Wednesday, June 29, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 31

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572

MWANAMKE 31

ILIPOISHIA

Niliposikia hivyo moyo wangu ulishituka. Kama namba za pikipiki yangu nazo zimeonekana nimekwisha!

Sikujua kama ile maiti ilikuwa ni ya shemeji yake mhasibu wetu. Nikaona nimejiingiza katika matatizo mengine ambayo sikuyatarajia.

“Hivi sasa nimeitwa polisi nikatoe maelezo, ile maiti imepelekwa hospitali kufanyiwa uchunguzi kujua kama ilibakwa. Kuna watu wanabaka maiti” Mhasibu aliendelea kutueleza.

“Inawezekana. Ni vizuri kama amepelekwa hospitali kufanyiwa uchunguzi. Binaadamu hivi sasa hawaaminiki kabisa” nikajidai kusema ili nisionekane nimefadhaika.

“Kumbe yule mlinzi alikwenda kuripoti polisi” Mwenzetu mwingine akauliza.

“Alikwenda polisi asubuhi. Ndio maana ninaitwa polisi” Mhasibu akamjibu kisha akatuaga na kuondoka.

Niliwaza kwamba kama mlinzi alikwenda kuripoti polisi, ile leseni yangu pia aliipeleka baada ya kuiokota pale ilipoanguka. Polisi watakuwa wameshaiona picha yangu. Bila shaka mhasibu wetu ameitwa ili kuoneshwa ile leseni ili athibitishe kama ndiye mimi.

Sasa sijui nikimbie kuepusha aibu, au niwangoje polisi waje wanikamate hapa hapa?

Kwa kweli nilikuwa nimechanganyikiwa.

SASA ENDELEA

Kwa dakika kadhaa sikuweza kujua nifanye nini. Wafanyakazi wenzangu walikuwa wakilizungumzia lile tukio la kufukuliwa kaburi, mimi nilikuwa kimya. Moyo wangu ulikuwa ukihangaika. Lakini hakukuwa na yeyote aliyeweza kunigundua.

Wasiwasi uliponizidi nilitoka nje ya duka letu. Kilichonitoa ni ule wasiwasi kwamba polisi wakitokea niweze kuwaona mapema. Nilikuwa nimeshapanga kuwakimbia.

Ilikuwa bora kupotea kuliko kupatwa na fedheha kama ile mbele ya wafanyakazi wenzangu.

Nilisimama nje ya duka letu kwa karibu nusu saa, nilipoona hakukuwa na polisi wowote waliokuwa wanakuja nikarudi ndani. Baadaye nikatoka tena. Nikaangalia pande zote za barabara kisha nikarudi.

Wakati nimekaa nikiendelea na mawazo yangu nilishituka nilipomuona mhasibu akiingia. Nilijua kuwa alikuwa amefuatana na polisi waliokuja kunikamata.

Lakini sikuona polisi. Alikuwa peke yake. Nikamkodolea macho ya tashiwishi. Nilikuwa na hisia kwamba alikuwa ameoneshwa leseni yangu na kunitambua.

Mfanyakazi mwenzetu mmoja akamuuliza kilichotokea huko polisi alikokwenda.

“Nimekwenda kutoa maelezo yangu” akasema na kuongeza.

“Ule mwili bado uko hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi”

“Huyo mtu aliyefukua hilo kaburi hakufahamika?’ nikauliza ili kuondoa dukuduku nililokuwa nalo.

“Si rahisi kufahamika. Mtu mwenyewe alikimbia na pikipiki” Mhasibu akanijibu.

Hapo wasiwasi ukanipungua kidogo.

Baada ya mhasibu kuzungumza na sisi kwa dakika chache akaingia ofisini kwake.

Haukupita muda mrefu, simu tuliyokuwa tunaitumia ikaita. Ilikuwa inapokelewa na mtu yeyote aliye karibu nayo. Akaipokea mfanyakazi mmoja akasikiliza kisha akaniita.

“Amour ni simu yako”

Moyo ukanipasuka.

Ni nani tena?

Nikaenda na kukipokea chombo cha kuzungumzia. Nikakiweka sikioni na kusema.

“Hello!”

“Naongea na bwana Amour?” Sauti nzito tena inayokwaruza ikauliza kutoka simu ya upande wa pili.

Moyoni mwangu nilikuwa nikijiuliza ni nani mwenye sauti hii? Akilini mwangu sikuweza kukumbuka mtu yeyote ninayemfahamu mwenye sauti inayolingana na ile.

Nikashuku kwamba anaweza kuwa afisa wa polisi ananipigia kuniita kituo cha olisi.

“Ndio. Wewe nani?”

“Hebu njoo hapa Tropicana, utanijua tu”

Tropicana ulikuwa mkahawa uliokuwa mtaa wa pili ambao wafanyakai wengi hupenda kunywa chai wakati wa saa nne na hata kula chakula cha mchana.

“Ni vizuri unifahamishe wewe nani?”

“Usiwe na wasiwasi. Ukifika hapa utaniona na utanijua”

Nikaurudisha mkono wa simu kisha nikatoka. Niliwaaga wenzangu kuwa ninakwenda kunywa chai.

Nilipotoka nje ya duka letu nilizunguka mtaa wa pili ambako kulikuwa na huo mkahawa wa Tropicana. Wakati natembea nilikuwa nikiwaza huyo mtu aliyeniita atakuwa nani kama si afisa wa polisi.

Nilikuwa na hakika kwamba sikuwa nikifahamiana na mtu aliyekuwa na sauti kavu kama ile.

Nilipofika kwenye mkahawa huo nikaingia. Nilisita kidogo kando ya mlango nikawatupia macho watu waliokuwamo ndani. Nikaona mtu mmoja aliyekuwa amekaa katika meza ya pembeni akinipungia mkono kuniita.

Sikuweza kumfahamu mpaka nilipofika karibu yake.

“Ah Mgosingwa!” nikasema mara tu sura yake iliponijia akilini mwangu.

Alikuwa mlinzi wetu ambaye alifukuzwa kazi kwa tabia yake ya ulevi wa kupita kiasi. Tulikuwa tunamuita Mgosingwa, neno la kabila la kizigua linalotokana na neno mgosi, yaani mwanamme.

Kwa vile yeye mwenyewe alikuwa mzigua, alikuwa akimuita kila mtu “mgosingwa” hasa pale anapotaka kumkopa mtu pesa ya kwenda kulewea. Na sisi tukampa jina hilo la mgosingwa. Nilizoea kumuita hivyo na jina lake halisi nilikuwa silijui.

“Vipi Mgosingwa?” akaniambia huku akinipa mkono kunisalimia.

“Salama tu Mgosingwa. Wewe ndio uliyenipigia simu kuniita?’

“Ndiye mimi Mgosingwa. Karibu ukae”

Nikakaa kwenye kiti.

“Ulikuwa unasemaje Mgosingwa?” nikamuuliza nikiwa na shauku ya kutaka kujua alichoniitia.

“Mgosingwa unatakiwa polisi!”

Kusema kweli nilishituka aliponiambia hivyo. Moyo wangu ukawa unadunda pu!pu!pu!

Nikajidai natabasamu.

“Nimefanya kosa gani Mgosingwa?”

Mgosingwa alitia mkono kwenye mfuko wa shati lake akatoa ganda kama la kitambulisho akaniwekea mezani.

“hii si leseni yako Mgosingwa?’ akaniuliza.

Nikalichukua lile ganda na kulifungua. Naam. Ilikuwa ni leseni yangu niliyokuwa nimeitupa kule makaburini. Pale pale uso wangu ulibadilika rangi kwa hofu iliyochanganyika na fadhaa. Nikamtazama mgosingwa huku nikijiuliza ameipata wapi leseni yangu.

“Huku nikiendelea na tabasamu langu la kulazimisha nilimuuliza.

“Mgosingwa umeipata wapi hii leseni yangu?’

“Si nimekwambia unatakiwa polisi?”

Jibu lake hilo lilizidi kunichanganya na kunifadhaisha. Midomo yangu niliyokuwa ninailazimisha kutabasamu huku nikiwa na fadhaa ilianza kutatizika na kutetemeka. Sasa haikuweza tena kutabasamu.

“Mgosingwa unanichanganya. Sasa nani kakupa hii leseni na kakupa kwa madhumuni gani?” nikamuuliza huku nikiizuia modomo yangu isitetemeke wakati nikimuuliza hivyo.

Mgosingwa aligundua kuwa nilikuwa nimetaharuki. Akacheka. Hata hivyo kwa vile uso wake ulikuwa umekunjana kutokana na kuendeleza kilevi, kicheko chake hakikuufanya uso wake upendeze, bali ulionekana kama anataka kulia.

“Mgosingwa hukumbuki uliiacha wapi leseni yako?” akaniuliza.

Nikatikisa kichwa.

“Sikumbuki” Nilimjibu hivyo ili nijue ataniambia nini.

“Mgosingwa jana usiku si ulikuja kule makaburi ukafukua lile kaburi nikakukurupusha”

JE NINI KITATOKEA? TUKUTANE KESHO PANAPO MAJALIWA

No comments:

Post a Comment