Sunday, September 6, 2015

WATUMISHI WA UMMA WAPEWA SOMO TANGA


Tangakumekuchablog

Tanga, WAFANYAKAZI na watumishi katika idara za Serikali na watu binafsi wametakiwa kuzingatia maadili ya kazi na kuacha vitendo vya rushwa jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Akizungumza katika hafla ya kuwakaribisha wanachuo wapya 1,500 Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) tawi la Tanga , Afisa Mchunguzi wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Tanga, Frank Mapunda, alisema rushwa imenea kila idara na watu kukosa haki zao.

Aliitaja rushwa ya ngono ambayo ndio imeenea kila idara jambo ambalo linakosesha haki na huduma na hivyo kusema kuwa Taasisi yake imejipanga kwa kuunda vitengo vya kukomesha tabia hiyo.

“Ni furaha yangu  kuzungumza na watu ambao baadae wanaweza kuwa wakuu wa idara za Serikali na watu binafsi----langu kwenu muwe waadilifu na epukeni vitendo vya rushwa “ alisema Mapunda na kuongeza

“Kuna rushwa za aina nyingi lakini kuna hii moja wakati muendapo kuomba kazi ya ngono----musikubali kutoa wala kupokea  na toeni taarifa  katika ofisi zetu ili kulikomesha” alisema

Akizungumzia kipindi hiki cha uchaguzi, Mapunda alisema Taasisi yake imejipanga kuhakikisha inawakamata watoaji na wapokeaji wa rushwa ikiwemo wagombea na wapiga kura.

Alisema kipindi hiki cha kampeni za kuelekea uchaguzi vitendo vya rushwa huongezeka jambo ambalo linawanyika haki wananchi kuchagua mgombea wanaemtaka na ambae  anakubalika.

“Kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi rushwa ziko kila kona hasa kwa wagombea kutoa zawadi za aina mbalimbali----jihadharini kwani maofisa wa kupambana na rushwa wamejipenyeza musije kutumbukia kwenye sheria” alisema Mapunda

Akizungumza katika hafla hiyo ya kuwakaribisha wanachuo wapya, Mkurugenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) tawi la Tanga, Issaya Hassanali,  aliwataka kuwa na upendo na kuunda timu moja ya ushindi.

Aliwataka kuzigatia maadili na nidhamu wakati wote Chuo na wajikite katika masomo yao ili kuweza kudumisha heshima na sifa ya Chuo iliyojijengea ndani na nje ya nchi.

“Niwakaribisheni chuoni hapa kwa heshima na upendo mkubwa ila cha msingi ni kuzingatia maadili na sheria za chuo----ni sifa ya chuo iliyojijengea na ndio maana hapa muko kutoka kila pembe na nchi yetu” alisema Hassanali

Aliwataka wanachuo hao kujibidiisha katika masomo yao na kuweza kutoa michango yao ya kimaendeleo katika ujenzi wa taifa na kizazi kijacho kwa kuwawekea misingi imara .

                                         Mwisho

 Mwanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma(TPSC) Tawi la Tanga, Hamis Mohammed, akiuliza swali wakati wa hafla ya kuwakaribisha wanafunzi wapya 1,500 chuoni hapo .
 Rais wa Wanafunzi wa Chuo Cha Utumishi wa Umma (TPSC) Tawi la Tanga, Gilbert Mushi, akimuapisha Devid Manyiliza kuwa Waziri Mkuu wa Wanafunzi wa chuoni hicho .

Rais wa Wanafunzi Chuo Cha Utumishi wa Umma Tawi la Tanga (TPSC) Gilbert Mushi, akimuapisha Mesaka Saimon kuwa Katibu Mkuu wa chuo hicho hafla iliyofanyika chuoni hapo .

No comments:

Post a Comment