Sunday, June 19, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 24

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI

MWANAMKE 24

ILIPOISHIA

Ule mchezo wangu wa kufungua madawati kuanzia la juu hadi la chini na kisha kurudia tena, uliwashitua wafanyakazi wenzangu wakaanza kuniuliza ninachotafuta.

“Amour mbona umeshughulika sana, unatafuta nini?” Mfanyakazi mmoja akaniuliza.

“Natafuta pesa. Jana tulipoondoka niliacha shilingi milioni kumi katika dawati hili la juu, sasa sizioni!” nikamwambia.

“Zimekwenda wapi?”

“Sijui!”

“Kwani ulipoondoka hukulifunga?”

“Nililifunga na funguo niliondoka nazo, sasa nashangaa pesa sizioni!”

“Haiwezekani! Hebu tazama vizuri”

“Nimetafuta sana, pesa hazimo. Sijui nani amezichukua!”

“Na haiwezeani zichuuliwe na mtu wa sababu funguo uliondoka nazo mwenyewe”

Nikanyamaza kimya huku macho yangu yakitanga tanga kwenye meza.

Wafanyakazi wengine waliposikia mazungumzo yetu wakasogea karibu.

“Umepoteza nini,  pesa?” mfanyakazi mmoja akaniuliza.

“Ndio pesa”

“Uliziweka wapi?”

“Nilizizifungia kwenye dawati hili hapa jana jioni tulipotoka kazini, sasa nashangaa pesa sizioni”

SASA ENDELEA

“Ulifunga kwa funguo?” Mhasibu aliniuliza.

“Nilifunga kwa funguo na funguo niliondoka nazo”

“Sasa nani atazichukua kama dawati ulilifunga?”

Katika maswali yote niliyokuwa nikiulizwa, swali hilo ndilo lililonikera kwa sababu sikuwa na jibu nalo na lilinifanya nionekane mzushi na mpumbavu.

“Hilo ndilo jambo la ajabu” nilijikuta ninatoa jibu hilo.

Baada ya muda mfupi nikawa nimezungukwa na wafanyakazi wenzangu waliokuwa wakilishangaa tukio hilo.

“Hebu jaribu kukumbuka kama uliziweka sehemu nyingine” Mhasibu akaniambia.

“Sikuweka sehemu nyingine, niliziweka kwenye dawati hili hapa” nilimuonesha lile dawati la kwanza.

“Sasa zitakuwa zimekwenda wapi?”

“Sijui bosi”

“Na ni kwanini hizo pesa  hazikupelewa benki tangu jana ?”

“Ni pesa za mauzo ya jioni, benki zilikuwa zimeshafungwa bosi”

“Mara ngapi umeshalaza pesa kwenye droo lako?”

“Mara nyingi tu lakini leo ndio nimekomolewa”

“Sasa umekomolewa na nani? Mhasibu akaniuliza.

“Siwezi kujua”

“Bado sikuelewi Amour, pesa uliziweka mwenyewe na hakuna aliyejua isipokuwa wewe mwenyewe. Sasa utasema umekomolewa, umekomolewa na nani?”

Nikabaki kimya. Sikuwa na jibu

Msibu akanitazama.

“Umehakikisha kuwa hizo pesa hazipo?” akaniuliza.

“Sizioni” nikamjibu kwa sauti iliyonywea

“Sasa njoo ofisini kwangu”

Moyo wangu ukashituka lakini nilijikaza kiume. Nikamfuata mhasibu ofisini kwake. Kwa pembeni mwa macho yangu niiwaona wafanyakazi wenzangu wakinitazama. Kuna niliowaona wakinihurumia na kuna waliokuwa wakiona nilikuwa nimefanya ulaghai wa kuiba pesa za shirika.

Nilipoingia ofisini mwa mhasibu, mhasibu aliniambia.

“Kaa hapa” alinionesha kiti.

Yeye mwenyewe alizunguka nyuma ya meza yake, naye akaketi.

“Nataka nikwambie kitu” akaniambia. Sauti yake na uso wake haukuonesha urafiki hata chembe.

“Ndiyo” nikamuitikia nikiwa sijui anataka kuniambia nini.

“Umekuwa mfanya kazi muaminifu kwa muda mrefu sana lakini hii haitufanyi tusikuchukulie hatua kutokana na wizi huu wa pesa za shirika. Ninachokuomba ni kuwa nakupa siku mbili tu utupatie zile pesa” Alipofika hapo alinikazia macho kisha akaniuliza.

“Sijui umenielewa?”

“Nimekuelewa” Sikuwa na jibu jingine zaidi ya hilo.

“Sasa nenda katuletee zile pesa”

“Si kwamba hizo pesa ninazo, pesa zimeibiwa”

“Sasa nenda katutafutie pesa za watu uzilete”

“Nitakwenda kuzitafuta wapi bosi?”

Nilijua kwamba niliuliza swali la kipumbavu lakini lilitokana na hoja ya kipumbavu.

“Popote utakapojua utazipata, sisi shida yetu ni pesa tu”

Nikageuza uso wangu pembeni kutafakari.

“Nimekupa siku mbili uje na hizo pesa, vinginevyo itabidi suala hilo nilifikishe polisi”

Nilihisi kijasho chembamba kikinitiririka kwenye mfereji wa uti wa mgongo wangu.

“Tumeelewana?” Bosi akaniuliza alipoona nipo kimya.

“Sawa bosi” nikamjibu kisha nikainuka kwenye kiti.

Nilikwenda kwenye mlango. Wakati naufungua mlango huo nikaisikia sauti ya mhasibu akiniambia.

“Kumbuka kwamba nimekupa siku mbili”

Nikageuza uso na kumtazama.

“Nimekuelewa” nikamjibu kisha nikafungua mlango na kutoka.

Wakati natoka, macho ya wafanyakazi wenzangu yaligeuka kwangu. Sikuwapatiliza wala kuwajali. Nilihisi walikuwa miongoni mwa walionikomoa. Mimi nimeshapewa onyo la kusulubiwa, wao wanafurahia milioni kumi za bure.

Nilitoka nje ya duka letu bila kuzungumza na mfanyakazi yeyote. Nilikuwa nimefadhaika kweli. Nilipanda pikipiki yangu nikaiwasha na kuondoka.

Sikujua nilikuwa naenda wapi, nikaona niende kwa mama nikamueleza kuwa nimefikwa na mitihani. Wakati naendesha nilikuwa najiuliza nitazipata wapi shilingi milioni kumi ili nirudishe pesa za watu.

Pale nilipomkubalia bosi, aliponiambia niende nikazitafute pesa hizo nilimkubalia tu ili niweze kuondoka kwani nilijua kuwa sitazipata.

Nilipofika kwa mama yangu nilimueleza mkasa ulionitokea, mama alitaharuki sana.

“Imekuwaje tena mwanangu?” akaniuliza.

“Kwa kweli sielewi kitu mama. Huyo mtu aliyenichezea mchezo huu amenikomoa kweli”

“hilo dawati ulikuta limevunjwa?”

“Halikuvunjwa. Watu wana mbinu nyingi za wizi. Inawezekana kuna ufunguo mwingine uliotumika”

“Kwanini usiwaeleze hivyo wakubwa wako wa kazi?”

“Nani atanisikiliza. Unapotoa malalamiko unatakiwa utoe na ushahidi, ushahidi uko wapi kwamba kuna mfanyakazi mwenzagu amefungua dawati langu kwa ufunguo mwingine na kuiba hizo pesa!”

“Sasa wewe utazipata wapi milioni kumi?”

“Hiki ni kifungo mama!”

“Umekwenda kumueleza kaka yako?”

“Sijakwenda bado”

“Hebu nenda kamueleze usikie atakupa ushauri gani?”

“Sawa. Acha niende nikamsikilize”

Nilipofika nyumbani kwa kaka Chuda, ilikuwa ikikaribia kuwa saa sita mchana.

“Leo hukwenda kazini?” kaka akaniuliza.

“Nimekwenda lakini kumetokea matatizo”

“Matatizo gani?”

“Kuna pesa zimeibiwa kwenye dawati langu”

“Lini?”

“Leo hii”

“Kiasi gani?”

“Shilingi milioni kumi”

Kaka akashituka. Enzi hizo pesa hizo zilikuwa nyingi sana.

“Zimeibiwaje?”

Nikamueleza kaka jinsi wizi huo ulivyotokea.

“Inawezekana huyo jamaa alikuwa na ufunguo mwingine ambao aliutumia kufungua dawati lako akaiba hizo pesa”

“Ndio hivyo lakini  sasa dhima imeniangukia mimi”

“Kwa hiyo umeambiwa nini”

Nitoke nikatafute pesa za shirika nizirudishe, nimepewa siku mbii tu”

HUYU JAMAA NAONA KAMA JELA INAMUITA. ATAPATA WAPI  SHILINGI MILIONI KUMI MASIKINI WA MUNGU? Je ni nani waliomchezea mwenzao? Ukinipa ahadi kuwa kesho utafungua blogy hii na mimi nitakupa ahadi kuwa ukifungua tu utanikuta nikiendelea na mkasa huu.

No comments:

Post a Comment