SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572
MWANAMKE 23
ILIPOISHIA
Mama akamuga mwenzake kisha akaingia kwenye kile chumba alichokuwemo mganga
akaagana naye kisha
akatoka.
Tulitoka nje tukapanda
pikipiki na kuondoka.
“Dawa inanuka kweli!”
nikamwambia mama.
“Dawa za kufukuza mashetani
ndivyo zilivyo, vumilia tu”
Nilipomfikisha mama nyumbani
kwake, nikaenda Msambweni nilikokuwa nikiishi.
Licha ya kuwa na hofu sikuona tatizo
lolote usiku ule. Nikalala hadi asubuhi.
Wakati naamka, shuka za
kitanda na ile niliyojifinika zilikuwa zikinuka ile harufu ya dawa za mganga.
Niliziondoa kitandani nikatandika zingine kisha
nikaenda kuoga. Licha ya kujisugua kwa sabauni zaidi ya mara moja, ile harufu
bado nilikuwa nikiisikia mwilini mwangu.
Nilikwenda mkahawani nikanywa
chai kisha nikapanda pikipiki yangu na kuelekea Chuda kwa kaka yangu.
Nilipofika nilimueleza
nilivyoshughulikiwa na yule mganga na alivyonieleza kuwa niende tena siku ile.
“Jana usiku yule mwanamke
hakukufuata?” akaniuliza.
“Sikumuona lakini nadhani kama nisingekwenda kwa
yule mganga wa Amboni, angenifuata. Naamini zile dawa ndizo zilizomzuia”
“Sasa leo utaakwenda na mama
au utakwenda peke yako?”
“Nitakwenda kumsikiliza mama,
kama atasema twende tutakwenda”
“Hata kama atakwambia uende
peke yako wewe nenda tu, ukirudi
utakuja kunieleza”
“Sawa kaka”
SASA ENDELEA
Nyumbani kwa mama nilimkuta
mama akinisubiri. Nilipomuuliza kuhusu safari ya Amboni
akaniambia tutakwenda sote. Mama yangu alikuwa na huruma sana. Nikampakia kwenye pikipiki tukaenda Amboni.
Tulipofika tulimkuta mganga
akiwa kwenye chumba chake cha uganga akishughulika. Tulisalimiana naye
akatuambia tumsubiri nje. Baada ya muda kidogo alitoka nje. Uso wake ulikuwa
umefadhaika sana.
Akatuambia.
“Jana niliwambia mje
lakini
usiku nilipolala yule jini wako alinifuata na kuniletea vitisho vikali
sana. Aliniambia kuwa kama nitaendelea kukushughulikia kitanikuta kile
kilichomkuta mganga wa Mnyanjani. Kwa kweli nilipata hofu
sana”
“Lakini jana si ulituambia
kuwa huyo jini unaweza hata kumpiga makofi?”
“Baba! Ni kweli nilisema
lakini sikujua kama jini mwenyewe ni yule
aliyenifuata. Yule jini ni mkali. Alipokuja, majini yangu yalinywea”
Maneno ya mganga huyo
yalinifanya nimtazame mama. Mama naye akanitazama kwa mshangao.
Kama ambaye aligundua kuwa maneno yake yalikuwa
yamemdhalilisha mwenyewe mganga huyo aliendelea kutuambia.
“Sidhani kama utaweza
kuepukana na jini yule. Ameniambia kuwa hakuna atakayeweza kuwatenganisha,
atakuwa na wewe mpaka kufa”
“Yaani ameshajihakikishia ushindi?” Mama akamuuliza
kwa mshangao.
“Yeye mwenzetu ni jini, sisi
ni binaadamu. Anatuona lakini sisi hatumuoni mpaka anapotaka mwenyewe” Mganga
akasema.
“Sasa unatushauri nini?”
“Lakini huyu jini hana
matatizo kama mnavyomdhania, tena ni jini
tajiri na kisha ni mganga, kwanini hutaki kuwa
naye?” Mganga akaniuliza.
“Siwezi kuwa na mke jini
wakati mimi mwenyewe ni binaadamu. Nitaishi naye vipi?” Nikamuuliza mganga.
“Sasa utafanyaje wakati ameshakuchunuka?”
“Nitajitahidi kuhangaika kwa
waganga wengine”
“Ukibahatika
kwenda Pemba naamini unaweza kupata waganga ambao
wataweza kukusaidia. Wapemba ni hodari sana
kwa majini”
“Kama hakuna budi nitafika
hata huko Pemba”
“Kama
utaweza kwenda naamini utafanikiwa”
Tuliondoka kwa yule mganga
tukiwa tumenywea. Mategemeo yangu yote yalififia ghafla. Suala lile sasa lilianza
kunipa changamoto kali.
“Maneno ya yule mganga
yamenitisha sana”
Nilimwambia mama wakati namuendesha.
“Hakuna lisilo na mwisho,
jini si Mungu, usitishike mwanangu. Endelea kumuamini Mungu. Jini ni kiumbe kama wewe naye ameumbwa na Mungu. Mungu ndiye wa
kumuogopa”
Maneno ya mama yalinipa
matumaini kidogo. Nilipomfikisha nyumbani kwake aliendelea kuniambia.
“Makosa yetu ndiyo
yanayotuponza. Imani za watu zimekuwa ndogo sana katika dini. Watu wanapenda dunia zaidi.
Sasa vile vitu ambavyo vilipaswa kuwa chini yetu vinakuwa juu yetu. Mwanaadamu
ndiye aliyetakiwa kutawala dunia hii lakini baada ya watu kupunguza kumcha
Mungu, sasa majini yanataka kututawala sisi”
“Leo mama umeniambia maneno
ya akili na ya kufikirisha sana”
nikamwambia mama.
“Rudi nyumbani na muamini
Mungu wako, jini hatakufuata”
“Asante mama”
Nikaondoka na pikipiki yangu
kurudi nyumbani nikiwa na imani tele. Nilijiambia kama mimi ndiye niliyepaswa
kuwa mtawala wa dunia hii sitakubali jini anitawale wala kunitia hofu.
Ni kweli imani ina nguvu,
nilikaa wiki nzima bila kuona kitisho chochote. Nikaona kama
vile tatizo langu lilikuwa limekwisha.
Wiki iliyofuata nikiwa kazini
kwangu, tuliendelea kufanya biashara hadi saa kumi jioni, yaani siku ile
kulitokea biashara ya ajabu. Tulipata wateja wengi kutoka vijijini kwa vile
ulikuwa msimu wa kuuza mazao.
Nikajikuta nilikuwa na pesa
nyingi kwenye dawati langu. Muda huo sikuweza kuzifikisha pesa hizo benki kwa
sababu benki zilikuwa zimeshafungwa.
Nilizihesabu pesa hizo,
zilikuwa shilingi milioni kumi. Hizo zilikuwa za mauzo ya jioni tu, za mauzo ya
asubuhi na mchana zilishapelekwa benki.
Nikaamua kuziacha pesa hizo
kwenye dawati langu kwa vile nilifunga kitasa kwa funguo. Tukafunga duka na
kuondoka.
Asubuhi ya siku ya pili yake
nilikwenda kazini kama kawaida. Nilipofika
kitu cha kwanza nilitaka nizitoe zile pesa ili zipelekwe benki. Nilipofungua
dawati sikuona kitu.
Nikashituka na kutumbua macho
yangu. Sikutosheka kutazama kwa macho, nilitia mkono wangu na kupapasa.
Hakukuwa na kitu. Dawati lilikuwa tupu kama
mkono uliorambwa!
“Pesa za watu zimewenda wapi
jamani?” nikajiuliza kwa fadhaa.
Meza yangu ilikuwa na
madawati matatu. Pesa niliziweka katika dawati la juu. Baada ya kuzikosa pesa
katika dawati hilo
nilianza kuzitafuta katika madawati ya chini yake japouwa nilikuwa na hakika
kuwa pesa hizo niliziweka katika dawati la juu.
Nilikuwa kama niliyerukwa na
akili. Licha ya kupekua kwenye madawati yote matatu, pesa sikuziona. Akili
yangu ilikuwa haiamini kama pesa hizo
hazikuwemo kwa sababu niliziweka mwenyewe na dawati nililifunga kwa funguo.
Nikarudi tena kwenye dawati
la juu kutazama tena. Nikaja kwenye dawati la pili na la tatu. Lakini hakukuwa
na pesa.
Ule mchezo wangu wa kufungua
madawati kuanzia la juu hadi la chini na kisha kurudia tena, uliwashitua wafanyakazi wenzangu
wakaanza kuniuliza ninachotafuta.
“Amour mbona umeshughulika sana, unatafuta nini?”
Mfanyakazi mmoja akaniuliza.
“Natafuta pesa. Jana
tulipoondoka niliacha shilingi milioni kumi katika dawati hili la juu, sasa
sizioni!” nikamwambia.
“Zimekwenda wapi?”
“Sijui!”
“Kwani ulipoondoka
hukulifunga?”
“Nililifunga na funguo
niliondoka nazo, sasa nashangaa pesa sizioni!”
“Haiwezekani! Hebu tazama
vizuri”
“Nimetafuta sana, pesa hazimo. Sijui nani amezichukua!”
“Na haiwezeani zichuuliwe na
mtu wa sababu funguo uliondoka nazo mwenyewe”
Nikanyamaza kimya huku macho
yangu yakitanga tanga kwenye meza.
Wafanyakazi wengine
waliposikia mazungumzo yetu wakasogea karibu.
“Umepoteza nini, pesa?” mfanyakazi mmoja akaniuliza.
“Ndio pesa”
“Uliziweka wapi?”
“Nilizizifungia kwenye dawati
hili hapa jana jioni tulipotoka kazini, sasa nashangaa pesa sizioni”
PESA ZA WATU ZIMEKWENDA WAPI
JAMANI? HII IMESHAKUWA BALAA SASA! TUONANE HAPO KESHO.
No comments:
Post a Comment