Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MTANZANIA
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU),
imetakiwa kukunjua kucha zake kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za
uongozi kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.
Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Prof. Ibrahim Lipumba,
alisema sasa umefika wakati kwa Takukuru kuhakikisha wanadhibiti
matumizi ya fedha kwa wagombea wanaotangaza nia katika vyama mbalimbali.
Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), alisema ni lazima Mkurugenzi wa Takukuru, Dk. Edward Hosea,
aeleze mikakati yake ya namna atakavyopambana na rushwa, hasa kwa
wagombea ambao si waadilifu na ambao wamekuwa wakitumia fedha.
“Ni
muhimu katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu, Dk. Hosea akaelezea
mikakati yake ya kupambana na wanaowania uongozi ambao wanakiuka maadili
ili waeleze fedha wanazotumia wanazitoa wapi. Na jambo hili liwe kwa
vyama vyote,”Prof. Lipumba.
Akizungumzia uteuzi wa wagombea ubunge
na urais kupitia Ukawa, alisema hivi sasa kila chama kipo katika
mchakato wa ndani kwa ajili ya kukamilisha taratibu zake.
“Ukawa
unaendelea vizuri, nami nimetangaza nia ndani ya chama changu kwa
nafasi ya urais, nasubiri mkutano mkuu wa chama chetu ndiyo utatoa
uamuzi wa mwisho.
“Tukishakamilisha
kazi hii kwa kila chama sasa ndiyo kamati maalumu ya viongozi itaketi
kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Ukawa na kisha utatoa na jina la
mgombea mmoja wa urais ambaye atapambana na vyama vingine,” Lipumba.
Alizungumzia pia utendaji kazi na weledi wa taasisi za Serikali ikiwamo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), ambao
walichunguza tukio la kupigwa kwa viongozi na wafuasi wa CUF Januari
27, mwaka huu wakati walipokuwa wanakwenda kuahirisha mkutano wa
hadhara.
Ripoti iliyotolewa na tume hiyo,
ilieleza kwa kina namna Jeshi la Polisi lilivyotumia nguvu kupita kiasi
na hata kusababisha majeruhi kadhaa kinyume cha sheria.
MTANZANIA
Mbunge wa Ukonga jijini Dar es Salaam, Eugen Mwaiposa, amefariki dunia usiku wa kuamkia jana mjini Dodoma akiwa usingizini.
Akitangaza msiba huo bungeni jana, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema Mwaiposa alifariki dunia akiwa nyumbani kwake eneo la Chadulu mjini hapa.
Alisema kwa muda mrefu mbunge huyo aliyeingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2010, alikuwa na tatizo la shinikizo la damu.
Wabunge walikuwa wakiendelea kuchangia bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge, Lediana Mng’ong’o
ambaye ghafla alimkatiza mchangiaji kuzungumza na kumpisha kwenye kiti
Naibu Spika Ndugai, ambaye alitoa taarifa za kifo cha mbunge huyo.
Ndugai, alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa uchunguzi zaidi wa wataalamu.
Alisema mwili wa marehemu utaagwa kesho mjini hapa baada ya ndugu wa marehemu kuwasili.
Alisema mwili wa marehemu utaagwa kesho mjini hapa baada ya ndugu wa marehemu kuwasili.
Kutokana na msiba huo, Ndugai alitangaza
kuahirishwa kwa Bunge hadi keshokutwa na kuagiza Kamati ya Uongozi
kukutana na wabunge watapatiwa taarifa kwa njia ya mtandao wa simu.
“Natumia kifungu cha 152 kuahirisha Bunge hadi Alhamisi saa 3:00 asubuhi,” Ndugai.
Mwaiposa ni mbunge wa pili kufariki dunia kwa mwaka huu, akimfuatia Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba, aliyefariki dunia Februari 28.
NIPASHE
Makada watano wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) leo watafungua pazia kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na chama
hicho kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Leo ndiyo siku ya kwanza ya uchukuaji
fomu ndani ya CCM kwa ajili ya kurithi nafasi ya Rais Jakaya Kikwete
ambaye anang’atuka kwa mujibu wa katiba ya nchi.
Makada watakaochukua fomu hizo leo baada ya kutangaza nia kuwania nafasi hiyo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa (UN), Balozi Amina Salum Ali na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Charles Makongoro Nyerere.
Makada hao watatangulia kuchukua fomu hizo huku chama hicho kikitoa masharti makali yanayotakiwa kufuatwa na wagombea.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wa Idara ya Oganizesheni, Dk. Mohamed Seif Khatibu, alisema makada watano wataanza kufungua pazia la uchukuaji fomu leo katika makao makuu CCM mjini Dodoma.
Alisema katika utaratibu huo, Prof. Mwandosya ndiye atakayekuwa wa kwanza kuchukua fomu saa 4:00 asubuhi akifuatiwa na Wasira.
Dk. Khatibu alisema Lowassa atakuwa wa
tatu kuchukua fomu hiyo saa 7:00 mchana, akifuatiwa na Balozi Amina saa
8:30 na Nyerere atafunga dimba kwa leo.
Alisema ratiba ya uchukuaji fomu hiyo
haikupangwa kwa kufuata umaarufu au cheo cha mtu ndani ya chama na
serikali bali umezingatia mgombea kuwahi kutoa taarifa katika chama
kwamba anataka kuchukua fomu.
Kwa upande wa Zanzibar, alisema wagombea
wanaowania urais wa Zanzibar watachukulia fomu katika ofisi za CCM na
wale wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watachukulia mjini
Dodoma.
NIPASHE
Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima,
amesema moja ya mambo ambayo hayakufanyika vizuri mwanzoni wakati wa
uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa ni kutovifanya vitumike kupiga
kura katika uchaguzi mkuu.
Amesema kama kitambulisho hicho
kingeboreshwa kingeweza kutumika kwa ajili ya kupiga kura, hivyo
kusingekuwapo uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Waziri huyo aliyasema hayo jana jijini
Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa kongamano la kimataifa la
uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa lijulikanalo kama ‘Govetnment Forum on Electronic Identity in Africa’, unaofanyika Afrika kwa mara ya kwanza na kujumuisha wataalam zaidi ya 300 wa ndani na nje ya Afrika.
“Kama
tungejipanga mwanzo vizuri ni wazi kusingekuwapo haja ya mchakato
unaoendelea wa kuandikisha kwa kutumia BVR, ni nafasi kwetu kujifunza na
kujirekebisha na pia watajifunza kutoka Tanzania,”.
Silima alisema siku zijazo vitambulisho
hivyo vitaboresha zaidi ili kutumika kwenye maeneo mbalimbali, na kwamba
kwa siku za usoni vitatumika kwenye malipo mbalimbali.
Aliwataka Watanzania wanaoshiriki katika
kongamano hilo kupokea na kutumia teknolojia inayotoka kwenye makampuni
mbalimbali duniani.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu,
alisema watu milioni 6.1 wameandikishwa katika maeneo ya Zanzibar, Dar
es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro na Tanga na kwamba watu
milioni 2.5 wamepatiwa vitambulisho.
Alisema kongamano hilo linalojulikana ‘Govetnment Forum on Electronic Identity in Africa’,
limeleta pamoja nchi 24 ambazo zitajadili kwa kina changamoto zilizopo
kwenye uandikishaji, uandaaji wa vitambulisho vya Taifa na jinsi gani
vitatumika kwa maendeleo ya Taifa.
NIPASHE
Waziri wa Uchukuzi Samuel Sitta, amevunja Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) iliyoundwa na mtangulizi wake, Dk. Harrison Mwakyembe, na kuunda bodi mpya yenye wajumbe wanane kuanzia Juni 2, mwaka huu.
Uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa
kifungu Namba 6 Kifungu kidogo cha 2 (b) cha Sheria ya Bandari namba 17
ya mwaka 2004 kinachompa mamlaka ya kuvunja na kuteua wajumbe wa bodi.
Sitta alitangaza uteuzi huo jana jijini
Tanga wakati wa ziara ya kikazi katika Bandari ya Tanga na baadaye
kuzungumza na wafanyakazi waliokusanyika katika uwanja wa Baraka na
kusisitiza kuwa mabadiliko hayo yametokana na vitendo vya uonevu
alivyokuta vikiendelea kufanywa ndani ya TPA.
“Uteuzi
huu unatengua uteuzi wa wajumbe wa sasa wa bodi hiyo kuanzia leo Juni
2, mwaka huu na lengo la uteuzi wa wajumbe hawa ni kuleta tija na
ufanisi wa utendaji kazi ndani ya wa Mamlaka na kwa nafasi ya Mwenyekiti
mpya wa Bodi nasubiri uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete kwani ndiye mwenye
mamlaka hiyo kisheria,” alisema.
Dk. Mwakyembe aliteua bodi ya TPA Novemba 6, 2012.
NIPASHE
Taasisi za serikali zinadaiwa Sh. bilioni 20 na mamlaka za maji nchini.
Hayo yalisemwa jana bungeni na Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Leticia Nyerere.
Mbunge huyo alisema ofisi ya Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mara inadaiwa Sh. milioni 102 na Jeshi la Wananchi wa
Tanzania linadaiwa Sh. milioni nane na kuhoji kwa nini serikali
haiingilii kati ili kuhakikisha kwamba madeni hayo yanalipwa ili
kuiwezesha Mamlaka ya Maji ya Musoma (MUWASA) kufanyakazi yao kikamilifu na kwa mafanikio.
Akijibu, Makalla alikiri serikali kutambua kuwapo kwa madeni hayo.
Alisema Jeshi la Wananchi linadaiwa Sh.
milioni 2.4, hospitali zinadaiwa Sh. milioni 113 na madeni mengine hivyo
mamlaka hiyo inaidai serikali jumla ya Sh. milioni 390 na kwamba
mamlaka zote za maji nchini zinaidai taasisi za serikali Sh. bilioni
20.
“Sisi (Wizara ya Maji) tutashirikiana na
Wizara ya Fedha kuona kwamba madeni haya yanalipwa ili mamlaka hizi
ziweze kufanyakazi kwa ufanisi,” alisema.
Awali katika swali la msingi, Mbunge wa
Musoma Mjini, Vicent Nyerere, alitaka kujua kama serikali ipo tayari
kutoa ruzuku kwa mamlaka za maji ikiwamo Muwasa ili ziweze kujiendesha
na kupunguza mzigo kwa wananchi.
Pia alihoji kama ni sawa wizara na idara za serikali kama JWTZ, Polisi, Ikulu kukatiwa maji kwa kushindwa kulipia huduma hiyo.
Akijibu, Makalla alisema serikali
ilianzisha mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira nchini ambazo ziko
katika madaraja matatu, ‘A’, ‘B’ na ‘C’.
Alifafanua kuwa mamlaka za daraja ‘B’ ni zile ambazo zinapata ruzuku ya kulipia sehemu ya gharama za umeme wa kuendesha mitambo.
HABARILEO
Watanzania milioni 25.4 wamejitokeza
kupima Ukimwi kwa hiari, ikiashiria kwamba nusu ya Watanzania wamepima
kujua hali yao kuhusu maambukizi ya Ukimwi.
Idadi hiyo ni ongezeko la watu milioni 4.9 waliopima kufikia Desemba 2013.
Takwimu hizo zimetolewa na Waziri wa
Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid wakati akiwasilisha bajeti ya
wizara yake katika kikao cha 19 cha mkutano wa 20 wa Bunge.
Alisema hadi kufikia Desemba 2014, idadi
ya watu waliopima virusi vya Ukimwi (VVU), walikuwa 25,468,564 na
kufanya ongezeko la watu 4,999,323.
Kwa mujibu wa Waziri wanaopima VVU kwa hiyari imeongezeka kutoka watu 11,640 mwaka 2009 na kufikia 20,469,241 kwa mwaka 2013.
Alisema mafanikio hayo yametokana na kutekelezwa mpango mkakati wa lll wa sekta ya afya katika kupunguza maambukizi ya Ukimwi.
Alisema takwimu zilizopo zinaonesha kuwa
kampeni imefanikiwa kuhamasisha wananchi na pia kupunguza kiwango cha
maambukizi ya VVU kutoka asilimia 5.8 mwaka 2008 hadi 5.3 mwaka 2012 .
Alisema pamoja na kuendelea kutekeleza
mpango mkakati huo wa tatu wa sekta ya afya wa kupambana na Ukimwi
(2013-2017) kwa kutoa ushauri nasaha na upimaji wa VVU kwa hiari, wizara
itaendelea kupanua huduma na upimaji kufikia ongezeko la watu 7,411,619
na kutoa dawa za ARV kwa waviu 880,681.
Aidha, alisema kwamba wizara yake
imewezesha kliniki 109 zinazotoa ARV kwa wanawake wajawazito wenye VVU
(Option B+) ziweze pia kutoa huduma za kupambana na Ukimwi kwa watoto
wanaosihi na VVU.
MWANANCHI
Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye
ametangaza nia ya kuwania urais kupitia CCM, huku akibainisha kuwa
amejipima, ametafakari na kujiridhisha kuwa anatosha kushika wadhifa huo
wa juu nchini.
“Kama kuna mtu mwingine amekamilika kuliko mimi niambieni na nitampisha (katika mbio za urais),”
alisema Sumaye wakati akitatangaza nia hiyo jana jijini Dar es Salaam
mbele ya wanahabari, akitumia takriban saa moja na nusu kueleza sifa za
Rais ajaye na vipaumbele vyake.
Sumaye, mmoja wa makada sita waliokuwa
wamefungiwa na CCM kwa kukiuka taratibu za kampeni, alikuwa Waziri Mkuu
kwenye Serikali ya Awamu ya Tatu kwa kipindi chote cha miaka kumi na pia
alikuwa mbunge wa Hanang hadi alipoamua kutogombea nafasi hiyo mwaka
2010.
Waziri huyo mkuu wa zamani amekuja na
kauli mbiu ya Uongozi Bora: Komesha Rushwa, Jenga Uchumi, huku
akibainisha vipaumbele vyake kuwa ni pamoja na kujenga na kuimarisha
uchumi.
Vipaumbele vingine ni kulinda Muungano,
mshikamano, amani na utulivu na kuboresha huduma za kijamii na maisha ya
Watanzania, kupambana na maovu ya rushwa, ufisadi, dawa za kulevya,
mauaji ya kishirikina, uhusiano wa kimataifa na masuala muhimu ya
uhifadhi wa mazingira, kilimo, ajira, ulinzi wa rasilimani na michezo na
utamaduni.
Sumaye alisema Watanzania wanataka Rais
anayetambua uzito wa kazi iliyopo mbele yake na wananchi wote na awe
tayari kuwa Jemedari wa Jeshi hilo ili kupata ufumbuzi wa matatizo yao
yanayowakabili.
Alisema wananchi wengi wanamfahamu kwa
utendaji wake naye anajua wanachokihitaji na sifa za Rais wanayemhitaji,
hivyo yeye ndiye anayefaa kwa nafasi hiyo.
“Mtu
anayetaka kuwa Rais ni lazima awe tayari kujipima, kutafakari,
ajiridhishe, kuwa anatosha kiafya, kiakili, kimaadili na kidhamira
kuwaongoza Watanzania.
“Kama kuna mtu anapungukiwa kimojawapo, hana sifa za kuwaongoza Watanzania,” alisema Sumaye huku akishangiliwa na baadhi ya wafuasi waliomsindikiza katika mkutano huo uliofanyika Hoteli ya Hyatt Regency.
Alisema kiongozi huyo awe tayari kupimwa na umma vigezo hivyo na siyo ajipime na kwamba yeye yupo tayari kupimwa na umma.
Katika hotuba yake hiyo iliyokuwa
ikirushwa na baadhi ya televisheni na redio nchini, alisema Watanzania
wanahitaji Rais atakayekuwa mtumishi wa kuwaongoza na siyo bosi, na pia
awe mtu atakayewaongoza kwa uadilifu.
Sifa nyingine za kiongozi huyo ni kuwa
mzalendo wa dhati anayejua Watanzania walipotoka, wanapopitia na
wanakoelekea; mwaminifu, mjasiri, mtiifu wa sheria na katiba na
anayeheshimu mipaka ya cheo chake.
MWANANCHI
Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Sepp Blatter ametangaza kuwa atajiuzulu nafasi yake hiyo kutokana na kashfa ya rushwa iliyolikumba shirikisho hilo.
Akitangaza uamuzi huo, Blatter mwenye miaka 79 alisema baada ya kuitisha mkutano wa dharula wa Fifa: ”Muda mfupi ujao kunatakiwa kuchaguliwe rais mpya.”
Blatter alichaguliwa wiki iliyopita
kuliongoza shirikisho hilo, licha ya wajumbe saba wa juu wa Fifa
kukamatwa na maafisa usalama wa Marekani siku mbili kabla ya uchaguzi
huo.
Blatter alisema: “Uamuzi huu hauungwi mkono na kila mtu.”
Awali Fifa ilikanusha madai kwamba katibu wao mkuu, Jerome Valcke alihusika katika kashfa ya ufisadi ambapo hongo ya mamilioni ya dola ilitolewa.
Fifa inasema hamna afisa wake yeyote wa ngazi ya juu aliyehusika kwa njia yoyote katika kashfa hiyo.
Inasemekana malipo hayo ya rushwa
yalitolewa na serikali ya Afrika Kusini kwa maafisa wa soka wa huko
Marekani ili waunge mkono wenzao Waafrika waliong’ambo katika nchi za
visiwa vya Caribbean.
Waendesha mashtaka wa Marekani wanasema
hongo hiyo ilinuiwa kusaidia kununua kura kuiwezesha Afrika Kusini kuwa
mwenyeji wa Kombe la Dunia lililofanyika mwaka 2010.
Kwa habari matukio na michezo kutoka pembe mbalimbali, ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment