Friday, June 17, 2016

NUSU YA BIDHAA NCHINI NI FEKI


nusu ya bidhaa nchini ni feki

Dar es Salaam.Wakati simu feki zikiwa zimezimwa usiku wa kuamkia leo, imeelezwa kuwa nusu ya bidhaa mbalimbali zinazotumika nchini zikiwamo dawa za binadamu ni feki.

Imeelezwa kuwa asilimia 50 ya bidhaa hasa dawa za binadamu na vifaa vya umeme havina sifa, hivyo kuhatarisha maisha ya watumiaji wake.

Kauli hiyo ilitolewa jana na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi katika utafiti alioufanya kuhusu tatizo la bidhaa feki nchini na kudhaminiwa na Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI).

Utafiti huo, alisema uliwashirikisha watumiaji wa bidhaa 250 na kampuni 47 zinazotengeneza bidhaa mbalimbali nchini.

“Nusu ya bidhaa zilizoko sokoni ni bandia, dawa za binadamu na vifaa vya umeme ni miongoni mwa bidhaa hizo; unaweza kuona namna hali ilivyo mbaya kwa maisha ya binadamu,” alisema.

Alisema watu wengi wanashindwa kutofautisha kati ya bidhaa bandia na bidhaa halisi, kwa sababu ya uelewa mdogo.

“Katika jamii yetu wako wanaotumia dawa bandia na hawaponi magonjwa wanayoumwa na wengine kufunga vifaa bandia vya umeme kwenye nyumba zao na kusababisha ajali za moto, mambo haya yanaweza kuleta maafa,” alisema.

Profesa Ngowi alisema wako wanaonunua bidhaa hizo kwa sababu ya umaskini.

“Baadhi wanazifahamu bidhaa halisi, lakini wananunua za bandia kwa sababu ya kutokuwa na uwezo,” alisema.

Akitoa mfano kwa wauzaji wa vipuri vya magari, Ngowi alisema wamekuwa wazi kuwaeleza wateja kuwa wanauza bidhaa bandia na bidhaa halisi.

“Hapo mnunuzi unachagua ununue bidhaa halisi ambayo bei yake ni kubwa au ununue bidhaa bandia, ambayo bei yake ni ndogo,” alisema.

Serikali yakosa mapato

Alisema Serikali inakoseshwa mapato kwa sababu waingizaji wa bidhaa bandia hawalipi kodi, kwa vile zinaingizwa nchini kwa kutumia njia zisizo rasmi.

“Nchi yetu ni kubwa yenye njia nyingi zisizo rasmi ambazo bidhaa hizo zinapitishwa, wakati umefika kwa Serikali kuweka mikakati ya kuzizuia,” alisema.

Alipendekeza Serikali kuongeza udhibiti katika njia zisizo rasmi na kushirikiana na kampuni zinazozalisha bidhaa, kuwaelimisha wananchi ili waweze kutambua bidhaa halisi na bidhaa bandia.

Alisema Serikali inatakiwa kuongeza vituo vya ukaguzi kwenye njia zisizo rasmi ili kudhibiti bidhaa hizo.

Alisema nchi ambazo ni maarufu kwa uingizaji bidhaa bandia nchini ni China, India, Indonesia, Taiwan, Singapore, Malaysia, Thailand, Chile, Afrika Kusini, Kenya, Msumbiji na Malawi.

Akichangia kuhusu utafiti huo, Ofisa Mwandamizi wa Tume ya Ushindani nchini (FCC), Braise Freedom alisema tume hiyo imekuwa ikitangaza kuhusu bidhaa feki kupitia vyombo vya habari.

Alisema kampuni zinatakiwa kuwaelimisha wananchi kuhusu bidhaa mbalimbali wanazozitengeza ili waweze kuzitofautisha na bidhaa feki.

Kwa upande wake, Mtafiti Ellis De Bruijin wa kampuni ya Compol Associates Ltd ya jijini Nairobi, alisema tatizo la bidhaa feki lipo katika sekta nyingi nchini.

Akitoa mfano, alisema hata baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikitoa habari ambazo si za kweli na kwamba hali hiyo ni sawa na uzalishaji wa bidhaa feki.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa CTI, Evarist Maembe alisema wametoa udhamini wa utafiti huo ili shirikisho hilo liweze kupata mapendekezo na kutoa ushauri kwa Serikali ili iweze kuchukua hatua.

Alisema kunapokuwa na bidhaa feki sokoni, kampuni zinashindwa kushindana na kusababisha kupunguza wafanyakazi, hali ambayo baadaye kampuni huja kulaumiwa kwa kutoajiri watu.

No comments:

Post a Comment