SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572
MWANAMKE 28
ILIPOISHIA
Niliporudi ofisini na polisi
Zena alikuwa yuko sambamba na mimi hadi zile pesa zipoonekana.
Sasa wakati ule navuka
barabara nikiwa na kaka alijipitisha kusudi ili nimuone kisha akapotea.
Nikazinduka usingizini. Wakati nazinduka niliisikia sauti ya Zena ikiniambia.
“Hilo ni onyo!”
Nikadhani kwamba zena alikuwa
mule chumbani. Nilipofumbua macho nikainuka na kuketi, nikaanza kutazama huku
na huku kwa hofu
kwamba ningemuona Zena mle chumbani. Lakini sikumuona.
Nikashuka kitandani na kutoka
sebuleni ambako nilikaa kwenye kochi
na kuifikiria ile ndoto.
Hapo ndipo nilipoanza
kufahamu kuwa zile pesa zilikuwa zimechukuliwa na Zena ili kunikomoa.
Nikajiambia kama asingezirudisha ndio
ningekiona cha moto.
“Huyu msichana ataendelea
kuniamndama hadi lini?” nikajiuliza.
Nilihisi kwamba kama sitachukua hatua thabiti za kuhakikisha kwamba
ninaepukana naye, mwisho wake anaweza kunitia katika matatizo makubwa.
Baada ya kufkiri sana nilitoa pikipiki
yangu nikaenda kumueleza mama kuhusu ile ndoto. Mama naye alistaajabu.
“Kumbe bado anakufuatilia!”
akaniambia
“Huyu jini atakuja kunitia
kwenye matatizo makubwa hapo baadaye” nikamwambia mama.
“Sasa fanya mpango wa kwenda
huko pemba”
“Inabidi nipate mwenyeji au
mtu wa kufuatana naye ndio nitaweza kufika”
SASA ENDELEA
“Ulizia kwa marafiki zako
unaweza kupata mtu anayekwenda. Hapa Tanga watu wa Pemba
wako wengi” Mama akaniambia.
“Nitaanza kuuliza uliza kwa
watu. Nikipata mwenyeji au mtu anayekwenda huko itabidi niende”
Baadaya kuzungumza na mama
nilikwenda kwa kaka, naye nikamueleza kuhusu ile ndoto.
“Mimi naamini majini wana
matatizo sana na huyo jini hawezi kukuachia
kirahisi lakini kwa vile humuhitaji nitakusaidia kukuulizia waganga kwa wenyeji
wa Pemba” Kaka akaniambia.
“Na mimi mwenyewe pia
nitakuwa naulizia ulizia kwa jamaa”
Ikapita wiki moja. Siku moja
ya jumapili kaka yangu akaja nyumbani. Hakuwa na kawaida ya kufika kwangu,
hivyo nilipomuona nilishituka.
Akaniambia kulikuwa na mganga
aliyetoka Pemba amefikia katika gesti moja
pale Chuda. Katika matangazo yake ameeleza pia kuwa anafukuza majini wabaya.
“Nataka twende umueleze
matatizo yako anaweza kukusaidia” Kaka akaniambia.
Nilipopata habari zile
nilimwambia kaka anisubiri. Baada ya dakika chache tukawa njiani tukielekea Chuda. Nilikuwa nimempakia nyuma ya pikipiki yangu.
Tulipofika Chuda alinipeleka
katika gesti alikofikia huyo mganga aliyeniambia. Ilikuwa
mtaa wa pili na ule aliokuwa akiishi yeye.
Wale watu niliowakuta hapo
nje wakisubiri zamu ya kuingia kwa mganga huyo walinipa matumaini kwamba huyo
mganga alikuwa mganga kweli.
Alikuwa ameweka tangazo lake mbele
ya gesti lililoandikwa matatizo aliyokuwa akiyashughulikia likiwemo tatizo la
majini.
“Ninafukuza majini mabaya
katika mwili au nyumba. Pia ninatuliza wale majini wa kichwa wanoleta maradhi
na matatizo mengine” Ilisema sehemu ya tangazo hilo.
Mwisho wa tangazo lake aliandika.
“Njoo ujaribu kwani wengi
wamefanikiwa. Nitakuwa Tanga kwa siku tatu”
Kutokana na wale watu
niliowakuta kuwa wengi nilitaka kumwambia kaka turudi baadaye, watu watakuwa
wamepungua lakini nilivyoona pameandikwa kuwa mganga atakuwa Tanga kwa siku tatu nikaamua nisubri
hapo hapo.
Siku tatu ni chache
sana. Kama
ningemkosa siku ile na pengine siku inayofuata, uwezekano wa kumpata tena
ungekuwa mdogo sana.
Nilijiambia.
Watu tuliowakuta
walifikia arobaini. Nilimwambia kaka kama
hatakuwa na muda wa kusubiri hapo aende zake.
“Niache niendelee
kusubiri hata kama itafika jioni” nilimwambia.
“Sawa, basi wewe
subiri ikifika zamu yako utaingia na utamueleza tatizo lako. Ukitoka hapa
utakuja nyumbani kuniambia”
Tulipokubaliana na
kaka aliondoka akaniacha pale. Mpaka inafika saa nane mchana walikuwa wamebaki
watu kumi nikiwemo mimi. Nikaendelea kusubiri hadi saa kumi jioni ndio ikafika
zamu yangu.
Nikaingia.
Chumba
cha mganga kilikuwa cha kwanza cha mkono wa kushoto. Niliingia katika chumba
hicho nikamkuta mganga aliyekuwa amekaa chini kwenye mswala. Kando yake alikuwa amechoma udi wa kijiti
uliokuwa unafuka moshi.
Mbele yake kulikuwa
na vitabu kadhaa vya kiarabu pamoja na chupa za dawa za kiasili.
Alikuwa amevaa
kofia ya darize aliyoiweka katika muundo wa jahazi. Pia alikuwa amevaa shati
jeupe na shuka nyeupe. Hakuwa amevaa suruali.
“Karibu” akaniambia
alipoona nimesita
baada ya kuingia humo chumbani.
“Asante” nikamjibu.
“Kaa kwenye kiti”
Kulikuwa na kiti
kilichokuwa kando ya ukuta kushotoni
kwake. Nikaenda kuketi.
“Niambie shida
yako” akaniambia.
Nikamueleza
matatizo yangu mwanzo hadi mwisho.
“Umepata bahati sana. Kule kwetu ukiwa na jini kama
huyo tayari unajihesabu kuwa ni tajiri” Mganga akaniambia baada ya
kunisikiliza.
“Huko kwenu kuna
watu waliooa majini”
“Enhe! Wapo”
“Mimi simuhitaji
huyu jini”
“kama
wewe umuhitaji ndipo anapokutia kwenye matatizo”
“Ndio nimekuja
kwako unisaidie”
“Unataka
nikusaidieje?”
“Umuondoe”
“Una uhakika kuwa
umuhitaji kabisa, usije ukajuta
baadaye”
“Hapana, siwezi
kujuta”
“Kwangu mimi si
kazi kubwa kama utanipatia vitu ninavyotaka”
“Unataka vitu
gani?”
“Ninahitaji kucha
zako na kucha za maiti aliyezikwa. Unaweza kuzipata kucha za maiti?”
“Mh! Itakuwa
ngumu!”
“Bila kupata kucha
za maiti kazi itakuwa ngumu. Nenda kanitafutie
kucha za maiti. Ukizipata
niletee nitamuondoa huyo jini siku hiyo hiyo. Mimi nikalipo (nitakuwepo) hadi
kesho kutwa. Ukiniletea
kesho itakuwa bora”
“Bila hizo kucha
haitawekana?” nikamuuliza”
Mganga akatikisa kichwa.
“Itakuwa vigumu”
Nikawaza kidogo kisha nikamwambia.
“Basi acha niende nikafikirie
nitakavyoweza kuzipata hizo kucha halafu nitakuja hapo kesho”
“Sikiliza. Kucha zenyewe ni
lazima ziwe za maiti aliyezikwa si za maiti ambaye hajazikwa”
“Sasa maiti ambaye amezikwa
nitampata wapi?”
“Kaburini”
“Yaani nikafukue kaburi?’
“Ndio”
“Si nitaonekana na watu”
“Huendi mchana, unakwenda usiku”
“Mh!” nikaguna nilipofikiria
kwenda usiku makaburini na kufukua kaburi.
“kama
hutaweza basi, tutakuwa tumeshindwa”
“Nitakupa jibu hapo kesho kama nitaweza au la”
“Kumbuka kwamba nitakuwa hapa
Tanga kwa siku tatu. Nikitoka hapa ninakwenda Arusha”
“Nimekuelewa, acha niende.
Nitakuja tena kesho”
Nikaagana na yule mganga na
kutoka, Nilipanda pikipiki yangu nikaenda nyumani kwa kaka. Kaka mwenyewe
sikumkuta, mke wake aliniambia kaka aliondoka tangu saa tisa na hakumwambia
anakwenda wapi.
Nikaona niende kwa mama.
Nilipofika nilimueleza kwamba kaka alinipeleka kwa mganga aliyetoka Pemba na mganga akanieleza kwamba nimpelekee kucha za
maiti.
“Kucha za maiti utazipata
wapi?” mama akaniuliza kwa mshangao.
“Tena anataka maiti
aliyekwishazikwa”
“Sasa utampataje huyo maiti
aliyezikwa ukate
kucha zake?”
“Sijui”
“Mh! Hayo ni makubwa”
“Maana yake niende nikafukue
kaburi”
“Kaburi gani utakalokwenda
kulifukua?”
“Kaburi lolote tu”
“Mh! Si utaonekana ni
mchawi!”
“Labda niende usiku”
MAKUBWA! MAMBO SASA NI YA
KUFUKUA ,AKABURI! MMH! KAZI IPO JAMANI!
HAYA TUKUTANE TENA HAPO KESHO
TUONE NINI KITATOKEA.
No comments:
Post a Comment