SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE 21Inaletwa kwenu na kituo cha Elimu Cha New Age Centre Tanga, New Age ni mabingwa wa Ufundishaji na Ufaulishaji wanafunzi wanaorisiti na kujiendeleza, New Age wapo Tanga mkabala na TOYOTA, wanapokea wanafunzi wa kozi fupi na ndefu pamoja na wanaojiendeleza kielimu maofisini, simu 0717 713866
ILIPOISHIA
Nikatazamana tena na mama
yangu, sasa kwa mshituko.
“Dakika chache tu zilizopita
si nilikuwa naye hapa?” nikauliza.
“Kufariki kwake kulikuwa kwa
miujiza sana.
Niliambiwa alikuwa akizungumza na mteja wake mmoja aliyefika na pikipiki,
nafikiri ulikuwa wewe”
“Nadhani nilikuwa mimi kwani
si muda mrefu sana
nilipoondoka hapa”
“Basi mara tu ulipoondoka,
yule mganga aliingia chumbani mwake. Mke wake alikuwa jikoni akasikia sauti ya
mume wake akipiga kelele kuwa anakabwa na mwanamke. Mpaka mke wake anaingia
chumbani alimkuta ameshakufa”
“Nikaguna na kumtazama mama.
“Mama umelisikia hilo tukio?”
“Nimelisikia” Mama akajibu
kwa sauti iliyonywea kisha
akaniambia.
“Basi twende zetu”
“Nilikuwa nimempa pesa kwa
ajili ya kunifanyia kazi yangu ambayo tulipatana aifanye kesho lakini
nitamsamehe” nikasema.
“Ulimpa kiasi gani?’ yule mtu
akaniuliza.
“Kama
laki mbili hivi. Lakini nitasamehe”
“Kama
umeamua kuzisamehe ni jambo zuri”
“Poleni sana kwa msiba huo” nikamwambia na kupanda
kwenye pikipiki yangu.
“Haya kwaheri baba” Mama
akumuaga yule mtu kabla ya kukaa nyuma yangu. Tukaondoka.
SASA ENDELEA
“Mama umeona mambo hayo!”
nikamwambia mama wakati ninaendesha pikipiki kurudi mjini.
“Nimeona. Kwa kweli ni kifo
cha kushangaza sana”
“Mimi nadhani ni yule jini
amekuja kumuua yule mganga”
“Itakuwa ndiye yeye, kwa
sababu alisema kuna mwanamke anamkaba. Sasa alikuwa mwanamke yupi kama sio yule jini?”
“Sasa haya yamekuwa
mapambano!”
“Tutatafuta mganga mwingine”
“Sasa usalama wangu
utakuwa wapi? Nimeshashuhudia
watu wawili waliouawa leo. Yule kijana aliyekuwa anatandikwa na huyu mganga.
Bado kuna na yule kijana mwingine. Naona pia atakuwa ameshakufa”
“Tukifika tutakwenda
kulizungumza vizuri hili suala pamona na kaka yako”
“Sasa nimeshaona huyu mwanamke ni wa hatari”
Nilimpeleka mama nyumbani
kwake kisha nikaenda Chuda
kumchukua kaka.
Nilimueleza kwa kifupi hayo
matukio.
“Mama ameniambia nije
nikuchkue twende tukayazungumze haya mambo”
Ule muhutasari wa habari
niliomueleza kaka tayari ulikuwa.
Nikampakia kwenye pikipiki
yangu tukaondoka.
Tulipofika nyumbani kwa mama
tukalizungumza lile suala ambalo kaka lilimshitua sana.
“Kumbe yule jini ni hatari sana. Tulivyomuona pale
mahakamani siku ile alionekana ni msichana mpole sana” Kaka akasema kwa mshangao.
“Lile umbile ulilomuona nalo
ni la kujipachika, si umbile lake
halisi.
Katika umbile lake
halisi
anatisha” nikamwambia kaka.
“Kwa kweli inabidi muepukane
haraka, sasa tutafanyaje wakati mtaalamu muliyemtegemea ndio ameuawa kwanza?”
“Itakuja kuwa yeye!” Mama
akamalizia akimaanisha mimi.
“Sasa tufanyeje jamani, jua
linakuchwa hili!” nikawahimiza wenzangu.
“Hapa la kufanya ni kumuona
mganga mwingine haraka iwezekanavyo” Kaka akashauri.
“Bila kupata mganga mwingine,
mimi leo sitalala, nina hofu” nikawambia.
“Usijali, tutkwenda kwa
mganga wa Amboni. Yeye pia namfahamu. Ni
hodari” Mama akasema.
“Sasa twende sasa hivi kwa
sababu jua linakuchwa”
“Ingekuwa kaka yako
anapafahamu angekupeleka lakini itabidi nikupeleke mimi”
“Mpeleke tu halafu mtakuja
kunijulisha” Kaka akamwambia mama.
Dakika chache baadaye
tulikuwa tumetoka nje, nilimpakia mama kwenye pikipiki. Kaka yangu naye
akaondoka kurudi kwake kwa miguu.
Amboni ni kitongoji cha mji wa Tanga kinachokuwa kwa
haraka. Kipo katika barabara ya Horohoro inayokwenda Mombasa
nchini Kenya.
Kutoka Tanga hadi Amboni ulikuwa mwendo upatao
kilometa nane hivi.
Kitongoji hicho kimepata
umaarufu kutokana na mapango yaliyoko katika eneo hilo,
maarufu kama Mapango ya Amboni.
Wakati tunafika Amboni jua lilikuwa limeshakuchwa. Matumaini yangu
yalikuwa madogo sana
kupata huduma katika muda ule. Hofu
yangu kubwa ilikuwa ni kwa usiku. Kama Zena
alikusudia kunifanyia jambo baya lolote, nilijua kuwa alikuwa akisubiri usiku
nikiwa niko nyumbani peke yangu.
Hapo Amboni palikuwa na eneo
linaitwa Mafuriko. Eneo hilo liliwahi kupata
mafuriko makubwa katika miaka ya nyumba na kusababisha kupewa jina hilo.
Mganga tuliyemuendea alikuwa
akiishi katika eneo hilo.
Kwa vile mama aliwahi kufika kwa mganga huyo katika siku za nyuma hatukusumbuka
kuuliza. Tulikwenda moja kwa moja kwenye nyumba yake.
Tulikuta mzee aliyeketi
barazani mwa nyumba hiyo akivuta Mtemba. Alikuwa amekaa kwenye kiti cha uvivu kando ya mlango wa
nyumba yake.
Kumbe alikuwa ndiye mganga
mwenyewe tuliyemuendea.
Tulisaliana naye. Mama
akamwambia kuwa tulikuwa tumemfuata yeye.
“Karibuni ndani” akatuambia.
Nikapata matumaini kidogo.
Mganga huyo alikuwa na chumba
chake maalum cha uganga. Tulipoingia katika chumba hicho alitukaribisha kwenye
majamvi, yeye mwenyewe aliketi kwenye kigoda kidogo kilichokuwa kwenye pembe
moja ya ukuta.
“Habari za huko mtokako?”
akatuuliza.
“Habari si nzuri. Tuna
matatizo” Mama akamwambia.
“Matatizo gani?”
“Ni matatizo ambayo si ya
kawaida. Huyu niliyenaye hapa ni mwanangu. Yeye ndiye anayehusika na hayo
matatizo….”
Mama akamueleza matatizo
yaliyokuwa yametupeleka. Mganga akatuambia.
“Subirini kidogo niwaite
wenyewe muwaeleze”
Akamuita mke wake. Mwanamke
huyo alipokuja alimwambia amletee moto. Baada ya muda kidogo mwanamke huyo
alileta makaa ya moto kwenye chetezo ambacho alikiweka mbele ya mganga huyo.
“Niletee
mavumba yangu na shuka yangu” Mganga akaendelea kumuagiza.
Mwanamke huyo alikwenda
pembeni mwa chumba hicho ambako kulikuwa na meza iliyokuwa na vitabu pamoja na
vichupa na vikopo kopo. Alichukua kikopo kimoja, akatungua na shuka moja ya
rangi nyeupe iliyokuwa imetundikwa kwenye ukuta.
Alikwenda navyo kwa mganga akakiweka
kile kikopo mbele yake kisha
akamfinika ile shuka pale alipokuwa amekaa.
“Na wewe ukae hapa hapa,
usiondoke” Mganga akamwambia mwanamke huyo.
Mwanamke huyo akakaa karibu
yetu.
Mganga alikisogeza kile
chetezo cha moto karibu yake kisha akakifungua
kile kikopo kilichokuwa na mavumba akachota kidogo na kuyatia kwenye ule moto kisha akajifinika shuka
vizuri ili ule moshi uliokuwa unafuka uingie ndani ya ile shuka.
Baada ya sekunde chache yule
mganga akaanza kusema maneno niliyodhani kuwa yalikuwa ya lugha ya Kijerumani.
Nilisikia maneno kama “Dachi…pontia…na mengine ambayo sikuweza kuyakariri.
Wakati huo uso wake alikuwa
ameufunika ndani ya shuka. Ghafla akafunua shuka na kuutoa uso wake.
Alikisogeza kile chetezo pembeni kisha
akatutazama.
“Dachi…jerumani nimekuja
hapa” akasema lakini hatukuelewa maana ya maneno yale.
Mke wa mganga akatueleza.
“Anasema yeye ni jini wa
Kijerumani anaitwa Dachi, amekuja kuwasikiliza”
“Sawa, tumemuelewa” Mama
akamjibu.
“Asalaam aleykum” mganga
akaendelea kwa kutupa salamu.
“Wa alaykumu salaam”
tukamuitikia.
“Nini shida yenu?”
“Mwanangu anasumbuliwa na
jini mwanamke” Mama akamwambia.
“Mwanao yuko wapi?”
“Huyu kijana niliyenaye hapa”
“Oh mwano amepata mchumba wa
kijini, anaitwa Zainush”
Mgnga huyo alipotuambia hivyo
mimi na mama tukatazamana. Tulitazamana kwa mshangao kwa jinsi alivyoweza kujua
lile jina la Zena ambalo hatukuwa tumelitaja.
“Mwanangu hataki mchumba wa
kijini, tunataka aondoke asimfuate tena mwanangu” Mama akamwambia.
ENDELEA KUFUATILIA HAPO KESHO
UJUE NINI KITAKACHOTOKEA.
No comments:
Post a Comment