Thursday, June 23, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 26

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572, 0713 340572

MWANAMKE 26

ILIPOISHIA

Nikajiuliza, je ndoto ile ndio inanitabiria hatima yangu, kwamba nitahukumiwa kifungo cha miaka thelathini kama jambazi?

Kama ni hivyo, niliendelea kujiambia, nitafia jela. Sitamuona tena mama yangu, sitamuona tena kaka yangu.

Wazo la kufungwa miaka thelathini lilinifanya nitaharuki. Nikajiambia “…sijui nikimbie nisiende tena kazini…”

Lakini nikajiuliza nitakimbilia wapi katika Tanzania hii ambapo mkono wa serikali hautakuwepo?

Kukimbia ni kama kujidanganya na kuonesha kuwa zile pesa niliiba mimi wakati sivyo, nikajiambia, la msingi ni kwenda kazini, litakalotokea na litokee. Kama ni kufungwa au kuachiwa, ingawa tegemeo la kuachiwa sikuwa nalo.

Mpaka inafika saa moja kamili asubuhi nilikuwa nimeshafika nyumbani kwa kaka. Nilitangulia kwenda kwa mama nikaagana naye. Mama aliniombea Mungu kile ‘kikombe’ kiniepuke.

Nilisubiri kaka ajitayarishe hadi saa moja na nusu ndipo tulipoondoka.

Tulifika kazini saa mbili kama na robo hivi nikaingia ndani na kaka. Tulikwenda katika ofisi ya mhasibu. Mhasibu aliponiona tu akaniuliza.

“Umekuja na pesa?”

Nikatikisa kichwa taratibu.

“Sikufanikiwa bosi”

“Mimi ni kaka yake” Kaka yangu akajitambulisha na kumuuliza mhasibu.

“Mheshimiwa kwani hiwezekani kumkata katika mshahara wake wa kila mwezi hadi hizo pesa zikaisha?”

Mhasibu akakasirika.

“Nyinyi mnaleta utani na kazi. Huu ni wizi, huyu hakukopa pesa hapa hadi tumkate kila mwezi. Shilingi milioni kumi tutamkata kwa miaka mingapi wakati pesa za shirika zinahitajika? Nimeshamwambia kama hakuja na pesa leo atakwenda kujieleza polisi” Mhasibu alifoka na kuinuka kwenye kiti, akaniambia.

“Twende!”

Tukatoka mle ofisini na akawaambia wafanyakazi wengine kuwa tunakwenda kituo cha polisi. Tulikuwa tuna magari mawili ya shirika yenye madereva wake. Tukapanda kwenye gari mojawapo. Kaka yangu tulimuacha pale pale.

Wakati napelekwa polisi na nikijua kuwa ninakwenda kufungwa nilimlaani sana yule aliyeiba zile pesa. Nilipata uchungu nilipowaza kwamba mimi ninakwenda kufungwa, yeye yuko ofisini akiwa ameficha shilingi milioni kumi nyumbani kwake.

Tulikwenda kituo cha polisi cha Chumbageni. Tulipoingia katika kituo hicho mhasibu akatoa maelezo yote kuhusiana na wizi huo.

SASA ENDELEA

Baada ya kumaliza kutoa maelezo yake na mimi nikatakiwa nijieleze.

Nikaeleze hali iliyotokea ambapo fedha hizo zilichukuliwa ndani ya ndroo yangu wakati ndroo hiyo  niliifunga kwa funguo. 

Baada ya maelezo yangu nikaanza kukabiliwa na maswali ya polisi.

“Baada ya kufungia hizo pesa kwenye droo yako, asubuhi ulipokwenda kazini kwako ulikuta droo imevunjwa?”

“Ndroo haikuvunjwa”

“Untaka utuambie huyo aliyeziiba pesa hizo alizichukuaje bila kuvunja droo?”

“Pengine alikuwa na ufunguo mwingine”

“Funguo za droo yako ziko ngapi?”

“Ni mbili na zote ninazo mimi”

“Unaona sasa unajiingiza mwenyewe, huo ufunguo wa tatu alioutumia huyo mtu umetokea wapi wakati funguo ni mbili na unazo mwenyewe?”

“Unaweza kuwa ufunguo wa kuchongesha. Kuna mafundi wa kuchonga funguo”

“Tunajua kuwa wapo lakini hata wao ni mpaka uwapelekee ufunguo wa sampuli ndio wanaweza kukuchongea”

“Wezi wana mbinu nyingi. Kama mtu alishapanga kufanya uwizi anaweza kuvizia hizi funguo ninapoziacha juu ya meza yangu wakati sipo, akaukandamiza ufunguo mmoja kwenye sabuni ili kupata meno yake halafu sabuni ile anaipeleka kwa fundi. Fundi anaweza kuchonga ufunguo kama ule”

“Unaweza kuzungumza mengi lakini hayana ushahidi. Hebu twendeni tukaione hiyo droo yako”

Huo ndio ukawa mwisho wa maswali.

Tulitoka na polisi. Mimi nilipakiwa kwenye gari la polisi, mhasibu akaondoka na gari la shirika.

Wakati tunaondoka ndio kaka yangu alikuwa anafika pale kituoni. Akatuona tunaondoka. Siku ile nilimsumbua sana kaka kwa sababu alikuwa akitembea kwa miguu.

Tulipofika kazini kwetu tuliingia ndani, mhasibu akawapeleka polisi kwenye meza yangu.

“Pesa ziliibiwa kwenye meza hii” Mhasibu aliwambia polisi.

“Hebu toa hizo funguo tuzione” Polisi mmoja akaniambia.

Nikazitoa funguo zangu kutoka mfukoni na kuwaonesha

Polisi walizitazama kisha polisi mmoja akaniambia nifungue ile droo. Nikaifungua.

Sote tuliokuwa tunashuhudia, mimi mhasibu na wale polisi pamoja na baadhi ya wafanyakazi, tuling'aka baada ya kuziona zile pesa zilizokuwa zimetoweka zikiwa ndani ya droo.

“Na hizo ni pesa zipi?” Polisi mmoja akaniuliza kwa mshangao.

“Sijui, ndio naziona sasa. Zilikuwa hazimo” nikamjibu.

“Hapo mwanzzo mlihakikisha kwa makini kuwa hizo pesa hazikuwemo?”

“Mimi nilihakikisha na mhasibu pia alihakikisha”

“Hebu zitoe”

“Nikazitoa na kuziweka juu ya meza

“Ni kiasi gani?” Mhasibu akaniuliza

Nikazihesabu na kuona zilikuwa shilingi milioni kumi.

“Sasa nani amezitia hizo pesa?” Mhasibu akauliza kwa mshangao.

Hakukuwa na jibu

“Asubuhi uliangalia kwenye hii droo?” akaniuliza tena

“Sikuangalia”

Mhasibu alipowauliza wafanya kazi wenzangu kuhusu zile pesa hakukuwa na yeyote aliyeeleza kuwa alijua chochote kuhusu pesa hizo.

“Mimi naamini kuwa hizi pesa zimerudishwa kwa sababu mimi mwenyewe niliangalia kwenye hii droo juzi, sikukuta kitu” Mhasibu akatuambia.

“Hapa pana mchezo umepita, mimi nimechezewa na wenzangu” nikasema kwa hasira. Sasa nilikuwa na nguvu baada ya zile pesa kuonekana.

“Sasa ni nani aliyefanya mchezo huu? Tunataka tumjue” Mhasibu akauliza.

“Huu ni wizi ulikuwa umefanyika. Huyo aliyeiba alipoona suala hili limefika polisi ndio aliamua kuzirudisha pesa hizi” Polisi mmoja akasema.

“Tunashukuru kwa vile amezirudisha lakini tunaomba mchezo huu usirudiwe tena” Mhasibu akaonya

“Basi sisi tunakwenda zetu” polisi wakatuambia.

“Mimi naona mwende kwa sababu tatizo lilikuwa ni kwenye hizi pesa ambazo zimeshaonekana” Mhasibu akawambia polisi

Polisi hao wakatuaga na kuondoka.

Mhasibu akachukua zile pesa na kuniambia nimfuate ofisini kwake.

Tulipokuwa ofisini aliniambia.

“Usirudie tena kuacha pesa kwenye droo, sasa hivi sina imani tena na wafanyakazi wa shirika hili”

“Kutokana na msukosuko huu ulionipata, sitarajii kulaza pesa tena kwenye droo yangu”

“Shukuru kwamba hizi pesa zimepatikana, vinginevyo ungelala ndani leo”

“Ni kweli. Hilo nilikwishalijua”

“Kuwa makini sana na wenzako”

“Nitakuwa makini”

Mhasibu akawa anahesabu zile pesa. Alipohakikisha kuwa zilikuwa shilingi milioni kumi taslim nilimuomba anipe mapumziko ya siku moja ili niende nikatulize presha yangu nyumbani.

Mhasibu akaniruhusu, nikaondoka. Wakati natoka mlangoni nikakutana na kaka akitokea kituo cha polisi. Alikuwa amechoka kwa mwendo.

“Imekuwaje?” akaniuliza huku akinitazama kwa uso wa sintofaham.

“Twenzetu” nikamwambia

Akanifuata. Tukashuka baraza.

“Tunakwenda wapi?” akaniuliza akionesha kuwa na wasiwasi

“Nyumbani”

Nikaona uso wake unachanua tabasamu.

“Kwani imekuwaje?”

“Zile pesa zimeonekana”

Kaka akashituka.

“Zimeonekana wapi?”

“Kwenye droo”

“Droo ya nani?”

“Droo yangu”

“Zimeonekana kivipi?”

“Ni tukio la ajabu sana” nikamwambia kisha nikamueleza jinsi tulivyozikuta pesa hizo kwenye droo yangu.

“Una maana huyo aliyeiba ameamua kuzirudisha?”

“Itakuwa ndio hivyo”

“Kwa hiyo zile pesa alikuwa amezificha sehemu nyingine, alipoona unapelekwa polisi akaamua kuzirudisha”

“Bila shaka. Lakini sasa nimepata fundisho sitaacha pesa tena kwenye droo yangu kwa maana wanataka kunitoa kafara”

“Ni tukio ambalo sikulitarajia”

“Naona dua za mama zinafanya kazi. Mama aliniombea sana”

“Wakati tunavuka barabara tukapishana na msichana mmoja ambaye naye alikuwa anavuka kutoka upande ule tuliokuwa tunakwenda sisi. Alinitupia jicho mara moja ili kujua kama nimemuona.

Nukta ile ile nikamtambua.

Alikuwa Zena!

DUH! Huyu ZENA JINI? AMETOKEA WAPI TENA? HALAFU NAONA DUA ZENU WASOMAJI ZIMESAIDIA KUMUOKOA HUYU JAMAA!

No comments:

Post a Comment