Tuesday, June 28, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 30

HADITHI na Faki A Faki 0655 340572
 
MWANAMKE 30
 
ILIPOISHIA
 
Nilitazama saa yangu na kuona ilikuwa saa saba ikielekea kuwa na nusu. Nikaona wakati huo pia ulikuwa muafaka kuondoka. Nikaenda kunawa uso kisha nikarudi sebuleni na kuvaa vile viatu vya mvua kwa ajili ya kujikinga na tope wakati wa kufukua kaburi.
 
Ile mipira ya mikononi sikuivaa kabisa. Nikatoa pikipiki yangu. Lile shepe nilikuwa nimeshalifunga katika siti ya nyuma ya pikipiki.
 
Kifaa cha kukatia kucha nilikuwa nimeshakitayarisha. Ulikuwa wembe mpya.
 
Nikaondoka.
 
Niliendesha piki piki yangu taratibu hadi nikafika Gofu. Usiku huo kulikuwa kimya. Hakukuwa na gari wala watu waliokuwa wakipita. Nilikuwa na hakika kwamba hakukuwa na mtu yeyote ambaye angeniona.
 
Nilifika katika lile eneo la makaburi. Nikaiingiza pikipiki yangu ndani ya eneo hilo lililokuwa na mti pamoja na vichaka vidogo vidogo.
 
Nikaiegesha pikipiki chini ya mti huku nikiangaza macho huku na huku. Mbalamwezi ililiangaza vizuri eneo hilo kiasi kwamba sikupata taabu kuyaona makaburi hayo.
 
Nilianza kuvaa mipira ya mikononi kisha nikalifungua lile shepe. Nililishika mkononi nikaanza kutafuta kaburi la kuchimba.
 
Makaburi mengi yalikuwa yamewekewa zege, nikaenda mbele zaidi. Nikakuta kaburi moja ambalo halikuwa limewekewa zege na lilionesha lilikuwa jipya. Huenda kulikuwa na mtu aliyekuwa
amezikwa siku iliyopita.
 
Nikaanza kulichimba. Kwa vile mchaga wake ulikuwa laini nililichimba haraka haraka huku nikirundika mchanga upande mmoja juu ya kaburi hilo. Shimo lilipokuwa kubwa niliweza kuingia ndani nikaendelea kuchimba.
 
Baada ya kama nusu saa tu nikawa nimelifikia sanduku lililokuwemo ndani. Nilipofanikiwa kuuondoa mchanga wote uliokuwa juu ya sanduku hilo nikaufungua mlango wa sanduku na kuuacha wazi. Ndani ya sanduku hilo niliona maiti ya mwanamke.
 
Nikatia mkono mfukoni mwangu na kutoa ule wembe. Niliufungua kwenye karatasi yake nikaushika kisha nikaushika mkono wa ile maiti ya mwanamke. Hapo hapo nikaona mwanga wa tochi unanimulika kutoka juu ya kaburi kisha sauti nzito ikaniuliza.
 
“Wewe nani na unafanya nini hapa?”
 
Kwa kweli nilishituka sana. Wembe uliniponyoka. Miguu ikanitepeta. Nikainua uso wangu haraka na kutazama juu ya kaburi hilo.
 
Nilijuta!
 
SASA ENDELEA
 
Nilimuona mtu aliyekuwa akinimulika tochi akiwa juu ya kaburi lakini sikuweza kumuona vizuri kwa sababu ule mwanga wa tochi ulikuwa unapiga kwenye macho yangu.
 
“Ulikuwa unafanya nini?’ Mtu huyo aliendelea kuniuliza kwa ukali.
 
Sikumjibu. Yeye alikuwa amesimama upande mmoja wa kaburi. Na mimi nilikurupuka kuelekea upande mwingine wa kaburi nikapanda juu haraka.
 
Wakati ninainuka ili nikimbie, alinirushia rungu. Nikainama na kulikwepa. Wakati nainama niliona kitu kikiruka kutoka mfuko wa shati langu na kuanguka chini. Sikujua kilikuwa kitu gani. Na sikuwa na muda wa kukitazama vizuri.
 
Yule mtu nilimuona. Kwa jinsi alivyovaa niligundua alikuwa mlinzi. Nikahisi alikuwa mlinzi wa eneo lile.
 
Nikatimua mbio kuelekea nilikoiacha pikipiki yangu. Wakati nakimbia nilijiuliza kama kulikuwa na mlinzi, alikuwa wapi wakati nafika na kufukua lile kaburi?
 
 
 
Nilitazama nyuma na kumuona alikuwa ananikimbiza. 
 
“Simama wewe, utakufa!” aliniambia.
 
Lakini sikugeuka wala sikusimama. Niliendelea kukimbia hadi nikaifikia pikipiki yangu, yeye bado akiwa mbali. Niliiwasha haraka haraka. Pikipiki ilikubali mara moja. Nikaipanda na kuondoka kwa kasi.
 
“Wewe…bahati yako!” aliniambia baada ya kunikosa.
 
Alikuwa amesimama akinielekeza rungu lake. Niligeuza uso mara moja tu nikamtazama.
 
Alipoona namtazama aliniambia kwa hasira.
 
“Usije tena hapa mchawi mkubwa. Ningekuua leo!”
 
Niligeuza uso wangu nikatazama mbele ninakoelekea. Kimoyomoyo nilikuwa nikijiambia.
 
“Ningekufa leo!”
 
Nilikuwa nimekaa kwenye pikipiki huku nikijihisi wazi kuwa nilikuwa natetemeka. Sikuwa nimezoea mapambano hivyo tukio lile la kufumwa na kutimuliwa kwa sime lilitosha kunifanya nitetemeke.
 
Nilikuwa nikijiambia laiti yule mtu angenishika angeniua kwa vile mwenzngu alikuwa na silaha, mimi niko mikono mitupu.
 
Nilirudi nyumbani nikiwa nimeacha shepe langu ndani ya lile kaburi.
 
Lakini halikuwa mali kuliko uhai wangu. Kucha za maiti zilitaka kunitoa roho yangu!
 
Nilipofika nyumbani nillikuwa nahema kama vile nilikimbia njia nzima kurudi nyumbani. Niliingiza pikipiki yangu. Nikavua vile viatu nilivyovaa kuzuia tope pamoja na mipira ya mikononi kisha nikaingia bafuni kuoga.
 
Nilipotoka bafuni niliona afadhali kidogo. Nikaenda kulala. Hata usingizi wenyewe sikuupata. Nilianndamwa na njozi za ajabu ajabu hadi kunakucha. Moja ya ndoto iliyonitisha ilikuwa ile maiti niliyoifukua imegeuka mzuka na kunifuata nyumbani ikiwa imetoka kucha ndefu vidoleni.
 
Kucha hizo ndizo zilizokuwa zinatoboa mlango wa chumbani kwangu. Wakati nashituka mlango wa chumbani kwangu ulikuwa umeshafunguka.
 
Laiti nisingewahi kuamka sijui ingekuwaje?
 
Ilikuwa miujiza mitupu!
 
Baada ya kuoga na kuvaa nilitoa pikipiki yangu. Hapo ndipo nilipogundua kuwa leseni yangu sikuwa nayo mfukoni. Usiku uliopita niliiweka kwenye mfuko wa shati langu na kwa muda ule sikuwa nayo.
 
Nikahisi ndio iliyonianguka kule makaburini usiku wakati yule mlinzi akinikurupusha.
 
Nikawa nimegwaya. Nilijiambia kama yule mlinzi ataiona ile leseni yangu ambayo ilikuwa na picha yangu anaweza kuipeleka polisi. Kwa vile tayari nilikuwa na rikodi mbaya polisi, kugunduliwa kwangu kungekuwa rahisi sana.
 
Polisi watakapoiona picha yangu watanifuata kazini kwangu na kunikamata.
 
Imeshakuwa balaa!
 
Licha ya kupatwa na fadhaa kiasi hicho nilipanda pikipiki yangu. Kwanza nilikwenda Chuda kumueleza kaka yangu mkasa mzima.
 
“Amour umefanya uzembe mwenyewe!” kaka akaniambia baada ya kunisikiliza.
 
Uso wake ulionesha wazi kuwa hakufurahishwa na kitendo changu.
 
“Nimefanya uzembe kivipi kaka?” nikamuuliza.
 
“Jana nilikwambia nini?”
 
“Hebu nikumbushe pengine nimesahau”
 
“Si nilikwambia kwamba tuma mtu”
 
“Kaka kutuma mtu kunaweza kuleta matatizo”
 
“Matatizo gani?’
 
“Sitakuwa na uhakika kama hizo kucha atakazoniletea ni za maiti kweli. Anaweza kwenda kujikata kucha zake mwenyewe akaniletea”
 
“Ungetafuta mtu unayemuamini”
 
“Wahuni hawaaminiki kaka. Wangechukua pesa zangu halafu wakaniletea kucha zao wenyewe”
 
Kaka yangu akanywea.
 
“Saasa umeshajitia kwenye balaa jingine!”
 
“Kwa kweli ni balaa, sasa sijui itakuwaje!”
 
“Kwani hivi sasa unakwenda wapi?”
 
“Ninakwenda kazini”
 
“Ukitoka kazini nenda ukamueleze yule mganga”
 
“Nitakwenda”
 
“Basi wewe nenda kazini kwako, punguza wasiwasi”
 
Nikaondoka kwa kaka na kwenda kazini. Lakini njia nzima nilikuwa nawaza tu.
 
Nilipofika niliingia kazini kama kawaida. Baadaye kidogo mhasibu alifika na kuingia ofisini kwake. Haukupita muda mrefu mhasibu alitufuata akatueleza kisa kilichonishitua.
 
“Jana tulikwenda kuzika kule Gofu, shemeji yangu alikuwa amefariki. Hivi sasa napigiwa simu naelezwa kwamba kuna mtu alikwenda kulifukua lile kaburi usiku. Sijui alitaka kuichukua ile maiti?”
 
“Labda ni wachawi, lakini hakuwahi kuichukua?” Mfanya kazi mmoja akamuuliza.
 
“Hakuwahi, alikurupushwa na mlinzi. Lile eneo linalindwa kwa ajili yakuzuia watu kama hao”
 
“Angemkamata ingekuwa vizuri kwa sababu angefahamika” Mfanyakazi mwingine alidakia.
 
“Alikimbia na pikipiki. Mlinzi amesema huyo mtu alikuja na pikipiki”
 
Niliposikia hivyo moyo wangu ulishituka. Kama namba za pikipiki yangu nazo zimeonekana nimekwisha!
 
Sikujua kama ile maiti ilikuwa ni ya shemeji yake mhasibu wetu. Nikaona nimejiingiza katika matatizo mengine ambayo sikuyatarajia.
 
“Hivi sasa nimeitwa polisi nikatoe maelezo, ile maiti imepelekwa hospitali kufanyiwa uchunguzi kujua kama ilibakwa. Kuna watu wanabaka maiti” Mhasibu aliendelea kutueleza.
 
“Inawezekana. Ni vizuri kama amepelekwa hospitali kufanyiwa uchunguzi. Binaadamu hivi sasa hawaaminiki kabisa” nikajidai kusema ili nisionekane nimefadhaika.
 
“Kumbe yule mlinzi alikwenda kuripoti polisi” Mwenzetu mwingine akauliza.
 
“Alikwenda polisi asubuhi. Ndio maana ninaitwa polisi” Mhasibu akamjibu kisha akatuaga na kuondoka.
 
Niliwaza kwamba kama mlinzi alikwenda kuripoti polisi, ile leseni yangu pia aliipeleka baada ya kuiokota pale ilipoanguka. Polisi watakuwa wameshaiona picha yangu. Bila shaka mhasibu wetu ameitwa ili kuoneshwa ile leseni ili athibitishe kama ndiye mimi.
 
Sasa sijui nikimbie kuepusha aibu, au niwangoje polisi waje wanikamate hapa hapa?
 
Kwa kweli nilikuwa nimechanganyikiwa.
 
KWA KWELI JINSI JAMAA ALIVYOANDAMWA NA MIKASA, ANATIA HURUMA. LIKITOKA HILI LINAKUJA HILI. DUH! SASA SIJUI ITAKUWAJE? Jamaa ataumbuka huyu!
 
Kesho si mbali. Tuombe uhai.

No comments:

Post a Comment