SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572
MWANAMKE 31
ILIPOISHIA
Niliposikia hivyo moyo wangu
ulishituka. Kama namba za pikipiki yangu nazo
zimeonekana nimekwisha!
Sikujua kama ile maiti
ilikuwa ni ya shemeji yake mhasibu wetu. Nikaona nimejiingiza katika matatizo
mengine ambayo sikuyatarajia.
“Hivi sasa nimeitwa polisi
nikatoe maelezo, ile maiti imepelekwa hospitali kufanyiwa uchunguzi kujua kama ilibakwa. Kuna watu wanabaka maiti” Mhasibu
aliendelea kutueleza.
“Inawezekana. Ni vizuri kama amepelekwa hospitali kufanyiwa uchunguzi. Binaadamu
hivi sasa hawaaminiki kabisa” nikajidai kusema ili nisionekane nimefadhaika.
“Kumbe yule mlinzi alikwenda
kuripoti polisi” Mwenzetu mwingine akauliza.
“Alikwenda polisi asubuhi.
Ndio maana ninaitwa polisi” Mhasibu akamjibu kisha akatuaga na kuondoka.
Niliwaza kwamba kama mlinzi alikwenda kuripoti polisi, ile leseni yangu
pia aliipeleka baada ya kuiokota pale ilipoanguka. Polisi watakuwa wameshaiona
picha yangu. Bila shaka mhasibu wetu ameitwa ili kuoneshwa ile leseni ili athibitishe
kama ndiye mimi.
Sasa sijui nikimbie kuepusha
aibu, au niwangoje polisi waje wanikamate hapa hapa?
Kwa kweli nilikuwa
nimechanganyikiwa.
SASA ENDELEA
Kwa dakika kadhaa sikuweza
kujua nifanye nini. Wafanyakazi wenzangu walikuwa wakilizungumzia lile tukio la
kufukuliwa kaburi, mimi nilikuwa kimya. Moyo wangu ulikuwa ukihangaika. Lakini
hakukuwa na yeyote aliyeweza kunigundua.
Wasiwasi uliponizidi nilitoka
nje ya duka letu. Kilichonitoa ni ule wasiwasi kwamba polisi wakitokea niweze
kuwaona mapema. Nilikuwa nimeshapanga kuwakimbia.
Ilikuwa bora kupotea kuliko
kupatwa na fedheha kama ile mbele ya
wafanyakazi wenzangu.
Nilisimama nje ya duka letu
kwa karibu nusu saa, nilipoona hakukuwa na polisi wowote waliokuwa wanakuja
nikarudi ndani. Baadaye nikatoka tena. Nikaangalia pande zote za barabara kisha
nikarudi.
Wakati nimekaa nikiendelea na
mawazo yangu nilishituka nilipomuona mhasibu akiingia. Nilijua kuwa alikuwa
amefuatana na polisi waliokuja kunikamata.
Lakini sikuona polisi.
Alikuwa peke yake. Nikamkodolea macho ya tashiwishi. Nilikuwa na hisia kwamba
alikuwa ameoneshwa leseni yangu na kunitambua.
Mfanyakazi mwenzetu mmoja
akamuuliza kilichotokea huko polisi alikokwenda.
“Nimekwenda kutoa maelezo
yangu” akasema na kuongeza.
“Ule mwili bado uko hospitali
kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi”
“Huyo mtu aliyefukua hilo kaburi hakufahamika?’
nikauliza ili kuondoa dukuduku nililokuwa nalo.
“Si rahisi kufahamika. Mtu
mwenyewe alikimbia na pikipiki” Mhasibu akanijibu.
Hapo wasiwasi ukanipungua
kidogo.
Baada ya mhasibu kuzungumza
na sisi kwa dakika chache akaingia ofisini kwake.
Haukupita muda mrefu, simu
tuliyokuwa tunaitumia ikaita. Ilikuwa inapokelewa na mtu yeyote aliye karibu
nayo. Akaipokea mfanyakazi mmoja akasikiliza kisha akaniita.
“Amour ni simu yako”
Moyo ukanipasuka.
Ni nani tena?
Nikaenda na kukipokea chombo
cha kuzungumzia. Nikakiweka sikioni na kusema.
“Hello!”
“Naongea na bwana Amour?”
Sauti nzito tena inayokwaruza ikauliza kutoka simu ya upande wa pili.
Moyoni mwangu nilikuwa
nikijiuliza ni nani mwenye sauti hii? Akilini mwangu sikuweza kukumbuka mtu
yeyote ninayemfahamu mwenye sauti inayolingana na ile.
Nikashuku kwamba anaweza kuwa
afisa wa polisi ananipigia kuniita kituo cha olisi.
“Ndio. Wewe nani?”
“Hebu njoo hapa Tropicana,
utanijua tu”
Tropicana ulikuwa mkahawa
uliokuwa mtaa wa pili ambao wafanyakai wengi hupenda kunywa chai wakati wa saa
nne na hata kula chakula cha mchana.
“Ni vizuri unifahamishe wewe
nani?”
“Usiwe na wasiwasi. Ukifika
hapa utaniona na utanijua”
Nikaurudisha mkono wa simu
kisha nikatoka. Niliwaaga wenzangu kuwa ninakwenda kunywa chai.
Nilipotoka nje ya duka letu
nilizunguka mtaa wa pili ambako kulikuwa na huo mkahawa wa Tropicana. Wakati
natembea nilikuwa nikiwaza huyo mtu aliyeniita atakuwa nani kama
si afisa wa polisi.
Nilikuwa na hakika kwamba
sikuwa nikifahamiana na mtu aliyekuwa na sauti kavu kama
ile.
Nilipofika kwenye mkahawa huo
nikaingia. Nilisita kidogo kando ya mlango nikawatupia macho watu waliokuwamo
ndani. Nikaona mtu mmoja aliyekuwa amekaa katika meza ya pembeni akinipungia
mkono kuniita.
Sikuweza kumfahamu mpaka
nilipofika karibu yake.
“Ah Mgosingwa!” nikasema mara
tu sura yake iliponijia akilini mwangu.
Alikuwa mlinzi wetu ambaye
alifukuzwa kazi kwa tabia yake ya ulevi wa kupita kiasi. Tulikuwa tunamuita
Mgosingwa, neno la kabila la kizigua linalotokana na neno mgosi, yaani
mwanamme.
Kwa vile yeye mwenyewe
alikuwa mzigua, alikuwa akimuita kila mtu “mgosingwa” hasa pale anapotaka
kumkopa mtu pesa ya kwenda kulewea. Na sisi tukampa jina hilo la mgosingwa. Nilizoea kumuita hivyo na
jina lake halisi nilikuwa silijui.
“Vipi Mgosingwa?” akaniambia
huku akinipa mkono kunisalimia.
“Salama tu Mgosingwa. Wewe
ndio uliyenipigia simu kuniita?’
“Ndiye mimi Mgosingwa. Karibu
ukae”
Nikakaa kwenye kiti.
“Ulikuwa unasemaje
Mgosingwa?” nikamuuliza nikiwa na shauku ya kutaka kujua alichoniitia.
“Mgosingwa unatakiwa polisi!”
Kusema kweli nilishituka
aliponiambia hivyo. Moyo wangu ukawa unadunda pu!pu!pu!
Nikajidai natabasamu.
“Nimefanya kosa gani
Mgosingwa?”
Mgosingwa alitia mkono kwenye
mfuko wa shati lake akatoa ganda kama la
kitambulisho akaniwekea mezani.
“hii si leseni yako
Mgosingwa?’ akaniuliza.
Nikalichukua lile ganda na
kulifungua. Naam. Ilikuwa ni leseni yangu niliyokuwa nimeitupa kule makaburini.
Pale pale uso wangu ulibadilika rangi kwa hofu iliyochanganyika na fadhaa.
Nikamtazama mgosingwa huku nikijiuliza ameipata wapi leseni yangu.
“Huku nikiendelea na tabasamu
langu la kulazimisha nilimuuliza.
“Mgosingwa umeipata wapi hii
leseni yangu?’
“Si nimekwambia unatakiwa
polisi?”
Jibu lake hilo
lilizidi kunichanganya na kunifadhaisha. Midomo yangu niliyokuwa ninailazimisha
kutabasamu huku nikiwa na fadhaa ilianza kutatizika na kutetemeka. Sasa
haikuweza tena kutabasamu.
“Mgosingwa unanichanganya.
Sasa nani kakupa hii leseni na kakupa kwa madhumuni gani?” nikamuuliza huku
nikiizuia modomo yangu isitetemeke wakati nikimuuliza hivyo.
Mgosingwa aligundua kuwa
nilikuwa nimetaharuki. Akacheka. Hata hivyo kwa vile uso wake ulikuwa
umekunjana kutokana na kuendeleza kilevi, kicheko chake hakikuufanya uso wake
upendeze, bali ulionekana kama anataka kulia.
“Mgosingwa hukumbuki uliiacha
wapi leseni yako?” akaniuliza.
Nikatikisa kichwa.
“Sikumbuki” Nilimjibu hivyo
ili nijue ataniambia nini.
“Mgosingwa jana usiku si
ulikuja kule makaburi ukafukua lile kaburi nikakukurupusha”
JE NINI KITATOKEA? TUKUTANE
KESHO PANAPO MAJALIWA