Thursday, September 17, 2015

KAMATI ZA MAZINGIRA KOROGWE ZAPEWA SOMO



Tangakumekuchablog
Korogwe, KAMATI za mazingira kata na vijiji Wilayani Korogwe Mkoani Tanga, zimeshauriwa kujipanga ili kutokomeza uvunaji haramu wa miti katika misitu Wilayani humo.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa Mtandao wa Tumaini kijiji cha Vugiri Tarafa ya Bungu jana, Mratibu wa mradi wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania kanda ya kaskazini (MJUMITA), Shaban Hamis, alisema iko haja ya kuongeza nguvu kulinda rasilimali ya misitu.
Alisema uvunaji haramu wa misitu umepungua lakini iko haja ya kuzidisha doria katika baadhi ya  maeneo na hivyo kutakiwa kuacha kubweteka jambo ambalo litawapa nguvu majangili wa ukataji miti katika  misitu.
“Tumekutana hapa kwa pamoja na wagombea nafasi za ubunge na udiwani kupeana elimu ya kulinda rasilimali zetu ndani ya misitu-----hii ni pamoja na kukomesha uvunaji haramu wa miti” alisema Hamis na kuongeza
“Nina imani wagombea hawa katika kampeni zao wataiweka sera ya utunzaji wa mazingira na kupinga uvunaji ovyo wa miti kwani  wanakutana na watu wengi kwenye mihadhara ya kujinadi” alisema
Kwa upande wake mlinzi wa msitu wa Vugiri, Jarnert Thomas, ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii, kuwapatia vifaa ya ulinzi ili kuweza kukabiliana na majangili wa uvunaji haramu wa misitu.
Alisema wamekuwa wakifanya kazi zao katika mzingira magumu zaidi ya kuwa na marungu na koti la kujizuia na baridi na mvua jambo ambalo majangili badala ya kuwafukuza wao ndio wanawafukuza walinzi.
“Walinzi katika hifadhi ya misitu tunateseka hatuna vitendea kazi zaidi ya marungu na makoti ya kujikinga na baridi----hii inatuwia vigumu zaidi usiku badala ya kumfukuza mwizi anakugeukia wewe kukufukuza” alisema Thomas
Akifunga mkutano huo mkuu, Kiongozi na  Mtetezi wa wanakijiji wa Mtandao wa Tumaini, Revocatus Njau, alikitaka kikundi hicho kuimarisha umoja wao na kuyafikia malengo yao waliojiwekea.
Alisema mbali ya shughuli za uuzaji wa miche na utunzaji wa mzingira pia kikundi hicho kinatakiwa kubuni vyanzo vya kitalii ili kuwezesha wageni kufika kwa wingi na kuweza kuingiza pesa.
“Muko na fursa nyingi za kuweza kujiimarisha na kuwa kikundi cha mfano-----hapa muko na msitu mkubwa wenye ndege na wanyama ambao huwezi kuwaona sehemu nyengine” alisema Njau
Aliwataka kuitumia elimu ambazo huwa wanapatiwa mara kwa mara na Mtandao wa Jamii wa Uismamizi wa Misitu Tanzania  jambo ambalo litawafanya vikundi vyengine kuiga kutoka kwao.
                                               Mwisho



 Mwanachama wa kikundi cha Mtandao wa Matumaini kijiji cha Vugiri Tarafa ya Bungu Wilayani Korogwe Mkoani Tanga, Jarnert Thomas, akilalamika juu ya uharibifu wa mazingira msitu wa Vugiri jana wakati wa mkutano mkuu wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) jana kijijini hapo.

 Mwenyekiti wa kikundi cha ufugaji nyuki cha Matumaini kijiji cha Vugiri Tarafa ya Bungu Wilayani Korogwe Mkoani Tanga, Gress Mshuza (kulia) , akipokea mzinga wa kufugia nyuki  kati ya miwili iliyotolewa na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA)  kutoka kwa Kiongozi Mtetezi wa Wanakijiji mradi wa Haki katika Misitu , Revocatus Njau (kulia) halfa iliyofanyika jana.

No comments:

Post a Comment