi, lakini akijibu muongozo huo Spika wa Bunge, Anna Makinda alisema jambo hilo ni la kisekta na kwamba lilitakiwa lianzie kwenye kamati inayohusika.
Hata hivyo, akichangia muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 wenye lengo la kuzifanyia marekebisho sheria 16 zinazohusu masuala ya fedha, kodi, ushuru na tozo mbalimbali nchini uliowasilishwa jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, mbunge huyo alirudia suala hilo la TRL akisema kuna haja ya jambo hilo kufanyiwa kazi kwani matumizi mabovu ya sh bilioni 230 hayawezi kufumbiwa macho.
Alisisitiza taarifa ya jambo hilo ipelekwe bungeni na kuhoji kampuni hiyo iliyohusika na kuagiza zabuni hiyo imelipwaje fedha zote hizo kabla ya kutimiza masharti na kumuomba Spika Makinda aagize taarifa iwasilishwe bungeni na sio kuwalinda.
Kauli hiyo ya kuwalinda ilimfanya Spika Makinda kusimama na kusema halindi mtu na kumtaka mchangiaji ajielekeze katika hoja husika.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta wakati akifanya majumuisho ya bajeti yake Mei mwaka huu, alisema maofisa watano wa serikali wanatarajiwa kupandishwa kizimbani hivi karibuni, kutokana na kashfa ya uagizaji wa mabehewa 274 kutoka India, huku wengine wakitarajiwa kuchukuliwa hatua za kiutawala.
Aprili mwaka huu, Sitta alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Kipallo Kisamfu na wengine wanne, ili kupisha uchunguzi wa kashfa ya uingizaji wa mabehewa feki ya mizigo.
Wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Mitandao, Ngosomwile Ngosomiles, Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa, Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiranga na Meneja Mkuu wa Manunuzi, Ferdinand Soka.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment