Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kimebobea na kuwa na walimu mahiri wa masomo. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Prof. Anna Tibaijuka jana alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuzomewa na wananchi wa jimbo lake mbele ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Hali hiyo ilijitokeza jana asubuhi katika Kata ya Nshamba wilayani hapa wakati msafara wa Kinana ulipofika kuzindua mradi wa maji.
Kadhia hiyo ilianza baada ya Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera, Ally Idd Ame
kumkaribisha mbunge huyo ili awasalimie wananchi. Hata hivyo, wananchi
hao walianza kuzomea kwa zaidi ya sekunde 40 wakipinga Profesa Tibaijuka
kupanda jukwaani, hali iliyomlazimu Mkuu wa Wilaya, Francis Isack kupanda jukwaani na kutoa kauli ya kiutawala ili kuwanyamazisha wananchi hao.
“Anayetaka kusikiliza abaki na asiyetaka aondoke,”
alisema Isack na kuwanyamazisha mamia ya wananchi hao. Baada ya kauli
hiyo wananchi walitulia na kuruhusu Profesa Tibaijuka kupanda na
kuhutubia kwa muda.
“Kama
hamnitaki siyo lazima niwe mbunge wenu, mnaruhusiwa kubadili. Huyo
aliyewapa viroba asubuhi hii ili mje mnitie aibu mbele ya katibu mkuu wa
chama nawaambia hiyo dhambi itawatafuna,” .
Aliwaambia wananchi hao kuwa anachokifanya ni kuwatumikia na kuwaletea maendeleo, hasa wanawake…
“Mimi
sitafuti kazi na wala sina njaa… na kama hela ya kula ninayo. Mimi
sigangi njaa na kama mnataka kuwa na kiongozi mganga njaa muwekeni muone
atawasaidia vipi,” alisema.
Akihitimisha salamu zake kwa wananchi
hao alisema kama wana jambo lao la ziada walifanye lakini wamuache
aendelee na jitihada za kuwaletea wanawake maji… “Sina kinyongo na yeyote kwa sababu “I am too sophisticated (mstaarabu). Nipo juu ya mambo madogomadogo yanayowasumbua.”
Mbunge huyo ambaye hivi karibuni
aliondolewa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na
kashfa ya Tegeta Escrow, alimweleza Kinana kuwa eneo hilo limekumbwa na
upinzani kutoka kwa mtu anayehitaji kulichukua ambaye ni kutoka ndani ya
CCM.
MWANANCHI
Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto, Zainab Omar Mohammed amesema wimbi la ndoa kuvunjika visiwani hapa limekuwa likisababisha familia nyingi kuishi katika mazingira magumu.
Waziri Mohammed alisema hayo jana
alipofunga mjadala wa makadirio na matumizi ya bajeti ya wizara ya mwaka
wa fedha 2015/2016 katika kikao cha bajeti kilichofanyika Chukwani,
Zanzibar.
Alisema ndoa zinapovunjika watoto wanakosa haki zao za msingi ikiwamo elimu, huku wanawake wakiishi katika mazingira magumu.
Waziri Mohammed alitaja sababu za ndoa
hizo kuvunjika kuwa ni migororo ya wanandoa, udhalilishaji, kukosa
uaminifu na watoto kutopewa matunzo.
Hata hivyo, alisema wizara inalifanyia
kazi suala hilo kwa kushirikiana na viongozi wa dini na jamii ili
kupunguza matatizo hayo.
Alisema kwamba kesi nyingi za
udhalilishaji wanawake na watoto zinashindwa kupata mwelekeo mzuri
katika Vyombo vya sheria kutokana na tatizo la kupatikana kwa ushahidi
wa kutosha pamoja na kesi zenyewe kuharishwa mara kwa mara na
kuwakatisha tamaa wahusika.
Awali, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Makame Mshimba Mbarouk, Hamza Hassan Juma, Viwe Khamis Abdalla na Wanu Hafidh Ameir walitaka kujua Serikali imechukua hatua gani kusimamia kesi za unyanyasaji wanawake na watoto.
Hata hivyo, Waziri Mohammed alisema suala hilo linahitaji ushirikiano na mamlaka mbalimbali zinazosimamia sheria.
Pia alisema wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano wakati wa upelelezi wa kesi husika ikiwamo kutoa ushahidi mahakamani.
MWANANCHI
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
itatakiwa kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha inatimiza mipango
yake kuelekea katika Uchaguzi Mkuu kutokana na ugumu unaoweza kutokea
katika kukamilisha uandikishaji wapigakura katika jiji la Dar es Salaam
na ugawaji wa mipaka ya majimbo nchini.
Ratiba ya uandikishaji ya NEC imelipatia
jiji la Dar es Salaam siku 13 za kuandikishaji wapigakura kwa kutumia
teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR).
Siku hizo ni pungufu kwa wastani wa siku
16 zilizotumika kwenye mikoa mingine nchini ambayo mingi ina nusu ya
idadi ya watu wenye umri wa kupiga kura ikilinganishwa na jiji la Dar es
Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi Mosena Nyambabe
aliliambia gazeti hili kuwa ili NEC iendane na kasi ya muda uliopo,
inatakiwa kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha inakamilisha
uandikishaji wapigakura na ugawaji wa mipaka ya majimbo.
“Uzuri
wa Dar es Salaam ni makao makuu ya kila kitu, tutaangalia mwenendo wa
uandikishaji kujua unafanyika kikamilifu au la na utatupa picha hali
ilikuwaje katika mikoa mingine. Bado wana kazi kubwa kwa sababu
hawajakamilisha kuchora ramani ya mikoa na majimbo…lazima wafanye kazi
ya kutisha,” Nyambabe.
Alisema kazi ya mwaka mmoja na nusu
haiwezi kufanyika ndani ya wiki mbili ndiyo maana wakati mwingine huwa
wanaona mipango ya NEC kama viini macho. Hata hivyo akasema angalau sasa
NEC wamejikita katika Uchaguzi Mkuu kuliko Kura ya Maoni ya Katiba
Inayopendekezwa.
Takwimu za Shirika la Takwimu la Taifa (NBS) za
makadirio ya watu wenye sifa ya kupiga kura zinaonyesha kuwa Dar es
Salaam ina zaidi ya watu 2.93 milioni, idadi ambayo ni sawa na jumla ya
wapigakura katika mikoa sita ya Katavi, Lindi, Shinyanga, Njombe, Iringa na Rukwa ambao wanakadiriwa kuwa 2.94 milioni.
NBS inakadiria Morogoro kuwa na wapigakura zaidi ya 1.28 milioni wakati Tanga ina watu zaidi ya 1.12 milioni.
MWANANCHI
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa
ameanza ziara ya siku nane barani Ulaya ambako atashiriki mijadala
kuhusu hali ya demokrasia na kukutana na jopo la wataalamu wa masuala ya
uchumi kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika kupata mifumo sahihi na
kujenga taasisi za kusaidia uwajibikaji na kusukuma maendeleo ya watu.
Katika ziara hiyo ya tatu baada ya mbili
alizofanya Marekani, Dk Slaa anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo
na viongozi mbalimbali wa Umoja wa Ulaya (EU) kuhusu hali ya
demokrasia, utawala bora na hali ya haki za binadamu nchini hasa kwa
kipindi hiki ambacho Watanzania wanaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa chama hicho, Deogratias Munishi ilisema: “Katika ziara hiyo, viongozi hao wa Ulaya watapata fursa ya kujadiliana na Dk Slaa hali ya siasa kwa ukanda wa Afrika Mashariki.”
Dk Slaa ambaye aliondoka Jumamosi iliyopita, ameongozana na Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa chama hicho, John Mrema na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene,
ameanza ziara akiwa ametoka katika mikoa ya Kagera, Mbeya, Rukwa na
Katavi akikagua uandikishaji wapigakura kwenye kwa mfumo wa BVR na
kuhamasisha wananchi wenye sifa kujiandikisha.
Kiongozi huyo ambaye anatajwa kuwania
nafasi ya urais ndani ya Ukawa, anafanya ziara hiyo ukiwa umepita mwezi
mmoja na nusu tangu alipofanya ziara ya pili nchini Marekani.
Aprili 13 mwaka huu, Dk Slaa alianza
ziara ya siku tisa Marekani ambako alishiriki mijadala inayohusu
uwekezaji, elimu na uongozi ikiwa na lengo la kuitangaza Tanzania.
Katika ziara hiyo alifanya mihadhara
kwenye vyuo vikuu vya Purdue, Indianapolis na Marion pamoja na vikao vya
mashauriano na baadhi ya wahadhiri wa vyuo hivyo kwa lengo la
kubadilishana uzoefu juu ya masuala ya kisiasa na maendeleo, kijamii na
ushiriki wa Chadema katika siasa za kimataifa.
Pia, alikutana na viongozi wa taasisi
pamoja na kampuni kubwa za uwekezaji kwa lengo la kubadilishana uzoefu
katika usimamiaji wa masuala ya uchumi na uwekezaji Afrika na kipekee
kwa Tanzania.
Septemba 21, 2013, Dk Slaa alifanya
ziara ya wiki tatu nchini humo na alitembelea majimbo mawili ambako
alizungumza na Watanzania waishio Marekani na kukutana na viongozi
pamoja na kutembelea vyuo vikuu kadhaa katika majimbo ya North Carolina
na Alabama.
Dk Slaa alihutubia katika Chuo Kikuu cha
Stamford ambako aliutangaza utalii na fursa za uwekezaji nchini,
akisema Tanzania ni nchi tajiri isiyohitaji misaada kutoka popote kama
haijapatwa na janga.
“Viongozi
wengi wa Afrika wanaaminika kwenda Ulaya na Marekani kuomba misaada.
Hii imewajengea taswira kuwa Waafrika wengi ni maskini na wavivu. Lakini
ukweli ni kwamba Afrika ipo katika kipindi cha mpito kujitegemea kwa
kila kitu. Sijaja hapa kuomba kwa sababu nchi yangu ni tajiri sana,” Dk Slaa
MWANANCHI
Serikali imefuta umiliki wa baadhi ya mashamba yaliyokuwa yanamilikiwa na wawekezaji na kuyakabidhi kwa wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa wizara yake katika kipindi cha 2015/2016.
Lukuvi alisema migogoro mingi kati ya
wananchi na wamiliki wa mashamba, wananchi na hifadhi za Taifa imepungua
baada ya mipaka kurekebishwa.
“Rais
amefuta umiliki wa shamba la Ufyomi Galapo Estate na kazi inayoendelea
kwa sasa ni kuhakiki, kupima na kumilikisha ardhi kwa wananchi ili
waweze kuitumia,”Lukuvi.
Aliyataja mashamba mengine kuwa ni
Utumaini la Halmashauri ya Wilaya ya Mafia lenye ukubwa wa ekari 4,040
pamoja na shamba la Malonje katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
Waziri Lukuvi alisema bado kuna changamoto nyingi za mashamba ambayo wananchi wanataka umiliki wake ufutwe.
Kuhusu umilikaji wa ardhi, alikiri bado
kuna tatizo katika maeneo mengi nchini ambayo licha ya viwanja kupimwa,
bado halmashauri zinashindwa kuandaa michoro na hati za kuwapa wananchi
wanaohitaji viwanja hivyo.
Akizungumzia Mji wa Kigamboni katika
Jiji la Dar es Salaam, alisema wizara baada ya kuchunguza imeona kuna
haja ya kupunguza eneo hilo baada ya marekebisho ya Tangazo la Serikali.
“Eneo
la mpango limepunguzwa kwa kuondoa kata tatu za Mpiji, Pembamnazi na
Kisarawe ambalo lina ukubwa wa hekta 44,440 ambazo hazikuwapo katika
mpango wa awali, hivyo kubaki na kata sita zenye ukubwa wa hekta 6,494,” Lukuvi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli aliitaka Serikali kusimamia kauli yake kwamba haiwezekani kupima ardhi kama haijawalipa fidia wamiliki wa maeneo hayo.
MTANZANIA
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama,
amehusishwa na tuhuma za kutaka kumiliki ardhi kwa njia za kifisadi
katika maeneo mbalimbali, ikiwamo Wilaya ya Rombo mkoani humo.
Kutokana na hali hiyo, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, imemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, William Lukuvi kuzuia mchakato wowote haramu utakaofanywa na
Gama kuhusu ardhi.
RC Gama, alitajwa bungeni na Waziri
Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee (Chadema)
wakati akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu
bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2015/16 mjini Dodoma jana.
Alisema Gama anashirikiana na kampuni
binafsi ya Jun Yu Investment International, anataka kumiliki ardhi
iliyokwishalipiwa fidia ya Sh milioni 168 na Halmashauri ya Wilaya ya
Rombo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe jijni
Dar es Salaam, katika hotuba yake, aliambatanisha vielelezo
vinavyomwonyesha Gama kuhusika katika kampuni hiyo.
Aliwataja wahusika wengine kuwa ni Wang
Zhigang raia wa China anayemiliki hisa 48,000, Feng Hu raia China mwenye
hisa 49 na Muyanga Leonidas Gama ambaye ni mtoto wa Gama anayemiliki
hisa 3,000.
“Habari tulizonazo, mkuu wa mkoa
anamiliki hisa 20,000 ambapo hisa 10,000 zimefichwa kwa mwanahisa wa
kwanza na 10,000 nyingine kwa mwanahisa wa pili kupitia mkataba wa pili
uliofichwa, ambao pia tumeuambatanisha katika hotuba hii.
“Katika hali ya kushangaza, Halmashauri
ya Rombo ambayo iliwekeza fedha zake Sh milioni 168 haitambuliwi na wala
haina hisa hata moja katika kampuni hiyo,” alisema Mdee.
Alisema kambi ya upinzani ina taarifa za
kiintelijensia ambazo zinaonyesha wawekezaji hao wa kichina walilipa Sh
milioni 500 kama fidia kwa wananchi katika ardhi hiyo ambayo
Halmashauri ya Rombo ilishalipa Sh milioni 168, lakini fedha hizo
hazijulikani zilipo.
Mdee, pia alimtaja Gama kutaka kufanya
ufisadi katika eneo lililopo Kilalacha ambalo linagusa Jimbo la Vunjo na
Rombo lenye ukubwa wa hekta 2,700.
Akizungumzia suala hilo, Mdee alisema
eneo hilo lilikuwa mali ya ushirika uliokuwa ukifahamika kwa jina la
Lokolova, lakini katika siku za karibuni kigogo huyo wa mkoa amekuwa
akilinyemelemea kwa kisingizio cha uwekezaji.
Alisema Gama yupo nyuma ya mgogoro wa
ardhi unaokihusisha kiwanja cha Mawenzi chenye hati namba C.T 056035
kilichokuwa chini ya miliki ya The Registered Trustees of Mawenzi Sport
Club.
“Kiwanja hiki kilikuwa na hatimiliki ya
miaka 33 iliyokwisha mwaka 1974. Mwaka 1994 kupitia kwa aliyekuwa waziri
wa ardhi wakati huo, Edward Lowassa, alitoa amri ya kutwaa maeneo
mbalimbali likiwamo hilo.
“Hali ilikuwa salama kwa wakuu wote wa
mikoa waliopita, lakini hali ilibadilika alipoletwa Gama ambaye amekuwa
akitumia ofisi yake kushinikiza kiwanja husika kikabidhiwe kwa matapeli
ambao wametengeneza nyaraka feki na kuziwasilisha kwa Wakala wa Udhamini
na Ufilisi (RITA) na kujitambulisha kama wadhamini wapya baada ya
kukabidhiwa na wadhamini wa awali.
“Wakati matapeli hawa wanaotambulika kwa
majina ya Amratlal N. Pattn na Hittesh H. Solan wakionyesha kikao cha
makabidhiano kilifanyika Januari 5, 2008 mbele ya wadhamini wa awali,
Devchad Nathu Shah na Mohamedal Sharriff, taarifa za uhakika ni kwamba
Shah alishafariki dunia tangu mwaka 1979 wakati Sharriff alifariki mwaka
1998,” alisema Mdee.
Awali akitoa hotuba ya makadirio ya
wizara yake kwa mwaka 2015/2016, Waziri Lukuvi alionya makundi
yanayochukua ardhi ya wananchi kwa ajili ya matumizi mbalimbali
kutokulipa fidia kwa mujibu wa sheria.
Alisema watumishi wa sekta ya ardhi,
watakaobainika kusababisha kero kwa wananchi, hususan katika halmashauri
nchini, watachukuliwa hatua ikiwamo kufukuzwa kazi.
NIPASHE
Mbunge wa Muleba Kusini mkoani Kagera, Profesa Anna Tibaijuka,
amesema kushindwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika baadhi ya mitaa
na vijiji kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa Desemba, mwaka jana,
hakukutokana na sakata la fedha za Escrow.
Profesa Tibaijuka alisema sababu ya
kuanguka kwa wagombea ni mchakato wa kura za maoni ndani ya chama hicho
na mivurugano waliyonayo ya ndani Chama.
Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza
mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Muleba na kufafanua
kuwa kuna baadhi ya maeneo chama chake kimeshindwa katika wilaya hiyo
lakini si kwa sababu ya Escrow kwani amejiridhisha baada ya kufanya
utafiti wa kisiasa.
Alisema kuwa yeye ni Mbunge wa Buleba
Kusini lakini wagombea walioanguka kwenye uchaguzi huo ni wa Muleba
Kaskazini ambako hawahusiki na sakata la Tegeta Escrow.
“Nimefanya
utafiti mdogo na takwimu zinanionyesha kuwa chama chetu hakijaangushwa
kwenye uchaguzi kutokana na sakata la Escrow bali kutokana na maneno ya
makada wake tunapaswa tubadilike mapema kwani tusipofanya hivyo
tutapoteza viti vya madiwani na wabunge,” alionya Profesa
Tibaijuka ambaye Rais Jakaya Kikwete, alimuondoa katika nafasi ya
Uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na kuhusishwa
na kashfa ya fedha za Tegeta Escrow.
NIPASHE
Katika halia isiyo ya kawaida, Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho ya Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki) visiwani Zanzibar, Sheikh Ahmed Farid
na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya kula njama na kujihusisha ya ugaidi
nchini waligoma kushuka kwenye basi la magereza ili kuingia mahakamani
jana kutokana na hatma ya upelelezi wa kesi yao kutojulikana.
Washtakiwa hao walifikishwa kwenye
viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam saa 2:50
asubuhi kwa ajili kusikiliza kesi yao iliyopangwa kutajwa jana.
Kabla ya mgomo huo, washtakiwa hao
wanaotoka visiwani Zanzibar, waliiomba mahakama kuwa Waziri wa Katiba na
Sheria, Jaji Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kuwatembelea mahabusu
kwa ajili ya kusikiliza kero zao kuhusiana na kushitakiwa kwao katika
mahakama za Tanzania Bara badala ya mahakama za kwao, Zanzibar.
Viunga vya mahakama hiyo vilifurika
askari kanzu na wenye sare za Jeshi la Polisi pamoja na wa Jeshi la
Magereza kwa ajili ya kuimarisha ulinzi.
Hata hivyo, baada ya kufikishwa
mahakamani hapo washtakiwa wote 23 waligoma kushuka kwenda kusikiliza
kesi yao kwenye ukumbi wa mahakama hiyo.
Saa 4:56 asubuhi, mahakama hiyo
iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Renatus Rutatinisibwa, huku upande wa
Jamhuri ukiongozwa na mawakili wa serikali, Peter Njike na George
Barasa, wakisaidiana na wakili wa serikali mwandamizi, Tumaini Kweka.
Wakili Njike alidai kuwa washtakiwa
wamegoma kushuka kwenye basi la Jeshi la Magereza tangu wafikishwe
mahakamani hapo kutoka mahabusu.
Wakili wa utetezi, Abdallah Juma, alidai
kuwa upande wao hauna taarifa kuhusiana na washtakiwa kugoma kuingia
mahakamani na kwamba, upande wa Jamhuri ndiyo una wajibu wa kujua
chochote kuhusu washtakiwa waliopo mahabusu.
Wakili Kweka, alidai kuwa askari
magereza wamefanya juhudi za kuwataka washuke kwenye basi ili kuingia
mahakamani lakini imeshindikana.
“Mheshimiwa, Mei 25 mwaka huu, mahakama
yako ilitoa amri kwamba kesi hii itatajwa leo… Jamhuri tunaomba
washtakiwa wahesabike kwamba hawajafika mahakamani. Pamoja na kwamba
wapo katika viunga vya mahakama, tunaomba mahakama itoe amri wapangiwe
tarehe nyingine na wafike mahakamani,” alidai Wakili Kweka wa upande wa
Jamhuri.
Hakimu Rutatinisibwa alisema mahakama
haiwezi kuwafuata washtakiwa nje ya ukumbi unaoendesha shughuli zake na
kwamba, (mahakama) inaendesha kazi zake kwa mujibu wa sheria, hivyo
inaahirisha kesi hiyo hadi Juni 18 mwaka huu itakapotajwa tena.
Mbali na Sheikh Farid, watuhumiwa
wengine ni Noorid Swalehe, Ally Hamis Ally, Jamal, Nassoro Hamad,
Hassan Bakari, Ahtari Humoud, Mohamed Isihaka, Abdallah Hassan, Hussein
Mohamed, Juma Sadala, Said Kassim, Hamis Amour, Abubakar Abdallah,
Salum Ali, Salum Amour, Alawi Othuman, Rashid Ally, Amir Hamis, Kassim
Salum na Said Shehe pamoja na wenzao.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao
wanakabiliwa na mashtaka manne likiwamo la kula njama ya kuingiza watu
nchini kushiriki katika vitendo vya ugaidi,, kusaidia na kuwezesha
kufanyika vitendo hivyo.
Ilidaiwa kuwa kati ya Januari 2013 na
Juni 2014, washtakiwa hao kwa pamoja walipanga njama ya kutenda makosa
hayo ya kula njama za kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo vya
kigaidi.
Ilidaiwa kuwa katika kipindi hicho na
maeneo tofauti nchini, Sheikh Farid na Sheikh Mselem Mselem
waliwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary nchini ili kushiriki kutenda
makosa ya ugaidi.
Shekh Farid anadaiwa kuwa katika kipindi hicho, akiwa anajua kuwa Sadick na Farah wametenda makosa ya kigaidi, aliwahifadhi.
Baaada ya kusomewa mashtaka hayo,
washtakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo
haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.
NIPASHE
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, amekana kuwa na undugu wa damu na Rais Jakaya Kikwete.
Membe ambaye ametangaza nia ya kugombea
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi
(CCM) na kisha jana kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea kiti
hicho, alisema ingawa amekuwa akifananishwa na Rais Kikwete mara kadhaa;
hakuna ushahidi wowote wa kibailojia unaothibitisha kwamba wana
uhusiano wa kindugu.
Membe alisema baadhi ya watu wamekuwa wakimfananisha na Rais Kikwete lakini hawana undugu wowote baina yao.
“Kungekuwa
na aibu gani au hasara gani kuficha kwamba mimi ni ndugu wa damu wa
Rais Jakaya Kikwete. Mimi siyo ndugu wa mheshimiwa Rais, lakini
binadamu tunafanana…rangi yangu, sura yangu na ufupi wangu nimeuchukua
kwa mama yangu,” alisema Membe na kuongeza:
”Aliyekuwa
Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika (sasa marehemu) wakati fulani pia
aliwahi kunifananisha na Rais Kikwete. Naomba nitamke wazi kwamba sina
undugu wa damu na mheshimiwa Rais.”
Alisema hali hiyo pia iliwahi kumkuta
baada ya Wamarekani weusi (Afro Americans) kumkaribisha Marekani wengi
walimuomba kupiga naye picha wakidhani ni Rais Kikwete lakini baadaye
aliwaeleza ukweli kwamba yeye hakuwa Rais Kikwete.
Luhaga Mpina ambaye naye ametangaza nia
ya kuwania nafasi ya Urais kupitia chama hicho, alisema akipata ridhaa
ya chama chake na baadaye watanzania wakimwamini na kumchagua
atahakikisha anasimamia ukusanyaji wa mapato ya serikali ili yapande
mara mbili au tatu zaidi ya sasa pamoja na kusimamia rasilimali za umma
ziwanufaishe wanyonge badala ya wachache.
“Mimi si mdogo wala mtu wa kudharauliwa
katika wagombea waliotangaza nia ya kugombea urais. Mkitaka kujua mimi
naweza fuatilieni, mimi ndiye mbunge wa kwanza Afrika kusimama hadharani
na kuzungumzia utoroshaji wa mabilioni ya fedha kwa nchi za Afrika
kwenda ughaibuni.
Ndiye niliyesababisha Afrika ikaunda
kamati iliyoongozwa na Rais Mstaafu wa Afrika ya Kusini, Thabo Mbeki
kushughilikia suala hilo kwa nchi za Afrika,” alisema Mpina.
Hadi kufikia jana mchana makada wa CCM
waliotangaza nia ya kugombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kupitia chama hicho na kisha kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa
kuwania kiti hicho walifikia 20
NIPASHE
Mamia ya wananchi katika wilaya za Chato na Geita wamejitokeza kumdhamini Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa ajili ya kugombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi(CCM).
Lowassa aliwasili jana saa sita mchana
kwa ndege akitokea Zanzibar na kupokelewa na mamia ya watu na kuelekea
wilaya ya Chato, kwenye jimbo la msaka urais mwingine wa CCM, John Pombe
Magufuli.
Akiwa Chato, Lowassa alidhaminiwa na
wanachama wa CCM 430 wakiwamo wa makundi ya wafugaji, watu wa daladala,
waendesha bodaboda. Wanachama wengine wa chama hicho zaidi ya 3,000
wakijitokeza wilayani Geita kwa nia ya kumdhamini.
Lowassa aliwashukuru wanachama hao kwa kumdhamini na pia kwa kuonyesha moyo wa upendo kwake katika hatua hiyo.
Kila anayewania kuteuliwa na CCM kuwa mgombea urais, anatakiwa awe na wadhamini 450 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
“Nimekuja kuleta fomu za kunidhamini na
ninashukuru mmenidhamini, mwezi wa kumi mnaenda kuchagua rais na
mwenyekiti wa CCM… ndiyo sababu nimekuja kuomba ridhaa yenu,”alisema
Lowassa.
Alisema hajafika kuomba kura isipokuwa
anawapa angalizo kuhakikisha wanapomchagua mwenyekiti wanaangalia
historia yake na amefanya nini.
Kwa upande wake, mbunge wa zamani wa
jimbo la Busega, Rafael Chegeni, alisema mtu pekee ambaye anaweza
kuwavusha wananchi walipo ni Lowassa.
NIPASHE
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya chama hicho, Philip Mangula,
ametaja sifa 13 muhimu anazotakiwa kuwa nazo mgombea urais
atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu
utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Mangula alitaja sifa hizo wakati
akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, huku tayari kukiwa
na makada 20 waliojitokeza kutangaza nia na wengine tayari wamechukua
fomu za kuwania kuwa wagombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kupitia chama hicho.
“Mchakato wa kumpata mgombea wa CCM kwa
ngazi ya urais umeanza. Kwa ngazi ya ubunge, uwakilishi na udiwani bado
mchakato wake haujaanza.
Lakini nazitaja sifa za msingi
zitakazozingatiwa kwa mgombea urais, hizi ziko kwenye kifungu cha 5,
kifungu kidogo cha (1) hadi cha 13…Na hizi ndizo zitakazotumika kumpata
mgombea katika mchakato mzima wa uteuzi ndani ya CCM,” alisema Mangula.
Mangula alizitaja sifa hizo kuwa ni,
mosi; Awe na uwezo mkubwa wa kuliongoza taifa kwa kuzingatia uzoefu wake
katika uongozi wa shughuli za serikali, umma na taasisi.
Pili; Awe mwadilifu, mwenye hekima na busara na Tatu; Awe na angalau elimu ya chuo kikuu au inayolingana na hiyo.
Alitaja sifa ya nne kuwa ni; Awe ni mtu
mwenye upeo mkubwa wa kuweza kudumisha muungano, amani, umoja na
mshikamano wa kitaifa uliopo.
Tano; Awe mwepesi wa kuona mbali na
asiyeyumbishwa, mwenye uwezo wa kufanya maamuzi ya busara kuhusu masuala
nyeti ya kitaifa kwa wakati unaofaa.
Ya sita awe na upeo mkubwa na uwezo
usiotiliwa shaka kuhusu masuala ya kimataifa na anayeweza kuwa kiongozi
imara atakayetuunganisha na mataifa mengine.
Aliitaja sifa ya saba kuwa ni; Asiwe mtu
mwenye hulka ya kidikteta au fashisti, bali awe mtu anayeheshimu
katiba, sheria, utawala bora na kanuni zilizopo. 8; Awe ni mtu anayeweza
kutetea wanyonge na haki za binadamu na sifa ya tisa; Awe mzingatiaji
makini na asiye mtu anayejitafutia umaarufu binafsi.
10; Awe mtu wa mstari wa mbele
kuzitekeleza sera na ilani ya CCM na awe ni mpenda haki na jasiri wa
kutetea maslahi ya umma, kupambana na dhuluma na uonevu.
Sifa ya 11, Mangula alisema mgombea wa
CCM anapaswa kuwa ni mtu asiyetumia nafasi yake ya uongozi
kujilimbikizia mali na sifa ya 12 ni lazima awe ni mtu anayekubalika na
wananchi na ya 13 ni lazima awe ni mtu makini katika kuzingatia masuala
ya uwajibikaji.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? ungana nami hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment