Tuesday, September 1, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO NA MAGAZETI YA LEO, SEPT 01 TZ

Uchumbazi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha elimu cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo pia kinatoa kozi mbalimbali za kielimu na kiufundi na kutoa Certeficate. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746

MWANANCHI
Baada ya kimya cha zaidi ya mwezi mmoja na kutoonekana hadharani, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa anatarajia kuzungumza na vyombo vya habari leo nane mchana jijini hapa.
Dk Slaa aliyekuwa anatajwa kuwa angepeperusha bendera ya vyama vinavyounda Ukawa kwenye kinyang’anyiro cha urais alikuwa adimu kwenye shughuli za chama hicho tangu aliyekuwa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa alipojiunga na Chadema Julai 28 akitokea CCM.
Dk Slaa anatarajia kuzungumza kuanzia saa 7.00 mchana na mkutano wake huo utarushwa moja kwa moja vituo vya runinga na redio.
Mara ya mwisho Dk Slaa alizungumza na Mwananchi Agosti 11 na kuikana akaunti ya Twitter yenye jina lake ambayo imekuwa ikitoa matamko mbalimbali kumhusu.
Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Dk Slaa kuzungumza na gazeti hili tangu alipojitenga na shughuli za Chadema, ikielezwa kuwa anapumzika na angejiunga nao mbele ya safari.
Matukio makubwa ambayo ameyakosa ni pamoja na kutambulishwa kwa Lowassa na kukabidhiwa kadi, kuchukua fomu za chama na kuzirudisha, kuchukua fomu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuzirudisha na uzinduzi wa kampeni.
Mbali na kukanusha kumiliki na kuendesha akaunti hiyo, Dk Slaa alirudia kauli yake aliyokuwa ameitoa kwa gazeti hili wiki moja kabla, kuwa angejitokeza kutoa msimamo wake muda muafaka utakapofika.
“Subira yavuta heri, sasa ili uipate hiyo heri unatakiwa kuvumilia. Kwa hiyo wakati ukifika nitazungumza tu na Watanzania,” alisema.
Alipoulizwa ni wapi alipokuwa wakati huo, alisema yupo Dar es Salaam anapumzika, lakini akasema yeye na mke wake, Josephine Mushumbusi walikuwa wanatarajia kusafiri kwenda nje ya nchi kwa wiki moja. , ingawa hakuweka wazi nchi wanayotarajia kuitembelea.
MWANANCHI
Mgombea urais wa Chadema kwa mwavuli wa Ukawa, Edward Lowassa amesema akichaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano atatumia fedha itakayopatikana katika uzalishaji wa gesi kama sehemu ya kutekeleza ahadi ya elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi Chuo Kikuu ambayo ipo katika ilani ya uchaguzi ya Ukawa, huku akisisitza, “Msiogope.”
Lowassa alisema mbali na gesi atatumia fedha zitakazopatika katika zao la pamba huku akihoji zilivyotumika fedha ambazo serikali ya awamu ya nne imekopa katika nchi wahisani.
Kivutio kingine katika mkutano huo alikuwa Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye ambaye alitumia mtindo wa kuwauliza wananchi, “CCM” na wao kujibu “Ni shiiiida”, kueleza mambo matatu yaliyofanywa na serikali ya CCM na kusababisha watanzania waishi kwa matabaka.
“Tumetengeza ilani kiboko ambayo ndani ya miaka mitano Tanzania yetu itabadilika, lazima tupunguze tabaka kati ya tajiri na masikini kwa uchumi wa pamba, chai, dhahabu na gesi kwanini tushindwe.
Mkitupa ridhaa na Mungu akikubali tukakwenda kasi na tutakuwa na maendeleo. Lowassa alisema akiwa rais kuanzia Januari mwakani wanafunzi hawatalipa chochote na elimu itakuwa bora, atahakikisha walimu wanalipwa madai yao yote, sambamba na watumishi wengine wa serikali.
Akizungumza katika mkutano huo Sumaye alisema Watanzania wamepata shida mpaka kufikia wakati wanaamini shida ni sehemu ya maisha yao, huku akisema nchi ya Libya iliingia katika matatizo kwasababu utawala uliokuwepo ulikataa kuwapisha wengine kuongoza nchi na kukandamiza watu.
HABARILEO
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amesema mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa anasahau haraka na kuanza kunadi miradi ambayo imeshaanza kujengwa na Rais Jakaya Kikwete kupitia Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akitoa mfano, Sitta alisema anamshangaa Lowassa kusema atajenga Reli ya Kati akichaguliwa kuwa rais wakati mradi huo ulishaanza maandalizi yake na sasa utawekewa jiwe la msingi na Rais Kikwete Septemba 15, mwaka huu, hafla itakayofanyika eneo la Soga Mpiji wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Aidha, amesema wananchi hawawezi kukaa kimya bila kuhoji suala la kashfa ya Richmond, kama alivyodai Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kwa sababu tu baada ya Lowassa kujiuzulu, kuna ufisadi mwingine ulitokea.
Sitta alisema mbali ya mradi wa Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, ujenzi wa reli nyingine ya Kusini kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay mkoani Ruvuma, utaanza kabla Rais Kikwete hajaondoka madarakani.
“Sijui hawa wenzetu waliotoka CCM sijui wana matatizo ya kusahau… wanataja miradi ambayo Rais Kikwete anaitekeleza. Lowassa anataka kujenga Reli ya Kati ipi? Yaani mgombea urais amesahau kuwa reli hii inajengwa na JK?” Sitta.
Kuhusu mradi huo, alisema baada ya Rais kuweka jiwe na msingi, ujenzi wa reli hiyo utafanywa na Kampuni ya China Railway Construction kwa miaka minne na nusu kwa gharama ya Sh trilioni 16.
“Hii kampuni ilikuwa inajenga reli kama hiyo ya kiwango cha juu, kati ya Addis Ababa hadi Djibouti, sasa wamemaliza ujenzi na Septemba 9, mwaka huu, baadhi ya vifaa vya ujenzi vitawasili nchini na nitavipokea pale bandarini,” alisema Sitta.
Alisema mipango ya ujenzi wa reli hiyo haijaanza sasa, kwani ilikuwepo kwa miaka mingi nyuma chini ya Waziri Dk Harrison Mwakyembe, na kuongeza kuwa mpango ni kujenga reli ya kisasa itakayowezesha treni kusafiri kwa kilometa 120 kwa saa na kubeba tani milioni 25 kwa mwaka.
“Kiwango hiki cha bidhaa si kidogo ni kikubwa sana na hapa ndipo linapokuja wazo la kujenga Bandari ya Bagamoyo kwani Bandari ya Dar es Salaam itazidiwa sana maana nchi nyingi zitapitisha mizigo yao nchini kutokana na urahisi wa kusafirisha mizigo kwa njia ya reli ya kati,” alisema.
Kuhusu Reli ya Kusini, alisema ujenzi wa reli hiyo ya kisasa pia utaanza kabla ya Rais Kikwete kuondoka madarakani na itaanzia Mtwara hadi katika Bandari ya Mbamba Bay ili kusafirisha rasilimali za chuma, makaa ya mawe na gesi, akisema hatua hiyo itakuza uchumi wa wananchi wa kusini ndani ya miaka minne ijayo.
Akizungumzia kuhusu kashfa ya Richmond iliyomfanya Lowassa ajiuzulu nafasi ya Uwaziri Mkuu Februari 2008, Sitta alisema si sawa kwamba wananchi wasihoji kashfa hiyo kwa vile baada ya Lowassa kuondoka madarakani, ufisadi mwingine ulitokea.
Alikuwa akijibu hoja ya Sumaye kwamba kwa nini suala la Richmond linahojiwa wakati zipo kashfa nyingine nyingi, ziliibuka baada ya Lowassa kujiuzulu, akizitaja za mabehewa mabovu, kusafirishwa kwa twiga kwenda nje ya nchi, kuchotwa kwa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow na nyinginezo.

HABARILEO
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mbunge wa zamani wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi amesema Tanzania inahitaji rais na sio mfano wa rais, huku akimmwagia sifa Mgombea Urais wao, Dk John Magufuli kuwa ni mwenye uwezo wa kufanya kazi, anayetimiza ahadi na anayependa watu.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofurika watu kwenye Uwanja wa Majimaji mjini hapa jana, Dk Nchimbi alisema CCM ina ushahidi wa kazi alizofanya Dk Magufuli na ahadi zake zinavyotekelezeka kwa heshima.
Alitoa mfano wa namna alivyomuomba barabara za lami, alipokwenda kumpigia kampeni katika jimbo lake mwaka 2005, na kuwahoji wananchi kuwa zimejengwa au hazikujengwa, huku wananchi wakiitikia zimejengwa.
“Tunahitaji rais mwenye uwezo wa kufanya kazi, anayetimiza ahadi, anayependa watu na huyo si mwingine ni Dk John Magufuli. “Magufuli angekuwa hana uwezo mnanifahamu, nisingesimama jukwaani,” alisema kada huyo aliyelelewa vyema na CCM na kuongeza kuwa Tanzania inahitaji rais na si mfano wa rais.
Awali, wabunge wawili waliopita bila kupingwa, Deo Filikunjombe wa Ludewa na Jenista Mhagama wa Peramiho, walionesha mapokezi ya aina yake kwa Dk Magufuli. Juzi jioni katika mkoa wa Njombe, Filikunjombe alikwenda katika mapokezi ya Dk Magufuli akiwa na gari lake aina ya Toyota Land Cruiser V8, likiwa na namba mbili tofauti.
Namba ya mbele ya gari la mbunge huyo imeandikwa MAGUFULI na namba ya nyuma, imeandikwa HAPA KAZI TU. Akizungumza katika kata mbalimbali za jimbo la Ludewa, Filikunjombe alisema moja ya maeneo ambayo alisimama bungeni na kuisifu Serikali ni Wizara ya Ujenzi, ambayo ilikuwa ikiongozwa na Dk Magufuli.
Alisema kwa heshima aliyopata ya kupita bila kupingwa katika jimbo hilo, ameomba wananchi hao kuhakikisha wanampa kura zote Dk Magufuli ili wagombea wengine wa urais wapate sifuri.
Katika Jimbo la Peramiho, ambako Mhagama amepita bila kupingwa, maji ya chupa yanayouzwa kwa Sh 500 aina ya Mbinga Drinking Water, yalikuwa na picha za Dk Magufuli. Chini ya picha ya Dk Magufuli katika chupa hiyo yenye alama ya vema, kumeandikwa ‘Chagua Magufuli, ndio jembe langu CCM Mbele kwa Mbele.’
Pembeni ya picha ya Dk Magufuli, kuna picha ya Leonidas Gama anayegombea Jimbo la Songea Mjini, Joseph Mhagama anayegombea jimbo jipya la Madaba na Jenista ambaye ameshapita bila kupingwa.
Akizungumza katika jimbo hilo, Dk Magufuli alimsifu Mhagama kwa uchapakazi aliouonesha baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri, kiasi cha kumshawishi Rais Kikwete amteue kuwa Waziri. Dk Magufuli alisema kuna mawaziri wengine wamekaa zaidi ya miaka 20 katika nafasi ya Naibu Waziri tu bila kupanda, mpaka wameamua kuhamia upinzani.
Akiwa katika Jimbo la Nyasa katika Kata ya Lituhi mkoani Ruvuma, Dk Magufuli alimsifu mbunge aliyepita, marehemu Kapteni John Komba kwa kupenda watu na kuleta maendeleo na kuahidi kuwa ili kumuenzi atahakikisha analeta maendeleo katika jimbo hilo.
Dk Magufuli pia alimuombea kura mgombea ubunge wa Nyasa, Stella Manyanya ili awe mbunge wao na akamkumbusha ahadi aliyotoa ya maendeleo kwa jimbo hilo. Mgombea huyo wa urais aliendelea kunadi sera na Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020, huku akitangaza kufutwa kwa ada kuanzia shule za msingi mpaka kidato cha nne, kukomesha ‘kamatakamata’ kwa wafanyabiashara wadogo, wakiwemo bodaboda na mama ntilie.
NIPASHE
Mwanafunzi, Zakia Juma, amefariki dunia na mwingine, Zakia Selemani, amejeruhiwa vibaya baada ya kugongwa na gari la polisi eneo la Misugusugu, Kibaha, mkoani Pwani.
Kufuatia tukio hilo lililotokea jana saa 1:00 asubuhi, polisi walilazimika kurusha risasi hewani na mabomu ya machozi katika eneo la ajali  ili kuwatuliza wananchi waliokuwa na hasira ambao walikuwa wakizuia magari na kuchoma matairi barabarani kushinikiza kuwekwa kwa matuta katika barabara hiyo ya Morogoro eneo la Misugusugu.
Wananchi hao walichukua hatua hiyo wakilalamika kuwa ajali zimekuwa zikitokea mara kwa mara katika eneo hilo. Aidha, walisema wamekasirishwa na ajali hiyo kwasababu  eneo walilogongewa wanafunzi hao ilikuwa ni kwenye kivuko cha waenda kwa miguu lakini dereva wa gari la polisi hakujali na kuamua kupita akiwa mwendo kasi bila kufuata sharia za usalama barabarani.
Hata hivyo, polisi walifanikiwa kuwatawanya wananchi hao.
Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani, Jafari Ibrahim, alisema polisi baada ya kutuliza ghasia hizo walikaa kikao na kamati ya ulinzi na usalama ikiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo na meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Pwani na kukubaliana  kuweka matuta katika eneo hilo ili kupunguza ajali zinazodaiwa kutokea mara kwa mara.
Kwa mujibu wa mashuhuda, ajali hiyo ilitokea wakati wanafunzi hao walipokuwa wakivuka barabara kuelekea Shule ya Msingi Misugusugu ambako wanasoma.
Wakizungumza kwa hasira, wananchi wa eneo hilo ambao walikuwa wakichoma matairi barabarani kuzuia magari yanayopita barabara hiyo ya Morogoro yasiendelee na safari wakishinikiza kuwekwa matuta katika eneo hilo, walisema wamesikitishwa na gari la polisi kugonga wanafunzi hao.
“Polisi ni walinzi wetu lakini wao ndiyo wanaotuua, maskini watoto hawa walikuwa wakivuka katika kivuko cha waenda kwa miguu lakini polisi bila kujali wakawagonga wakati sheria inasema lazima gari zisimame  ili kupisha waenda kwa miguu”, alisema Hussen Hamisi, mkazi wa Misugusugu.
Shuhuda mwingine, Joyce Aloyce, alisema alikuwa anawahi kazini asubuhi na alipofika katika kivuko hicho walisimamisha magari ili wapite na magari yote yalisimama isipokuwa la polisi lililokuwa linatokea Mlandizi liliyapita magari yale na kuwagonga watoto hao waliokuwa wakivuka barabara.
Msemaji wa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi,  Lucy Semindu, alisema wamepokea mwili wa mwanafunzi Zakia Juma na majeruhi Zakia Seleman ambaye hali yake ni mbaya.
“Hali ya Zakia Selemani ni mbaya na ameumia kifua na mguu wa kulia juu ya paja, muda huu anafanyiwa vipimo vya kifua yuko chumba cha X-ray”,  Semindu
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Misugusugu, Mwalimu Mnubi, alithibitisha kuwa wanafunzi hao waliogongwa ni   wa shule yake na kuwataja kuwa ni Zakia Juma ambaye anadaiwa kufariki papo hapo na  Zakia Sulemani ambaye amejeruhiwa vibaya.
Alisema wanafunzi hao ambao ni wa familia moja, marehemu alikuwa anasoma darasa la tatu na aliyejeruhiwa anasoma darasa la nne.
Kamanda Ibrahim, alisema mwili wa mtoto aliyefariki umehifadhiwa katika Hosptali ya Tumbi Kibaha na aliyejeruhiwa amelazwa katika hospItali hiyo kwa ajili ya matibabu na hali yake bado ni mbaya.
Alisema ajali hiyo ambayo imehusisha gari la polisi Defender Landrover ilitokea barabara ya Misugusugu kulekea Kibaha Maili Moja wakati gari hilo likisambaza askari katika vituo vyao vya kazi.
Kamanda Ibrahim alisema chanzo cha ajali hiyo kinachunguzwa na kwamba dereva wa gari hilo ambaye ni polisi anashikiliwa hadi uchunguzi utakapokamilika ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
Aliwasihi wananchi wanaojichukulia sheria mkononi kuacha kufanya hivyo, badala yake wafuate taratibu kufikisha malalamiko yao.
NIPASHE
Serikali imewatoa hofu wananchi kuhusu Sheria ya Makosa ya Mtandao inayoanza kutumika rasmi leo kuwa haijatungwa kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, bali kwa maslahi mapana ya taifa na kuleta maendeleo ya nchi, kujenga uchumi imara na kupambana na wahalifu.
Aidha,  serikali imewasisitizia wananchi kutumia vizuri mitandao kwa faida yao na taifa na kujiepusha na mambo ambayo yanakatazwa na sheria hiyo  ili kutoingia matatani.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Makame Mbarawa, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu kuanza rasmi kutumika kwa sheria hiyo na ya miamala ya kielektroniki.
“Serikali imejiridhisha baada ya kufanya maandalizi yote muhimu ikiwamo kutoa elimu kwa umma na kujenga uelewa kwa watekeleza wa sheria hizi. Sasa sheria hizi zitaanza kutumika rasmi Septemba 1 (leo),”  Prof. Mbarawa.
Alisema sheria hiyo itasaidia kupambana na uhalifu kwenye mtandao kutokana na watu wengi kutumia vibaya mtandao na kuwalaghai watu kutuma fedha ama kuiba katika mabenki.
Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, watu wanaosambaza meseji za uchochezi ama za uongo kwa watu wengine ni kosa la kisheria na kufanya hivyo watakumbana na adhabu kali.
Alisema mtumiwaji wa meseji za aina hiyo akifuta pasipo kusambaza kwa watu wengine sheria hiyo haitamwadhibu wala kumhusu.
“Sehemu ya kifungu cha sheria ya makosa ya mtandao, kifungu cha 16 kinaeleza: mtu   atakayechapisha   taarifa au data katika picha, maandishi, alama au katika namna nyingine yoyote katika mfumo wa kompyuta, huku akijua kwamba taarifa au data hizo ni za uongo, zinapotosha, zisizo sahihi, na kwa lengo la kudhalilisha, kutishia, kuudhi au kwa njia nyingine au kudanganya umma au kuchochea utendaji wa kosa, atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atalipa faini isiyopungua Sh. milioni tano au kutumika kifungo kisichopungua miaka mitatu au vyote kwa pamoja,” alisema.
Prof.   Mbarawa alitoa wito kwa wananchi wazingatie matumizi salama na sahihi ya huduma za mawasiliano na mitandao kwa manufaa ya kila mtu na kwa maendeleo ya taifa na kuepuka matumizi yasiyo sahihi.
NIPASHE
Mwanaume mmoja ambaye amejulikana kwa jina moja la Mandela, ameuawa kikatili  ndani ya hoteli moja maarufu jijini Arusha, huku baadhi ya viungo vyake vya kichwa, sehemu za siri, viganja vya mikono na matiti vikiwa vimenyofolewa.
Akizungumza katika eneo la hoteli hiyo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Levolosi, Sauda Haruna, alisema alipata taarifa juu ya kifo hicho kutoka kwa mjumbe wa serikali ya mtaa, Mary Shayo na alipofika alishuhudia mtu huyo akiwa ameuawa kikatili.
“Huu ni unyama aliofanyiwa huyu mtu, wito wangu kwa wenye hoteli wahakikishe wanaandikisha wageni wao taarifa muhimu ili kuwatambua linapotokea tatizo kama hili,” alisema.
Alisema imekuwa vigumu kufahamu marehemu ni mkazi wa wapi kwani hakuandika jina lake kamili na hata namba ya simu aliyoandika ikipigwa anapokea mtu mwingine na anashangaa kuulizwa taarifa asizofahamu.
Mmoja wa wapangaji waliokuwa katika hoteli hiyo (jina linahifadhiwa), alisema yeye ana ndugu yake walilala katika hoteli hiyo jirani na chumba cha marehemu, lakini hawakusikia chochote na asubuhi walishangaa kuambiwa chumba cha jirani kuna mauaji yamefanyika. Alisema ni vema hoteli kubwa kama hiyo wafunge kamera ili tukio linapotokea iwe  rahisi kuwafahamu wahusika.
“Muuaji anaonekana ni mtaalam wa kuua sababu hakuna hata damu iliyotapakaa chumbani jambo ambalo linashangaza na Marehemu alivuliwa nguo zote amekutwa kama alivyozaliwa,” alisema. Mmoja wa watu waliokuwa eneo la tukio ambaye hakutaka kutaja jina lake, alidai kuwa marehemu huyo anafahamika ni mkazi wa Mianzini na muuza mabegi ila jina lililoandikwa katika kitabu cha wageni  siyo la kweli.
Hata hivyo, jitihada za Nipashe kumpata msemaji wa hoteli hiyo zilishindikana baada ya polisi kusomba wafanyakazi wote na kuwapeleka kituoni kwa mahojiano.
Mwili huo ulitolewa katika hoteli hiyo jana saa 5:45 asubuhi na kuchukuliwa  na gari la polisi lenye namba za usajiliT.422 AGA kupelek wa kuhifadhiwa hospitalini katika chumba cha kuhifadhia mwili, huku umati mkubwa wa watu ukiwa umezingira eneo la tukio.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas (Pichani) , amethibitisha tukio la mauaji hayo ya kinyama na kueleza kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha aliyechukua chumba ni mtu mwingine na  aliyefariki ni Mandela, mfanyabiashara wa mabegi soko kuu.
Alisema marehemu anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 na upelelezi unaendelea ili kubaini waliohusika na mauaji hayo.
NIPASHE
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imepitisha rufaa 13 zilizokuwa zimewekewa pingamizi za kugombea ubunge katika baadhi ya majimbo nchini yakiwamo ya Ludewa la Deo Filikunjombe (pichani kushoto), mkoani Njombe na Bumbuli mkoani Tanga linalotetewa na Januari Makamba.
Ofisa wa Tume, Athumani Masesa, alisema uamuzi huo umetolewa baada ya kusikiliza rufaa 40 kati ya 56 zilizowekewa pingamizi. Makamba na Filikunjombe ni miongoni mwa wagombea waliotarajiwa kupita bila kupingwa baada ya kuwawekea pingamizi wapinzani wao, hasa kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Alisema tume hiyo ilitulipia mbali pingamizi nyingine  27 baada ya kupitia maelezo na kubaini kuwa hazikuwa na hoja za msingi za kuishawishi .
Aliyataja majimbo mengine kuwa ni Bumbuli ambalo mgombea wake  wa CCM, January Makamba,  Peramiho la mgombea wa chama hicho, Jenister Mhagama na Ludewa la Deo Filikunjombe.
Alisema Nec leo inatarajia kuendelea kupitia rufaa nyingine zilizobakia na baada ya kukamilisha kazi hiyo, wataanza kupitia  196 za madiwani kwa ajili ya maamuzi.
Awali waliotangazwa kupita bila kupingwa ni Makamba, Rashid Shangazi, Abdallah Chikota(Nanyamba) na Filikunjombe.
MTANZANIA
Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amewataka Watanzania wasiogope kufanya mabadiliko ya uongozi kwa kuwa hata Biblia inasisitiza watu wasiogope.
Amesema ili mabadiliko hayo yafanikiwe, Watanzania wanatakiwa kujitokeza kwa wingi Oktoba 25, mwaka huu na kumpigia kura za ndiyo pamoja na wagombea ubunge na udiwani kupitia Ukawa.
Lowassa aliyasema hayo jana katika mji wa Makambako, mkoani Njombe alipokuwa akihutubia maelfu ya wakazi wa Jimbo la Makambako.
“Jamani wananchi wa Makambako, nawaambia nataka kura za kutosha kuniingiza Ikulu, nikiingia madarakani nchi itakuwa tulivu na hakuna atakayemwaga damu.
“Tukichukua nchi hii itakuwa tulivu, hatutaki kumwaga damu na kama ni damu kumwagika, watamwaga wao na wala siyo sisi.
“Kwahiyo, nasema ‘I am serious’, nataka kura za kutosha kwa sababu naambiwa wale wenzetu (CCM) ni mabingwa wa kuiba kura. Nataka watakapoiba, zibaki nyingine za kutuwezesha kushinda.
“Hata nyie mnaotaka kuhama hameni wala msiogope kufanya mabadiliko kwa sababu neno usiogope limeandikwa mara 365 katika Biblia… nawaambia msiogope kwa sababu hata mimi siogopi,” alisema Lowassa na kushangiliwa.
Akizungumzia baadhi ya kero zinazowakwaza Watanzania, Lowassa alisema kama atafanikiwa kuingia madarakani, Serikali yake itakuwa makini, kwa kuondoa michango yote ya elimu ya sekondari ili wazazi wapate nafasi ya kusomesha watoto wao.
“Kuna kero nyingi sana nimeambiwa ziko hapa Makambako, ambazo naamini ninaweza kuziondoa pindi tu nitakapoingia madarakani.
“Kwanza kabisa, nitaondoa kero ya maji iliyoko hapa Makambako kwa sababu najua namna ya kuitatua kwa kuwa nilikuwa Waziri wa Maji enzi za utawala wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa.
“Pili, hili tatizo la mashine za kukusanya kodi za EFD nitaliangalia kwa kina kwa sababu haiwezekani nchi ikawa ya kibabekibabe tu, yaani wafanyabiashara wanasema hivi na wewe hutaki kuwasikiliza.
“Chuo cha VETA kitajengwa hapa Makambako ili kiwasaidie vijana, matatizo yote ya walimu na wafanyakazi wote serikalini, nitayatatua kwa sababu uwezo ninao.
“Nitafuta pia michango yote shule za sekondari kwa sababu chini ya Serikali yangu, elimu itatolewa bure kwani haya yote yako kwenye ilani ya chama chetu.
“Kwa maana hiyo, nawaomba tena, ikifika Oktoba 25, mwaka huu, mjitokeze kwa wingi kunipigia kura mimi, wabunge wa Ukawa na madiwani wetu wote ili nikaunde Serikali yenye nguvu,” alisema.
Katika maelezo yake, Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani, alisema suala la umasikini kwa Watanzania ni la kujitakia kwa kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi zinazoweza kuchangia kukuza uchumi wa Taifa.
Alizitaja baadhi ya rasilimali hizo ambazo alisema atazitumia kukuza uchumi, kuwa ni pamoja na dhababu, gesi na mazao kama chai na pamba.
“Kama Mwenyezi Mungu akinijalia, nitaendesha nchi hii kwa spidi ya ajabu, kwani hatuna sababu ya kuwa masikini.
“Nawahakikishia uchumi wa nchi hii utakua kwa kasi kwa sababu rasilimali zipo na kinachotufanya tuwe masikini ni kutojua vipaumbele vyetu,” alisema.
Juu ya migogoro ya muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji, Lowassa alisema itatoweka kwa sababu haiingii akilini Watanzania waendelee kugombana katika nchi yao, na kwamba ardhi yote itapimwa na wananchi kumilikishwa ili waitumie kuinua maisha yao.
Baada ya kuhutubia mkutano huo, Lowassa alihutubia mkutano mwingine mkubwa wa hadhara katika mji wa Njombe na kuwaombea kura wabunge na madiwani wa Ukawa, huku akisisitiza wananchi wasiichague CCM.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment