Wednesday, June 10, 2015

POLISI YAMNASA KIJANA AKIJARIBU KUMTAPELI WAKALA WA TIGO PESA

Tangakumekuchablog

Tanga, JESHI  la Polisi Wilayani Korogwe Mkoani Tanga, linamshikilia mkazi wa kijiji cha Mnyuzi, Habib Rajab (19) kwa tuhuma za kupatika na pesa bandia 18  zenye mfano wa  elfu kumi kila moja wakati akijaribu kutuma kwa wakala wa  tigo pesa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kaimu kamanda wa polisi Tanga, Mayala Towo, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 12 jioni wakati kijana huyo akiwa katika hatua za mwisho za kutuma pesa.

Alisema wakati akikabidhi pesa hizo wakala wa tigo pesa aliweza kuzigundua na ndipo alipotuma ujumbe mfupi wa maandishi  kwa askari wa  kituo kidogo cha Hale na kuweza kufika na  kukamatwa.

“Wakala tunampa hongera kwa ujasiri wake wa kuweza kijana kutiwa mikononi kwani hakubabaika na kuchukua simu na kutuma sms kwa askari kituo cha polisi----wakati akifanya hivyo alimrubuni kuwa mtandao unasumbua” alisema Towo

Aliwataka wananchi kuwa na umakini wa kuzitambua pesa  ikiwa na pamoja na kutoa taarifa kwa polisi ili kukomesha matukio kama hayo ambayo wezi wengi wamekuwa wakipitia kwa mawakala ili kutimiza malengo yao.

Alisema  uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea na mara baada ya kukamilika Rajab atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili na kuwa fundisho kwa watu wengine wenye mchezo kama huo.

Katika tukio jengine, wahamiaji haramu wawili raia wa Ethopia wamekamatwa ndani ya basi wakati wa ukaguzi katika kizuizi cha magari kijiji cha Makuyuni Wilayani Korogwe Mkoani Tanga.

Wahamiaji hao ni Johans Jeffary (26) na Ayele Abede (22)  waliokuwa wakielekea Dar es Saalam na kupelekwa kituo cha polisi kwa mahojiano kujua waliokuwa wakiwasafirisha.

“Hawa wahamiaji kwanza tumewahifadhi na kesho tutawahoji kwani tumewaona wamechoka kama watu ambao hawajala kwa siku mbili-----tunataka kujua ni nani wamewasafirisha ili kuvunja ngome hiyo” alisema Towo

Akitoa wito kwa wananchi kaimu kamanda aliwataka wananchi kuipa ushirikiano jeshi la polisi katika masuala mbalimbali ya kihalifu yakiwemo wageni ambao hujipenyeza kuingia nchini  kinyume cha sheria.

                                                      Mwisho

No comments:

Post a Comment