Friday, June 24, 2016

MWANAMKE SEHEMU YA 27

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572

MWANAMKE 27

ILIPOISHIA

Kaka akashituka.

“Zimeonekana wapi?”

“Kwenye droo”

“Droo ya nani?”

“Droo yangu”

“Zimeonekana kivipi?”

“Ni tukio la ajabu sana” nikamwambia kisha nikamueleza jinsi tulivyozikuta pesa hizo kwenye droo yangu.

“Una maana huyo aliyeiba ameamua kuzirudisha?”

“Itakuwa ndio hivyo”

“Kwa hiyo zile pesa alikuwa amezificha sehemu nyingine, alipoona unapelekwa polisi akaamua kuzirudisha”

“Bila shaka. Lakini sasa nimepata fundisho sitaacha pesa tena kwenye droo yangu kwa maana wanataka kunitoa kafara”

“Ni tukio ambalo sikulitarajia”

“Naona dua za mama zinafanya kazi. Mama aliniombea sana”

“Wakati tunavuka barabara tukapishana na msichana mmoja ambaye naye alikuwa anavuka kutoka upande ule tuliokuwa tunakwenda sisi. Alinitupia jicho mara moja ili kujua kama nimemuona.

Nukta ile ile nikamtambua.

Alikuwa Zena!

SASA ENDELEA

Niliendelea kuvuka barabara huku uso wangu nimeugeuza nyuma  nikimtazama yule msichana.

Baada ya yeye kunitupia macho mara moja tu, aliugeuza mbele uso wake akaendelea na safari yake. Mimi ndiye niliyekuwa nikiendelea kumtazama.

Kaka yangu alikuwa akinisemesha bila kujua kwamba akili yangu ilikuwa imeshughulishwa na kitu kingine.

Tulipomaliza kuvuka barabara nilimuona Zena akikata kona kwenye jengo lililokuwa na ofisi yetu na kupotea

Hapo ndipo nilipomshitua kaka.

“Nimemuona zena!” nikamwambia.

“Zena….Zena yupi?” akaniuliza.

“Yule msichana wa kijini”

Kaka akageuka kwa hamaki.

“Yuko wapi?”

“Wakati sisi tunavuka barabara na yeye alikuwa anavuka kutoka huku kwenda kule upande wa pili. Tulipishana katikati ya barabara. Nimemuona na yeye ameniona lakini hakunisemesha kitu”

Kaka alikuwa akigeuza uso huku na huku kumtafuta.

“Yuko wapi sasa?”

“Ameshakata kona kwenye hili jengo, hebu njoo tumuangalie”

Tukasogea kwenye ile barabara aliyoelekea Zena na kumchungulia.

Hatukumuona tena.

“Ameshapotea”

“Ungenishitua pale pale ulipomuona” Kaka akaniambia

“Sijui anatoka wapi na anakwenda wapi?”

“Labda ana safari zake mwenyewe”

“Unajua tangu nilipokwenda kwa mganga wa Amboni sjakutana naye hadi hii leo!”

“Lakini yule mganga si alisema asingeweza kumuondoa”

“Alituambia hivyo lakini mama alinipa moyo. Niliamini Mungu”

Baada ya kutomuona yule msichana tukawa tunatembea kurudi nyumbani.

“Sasa ni kwanini unarudi nyumbani?” Kaka akaniuliza.

“Nimeomba mapumziko ya siku moja, unajua ule msukosuko ulikuwa mkubwa”

“Ni kweli inabidi upumzike”

Tulitangulia kwenda kwa mama. Aliponiona nikiwa na uso wa tabasamu alishangaa.

“Imekuwaje wanangu?” akatuuliza.

“Kesi imekwisha mama, dua zako zimesaidia” nikamwambia huku nikiendelea kutabasamu

“Imekwisha kivipi?”

“Zile pesa zimeonekana” Kaka ndiye aliyejibu.

“Zimeonekana!” mama akauliza kwa mshangao.

“Kuna mchezo walinichezea pale kazini” nikamwambia mama.

“Hebu nielezeni vizuri Nataka kujua hizo pesa zimeonekana wapi?”

Nikamueleza tukio lilivyotokea.

“Wenzako unaofanya kazi nao si wazuri” mama akaniambia na kuongeza.

“Jihadhari nao”

“Nimemwambia hivyo hivyo, kesho na kesho kutwa wanaweza kukufanyia tena” Kaka akasema.

“Nimepata fundisho. Sitaacha tena pesa kwenye droo, hata iweje”

“Usiache mwanangu, utajitafutia matatizo ya bure”

Tuliongea mengi na kaka yangu pamoja na mama yangu. Baadaye mimi na kaka tukaondoka kwa mama. Nilimpeleka kaka Chuda kisha nikarudi nyumbani kwangu.

Nilipofika nilipanda kitandani nikajilaza. Wakati nawaza hili na hili usingizi ukanipitia nikalala. Wakati niko usingizini nikaota ilikuwa ni siku ile niliyoweka pesa kwenye droo yangu. Usiku wake Zena akafika kwenye mlango wa duka letu.

Alisimama mbele ya mlango wa duka hilo, milango ukafunguka yenyewe. Akaingia ndani.

Alikwenda hadi ilipokuwa meza yangu akavuta ndroo ambayo ilifunguka. Akachukua zile pesa nilizokuwa nimeziweka akazitia kwenye pochi yake. Wakati akifanya hivyo nilimsikia akisema. “Akijifanya anajua vile na mimi najua hivi, atakoma!”

Alipozitia zile pesa kwenye mkoba wake akatoka. Alipotoka ile milango ya duka ikajifunga yenyewe.

Wakati ule nahangaika kutafuta zile pesa Zena alikuwa yuko mle ofisini lakini alikuwa haonekani. Mpaka siku ile ambayo nilipelekwa polisi alikuwa amekwenda tena usiku kwenye duka letu akazirudisha zile pesa alizokuwa amezichukua kwenye droo yangu kisha akafunga ndroo na kutoka.

Vile nilivyokuwa napelekwa polisi Zena alikuwa ameketi kando yangu kwenye gari lakini tulikuwa hatumuoni. Wakati ule nahojiwa na polisi na yeye alikuwa akisikiliza.

Niliporupi ofisini na polisi Zena alikuwa yuko sambamba na mimi hadi zile pesa zipoonekana.

Sasa wakati ule navuka barabara nikiwa na kaka alijipitisha kusudi ili nimuone kisha akapotea.

Nikazinduka usingizini. Wakati nazinduka niliisikia sauti ya Zena ikiniambia.

“Hilo ni onyo!”

Nikadhani kwamba zena alikuwa mule chumbani. Nilipofumbua macho nikainuka na kuketi, nikaanza kutazama huku na huku kwa hofu kwamba ningemuona Zena mle chumbani. Lakini sikumuona.

Nikashuka kitandani na kutoka sebuleni ambako nilikaa kwenye kochi na kuifikiria ile ndoto.

Hapo ndipo nilipoanza kufahamu kuwa zile pesa zilikuwa zimechukuliwa na Zena ili kunikomoa. Nikajiambia kama asingezirudisha ndio ningekiona cha moto.

“Huyu msichana ataendelea kuniamndama hadi lini?” nikajiuliza.

Nilihisi kwamba kama sitachukua hatua thabiti za kuhakikisha kwamba ninaepukana naye, mwisho wake anaweza kunitia katika matatizo makubwa.

Baada ya kufikiri sana nilitoa pikipiki yangu nikaenda kumueleza mama kuhusu ile ndoto. Mama naye alistaajabu.

“Kumbe bado anakufuatilia!” akaniambia

“Huyu jini atakuja kunitia kwenye matatizo makubwa hapo baadaye” nikamwambia mama.

“Sasa fanya mpango wa kwenda huko Pemba”

“Inabidi nipate mwenyeji au mtu wa kufuatana naye ndio nitaweza kufika”

YAAP! Je jamaa huyo atakwenda pemba na nini kitatokEa? Tukutane tena hapo kesho hapa hapa tangakumekuchablog


No comments:

Post a Comment