Thursday, September 3, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO, SEPT 03 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo ch Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu, kituo pia kinatoa kozi mbalimbali za kielimu na kiufundi ukiwemo Umeme na Computer. Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746


MWANANCHI
Rais Kikwete alisema hayo juzi katika hafla ya kuagana na wapiganaji na walinzi wa usalama iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Alisema ili kuimarisha ulinzi na usalama wa raia, Serikali inakamilisha mpango wa kufunga kamera hizo.
“Tutakomesha huu wizi wa kupora mali za watu kwa kutumia pikipiki kwa sababu kamera hizo zitakuwa zinaona sehemu zote za mji,” alisema Rais Kikwete.
Alisema Tanzania lazima iendelee kuwekeza ipasavyo katika ujenzi na uimara wa majeshi yake kila wakati.
“Hata katika mambo ya kiraia, msipowekeza katika usalama wa raia, wezi watawasumbua kila siku kwa kuvamia benki na kuiba pesa za wananchi.
“Kadri uchumi wa Tanzania unavyozidi kukua ni lazima majeshi ya ulinzi nayo yaboreshwe kwa sababu uchumi imara ni lazima ulindwe na jeshi imara,” alisema.
Rais Kikwete pia alisifia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kuiletea nchi sifa na heshima kubwa katika kipindi cha uongozi wake.
Alisema anaondoka madarakani akiwa na furaha kwa sababu ya mchango wake katika ujenzi mkubwa wa majeshi kwa miaka 10. Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na maofisa wa JWTZ, polisi, magereza, idara ya usalama wa Taifa na uhamiaji alisema: “Tumelinda amani na utulivu, katika mipaka ya nchi yetu.
Pia tumegundua gesi asili, hivyo ni lazima ilindwe vingivevyo nchi itakuwa na watu wa ajabu.
“Watu wanaiba samaki wetu katika bahari kuu na ndiyo maana tulizindua meli mbili mpya kubwa za MV Butiama na MV Msoga kwa ajili ya Kamandi yetu ya Maji.” Rais Kikwete alimkariri Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Winston Churchill ambaye alikuwa askari na alisema: “Uimara wa uchumi lazima ulindwe na uimara wa jeshi la nchi.
Uchumi wa nchi lazima ulindwe kwa upanga.” Rais Kikwete alisema: “Mwaka 2005, hatukuwa na ndege ya kijeshi iliyokuwa inaruka. Sasa tuna Jeshi la Anga lililo kamili. “Tumejenga kikosi cha mizinga na vifaru…pia tuna uwezo wa kuaminika.”
MWANANCHI
Watuhumiwa watatu wa uvuvi haramu wamekufa baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama katika Ziwa Victoria wakati wakipelekwa kituo cha polisi na askari waliowakamata.
Katika tukio hilo, bunduki ya kivita aina ya AK-47 yenye namba 30900 pia ilizama ziwani na askari wa kikosi maalum cha wapiga mbizi kutoka kitengo cha Marine na Bandari kulazimika kufanya kazi ya ziada kuiopoa majini.
Ajali hiyo ilitokea juzi baada ya mtumbwi huo kupigwa na dhoruba kali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo (pichani), alithibitisha tukio hilo lilitokea Agosti 18, mwaka huu, wakati askari hao walipokuwa wakisafiri na watuhumiwa hao katika mtumbwi uliozama wakati wakiwapeleka Kituo cha Polisi Kageye.
Aliwataja waliokufa katika tukio hilo kuwa ni, Dioniz Masatu (26), Revocatus William (26) na Stadius Audaxi (23), wote wakazi wa kjiji cha Kazilatemwa, wilayani Muleba na walionusurika ni Shabaan Maiga (45) na Fikiri Mafulu (46) ambao walijiokoa kwa kuogelea.
Kamanda Konyo alisema askari mmoja wa hifadhi aliogelea umbali wa zaidi ya mita 800 na kujiokoa, huku mwingine akishikilia mtumbwi uliopinduka na baadaye kuokolewa kabla haujazama.
MWANANCHI
Hotuba ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, imepondwa vikali na wasomi mbalimbali wasiofungamana na upande wowote kisiasa.
Juzi Dk. Slaa baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu kufuatia kujiweka kando kujishughulisha na Chadema kutokana na na chama hicho kumpokea Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa na kumpitisha kugombea nafasi ya urais akiviwakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ajitokeza hadharani na kutoa msimamo wake wa kustaafu siasa, huku akimtuhumu mgombea huyo kuwa alihusika moja kwa moja na sakata la Richmond, jambo ambalo limezua mjadala mkubwa kwa jamii.
Mkufunzi Msaidizi kutoka Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Godlisten Malisa, alipotakiwa na Nipashe kutoa maoni yake, alisema pamoja na kukubaliana na hotuba ya Dk. Slaa, lakini haikutolewa katika muda muafaka.
“Dk. Slaa ni kiongozi anayeheshimika kutokana na mchango wake mkubwa wa kuuimarisha upinzani na hasa Chadema, lakini alichokisema na hasa dhidi ya Lowassa kilipaswa kusemwa wakati wa mchakato wa kumpokea Chadema ama kabla ya kuingia kwenye kipindi cha kampeni,” alisema.
Malisa alisema, alipaswa kusema kabla, ili kuwasaidia watu ambao tayari wameshaamua kuwa na Lowassa na pengine kumpigia kura kutokana na ushawishi wa kampeni zinazoendelea, na hivyo hotuba yake hiyo kutokuwa ya msaada sana kwa wakati huu.
Kwa upande wa Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Alexander Makulilo, alisema uamuzi alioufanya Dk. Slaa ni haki ya kidemokrasia ya mtu kama sheria za nchi zinavyoeleza.
“Alichokifanya ni haki ya kidemokrasia kwa kuwa katiba ya nchi imeeleza mtu halazimishwi kuwa chama fulani bali ni utashi wake,” alisema Dk. Makulilo.
Aidha, alisema kitendo hicho hakina haja ya kupingwa kwa kuwa watu wengi ni wafuasi na siyo wanachama.
Naye Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Idara ya Mawasiliano, Danford Kitwana, alisema amesikitishwa na kitendo cha Dk. Slaa ambaye anaamimika kuwa na dhamira ya kulikomboa taifa na kuliletea mabadiliko baada ya kusema Chadema kimaadili kibaya kuliko chama tawala.
Kitwana alisema hana tatizo na mtazamo alioutoa Dk. Slaa, bali mashaka yanakuja kutokana na hotuba yake kuonyesha mafisadi wapo Chadema wakati inaaminika CCM ndicho chenye idadi kubwa ya mafisadi.
Profesa wa uchumi, ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Tawi la Dar es Salaam, Prosper Ngowi, amesema kujiuzulu kwa Dk. Slaa kumetokana na upeo na mtazamo alionao kiongozi huyo katika kutazama mambo.
Prof. Ngowi alisema uamuzi wa kujiweka pembeni na siasa ya vyama au kushiriki ni hiari ya mtu hailazimishwi.
NIPASHE
Wakati kampeni za mgombea urais wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kupitia Chadema zikiingia siku ya sita, chama hicho kimetangaza kuanza kampeni zake kwa kutumia helikopta (chopa) nne ambazo zitatikisa anga katika mikoa yote nchini kuomba ridhaa ya wananchi kukichagua katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, akiwahutubia maelfu ya wananchi, alisema kwa sababu Chadema imejipanga kushinda uchaguzi na usalama ni kazi ambayo ni ya wote.
Alisema Tanzania nzima kuna majimbo ya uchaguzi 265 ambako Zanzibar yako 50 na Tanzania Bara 215.
Aliongeza kuwa siku za kampeni ni siku 60 mgombea urais Ukawa hawezi kufikia majimbo yote hivyo Chadema imeunda vikosi vinne vya askari wa mapambano ambavyo vitaundwa na wabunge makini na baadhi ya viongozi ambao watafanya kampeni nchi nzima kwa kutumia helikopta nne.
Aliwataja wabunge hao watakaounda kikosi hicho wanaomaliza muda wao kuwa ni Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Ezekiel Wenje (Nyamagana), David Silinde (Momba), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu (Mbeya Mjini), John Mnyika (Ubungo), Halima Mdee (Kawe) na yeye (Mbowe) ambaye ni wa Hai.
“Vikosi hivi vitachana nchi nzima kwa kutumia helikopta kuanzia wiki ijayo, hivyo majimbo ambayo mgombea urais hatafika vikosi vitafika na maeneo mengine atakwenda mgombea mwenza,”alisema.
Mbowe alisema CCM wameshakuwa laini kama maini hivyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni lazima wataondoka madarakani.
NIPASHE
Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz, amemvaa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, akimuita kuwa ni mtu mwongo, mbinafsi na mpotoshaji mkubwa.
Rostam alieleza hayo katika taarifa yake jana kwa vyombo vya habari kuhusiana na tuhuma zilizotolewa na Dk. Slaa dhidi yake jijini Dar es Salaam juzi, alipozungumza na vyombo vya habari kuelezea mambo kadhaa zikiwamo sababu za kujiondoa ndani ya Chadema.
Dk. Slaa alidai kuwa mwaka 2009 baada ya kutaja orodha ya mafisadi 11 nchini katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mwembeyanga, Dar es Salaam,  Rostam alimpigia simu na kumtishia maisha.
Dk. Slaa pia alidai juzi katika mkutano wake na vyombo vya habari uliorushwa na vituo vitatu vya runinga kuwa Rostam anaifadhili Chadema.
Katika taarifa yake jana, Rostam alisema: “Nilimsikiliza Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Willibrod Slaa jana (juzi) alipokuwa akizungumza katika hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
“Kwa mara nyingine kama ilivyo hulka yake miaka yote, Dk. Slaa kathibitisha pasipo na shaka kwamba yeye ni mbinafsi na mpotoshaji mkubwa.”
“Nimesikitishwa na kushtushwa japo sikushangazwa hata kidogo na hatua ya Slaa ambaye sasa anaonekana kukubuhu kwa uzushi kutoa matamshi ya namna hiyo.
Sijapata hata mara moja kuwa na mawasiliano na Dk Slaa wakati wowote. Madai yake kwamba eti nilimtisha ni ya kupuuzwa na yasiyo na msingi hata kidogo,” alisema Rostam.
Rostam alieleza kuwa ni jambo lisiloingia akilini hata kidogo kwa watu wanaomfahamu Slaa kwamba anaweza kumtishia maisha na yeye akakaa kimya bila  kuchukua hatua ya kwenda polisi na kumshitaki halafu anakaa na jambo hilo kwa miaka yote hadi juzi ndipo alisema hadharani.
“Ili kuthibitisha madai yake hayo, namtaka Dk. Slaa kujitokeza hadharani na kutoa ushahidi wa jambo hilo,” alisema Rostam.
Huu ni uongo mwingine wa dhahiri. Namtaka Dk. Slaa kutoa ushahidi pia katika madai yake haya.
“Ni huyu huyu Dk. Slaa ambaye mwaka 2010 alizusha kwamba eti mimi, tukiwa na Rais Jakaya Kikwete na Edward Lowassa tulikutana katika hoteli ya La Kairo, Mwanza na kupanga njama za kumuibia kura zake za urais,” alisema na kuongeza:
“Wakati Slaa akitoa madai hayo ya uongo, mimi nilithibitisha kwamba wakati huo nilikuwa Afrika Kusini na Rais Kikwete akiwa Lindi huku Lowassa akiwa Arusha. Ni wazi kwamba tusingeweza kukutana La Kairo kama alivyodai yeye.”
Kwa mujibu wa Rostam, Dk. Slaa kuna wakati alimzushia hadi Rais Kikwete alipodai kwamba alisafiri kwa usiku mmoja kwenda China kumtoa mwanaye aliyekuwa amekamatwa na vyombo vya usalama, kisha kurejea Dar es Salaam usiku huo.
HABARILEO
Serikali imesaini mkataba wa makubaliano ya mkopo wa Dola za Marekani milioni 91.032 sawa na Sh bilioni 154.39 na Serikali ya Korea kwa ajili ya ujenzi wa daraja jipya la Selander jijini Dar es Salaam.
Akisaini mkataba huo, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim Korea, Yim Seong-hyeog alisema mradi huo ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania kwa kuwa eneo hilo lina foleni.
Salum alisema mradi huo utaleta manufaa makubwa kiuchumi kwa kuwa utapunguza msongamano ambao umekuwa ukiwachelewesha watu kwenye shughuli zao za kila siku.
Alisema mradi wote mpaka utakapokwisha utatumia Dola za Marekani milioni 110.033 (Sh bilioni 186.6).
“Kwa mradi mzima Korea imetoa asilimia 83 na Tanzania itatoa asilimia 17,” alisema Waziri huyo na kusisitiza kuwa mradi huo utarahisisha kupunguza msongamano.ningehangaa “Kwa mradi mzima Korea imetoa asilimia 83 na Tanzania itatoa asilimia 17,” alisema Waziri huyo na kusisitiza kuwa mradi huo utarahisisha kupunguza msongamano.
Pia alisema litawawezesha watalii kufika katika eneo hilo haraka kwa kuwa daraja hilo litajengwa karibu na Bahari ya Hindi.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale alisema baada ya kusaini mkataba huo, miezi sita ijayo watakuwa wameshampata mkandarasi wa ujenzi huo linalotegemewa kumalizika baada ya miaka miwili.
Mfugale alisema kutoka Coco Beach hadi Aga Khan itakuwa urefu wa kilometa saba kutoka Aga Khan hadi Barabara ya Upanga urefu kilometa 0.68 na urefu wa daraja lenyewe kupitia baharini ni kilometa 1.3.
Kwa upande wake, Seonghyeog alisema kutiliana saini kwa mradi huo kunaonesha ni jinsi gani nchi hiyo inavyothamini Tanzania. Aliongeza kuwa sio mara ya kwanza kwa nchi hiyo kuisaidia Tanzania kwani mpaka sasa mikopo waliyoitoa imefikia Dola za Marekani 363,980,883.
Alisema miongoni mwa miradi waliyoisaidia ni ya Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili awamu ya kwanza na ya pili, miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji Zanzibar na mingineyo.
HABARILEO
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kunyesha mvua nyingi za El–nino katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka huu.
Hivyo imetaka mamlaka zinazohusika kuchukua tahadhari kwani kuna dalili za wazi za kunyesha mvua hizo ikiwemo kuongezeka kwa joto katika Bahari ya Pasifiki zaidi ya ilivyokuwa mwaka 1997 kuliponyesha mvua hizo.
Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Dk Agness Kijazi alisema hayo jana wakati akitoa utabiri wa mvua za vuli kwa kipindi hicho na kueleza kuwepo kwa mvua za juu ya wastani na wastani katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua na baadhi ya maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua.
Kijazi alisema suala la kunyesha mvua za El-nino linatokana na kuongezeka kwa joto katika Bahari ya Pasifiki pamoja na Bahari ya Hindi, lakini mpaka sasa joto la Bahari ya Pasifiki liko juu kufikia nyuzi joto 2.5 juu ya joto lililokuwa wakati wa mvua hizo mwaka 1997.
Alisema lakini joto la Bahari ya Hindi bado la wastani hivyo kuendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa ili kuangalia iwapo joto hili litaongezeka kutakuwa na uhakika wa mvua hizo.
Dk Kijazi alisema kulingana na utabiri huo mvua zitaanza kunyesha kwa baadhi ya maeneo kuanzia wiki ya tatu ya mwezi huu hadi wiki ya nne ya Novemba na kumalizika Aprili mwakani.
Alisema katika maeneno machache ya kusini mwa nchi yatapata mvua chini ya wastani na mvua zitaanza mapema katika maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria na baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani kaskazini.
Akizungumzia baadhi ya maeneo, alisema ya ukanda wa pwani kaskazini katika maeneo ya Morogoro, Dar es Salaam, Tanga, Pwani na visiwa vya Unguja na Pemba, mvua inatarajia kuanza wiki ya mwisho ya mwezi huu na kuwa juu ya wastani na wastani.
Alisema kutokana na utabiri huo kuna hatari ya athari za unyevunyevu mkubwa wa udongo na kusababisha uharibifu wa mazao, ongezeko la magugu na magonjwa ya mimea pamoja na matumizi makubwa ya pembejeo hivyo kuongeza gharama za uzalishaji.
HABARILEO
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dk John Magufuli, amewataka Watanzania kuwa makini wasije kudanganywa na matapeli wa kisiasa watakaokuja na ahadi za uongo.
Akizungumza katika Uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara jana, Dk Magufuli alisema matapeli hao watakuja na ahadi nyingi, akawataka wananchi wawasikilize na kuwapima kwa kauli na sifa zao kwa kuwa kuahidi ni rahisi kuliko kutekeleza.
“Tusije tukadanganywa na matapeli wa kisiasa, wakinamama mnafahamu matapeli wa mjini walivyo na maneno matamu. Maendeleo ni changamoto na yataletwa na sisi Wanamtwara,” alisema.
Miongoni mwa matazamio ya Dk Magufuli ya Serikali atakayoiongoza kama akichaguliwa kuwa rais, ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mtwara kupitia Songea mpaka Mbambabay, baada ya kuboresha Bandari ya Mtwara na kuwa ya kisasa kama ya Dar es Salaam.
Alisema bandari itaboreshwa ili pia iongeze ajira kwa wakazi wa mji huo huku mizigo ya nchi za Zambia na Malawi, ikipitia mkoani humo.
Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Tano atakayoiongoza, itajielekeza zaidi katika kukuza uchumi kwa watu. Akizungumza katika mikutano mikubwa na midogo katika wilaya za Newala, Tandahimba na Mtwara Vijijini kuhusu zao la korosho, Dk Magufuli alisema katika uongozi wake, lazima korosho ilete uchumi mzuri kwa wakazi wa Mtwara.
“Mimi shahada yangu ya tatu (PHD) nimesomea korosho. Hakuna anayeweza kunidanganya. Korosho siyo tu tunda la ndani, bali hata ganda ni uchumi kwa kuwa linatengeneza gundi na dawa ya kuzuia kutu,” alisema Dk Magufuli.
Alisema korosho ya Tanzania ni tofauti na korosho nyingine duniani, kwa kuwa yenyewe huanza kuvunwa wakati maeneo mengine duniani wamemaliza kuvuna.
Kwa mujibu wa Dk Magufuli, katika uongozi wake hataruhusu korosho kuuzwa ghafi nje ya nchi, bali Serikali itahakikisha kunajengwa viwanda vitakavyotumia malighafi ya korosho ili zao hilo lipande bei.
Kuhusu tatizo la stakabadhi ghalani ambalo limekuwa likilalamikiwa na wakulima, Dk Magufuli alisema wamuachie yeye atahakikisha kero ya mfumo huo inaondoshwa na wakulima hawadhulumiwi haki yao.
Akiwa Mtwara vijijini, alisema Tanzania imegundua gesi mkoani Mtwara, hivyo akaahidi kuhakikisha gesi hiyo inaanza kunufaisha wakazi wa Mtwara kabla ya kunufaisha wananchi wa mikoa mingine.
Katika hilo, alisema atasimamia ujenzi wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo, ili vitoe ajira kwa vijana wa Mtwara, ambao watakuwa wamesoma katika shule mbalimbali, ambazo kuanzia mwakani kutoka shule ya awali mpaka kidato cha nne, itakuwa bure.
Awali kabla ya kutoa ahadi hizo na zingine nyingi katika sekta mbalimbali, Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, William Lukuvi, alisema Dk Magufuli ndiye mgombea pekee wa urais kwa sasa aliyetembea kwa barabara umbali mrefu.
Kwa mujibu wa Lukuvi, Dk Magufuli ambaye amemaliza awamu ya kwanza ya ziara ya kampeni katika mikoa saba, kutoka Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe, Ruvuma na kumalizia Mtwara jana kwa barabara, pia ndiye mgombeapekee wa urais aliyechaguliwa katika mchakato bora na ulio wazi.
MTANZANIA
Masheikh sita wa Tanzania waliochukuliwa mateka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wameachiwa huru usiku wa kuamkia jana.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Liberata Mulamula, alisema Balozi wa Tanzania nchini DRC kwa sasa yupo njiani kuelekea katika mji mkuu wa nchi hiyo, Goma kwa ajili ya kuwaona mateka hao.
Alisema taarifa za kutekwa watu hao zilitolewa mwanzoni mwa Agosti mwaka huu ambapo Serikali ilifanya juhudi ya kufuatilia na kufanya uchunguzi juu ya taarifa hizo.
Mulamula alisema  inasemekena watu hao wa taasisi ya kuhubiri dini ya Kiislamu walitekwa na kikundi cha waasi ambapo hadi sasa hakijajulikana.
Alisema watekaji wao walidai wapewe kiasi cha dola za Marekani 40,000 (sawa na Sh milioni 128.7 ) ili wawaachie Watanzania hao huru ambapo waliwaomba kupunguziwa hadi kufikia dola 20,000.
“Nchi yetu haijawahi kutokea kukamatwa mateka, lakini tunaipongeza Serikali ya DRC kulifuatilia hili na kutupatia taarifa,” alisema Mulamula.
Aliwataka wananchi wanaokwenda nchi za ugenini kutoa taarifa katika ubalozi au Wizara ya Mambo ya Ndani ili waweze kutambua haraka linapotokea tatizo kama hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya nje Zanzibar, Silima Kombo Haji, alisema watekaji hao walitumia ujanja wa kupiga simu kwa ndugu zao pamoja na watu wa karibu na Kijiji cha Goma.
Alisema juzi watekaji hao walikuwa wakipiga simu wakisisitiza kuwa muda umekwisha, hivyo fedha hizo zipelekwe haraka kabla hawajawadhuru.
MTANZANIA
Siku moja baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, kutangaza kuachana na siasa na kushusha tuhuma kwa chama chake, maaskofu wa Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), imebainika kuwa kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari alikutana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwamo Dk. Harison Mwakyembe.
Dk. Slaa ambaye alimshambulia mgombea urais wa Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa, alikiri kukutana kwa takribani saa mbili na Dk. Mwakyembe akisema lengo lilikuwa ni kujikumbusha taarifa ya Richmond na ndipo alipopata ujasiri wa kutamka aliyoyasema.
“Hivi kukaa kwangu na Mwakyembe kuna kosa gani? Je, ni dhambi? Watanzania sijui kwanini huwa hawataki kuelewa mambo, mimi nilionana na Mwakyembe kabla ya kuanza mkutano wangu na waandishi wa habari, na tulikaa kuanzia saa nne asubuhi hadi sita mchana.
“Katika suala la Richmond hakuna ‘source ya information’ (chanzo cha habari) zaidi ya Mwakyembe na ndiyo maana nilikaa naye…nilirudia kufanya utafiti.
“Sasa anayeshangaa Dk. Slaa kuongea na Mwakyembe nadhani kwa bahati mbaya akili yake haina upeo wa kutosha, kwa sababu unapofanya ‘research’ (utafiti) lazima urudi kwenye ‘source’ (chanzo) ya hilo jambo na ndiyo maana nilikuwa na jeuri ya kuzungumza kwa kujiamini,” alisema Dk. Slaa.
 Dk. Slaa pia alikiri kusindikizwa na usalama wa taifa akisema alifanya hivyo kwa sababu tangu amejiuzulu ukatibu mkuu wa Chadema, amekuwa akitishwa hivyo alitoa taarifa polisi kwa ajili ya kulindwa.
“Nikiwa pale mkutanoni nilihoji kama polisi wapo ili tu watu wajue kuwa pale kuna usalama, nilisema kabisa kwamba hakuna kipindi nilichopata vitisho kama hiki, kuliko hata wakati nilipotangaza ‘list of shame’ pale Mwembeyanga, hivyo nilitoa taarifa polisi ili nilindwe.
“Tangu nimejiuzulu ukatibu mkuu, nyumba yangu imekuwa ikilindwa na polisi. Polisi ni maadui zetu, lakini kuna wengine ni wazuri kwa ajili ya usalama,” alisema Dk. Slaa.
Kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, baadhi ya taarifa zilizokuwa zikizagaa zilidai kuwa umeandaliwa na watu wa CCM na Serikali.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment