Saturday, September 5, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO, SEPT 05 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo pia kinatoa kozi mbalimbali za kielimu na Ufundi ukiwemo Umeme na Computer. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
NIPASHE
Viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, wamekemea wagombea wa vyama vya siasa wanaotumia lugha za kashfa katika kampeni hali inayoweza kutishia uvunjifu wa amani.
Mwenyekiti wa Bakwata Wilaya ya Arumeru, Ustadhi Haruna Hussein alisema, wanasiasa hao wanachopaswa kufanya ni kunadi sera na sio kutukanana kwenye majukwaa hali ambayo inaashiria kuwapo kwa uvunjifu wa amani kutokana na mienendo yao.
Aidha aliwataka wanasiasa hao kunadi sera zao kwa wananchi kuwa watawafanyia mambo gani pindi watakapochaguliwa badala ya kusimama kwenye majukwaa na kuanza kutoa lugha za kashfa na matusi kitendo kinachochagia wananchi kukosa imani nao.
Alisema viongozi hao ni kioo kwa jamii hivyo wanapaswa kuonyesha dira ya uongozi na sio kuwa na matusi na kashfa.
Naye mjumbe wa Bakwata Wilaya ya Arumeru, na Kaimu Sheikh wa Msikiti wa Patandi, Ally Ramadhani Haji, alisema madhara ya kutaja mambo ya aibu za watu majukwaani ni kutengeneza chuki zisizokuwa na maana, kwa sababu dunia inapita kwenye kipindi kigumu na moja ya mambo yanayosababisha chuki na vurugu ni siasa za chuki baina ya viongozi ambapo mwisho wa siku watu wanaingia kwenye matatizo.
Kwa upande wake, Sheikh wa Wilaya ya Arumeru, Ally Isa Ibrahimu alisema, viongozi hawatakiwi kufarakana na kutukanana pamoja na kuchafuana kwenye kampeni bali wawe wamoja katika mambo yao huku wakizungumzia suala zima la amani ya nchi ili kufanyika kwa kampeni za kistaarabu.
Alisema katika kuelekea kipindi hiki cha uchaguzi vyama vya siasa pamoja na viongozi wa siasa wanapaswa kutangaza amani ya nchi, kwani jamii haipo tayari kuona viongozi hao wa kisiasa wakifanya kampeni chafu zinazochangia        viasharia vya amani.
Sheikh wa Msikiti wa  Patandi,  Abdalah Said Omar alisema, kwa ujumla baraza hilo wilayani Arumeru halifurahishwi na  siasa chafu zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa siasa ikiwamo kutoleana lugha za matusi hatua ambayo inaipeleka nchi pabaya hivyo ni wajibu wao kuhakikisha kuwa wanazungumza maneno mazuri yenye kuiletea nchi amani.
NIPASHE
Mgombea ubunge wa CUF katika jimbo la Mtama, Isihaka Mchinjita, amemchana Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa , anayemaliza muda wake, Bernard Membe, kuwa licha ya kuwa na nyadhifa kubwa serikalini hajaliendeleza jimbo hilo.
Pamoja na kutoa lawama hizo Mchinjita, ametaja vipaumbele sita atakavyovisimamia endapo atachaguliwa kuwa mwakilishi wa wananchi katika uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kuzindua kampeni uliofanyika kata ya Mnolela wilayani Lindi Mchinjita alisema: Ndugu zangu jimbo hili limetelekezwa kwa muda mrefu kiti cha ubunge wa miaka 15 ya Bernad Membe, licha ya kuwa na nyadhifa serikalini, ikiwamo uwaziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa limelala alilalamika.
Alisema hakuna maji wananchi wanachotaka kutoka mapangoni , wanafunzi hawana vyoo na kwa ujumla Mtama umaskini unatisha.
Maelezo yake yaliungwa mkono na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Oliver Vavunge alikiri kuwapo kwa changamoto hizo na kueleza kuwa yote hayo yanachangiwa na hali ndogo ya kiuchumi, akiwaomba wananchi kusaidia kupunguza tatizo hilo.
NIPASHE
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imewataka wananchi kujitokeza kuhakiki taarifa zao kwenye daftari la wapiga kura kwa kuwa mwisho wa zoezi hilo ni keshokutwa.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Nec, Kailima Kombwey, kwa vyombo vya habari jana, ilisema zoezi hilo lilianza Agosti 19 mwaka huu na  linatarajiwa kumalizika Septemba 7. Daftari la awali la Wapiga Kura limewekwa wazi katika kata    zote za jiji la Dar es Salaam.
Mashine za Biometric Voter Registration (BVR) zinazotumika kufanyia marekebisho zimewekwa katika kata zote ili wananchi wapate huduma hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza madhumuni ya zoezi hilo ni kurekebisha taarifa za Mpiga Kura zilizokosewa wakati wa uandikishaji, kutoa kadi mpya kwa      wapiga kura waliopoteza      kadi zao na  wamo     katika Daftari la   awali la Wapiga Kura.
Kuondoa wapiga Kura waliofariki au waliokosa sifa kwa mujibu wa sheria, Kuhamisha taarifa za wale waliohama toka kata au Jimbo kwenda Kata au Jimbo lingine, kutoa nafasi kwa wapiga kura walioandikishwa kukagua taarifa kama zipo kwenye daftari.
Alisema wenye kadi za mpiga kura lakini majina yao hayaonekani katika daftari la awali la wapiga kura watafanyiwa uhakiki katika mifumo ya BVR na iwapo itathibitika kuwa wamo watarudishwa katika mfumo wa daftari.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo mtu anaweza kukagua taarifa zake kwa njia ya simu kwa kubonyeza 15200# au tovuti www.nec.go.tz na kufuata maelekezo.
NIPASHE
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amesema kama wananchi watampa ridhaa atahakikisha serikali yake inatunga sera ya kuhakikisha nyumba za nyasi zinaondolewa nchi nzima.
Ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza na wakazi wa mji wa Kigoma katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika viwanja vya Community Center ikiwa ni siku ya sita tangu alipoanza ziara ya kuomba kura mikoani kwa wananchi.
Lowassa ameshafanya mikutano ya kampeni katika baadhi ya majimbo yaliyopo mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Katavi na Kigoma na leo anaendelea na ziara yake katika mkoa wa Tabora.
Alisema iwapo wananchi watamchagua na kuwa Rais wa awamu ya tano suala la ujenzi wa nyumba bora litazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha nyumba zote za nyasi zinaondolewa ili Tanzania iweze kufanana na mataifa mengine.
Kuhusu wakimbizi waliopo mkoani Kigoma, alisema wamepata taarifa kuwa wakimbizi hao wamepewa vistisho kwamba wasipoipigia kura CCM watanyang’anywa uraia wa Tanzania.
Alisema kutokana na hali hiyo wamemtuma aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, afuatilie suala hilo.
“Hakuna serikali inayoweza kusema usiponichagua nitakunyang’anya uraia, mkinipata kura nitafanya mabadiliko katika nchi yetu ili kila mtanzania aone mabadiliko katika maisha yake,” alisema.
Lowassa alisema kama wananchi watamchagua serikali yake haitataka kusikia suala la michango katika shule na badala yake elimu itakuwa bure kuanzia msingi hadi chuo kikuu.
Aliongeza kuwa ushuru wa mazao utaondolewa kwa wakulima na wataruhusiwa kuuza mazao yao nje ya nchi bila ya kuwekewa vikwazo vyovyote na kilimo cha umwagiliaji kitaboreshwa ili kuongeza ajira nchini.
Aliwaeleza wananchi wa Kigoma kuwa tatizo la usafiri katika Ziwa Tanganyika analifahamu  hivyo serikali yake italipatia ufumbuzi haraka na uvuvi utaboreshwa uwe wa kisasa.
Lowassa aliahidi kujenga bandari ya kisasa mkoani Kigoma pamoja na kujenga reli ya kati na kwamba kama reli itakayojengwa na serikali ya sasa itakuwa haina viwango itachimbuliwa na kujengwa mpya.
Aidha, aliahidi kuwa serikali yake itajenga viwanda vya mawese ili kuwawezesha wakulima kupata soko la uhakika la zao hilo na hivyo kuongeza ajira.
Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Kusini anayemaliza muda wake, David Kafulila alisema CCM hivi sasa kimekuwa ni chama ambacho hakikubaliki na maaskofu, masheikh na wapagani .
Alisema CCM imepoteza uhalali na ndiyo maana Serikali ya Marekani imezuia Dola za Marekani milioni 700 na Ulaya Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya miradi ya Mileniaum Challenge (MCC) kwa kuhofia zitatafunwa.
Kafulila alisema Lowassa ana kila sababu ya kuwa rais wa awamu ya tano kwa kuwa ana uwezo wa kuwaunganisha wananchi wa dini zote.
Alisema kashfa ya Richmond ambayo CCM wanaitumia kama rungu la kumsema Lowassa kimsingi lilishafafanuliwa kwamba mhusika mkuu wa suala hilo anajulikana.
Aliwashangaa baadhi ya viongozi wa CCM ambao wanasema wana nyaraka za Richmond lakini kwanini hawakuzitoa tangu awali hadi wahubiri wakati wa uchaguzi mkuu.
Kafulila alisema hakuna mpinzani atakayeiondoa CCM nje ya Ukawa.
Naye Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alisema bado siku 50 taifa hili liandike historia Watanzania watafanya maamuzi kuhusu ustawi wa taifa lao.
Alisema Kigoma ni miongoni mwa mikoa ambayo imepokea mageuzi toka mwaka 1993 na kutoa wabunge wa upinzani hivyo ushirika wa Ukawa utafanya maamuzi ya kufanya mabadiliko Oktoba 25, mwaka huu.
Mbowe alisema yeye kama Mwenyekiti amefanya kila jitihada kuviunganisha vyama vya upinzani ili viweze kuiondoa CCM madarakani ambayo imelifanya taifa kama la kilio.
Alisema Ukawa walipoamua kumchukua Lowassa baadhi ya watu walihoji suala hilo lakini lengo ni kutaka kuleta mabadiliko ambayo Watanzania wanayahitaji.
Aliongeza kuwa itakuwa ni haramu kwa mtu anayetumia nguvu kufifisha mabadiliko yanayohitajiwa na Watanzania wengi ambao wamechoshwa na serikali ya CCM.
MWANANCHI
Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amewaahidi wakazi wa mkoa wa Kigoma kuwa atajenga bandari ya kisasa ikiwa watamchagua kuwa rais wa awamu ya tano katika uchaguzi mkuu ujao.
Lowassa ambaye alitua mjini hapa kwa chopa akitokea Nguruka na Kalinze alikofanya mikutano ya kampeni, alisema mbali ya bandari pia atajenga reli ya kati ya kisasa (standard gauge).
Lowassa aliipiga kijembe Serikali akidai imekumbuka shuka kumekucha, baada ya hivi karibuni Waziri wa Uchukuzi, Samwel Sitta kusema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho kuanza ujenzi wa reli hiyo. Katika mkutano huo wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Mwanga Community Centre, Lowassa alisema:
“Ninataka mnipe kura nikafanye mabadiliko ya kweli kwa kila Mtanzania.
Nitahakikisha unafanyika uvuvi wa kisasa katika Ziwa Tanganyika na Bandari ya Kigoma lazima ijengwe iwe ya kisasa.” Lowassa anayegombea urais kwa tiketi ya Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa alitumia dakika 11 kuzungumza na wananchi hao, akisema akiwa rais atahakikisha Watanzania wanajenga nyumba bora na kuwa na makazi ya kisasa.
“Tutatunga sera kuhakikisha tunaondoa nyumba za nyasi nchi nzima.
Lazima tufanane na mataifa mengine, hatuwezi kubaki nyuma kila siku,” alisema.
Awali ilizuka hali ya sintofahamu katika uwanja huo kutokana na wananchi waliokuwa wamekaa nyuma ya uwanja huo kuonekana kupingana na kilichokuwa kikizungumzwa na viongozi wa Chadema kwa kunyoosha mikono juu, lakini mara baada ya Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe kupanda jukwaani na kuzungumza, hali ya kupinga ilibadilika wakaanza kuwashangilia.
Mbowe alisema kuwa lengo la Ukawa ni kuipeleka CCM likizo kutokana na kushindwa kuwaletea maendeleo wananchi. “Hatuwezi kujenga umoja kwa kutumia vyama 20, tutajenga taifa kwa kuuganisha nguvu na kushirikiana. Vyama vya mageuzi kazi yake kubwa ni kupambana na chama kilichopo madarakani.”
Mkoa wa Kigoma ni kati ya mikoa ambayo ni ngome ya vyama vya upinzani, ushindani umeongezeka zaidi baada ya aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Kabwe kujitosa kugombea ubunge jimbo la Kigoma Mjini kwa tiketi ya ACT­Wazalendo kupambana na kada wa zamani wa Chadema, Dk Amani Kaburou anayegombea kupitia CCM.
Lowassa alisema akichaguliwa atafuta michango na ada ya shule, kubadili mfumo mzima wa elimu ili uwe na manufaa kwa wananchi na kuwawezesha vijana kujiajiri. Aidha, alisema ataanzisha kilimo cha umwagiliaji, kuwawezesha vijana kupata ajira, kufufua kilimo cha michikichi kwa kuanzisha viwanda vya kuzalisha mafuta ya mawese kutokana na zao hilo. “Umeme ni kero kubwa sana, lakini nawaahidi kuwa nitalishughulikia kuhakikisha kuwa umeme unakuwa si kero tena. Kama niliweza kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika mikoa mbalimbali sitashindwa kutoa maji katika Ziwa Tanganyika kuwafikia wananchi wa Kigoma,” alisema Lowassa. Mbunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR­Mageuzi aliyemaliza muda wake, David Kafulila alisema Kigoma ni ngome ya upinzani na itadhihirika katika uchaguzi mkuu, huku akisisitiza kuwa mwaka huu ni wa mabadiliko na kwamba wanashindana na CCM isiyokubalika kokote. “CCM imepoteza uhalali kitaifa na kimataifa na hata misaada kutoka nje haipati tena. Marekani imezuia misada ya Dola 700 milioni. Lowassa ana sababu na sifa zote za kuwa rais wa nchi hii. Ukimtizama na kumsikiliza unaona anatosha kuunganisha Waislamu na Wakristo, Watanzania na raia wa nchi nyingine,” alisema Kafulila.
MWANANCHI
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli amewataka wahandisi wanaofanya kazi chini ya kiwango na kudhalilisha taaluma hiyo wajiondoe mapema kwa kuwa endapo atapata ridhaa ya kushika dola hatawavumilia.
Dk Magufuli ambaye ni Waziri wa Ujenzi alisema hayo jana wakati akifunga mkutano wa wahandisi jijini Dar es Salaam. Alisema hatakubali kufanya kazi na wahandisi wanaoitia doa taaluma hiyo, hivyo ni vyema wakajitoa mapema kwani hawataendana na kasi ya utendaji wake.
Mgombea huyo wa urais alisisitiza kuwa maendeleo ya nchi yoyote duniani yamekuwa yakitegemea uwapo wa wahandisi, hivyo, endapo atashinda atahakikisha wanatumika ipasavyo kupandisha uchumi wa taifa.
“Ninawafahamu vizuri wahandisi kwa kuwa nimefanya kazi nanyi kwa muda mrefu. Niseme wazi kuwa sitawaangusha, nitakuwa nanyi bega kwa bega kuhakikisha taaluma hii inazidi kukua na kuheshimika,” alisema.
“Kama inavyofahamika kilichopo mbele yetu ni kazi, watakaokuwa tayari kufanya kazi kwa juhudi na uaminifu tutakuwa pamoja ila wale wachache wanaoitia doa taaluma hii ni bora wakajitoa mapema,” alisisitiza.
Magufuli alieleza kuwa anatambua changamoto ya utendaji wa wahandisi wilayani kuingiliwa na wanasiasa hivyo atafanya kila linalowezekana kutenganisha taaluma hiyo na siasa.
“Wahandisi wa halmashauri najua mnakutana na changamoto ya taaluma yenu kuingiliwa na siasa, hilo nitalishughulikia na nawaahidi mishahara yenu itakuwa mikubwa ila kuipata lazima mfanye kazi kubwa pia,” alisema.
“Siwezi kuwaangusha hata kidogo. Siku za nyuma nilikuwa naagizwa lakini endapo nitashinda nitakuwa natoa maagizo na nitahakikisha nitakayoagiza yanakuwa na faida kwa wahandisi na Watanzania kwa ujumla.” Akijipigia chapuo kwa wahandisi Dk Magufuli aliwataka kumchagua rais anayeifahamu taaluma hiyo kwa kina ili washirikiane naye katika kulisukuma gurudumu la maendeleo.
Kwa upande wake, Mhandisi Ramo Makani alisema wakati umefika kwa wahandisi wa Tanzania kuongeza nguvu za ziada katika utendaji wao ili kuhakikisha wanasaidia kusukuma gurudumu la maendeleo na kuliondoa taifa kwenye umaskini.
“Tunajisikia vibaya kuona nchi yetu haiendelei na kwenye mkutano huu tumekubaliana kuacha kulalamika na kutimiza majukumu yetu kama wahandisi katika harakati za kuleta maendeleo katika taifa hili,”alisema Makani ambaye ni mbunge wa Tunduru kwa tiketi ya CCM.
Wakati Dk Magufuli akiwaahidi neema wahandisi makini, mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan alifanya ziara maeneo kadhaa wilayani Kinondoni ambako aliahidi kuchimbua mifereji na kuchimba Mto Ng’ ombe ili kuondokana na adha ya mafuriko.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Mwananyamala, Samia alisema kumekuwa na kero ya mafuriko kwa miaka mingi, hivyo Serikali ya awamu ya tano italifanyia kazi suala hilo kwa kutumia fedha ya Benki ya Dunia kuchimba mifereji yote, kuchimba mito na kuzibua njia zote za maji ili yapate njia ya kupita na yasiingie kwenye makazi ya watu.
Alisema suala la kupata maji safi na salama litakuwa la uhakika kutokana na mradi mkubwa wa maji wa Ruvu Juu ambayo yataongezeka kutoka asilimia 65 ya sasa kufikia
MTANZANIA
HATIMAYE mke mdogo wa Dk. Willibrod Slaa, Josephine Mushumbusi, ameibuka na kujibu baadhi ya hoja ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake yeye binafsi na kwa mume wake na zaidi akisema yote yanayosemwa dhidi yao hayako katika fikra zao kwani kwa sasa baada ya kuachana na siasa wanajipanga kuelekea upande mwingine wa kuwa wawekezaji.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya simu jana, Mushumbusi aliitaja mipango yao hiyo kuwa ni pamoja na kujenga shule na hospitali.
Mushumbusi ametoa kauli hiyo wakati ambapo gharama zinazokadiriwa kufikia shilingi milioni 50 alizozitumia mume wake katika mkutano wake na waandishi wa habari mapema wiki hii zikizua mjadala mpana wa alikopata fedha hizo zote.
Pamoja na hilo, Mushumbusi ambaye anatajwa kuwa katikati ya mpango wa kumrubuni mume wake licha ya kupuuza hoja kama hizo alipoulizwa walikopata fedha za kutekeleza miradi mikubwa kama hiyo alisema zimetoka kwa watu aliodai kuwa ni marafiki zao na kiasi kingine ni asilimia 20 ya vipato vyao ambavyo walikuwa wakiviweka kwa muda mrefu.
Mushumbusi ambaye tangu Dk. Slaa azungumze na waandishi wa habari Jumanne wiki hii hajawahi kuzungumza lolote, alianza kujibu yale yaliyozungumzwa na mke mwenzake ambaye ni mke wa ndoa wa Dk Slaa aitwae Rose Kamili ambaye juzi alizungumza na vyombo vya habari na kumtupia tuhuma nzito yeye (Mushumbusi) na mume wake huyo wa zamani.
Rose alikaririwa na vyombo vya habari akimtuhumu mumewe kuwa ni muongo na anapelekeshwa na mwanamke anayeishi naye kwa sasa ambaye ni Mushumbusi.
Akijibu shutuma hizo, Mushumbusi alisema yeye ni zaidi ya siasa rahisi zinazoenezwa dhidi yake.
Alimpuuza Rose kwa kusema kuwa ameamua kuchanganya matatizo binafsi ya familia na propaganda za kisiasa, hivyo jambo hilo liko mbali na uwezo wa fikra na mipango yake kwa sasa.
Mushumbusi alisema yeye si mwanasiasa kwani ana mambo mengi anayoyafanya mbali na siasa hivyo shutuma alizotoa Rose kwa Dk. Slaa zingefaa pia kama angewaeleza Watanzania sababu za kuachwa kwake.
“I’m above with that cheap politics, you know? (Unajua niko juu ya siasa hizo rahisi?), I’m activist, I can’t deal with them and I have a lot of things to do out of politics by the way, I’m not a politician as I told you (mimi ni mwanaharakati, siwezi kushughulika nao na nina mambo mengi ya kufanya nje ya siasa, hata hivyo mimi sio mwanasiasa kama nilivyokueleza),” alisema Mushumbusi.
Mushumbusi alifafanua kuwa hivi sasa yuko mbali na mambo ya siasa na anaangalia mbele kulisaidia taifa katika nyanja za elimu, afya na uchumi.
Alisema mipango yao kwa sasa ni kujenga shule, hospitali pamoja na kuwasaidia kina mama katika masuala ya ujasiriamali.
Alisema tayari mipango yao hiyo mipya ilikwishapangwa kwa kushirikiana na Dk. Slaa.
Alisema mbali na fedha za marafiki yeye ni mfanyabiashara wa nafaka na kwa muda mrefu pamoja na mumewe wamekuwa wakiweka akiba.
Hata hivyo, wakati Mushumbusi akisema kuwa anafanya biashara ya nafaka, gazeti moja la kila siku (Si MTANZANIA) liliwahi kumkariri hivi karibuni akidai kuwa kwa sasa anafanya biashara ya mkaa.
“Brother I’m not there as they think, I’m a focused woman (Kaka sipo hapo kama wanavyofikiri, mimi ni mwanamke makini), nina mambo mengi ya kulifanyia taifa langu, nashangaa hata hiyo hoja ya kutelekeza watoto, waulizeni hao watoto kama hawapajui kwangu, huyo kijana wa kiume kila mara anakuja kwangu hata wadogo zake wanamfahamu vyema, eti  wanasema Dk. Slaa kawatelekeza wanataka awafanyie nini na wakati watoto wote hao ni above eighteen (zaidi ya miaka 18) na tayari wamezaa kila mmoja, hoja nyingine you must think big (kufikiri zaidi),” alisema Mushumbusi.
HABARILEO
MASHEHE sita waliokuwa wametekwa na waasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC) wamerejea nchini jana, huku wakieleza kuwa kulitaja jina la Tanzania kumewaokoa na kifo kutoka kwa waasi hao.
Kitendo cha mashehe hao kutaja wanatokea Tanzania kimewasaidia kwani kwa mujibu wao, waasi hao walisema hawana shida na Tanzania, lakini Wakongo waliwadanganya hivyo hawawapendi.
Akizungumza baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kiongozi wa mashehe hao, Mohammed Abdallah Khamis alisema, wakiwa njiani kuelekea nchini humo walivamiwa na watu hao wakiwa na silaha za kivita kisha kutekwa na kupelekwa porini.
“Mwanzo hatukuelewa kama ni wanajeshi wa serikali au wanajeshi wa porini, tulipofika nao porini ndiyo wakajitambulisha wao ni askari wa porini na wanahitaji fedha ili watuachie ama watatuua,” alisema Khamis.
Akisimulia jinsi walivyoishi porini alisema, walikuwa wanapata tabu kwani hata chakula walikuwa wakipewa ndizi, maharage na magimbi ambayo waliambiwa wale ili wasife, huku wakati mwingine wakiteswa na waasi hao kwa kupigwa na magongo na vibao.
Alisema waasi hao walihitaji wapewe kiasi cha dola za Marekani 20,000 (zaidi ya Sh milioni 60) ili waweze kuachiwa. Khamis aliishukuru serikali ya Tanzania kwa jitihada ilizofanya ili kuhakikisha wapatikana wakiwa salama. “Kwa kweli tunaipongeza sana serikali ya Tanzania na DRC maana wamefanya juhudi kubwa sana za kutuokoa.
Bora kuishi mwaka mmoja gerezani lakini si kukaa na watu wale siku moja,” alisema. Khamis alisema, hata hivyo baadaye waliachiwa na waasi hao baada ya kuona hawana fedha lakini pia ni wazee, hivyo waliwaachia kwa huruma na hasa kwa kuzingatia hawana shida na Watanzania.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim akizungumza baada ya kuwapokea mashehe hao alisema, wakati wote serikali ilikuwa ikifuatilia suala hilo ili kujua usalama wao.
Hata hivyo, alisema kuna umuhimu kwa Watanzania wanaosafiri kwenda katika nchi tofauti kwa shughuli mbalimbali kuhakikisha wanatoa taarifa katika Balozi zilizopo katika nchi hizo ili serikali iwe na taarifa ya Watanzania hao.
“Tunaishukuru sana serikali ya Congo na jamii nzima ya watu wa Goma ambao walitoa msaada mkubwa na hata walinzi wa amani wa Congo walishiriki vizuri katika kuhakikisha mnapatikana mkiwa salama,” alisema.
Alisema kutokana na kuwa vikosi vya usalama vilikuwa vikifuatilia tukio hilo kwa ukaribu, hata baada ya kuachiwa kwa mashehe hao, vikosi hivyo vilifanikiwa kuwakamata watekaji hao.
Balozi wa Tanzania nchini DRC, Anthony Cheche alisema, baada ya kupokea taarifa hizo walifuatilia na baada ya kubaini ni Watanzania ndiyo juhudi za kuwakomboa zikaanza. Alisema alikuwa akipokea simu nyingi kutoka kwa vyombo vya habari na ndugu, jamaa na marafiki za kutaka kujua hali za mashehe hao lakini wakati mwingine alilazimika kuficha ukweli ili kuepusha kuhatarisha usalama wa mashehe hao.
“Tulipewa tahadhari kuwa kuna mazingira hatarishi, hivyo kuna baadhi ya taarifa zikitolewa zinaweza kusababisha tukawapoteza watu wetu na ndiyo sababu kuna taarifa nilikuwa nikiziminya,” alisema.
Baada ya kuachiwa kwa mashehe hao ambao wote ni wakazi wa Zanzibar, walipokewa na Jeshi la DRC na kupewa ulinzi hadi Mji wa Goma ambapo walikutana na viongozi wa mji huo pamoja na Balozi Cheche ambaye waliondoka naye hadi mjini Kigali, Rwanda kwa ajili ya kurejea nchini.
Mashehe hao ambao walienda nchini humo kwa ajili ya kutangaza dini, walirejea jana kwa ndege ya Shirika la Rwanda saa 9:55 mchana ambapo pia jana hiyohiyo waliondoka saa 12:00 kuelekea Zanzibar kwa ndege ya Shirika la Precision.
HABARILEO
RAIS Jakaya Kikwete amezitaka asasi za kiraia kuweka wazi fedha wanazozipata kutoka kwa wafadhili na namna wanavyozitumia, na wanapotakiwa na Serikali kutoa taarifa hizo wasione kama wanaingiliwa utendaji wao.
Mwito huo ulitolewa na Rais Kikwete jana alipokuwa akifungua mkutano wa kwanza wa Takwimu Huria Kanda ya Afrika (Africa Open Data) uliofanyika kwa mara ya kwanza Afrika na kuhudhuriwa na washiriki kutoka nchi 30 za Afrika ambapo Tanzania ilikua mwenyeji.
Rais Kikwete alisema watu wanahitaji kujua asasi hizo zinafanya nini, fedha wanazozipata zinatumikaje na pia serikali inaweza kuhitaji taarifa hizo kwa sababu za kiusalama, hivyo wasione usumbufu wanapotakiwa kutoa taarifa hizo.
“Asasi hizi zinapoulizwa taarifa zao ziwe wazi lakini ukiuliza wanaona wanaonewa, serikali inapata fedha kutoka kwa wafadhili hao, lakini ukiwauliza inaonesha kama kuwaingilia, serikali taarifa zake zinakua wazi tu,” alisema Rais Kikwete.
Kikwete alisema serikali kwa kiasi kikubwa inajitahidi kutoa taarifa kwa umma zinazohusu takwimu katika mambo ambayo ni wazi, vivyo hivyo iwe katika sekta binafsi pamoja na asasi hizo ili kuweka uwajibikaji.
Aidha, Rais Kikwete alisema ni vizuri wananchi wakajua fedha zimepokewa kiasi gani, lini, kwa shughuli gani na kama matumizi yaliyokusudiwa yameweza kufanyika ipasavyo na hiyo haimaanishi kuwaingilia katika majukumu yao.
Akielezea Tanzania ilivyotekeleza masuala ya takwimu huria, alisema serikali yake iliweza kuajiri wahasibu 780 katika halmashauri mbalimbali hapa nchini ili kuondoa hati chafu, jambo ambalo limefanikiwa na sasa ni halmashauri zisizozidi mbili ambazo hazijafanikiwa.
“Niliwaambia halmashauri zote lazima ziajiri wahasibu hao na baada ya muda mfupi hali ya kuwa na hati chafu ikapotea, lakini haitoshi kuwa na hati safi pekee lakini sasa inaonyesha kwa uwazi fedha zinatumikaje,” alisema Rais Kikwete.
Alisema katika suala hilo serikali pia iliamua kuanza kujadiliwa kwa uwazi taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bungeni na hatua kuchukuliwa kwa taasisi ambazo hesabu zake hazitakuwa sawa.
“Haitoshi tu kusema kila kitu kiko sawa pasipo kuhusisha tukio halisia na usimamizi mzuri utasaidia Tanzania watu kuona moja kwa moja…hata hivyo hatuwezi kufika mahali tukasema kila jambo la serikali liwe wazi, hiyo haiwezi kuwa sahihi,” alisema Rais Kikwete.
Alisema kuna mambo ambayo serikali haiwezi kuweka wazi na hii ni kwa sababu za usalama wa nchi au unyeti wa jambo lenyewe na hivyo kuliacha mpaka pale ambapo linakuwa tayari kuwekwa wazi.
Akieleza mafanikio ambayo yamefikiwa kwa kuwa na uwazi alisema, katika sekta ya madini serikali imeweza kuweka wazi ni madini kiasi gani yanapatikana, kilichouzwa na pia ni kodi kiasi gani imeweza kukusanywa katika sekta hiyo.
Aidha Rais Kikwete alisema kutokana na kwamba takwimu huria inasaidia katika kuinua uchumi wa nchi basi ni vema nchi za Afrika kukumbatia mfumo huo ili kuongeza uwajibikaji katika sekta zote.
“Kuna haja kwa bara la Afrika kukumbatia masuaa haya kwa ajili ya kuboresha utendaji katika sekta zote, hii ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi,” alisema.
Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alisema ni jambo la fahari kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kwanza katika bara la Afrika ambao una lengo la kudumisha uwazi wa utoaji takwimu mbalimbali na katika sekta mbalimbali ambao ni kichocheo cha maendeleo.
Alisema thamani ya mfumo huo inaharakisha maendeleo ya nchi na pia kutoa nafasi kwa wananchi kushuhudia maendeleo ya nchi na pia mambo mbalimbali yanayofanywa na serikali na kuweza kuhoji.
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bella Bird alisema matumizi mazuri ya utoaji taarifa za takwimu yatasaidia kuondokana na umasikini. Bird alizitaja nchi ambazo zimenufaika katika suala hilo mbali na Tanzania kuwa ni pamoja na Kenya, Ghana, Liberia, Malawi, Tunisia na Nigeria ambapo alisema kwa nchi ya Kenya wakulima wameweza kuwafikia wafanyabiashara moja kwa moja bila kupita kwa watu wa kati na hivyo kupata faida nzuri katika mazao yao.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment