Thursday, September 3, 2015

HADITHI SEHEMU YA (3)

MCHIRIZI WA FAKI unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Mkombozi Sanitarium Clinic, mabingwa wa magonjwa sugu na yale yaliyoshindikana. Mkombozi wako na mashine za kisasa za kupima mwili mzima na kutoa tiba na ushauri wa kitaaluma, Mkombozi wapo Tanga eneo la Chuda, simu 0654 361333
 
MIMI NA FACEBOOK, NIMEKOMA! (3)
 
ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA
 
Teksi iliponifikisha nyumbani niliingia chumbani nikaketi kitandani na kuanza kuhesabu zile pesa. Si kwamba sikuwa na hakika zilikuwa kiasi gani. Nilijua kuwa zilikuwa shilingi milioni mbili na laki nne bali nilizihesabu tu kujifurahisha.
 
Wakati nazihesabu nilikuwa nikiimba wimbo wa taarabu wa zamani ulioimbwa na Shakilla Saidi, kifo cha mahaba. Sikujua ni kwanini niliimba wimbo huo ambao sikuwahi kuuimba hata siku moja ingawa nilikuwa naujua vizuri.
 
Baada ya kuzihesabu pesa hizo niliziweka pembeni mwa mto nikajilaza kitandani.
 
Sikuwaza kitu kingine zaidi ya zile shilingi milioni mbili nilizopewa na Hamid Al-Kadarush. Nilitaka kujiridhisha kimawazo kwamba pesa hizo nikanunue pikipiki. Lakini niliona niliache suala hilo hadi kesho yake ambapo nitakuwa na uamuzi wa uhakika.
 
Nilishinda siku ile nikiwa na furaha. Nilimpigia simu rafiki yangu Najma aliyekuwa anaishi Dar nikamjulia hali kisha nikampigia rafiki yangu mwingine anayeitwa Salma. Yeye aliuwa akiishi eneo la Donge. Hapo hapo Tanga.
 
SASA ENDELEA
 
Baada ya kuzungumza na marafiki zangu hao kwenye simu niliona niliuwa na wakatimzuri wa kutafakari kuhusu wazo langu la kununua pikipiki.
 
Siku iliyofuata nilizunguka katika maduka mbalimbali yanayouzwa pikipiki. Nilikuwa nikiangalia kila pikipiki nilioiona pamoja na kuuliza bei. Katika kuzungukazunguka kwangu nilitokea katika duka moja ambapo niliona pikipiki niliyokuwa ninaitaka. Ilikuwa ni aina ya pikipii zinazotumiwa sana na wanawake.
 
Baada ya kuinunua nilikwenda nayo nyumbani. Sasa nikaanza utaratibu wa kupata leseni ya mwanafunzi ya kuendeshea. Nilichagua nianze na leseni ya aina hiyo badala ya leseni kamili kwa sababu nilijua ingekuwa rahisi kupatikana kuliko leseni yenyewe.
 
Nilipofanikiwa kuipata nilibandika alama ya L nyekundu sehemu ya mbele nay a nyuma ya pikipiki yangu kuonesha nilikuwa mwanafunzi wa kuendesha.
 
Huo ulikuwa ni utaratibu wa kawaida, si kwa piipiki tu bali hata kwa magari. Iwapo anayetumia chombo husika ni mwanafunzi wa kuendesha anatakiwa aweke alama ya L nyekundu kwenye sehemu ya mbele nay a nyuma ya chombo chake.
 
Kabla sijaanza kuitumia pikipiki yangu nilishauriwa niipeleke kwa fundi ili ikaguliwe vizuri na kuwekwa sawa.
 
Nikaipeleka wa fundi. Ikashughulikiwa kutwa nzima. Fundi aliichangua yote akaifunga upya. Nilipokwenda jioni nilikuta pikipiki yangu ikiwa tayari. Nilikwenda kuijaza mafuta na kuanza kuitumia.
 
Kwa kweli ilinirahisishia nyendo zangu nyingi. Nikawa namshukuru yule mtu aliyenitumia pesa ambaye hata hivyo nilikuwa simfahamu.
 
Sisi binaadamu tumeumbwa na tama na tuna hulka ya kutotosheka. Nilikuwa nikijiambia kwamba yule mtu nitaendelea kumla hadi basi kwa sababu alionekana tajiri na mwenye roho safi.
 
 
Nilikaa karibu mwezi mzima nikirandaranda na pikipiki yangu huku nikiendelea kuchat na Hamid Al-Kadarush kwa kutumia facebook na wakati mwingine e mail. Mara nyingi Al-Kadarush alikuwa akiniuliza ninapendelea nini?.
 
Nilikuwa nikimjibu. “Napendelea kusoma vitabu, kuogelea, kupumzika kwenye fukwe na pia kuendesha pikipiki”
 
Yeye alinitumia ujumbe wake na kuniambia. “Mimi napendelea kuogelea na kupumzika kwenye fukwe za bahari kama wewe. Naona tumefanana kwa hilo”.
 
Akaendelea kuniambia “Pia napendelea kutembea nchi mbalimbali kama vile mashariki ya mbali, Iran, China, India na Bara Arab. Katika Afrika napendelea kutembea Afrika Mashariki ikiwemo Zanzibar, Afika Kusini Nigeria na visiwa vya Comoro.
 
Aliponieleza hivyo na mimi nikamtumia ujumbe na kumwambia. “Mimi sijatembea nchi yeyote zaidi ya Tanzania”
 
Akaniuliza “Hujawahi kufika Zanzibar”
 
Nikamjibu “Sijawahi kufika”
 
Akaniambia “Nina nyumba yangu pale Zanzibar itabidi nikupeleke siku moja nikija Afrika Mashariki”
 
Nikamjibu na kumwambia. “Nitashukuru sana”
 
Nikakumbuka siku za nyuma aliwahi kuniambia amenipenda na alitaka niwe mchumba wake lakini kauli ile hakuirudia tena. Sasa umbea wangu ndio ulionifanya nimuulize. “Kuna siku uliniambia utanichumbia, naona kimya kinazidi!”
 
Baada ya kimya kirefu akanitumia ujumbe na kunijibu.”Hilo jambo limo ndani ya akili yangu. Subiri ninajiandaa. Muda ukifika nitakuarifu”
 
Nilikuwa na lengo langu la kutaka kumla pesa. Niliona nikitia habari ya uchumba ndio ningeweza kumpatia zaidi. Nikamwambia. “Mimi tayari ni mchumba wako, unatakiwa uniletee pesa za matumizi”
 
Akanijibu. “Hujaniambia”
 
Nikaona alikuwa anaingia kwenye mtego wangu nikamwambia. “Sasa ndio nakwambia, nahitaji pesa za kutumia”
 
Akanijibu “Pesa zipo, usiwe na wasiwasi”
 
Hapo nilivunga nikajidai kumuuliza. “Wewe una mke na watoto? Kama unao wako wapi?”
 
Jibu lake lilikuwa “ Sina mke na sina watoto”
 
Nikamuuliza tena. “Una umri gani?”
 
Akanijibu. “Umri wangu ni x. Huwezi kuujua kwa sasa”
 
Nikaendelea kumuuliza. Una maana ni mkubwa sana au…?”
 
Baada ya kumuuliza hivyo hakunijibu tena. Nikajua alikuwa hapendi kuulizwa kuhusu umri wake. Siku ya pili yake asubuhi nilipoamka nikakuta ujumbe wake kwenye sfacebook akiniuliza nilivyoamka.
 
Sikumjibu mpaka nilipomaliza kuoga na kuvaa. Nikamjibu kuwa niliamka vyema. Tukaendelea kuchat hadi nikamuuliza. “Jana uliniambia huna mke na wala watoto, je unaye rafiki wa ike?”
 
Akanijibu “Kwa sasa sina rafiki labda wewe”
 
Nikamuuliza tena “Umesema kwa sasa huna rafiki, una maana zamani ulikuwa naye?”
 
Baada ya muda kidogo akanijibu “Nilikuwa naye rafiki wa kike nchini Nigeria”
 
Maswali yangu yakaendelea. “Kwanini mliachana”
 
Akanijibu “Alifariki kwa ajali ya gari mwaka jana, ndio nikawa natafuta rafiki mwingine”
 
Rafiki mwingine tena! Nikajiuliza kimoyomoyo. Nikataka kujua kama alikuwa anaendelea kutafuta ili nimzuie. Sikutaka tuwe wengi.
 
Nikamuuliza “Sasa rafiki si umeshanipata au bado unatafuta?”
 
Akanijibu “Mimi nataka rafiki mkweli na muaminifu ambaye atakuwa mchumba wangu”
 
Na mimi nikamwambia. “Ndio mimi. Na wewe pia uwe mkweli na muaminitu.
 
Al-Kadarush akayaacha yale maneno na kuniuliza “Unahitaji kiasi gani?”
 
Sikutaka kumtajia kiasi. Nilitaka akdirie yeye mwenyewe.
 
Nikamwambia. “Fikiria wewe mwenyewe”
 
Akanijibu tena. “Hapana. Sema wewe mwenyewe kiasi unachotaka”
 
Nikamwambia “Nitumie milioni tano”
 
Akaniuliza “Utatumia wa muda gani?”
 
Sikuwa na jibu. Nikamwandikia “Sijui”
 
“Basi kesho nitakutumia kwa njia ileile ya kwanza” Ulikuwa ndio ujumbe wake wa mwisho kunitumia kwa siku ile.
 
ITAENDELEA kesho na usikose uhondo huu hapahapa tangakumekuchablog
 
.

1 comment: