SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE 22
ILIPOISHIA
Baada ya sekunde chache yule
mganga akaanza kusema maneno niliyodhani kuwa yalikuwa ya lugha ya Kijerumani.
Nilisikia maneno kama “Dachi…pontia…na mengine ambayo sikuweza kuyakariri.
Wakati huo uso wake alikuwa
ameufunika ndani ya shuka. Ghafla akafunua shuka na kuutoa uso wake.
Alikisogeza kile chetezo pembeni kisha
akatutazama.
“Dachi…jerumani nimekuja
hapa” akasema lakini hatukuelewa maana ya maneno yale.
Mke wa mganga akatueleza.
“Anasema yeye ni jini wa
Kijerumani anaitwa Dachi, amekuja kuwasikiliza”
“Sawa, tumemuelewa” Mama
akamjibu.
“Asalaam aleykum” mganga
akaendelea kwa kutupa salamu.
“Wa alaykumu salaam”
tukamuitikia.
“Nini shida yenu?”
“Mwanangu anasumbuliwa na
jini mwanamke” Mama akamwambia.
“Mwanao yuko wapi?”
“Huyu kijana niliyenaye hapa”
“Oh mwano amepata mchumba wa kijini,
anaitwa Zainush”
Mgnga huyo alipotuambia hivyo
mimi na mama tukatazamana. Tulitazamana kwa mshangao kwa jinsi alivyoweza kujua
lile jina la Zena ambalo hatukuwa tumelitaja.
“Mwanangu hataki mchumba wa
kijini, tunataka aondoke asimfuate tena mwanangu” Mama akamwambia.
SASA ENDELEA
“Yule jini ni mkorofi, ameshaua watu watatu”
Mganga huyo aliendelea kutuambia.
Tukatazamana tena na mama.
Mama hakulieleza suala hilo
la watu waliouawa, yaani yule mganga wa Mnyanjani na wale vijana wawili
walioiba mkoba wa Zena.
Tukawa tunajiuliza amelijuaje
tukio hilo la
kuuawa kwa yule mganga na wale vijana.
Kama ambaye aliyagundua mawazo yetu, mganga huyo akacheka.
“Huyo jini anakufuata wewe
kila wakati, ameshapata
wasiwasi. Anajua unataka kumfukuza” akatuambia.
Alinyamaza kimya kisha akaendelea.
“Lakini mimi haniwezi, naweza
kumpiga makofi mara moja”
“Sasa utatusaidiaje?”
nikamuuliza mganga huyo.
“Mimi naweza kumuita halafu
nitamfunga kamba, hataweza kukufuata tena”
“Utamuita lini?” nikamuuliza
tena.
“Nitamuita kesho”
“Sasa leo akija kunidhuru
usiku?”
“Nitamzuia” Mganga akaniambia
kisha akaitenga
shuka na kunyanyuka.
“Nisubirini hapa hapa”
akatuambia na kutoka.
Tulisubiri kwa karibu nusu
saa. Mke wake alituambia kuwa mganga huyo alikuwa amekwenda kuchuma dawa
makaburini.
Aliporudi alikuwa ameshika rundo la majani,
akampa mke wake.
“Yaroweke kwenye maji”
alimwambia.
Mke wake aliyekuwa ameketi na
sisi aliinuka na kuyachukuaa yale majani.
“Changanya na huu mvuje”
Mganga aliendelea kumwambia mke wake huku akielekea kwenye meza iliyokuwa na
chupa na makopokopo. Alichukua kopo mojawapo akachota kiasi cha mvuje uliokuwa
umesagwa na kumpa mke wake.
Baada ya hapo mganga alirudi
kwenye kigoda chake.
“Nimekutayarishia dawa ambayo
utakwenda kuoga na nyingine utajifukiza” akaniambia.
“Sawa. Kwa hiyo nitakwenda
kuoga nyumbani?”
“Hapana. Utaoga hapa hapa na
utajifukiza hapa hapa”
“Sawa”
Baada ya kama
dakika tano hivi mke wa mganga alirudi akiwa amebeba ndoo ya maji ambayo
aliitia yale majan.
“Tayari”
akasema.
“Sasa nenda kamuwekee chooni”
Mgnaga akamwambia.
Mwanamke huyo akaibeba tena
ndoo hiyo na kutoka nayo.
Mganga akanitazama.
“Mfuate, utakwenda kuyaoga
yale maji yote” akaniambia.
Nikanyanyuka na kumfuata yule
mwanamke. Tulitoka uani mwa ile nyumba. Mwanamke huyo aliingia kwenye choo
akaiweka ile ndoo kisha
akatoka.
“Haya nenda sasa’ akaniambia.
Nikaingia kwenye kile choo.
Nilivua nguo nikazitundika kwenye mlango wa choo. Niliona kata iliyokuwa
imetiwa kwenye ndoo nyingine niliyoikuta mle chooni, nikaichukua na kujimwagia
yale maji. Yalikuwa yakinuka harufu mbaya sana
isiyovumilika.
Lakini kwa vile nilikuwa na
shida nilivumilia hivyo hivyo. Nilipomaliza nilijifuta futa maji kwa mikono kisha nikavaa nguo zangu
na kutoka na ile ndoo ambayo niliiacha pale uani.
Nilienda kule chumbani kwa
mganga huku maji yakiwa yametosa shati langu.
“Umeshaoga?”
Mganga akaniuliza.
“Nimeoga” nikamjibu.
“Umemaliza
maji yote?”
“Nimeyamaliza yote”
“Sasa bado dawa ya
kujifukiza” Mganga aliniambia kisha
akawageukia mke wake na mama yangu.
“Hebu mpisheni ajifukize
dawa” akawambia.
Mama yangu na yule mwanamke
wakatoka.
Mganga akanipa shuka.
“Vaa shuka. Vua nguo zako kisha chutama ujifukize
dawa”
Nikajifunga ile shuka kiunoni
kisha nikavua
suruali yangu pamoja na shati. Mganga alinisogezea kile chetezo cha moto.
Akakitia aina fulani ya dawa ya unga. Chetezo kikawa kinatoa moshi.
Nilikuwa nimeshachutama. Ile shuka ndio nilijifunika
kukinga ule moshi uingie mwilini mwangu. Harufu yake ilifanana na yale maji
niliyooga.
Wakati ule moshi ukinipata
mwilini. niliisikia sauti ya mganga akisema maneno kwa lugha ambayo sikuweza
kuijua huku akilitaja jina la Zainush.
Moshi ulipokwisha, mganga
aliniambia nininuke na nivae nguo zangu. Nikainuka na kuvaa nguo.
“Sasa kazi yako imekwisha kwa
leo, rudi nyumbani ila kesho asubuhi uje tena” Mganga akaniambia.
“Hii kazi yaa leo ni shilingi
ngapi?” nikamuuliza mganga huyo.
“Kwa leo utanipa shilingi
elfu ishirini”
“Nikatoa shilingi elfu
ishirini na kumpa mganga huyo.
“Sasa mnaweza kwenda zenu”
“Yule jini hataweza kunifuata
tena leo?” nikamuuliza.
Mganga akatikisa kichwa.
“Hawezi kukufuata. Hiyo
harufu unayonuka hataweza hata kukusogelea”
“Nashukuru sana’
“Ila kumbuka kitu kimoja. Ukifika
nyumbani usioge tena. Lala hivyo hivyo”
“Sawa”
Baada ya kumalizana na mganga
huyo nilitoka ukumbini.
Mama yangu alikuwa amekaa na mke wa mganga, nikamwambia.
“Twenzetu”
“Umeshamaliziwa?”
Mama akaniuliza.
“Tayari”
Mama akamuga mwenzake kisha akaingia kwenye kile chumba alichokuwemo mganga
akaagana naye kisha
akatoka.
Tulitoka nje tukapanda
pikipiki na kuondoka.
“Dawa inanuka kweli!”
nikamwambia mama.
“Dawa za kufukuza mashetani
ndivyo zilivyo, vumilia tu”
Nilipomfikisha mama nyumbani
kwake, nikaenda Msambweni nilikokuwa nikiishi.
Licha ya kuwa na hofu sikuona tatizo
lolote usiku ule. Nikalala hadi asubuhi.
Wakati naamka, shuka za
kitanda na ile niliyojifinika zilikuwa zikinuka ile harufu ya dawa za mganga.
Niliziondoa kitandani nikatandika zingine kisha
nikaenda kuoga. Licha ya kujisugua kwa sabauni zaidi ya mara moja, ile harufu
bado nilikuwa nikiisikia mwilini mwangu.
Nilikwenda mkahawani nikanywa
chai kisha nikapanda pikipiki yangu na kuelekea Chuda kwa kaka yangu.
Nilipofika nilimueleza
nilivyoshughulikiwa na yule mganga na alivyonieleza kuwa niende tena siku ile.
“Jana usiku yule mwanamke
hakukufuata?” akaniuliza.
“Sikumuona lakini nadhani kama nisingekwenda kwa
yule mganga wa Amboni, angenifuata. Naamini zile dawa ndizo zilizomzuia”
“Sasa leo utaakwenda na mama
au utakwenda peke yako?”
“Nitakwenda kumsikiliza mama,
kama atasema twende tutakwenda”
“Hata kama atakwambia uende
peke yako wewe nenda tu, ukirudi
utakuja kunieleza”
“Sawa kaka”
WASOMAJI MPO? MAMBO
YATAENDELEA KESHO.
MSIKOSE.
No comments:
Post a Comment