SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572
MWANAMKE 25
YAAP! TUMEKUTANA TENA. JANA
TULIISHIA WAPI? TULIISHIA HAPA……
TUJIKUMBUSHE.
Nilipofika nyumbani kwa kaka
Chuda, ilikuwa ikikaribia kuwa saa sita mchana.
“Leo hukwenda kazini?” kaka
akaniuliza.
“Nimekwenda lakini kumetokea
matatizo”
“Matatizo gani?”
“Kuna pesa zimeibiwa kwenye
dawati langu”
“Lini?”
“Leo hii”
“Kiasi gani?”
“Shilingi milioni kumi”
Kaka akashituka. Enzi hizo pesa hizo zilikuwa
nyingi sana.
“Zimeibiwaje?”
Nikamueleza kaka jinsi wizi huo
ulivyotokea.
“Inawezekana huyo jamaa
alikuwa na ufunguo mwingine ambao aliutumia kufungua dawati lako akaiba hizo
pesa”
“Ndio hivyo lakini sasa dhima imeniangukia mimi”
“Kwa hiyo umeambiwa nini”
Nitoke nikatafute pesa za
shirika nizirudishe, nimepewa siku mbii tu”
SASA SONGA NAYO…
“Kama
hukuzipata itakuwaje?”Kaka akaniuliza.
“Suala hilo litapelekwa polisi”
“Ukisikia
balaa ndio hilo,
wadhani utazipata wapi milioni kumi?”
“Hiki ni kifungo kinaningoja”
Kaka akatikisa kichwa
kusikitika.
“Nakuhurumia sana mdogo wangu sijui
nitakusaidiaje?”
“Msaada ni kupata hizo pesa
na pesa hazipo”
“Umekwenda
kumueleza mama?”
“Nimekwenda, nimemueleza”
“Amesemaje?”
“Hakuwa na usemi, amesikitika tu”
Wakati ninasema hivyo
nilimuona kaka amezama katika fikira. Nikajua lile tatizo lilikuwa limeugusa
moyo wake.
“Sasa itabidi tusubiri tuone
uamuzi wa wakuu wako” Kaka akaniambia baada ya kimya kifupi.
“Uamuzi! Kuna uamuzi gani
tena kaka zaidi ya kufunguliwa kesi ya wizi. Kwani si nimeshaambiwa
kama pesa hazitapatikana baada ya siku mbili,
hili suala linafikishwa polisi!” Nikamwambia kaka.
Kaka alikuwa amejishika
kichwa akisikitika.
“Kilichobaki sasa ni kuomba
Mungu hizo pesa zipatikane”
Wakati kaka akisema hivyo
mimi nilikuwa kimya.
“Mungu amtie imani huyo aliyeziiba
azirudishe kabla ya hizo siku mbili” Kaka aliendelea kuniombea.
Hakuna mwizi au jambazi
anayerudisha kile alichokiiba lakini kwa vile kaka yangu alikuwa akiniombea
ilibidi nimsikilize.
Siku ile nilishinda bila
furaha na kusema kweli nilishindwa hata kula chakula. Nilikwenda nyumbani
kulala tu.
Siku ya pili yake nilikwenda
kazini. Mhasibu aliponiona akaniita ofisini kwake. Nilipokwenda aliniuliza kama nimefanikiwa kupata zile pesa.
“Sijazipata bosi”
nikamwambia.
Uso wa mhasibu ukaonesha
kuhamaki.
“Unajua kuwa zile ni pesa za
shirika?” akaniuliza kwa ukali
kidogo.
“Ninajua bosi”
“Na unajua kuwa nilikupa siku
mbili urudishe
zile pesa?”
“Ninajua”
“Kama
unajua hivyo sawa. Kesho uje na hizo pesa vinginevyo sitakuelewa”
Sikuwa na jingine la kumjibu
zaidi ya kumuitikia. Nilishajua kuwa nisipokuja
na pesa hizo atanifikisha polisi. Na mimi nilikuwa nimeshajitolea kwenda jela.
Siku ile nilishinda kazini
hadi muda wa kutoka kazini nikatoka na wenzangu. Tulipokuwa nje baadhi ya
wafanyakazi wenzangu waliniuliza kuhusu upotevu wa zile pesa. Kila mtu
alionekana kushangaa jinsi pesa hizo zilivyoibiwa.
“Nimepewa siku mbili
nizirudishe hizo pesa vinginevyo suala litafikishwa polisi kwa hatua zaidi”
nikawambia.
Kila mtu aling’aka na
kunihurumia.
“Sasa ni nani aliyefanya
mchezo huo. Hapa kazini kweli hakuna mchezo wa kuibiana pesa” Mfanyakazi mmoja
akaniambia.
“Hata mimi nashindwa kuelewa”
Baadhi ya wafanyakazi
wenzangu walikuwa wamenizunguka wakinisikiliza na kunihoji. Baadaye
tulichangukana tukarudi majumbani.
Lakini mimi sikurudi
nyumbani. Nilikwenda nyumbani kwa mama. Ukiwa
na mama, hata ukiwa
mtu mzima utamdekea tu. Pale kwa mama ndipo nilipopaona mahali muafaka wa
kupeleka kilio changu ingawa hakuwa na uwezo wowote lakini alikuwa ni mama.
Nikamueleza mama yaliyojiri
huko kazini kwangu. Nikamwambia kwamba kesho ndio natakiwa kupeleka hizo pesa
vinginevyo ninafikishwa polisi.
“Itabidi hapo kesho uende
kazini na kaka yako ili litakalotokea aweze kulijua” Mama akaniambia.
Jioni ile ile nilikwenda kwa
kaka nikamueleza na tukakubaliana kwamba nimpitie asuhuhi anisindikize kazini.
Siku ile nilipanga vizuri
vitu vya nyumbani nikijua kwamba kesho yake ninakwenda jela. Usiku wake
sikupata usingizi kwa mawazo.
Nakumbuka nilipata usingizi
majira ya saa kumi alfajiri nikaota ndoto ya kutisha. Niliota nimesimamishwa kizimbani nikihukumiwa kwa
kosa la wazi wa fedha za shirika.
Hakimu aliniambia. “Ushahidi
uliotolewa hapa mahakamani umeonesha na kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba
umeiba shilingi milioni kumi fedha za shirika ukiwa
mfanyakazi wa shirika hilo.
Hivyo mahakama hii imekutia hatiani”
Hakimu akainua uso wake na
kunitazama kisha
akaniuliza.
“Una lolote la kuiambia
mahakama hii kwanini isikupe adhabu kali?”
“Mheshimiwa hakimu ninaiomba
mahakama yako tukufu isinipe adhabu kali kwa kuzingatia kuwa fedha zenyewe
sikuziiba mimi na kwa kweli sijui zimeibiwa na nani” nikasema.
Hakimu akaandika maelezo
yangu kisha
akainua tena uso wake na kuniambia.
“Maelezo yako hayawezi
kuizuia mahakama hii isikupe adhabu kali. Ninakuhukumu kifungo cha miaka
thelathini jela ili iwe fundisho kwa wengine”
Hapo hapo nikaacha mdomo wazi
kwa mshangao kama ambaye sikuamini kuwa
nilihukumiwa kifungo hicho. Uso wangu ukiwa umenywea nilimtazama mama
yangu na kaka yangu waliokuwa wamekaa katika safu za mbele.
Nikamuona mama yangu anaangua
kilio akinililia…
Sauti yake ya kizee ndio
iliyoniamsha usingizi. Wakati nazinduka moyo ulikuwa ukinienda mbio na mwili wote
ulikuwa umenitota jasho. Nilijiinua kitandani nikaketi.
Nikajiuliza, je ndoto ile
ndio inanitabiria hatima yangu, kwamba nitahukumiwa kifungo cha miaka
thelathini kama jambazi?
Kama ni hivyo, niliendelea kujiambia, nitafia jela.
Sitamuona tena mama yangu, sitamuona tena kaka yangu.
Wazo la kufungwa miaka
thelathini lilinifanya nitaharuki. Nikajiambia “…sijui nikimbie nisiende tena kazini…”
Lakini nikajiuliza
nitakimbilia wapi katika Tanzania
hii ambapo mkono wa serikali hautakuwepo?
Kukimbia ni kama
kujidanganya na kuonesha kuwa zile pesa niliiba mimi wakati sivyo, nikajiambia,
la msingi ni kwenda kazini, litakalotokea na litokee. Kama
ni kufungwa au kuachiwa, ingawa tegemeo la kuachiwa sikuwa nalo.
Mpaka inafika saa moja kamili
asubuhi nilikuwa nimeshafika
nyumbani kwa kaka. Nilitangulia kwenda kwa mama nikaagana naye. Mama aliniombea
Mungu kile ‘kikombe’ kiniepuke.
Nilisubiri kaka ajitayarishe
hadi saa moja na nusu ndipo tulipoondoka.
Tulifika kazini saa mbili kama na robo hivi nikaingia ndani na kaka. Tulikwenda
katika ofisi ya mhasibu. Mhasibu aliponiona tu akaniuliza.
“Umekuja
na pesa?”
Nikatikisa kichwa taratibu.
“Sikufanikiwa bosi”
“Mimi ni kaka yake” Kaka
yangu akajitambulisha na kumuuliza mhasibu.
“Mheshimiwa kwani hiwezekani
kumkata katika mshahara wake wa kila mwezi hadi hizo pesa zikaisha?”
Mhasibu akakasirika.
“Nyinyi mnaleta utani na
kazi. Huu ni wizi, huyu hakukopa pesa hapa hadi tumkate kila mwezi. Shilingi
milioni kumi tutamkata kwa miaka mingapi wakati pesa za shirika zinahitajika? Nimeshamwambia kama
hakuja na pesa leo atakwenda kujieleza polisi” Mhasibu alifoka na kuinuka
kwenye kiti, akaniambia.
“Twende!”
Tukatoka mle ofisini na
akawaambia wafanyakazi wengine kuwa tunakwenda kituo cha polisi. Tulikuwa tuna
magari mawili ya shirika yenye madereva wake. Tukapanda kwenye gari mojawapo.
Kaka yangu tulimuacha pale pale.
Wakati napelekwa polisi na
nikijua kuwa ninakwenda kufungwa nilimlaani sana yule aliyeiba zile pesa. Nilipata
uchungu nilipowaza kwamba mimi ninakwenda kufungwa, yeye yuko ofisini akiwa
ameficha shilingi milioni kumi nyumbani kwake.
Tulikwenda kituo cha polisi
cha Chumbageni. Tulipoingia katika kituo hicho
mhasibu akatoa maelezo yote kuhusiana na wizi huo.
DUH! JAMAA ANATIA HURUMA
KWELI! SI ATAFUNGWA TU HUYU? Jamani Tumuombee mwenzetu, yuko kwenye wakati
mgumu.
No comments:
Post a Comment