SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572
MWANAMKE 29
ILIPOISHIA JANA
“Yaani nikafukue kaburi?’
“Ndio”
“Si nitaonekana na watu”
“Huendi mchana, unakwenda usiku”
“Mh!” nikaguna nilipofikiria
kwenda usiku makaburini na kufukua kaburi.
“kama
hutaweza basi, tutakuwa tumeshindwa”
“Nitakupa jibu hapo kesho kama nitaweza au la”
“Kumbuka kwamba nitakuwa hapa
Tanga kwa siku tatu. Nikitoka hapa ninakwenda Arusha”
“Nimekuelewa, acha niende.
Nitakuja tena kesho”
Nikaagana na yule mganga na
kutoka, Nilipanda pikipiki yangu nikaenda nyumani kwa kaka. Kaka mwenyewe
sikumkuta, mke wake aliniambia kaka aliondoka tangu saa tisa na hakumwambia
anakwenda wapi.
Nikaona niende kwa mama.
Nilipofika nilimueleza kwamba kaka alinipeleka kwa mganga aliyetoka Pemba na mganga akanieleza kwamba nimpelekee kucha za
maiti.
“Kucha za maiti utazipata
wapi?” mama akaniuliza kwa mshangao.
“Tena anataka maiti
aliyekwishazikwa”
“Sasa utampataje huyo maiti
aliyezikwa ukate
kucha zake?”
“Sijui”
“Mh! Hayo ni makubwa”
“Maana yake niende nikafukue
kaburi”
“Kaburi gani utakalokwenda
kulifukua?”
“Kaburi lolote tu”
“Mh! Si utaonekana ni
mchawi!”
“Labda niende usiku”
SASA ENDELEA
“Utaweza kufukua kaburi mpaka
uipate maiti kisha
uikate kucha?” Mama aliniuliza kwa mshangao.
“Nitajaribu, nikishindwa
nitaacha”
“Mh!”
“Sasa nitafanyaje mama?”
“Najua kuwa huna la kufanya”
“Basi ngoja nijaribu”
Nilipoondoka kwa mama
nikaanza zoezi la kuzungukia makaburi niliyokuwa nayafahamu. Pale jirani na
nyumba niliyokuwa nikiishi paliwa na makaburi lakini yalikuwa karibu na makazi
ya watu, ningeweza kuonekana.
Nilikwenda katika eneo la Usagara ambako
pia kulikuwa na makaburi. Nikaangalia angalia kisha niliondoka tena nikaenda Gofu. Kulikuwa
na makaburi yaliyokuwa kando
ya barabara. Mahali hapo ndipo paliponiridhisha.
Laiti ningejua ni balaa gani
ambalo ningekutana nalo usiku kwenye makaburi hayo, nisingekwenda na mpango huo
ningeuacha kabisa!
Baada ya kupata uamuzi kuwa
niende katika makaburi yale wakati wa usiku, nilikwenda katika duka moja la
vifaa vya ujenzi nikanunua shepe, viatu vya mvua na mipira ya kuvaa mikononi.
Nikavifunga nyuma ya pikipiki yangu kisha
nikarudi nyumbani kwangu.
Nilikuwa nimepanga nitoke saa
nane usiku ambapo hakutakuwa na watu mitaani na hivyo nisingeweza kuonekana na mtu.
Wakati nimekaa sebuleni
nikiwaza nikasikia mlango wa mbele ukigongwa.
Nilisubiri, ulipogongwa tena
ndipo nilipoinuka na kwenda kunako mlango huo.
“Nani?”
nikauliza.
“Ni mimi Marijani”Sauti ya
kaka yangu ikajibu kutoka nje.
Nikafungua mlango.
“Karibu kaka” nikamkaribisha
ndani huku nikimpisha kwenye mlango.
Kaka aliingia ndani,
nikafunga mlango.
“Umenishitua kidogo”
nikamwambia.
“Kwanini?”
“Nilivyokuona umekuja kwangu
huu usiku moyo wangu umeshituka”
“Nimekuja na wazo”
“Kaa kwenye sofa” nikamwambia
kwa shauku ya kutaka kulisikia wazo alilokuwa amekuja nalo.
“Sitakaa. Nimekuja mara moja
tu. Nataka niwahi kurudi”
“Pikipiki ipo nitakurudisha
kaka”
“Usijali Amour tunaweza
kuzungumza tukiwa tumesimama, sisi bado ni vijana. Tusiogope kusimama”
“Sawa kaka, nieleze hilo wazo ulilokuja nalo”
“Kwanza
nilipata salamu kutoka kwa mke wangu kwamba ulikuja nyumbani ulipotoka kwa yule
mganga”
“Ndio nilikuja lakini nikaambiwa
na shemeji kuwa ulitoka”
“Ni kweli nilitoka,
niliporudi ndio nilipata hizo salamu. Nikaenda kumuuliza mama kama
ulifika kwake akaniambia ulifika na akanieleza ulivyoelezwa na yule mganga”
“Umeona kuwa mganga wako
amenipa mtihani mkubwa”
“Ni mtihani mkubwa. Mama
ameniambia ametaka umpelekee kucha za maiti”
“Tena maiti aliyezikwa, yaani
niende nikafukue kaburi”
“Sasa mimi nilikuwa na wazo”
“Ndio”
“Kwanini usiwatumie vijana?’
“Kuwatumia kivipi?”
“Yaani unamtafuta kijana wa
maskani unampa pesa kisha unamtuma hiyo kazi na unamuahidi kuwa akikuletea hizo
kucha za maiti utampa pesa nyingine”
“Ni wazo zuri, sikuwahi
kulifikiria wazo hilo”
“Yaani badala ya wewe kupata kazi ya kufukua kaburi, kazi hiyo
unampa yeye. Hawa vijana ukiwapa elfu ishirini tu ya kunywea gongo na bangi
wanaweza kukupatia hizo kucha”
“Ni kweli. Nitawatafuta huu
usiku”
“Tena makaburi yako pale
karibu tu. Kuna vijana wanaovutavuta bangi pale”
“Nashukuru kaka kwa wazo
lako, umenisaidia sana”
Baada ya kunipa wazo lake hilo
nilimrudisha kaka nyumbani kwake kwa pikipiki yangu.
Wakati narudi nyumbani nikawa
nalitafakari lile wazo alilonipa kuona kama
lilikuwa la busara.
Kwa upande mmoja wa akili
yangu niliona lilikuwa wazo la busara kwa sababu lingenigharimu pesa lakini
lingenirahisishia kazi. Badala ya mimi kwenda kufukua kaburi, ningempa pesa mtu
mwinginne akanifanyie kazi hiyo.
Wahuni walikuwa wengi tu
katika mtaa niliokuwa nikiishi, ningeweza kumtuma mmojawapo na akanifanyia kazi
hiyo bila wasiwasi.
Lakini kwa upande mwingine
niliona halikuwa wazo zuri. Halikuwa wazo zuri kwa sababu huyo mtu
nitakayemtuma hiyo kazi nitamuaminije. Atakaponiletea hizo kucha akaniambia
kuwa ni za maiti, nitaaminije kuwa ni kucha za maiti kweli?
Je kama atakwenda kukata
kucha zake mwenyewe na kuniletea, nitajuaje?
Muhuni ni muhuni tu, anaweza
kuona kazi ya kufukua kaburi ni ngumu na pesa haiachiki hivyo akaenda kujikata
kucha zake mwenyewe na kuniletea. Sitaweza kujua kama
kucha hizo si za maiti au ni zake mwenyewe.
Hivyo nikajiambia, si vizuri
kufanya jambo la kubahatisha. Ni vizuri nifanye jambo la uhakika. Na nitakuwa
na uhakika wa kucha hizo endapo nitakwenda mimi mwenyewe kufukua hilo kaburi na kukata
kucha hizo.
Nilipofika nyumbani
niliingiza pikipiki yangu nikasubiri saa nane ifike. Wakati nimeketi sebuleni
nikiendelea kusubiri muda, nikapitiwa na usingizi.
Katika usingizi huo eti
nikaota nimekwenda kufukua kaburi. Nikakuta mtoto mchanga aliyezikwa, hana hata
kucha, Nikalifukia na kufukua kaburi jingine, hilo nalo nilikuta mtu aliyekuwa amekatwa
mikono na miguu. Alikuwa amefariki kwenye ajali ya gari.
Nikalifukia tena na kutafuta
kaburi jingine ambalo nilianza kulifukua. Wakati nakaribia kulifikia sanduku
mvua ikanyesha kwa kishindo. Kaburi likawa linajaa maji. Kazi ikanishinda!
Kutahamaki kulikuwa kunaanza kupambazuka.
Ikabidi niondoke nikiwa
nimechukia. Hapo hapo nikazinduka.
Nilitazama saa yangu na kuona
ilikuwa saa saba ikielekea kuwa na nusu. Nikaona wakati huo pia ulikuwa muafaka
kuondoka. Nikaenda kunawa uso kisha nikarudi sebuleni na kuvaa vile viatu vya
mvua kwa ajili ya kujikinga na tope wakati wa kufukua kaburi.
Ile mipira ya mikononi
sikuivaa kabisa. Nikatoa pikipiki yangu. Lile shepe nilikuwa nimeshalifunga
katika siti ya nyuma ya pikipiki.
Kifaa cha kukatia kucha nilikuwa
nimeshakitayarisha. Ulikuwa wembe mpya.
Nikaondoka.
Niliendesha piki piki yangu
taratibu hadi nikafika Gofu. Usiku huo kulikuwa kimya. Hakukuwa na gari wala
watu waliokuwa wakipita. Nilikuwa na hakika kwamba hakukuwa na mtu yeyote
ambaye angeniona.
Nilifika katika lile eneo la
makaburi. Nikaiingiza pikipiki yangu ndani ya eneo hilo lililokuwa na mti pamoja na vichaka
vidogo vidogo.
Nikaiegesha pikipiki chini ya
mti huku nikiangaza macho huku na huku. Mbalamwezi ililiangaza vizuri eneo hilo kiasi kwamba sikupata
taabu kuyaona makaburi hayo.
Nilianza kuvaa mipira ya
mikononi kisha nikalifungua lile shepe. Nililishika mkononi nikaanza kutafuta
kaburi la kuchimba.
Makaburi mengi yalikuwa
yamewekewa zege, nikaenda mbele zaidi. Nikakuta kaburi moja ambalo halikuwa
limewekewa zege na lilionesha lilikuwa jipya. Huenda kulikuwa na mtu aliyekuwa
amezikwa siku iliyopita.
Nikaanza kulichimba. Kwa vile
mchnaga wake ulikuwa laini nililichimba haraka harka huku nikirundika mchanga
upande mmoja juu ya kaburi hilo.
Shimo lilipokuwa kubwa niliweza kuingia ndani nikaendelea kuchimba.
Baada ya kama
nusu saa tu nikawa nimelifikia sanduku lililokuwemo ndani. Nilipofanikiwa
kuuondoa mchanga wote uliokuwa juu ya sanduku hilo nikaufungua mlango wa sanduku na kuuacha
wazi. Ndani ya sanduku hilo
niliona maiti ya mwanamke.
Nikatia mkono mfukoni mwangu
na kutoa ule wembe. Niliufungua kwenye karatasi yake nikaushika kisha
nikaushika mkono wa ile maiti ya mwanamke. Hapo hapo nikaona mwanga wa tochi
unanimulika kutoka juu ya kaburi kisha sauti nzito ikaniuliza.
“Wewe nani na unafanya nini
hapa?”
Kwa kweli nilishituka sana. Wembe uliniponyoka.
Miguu ikanitepeta. Nikainua uso wangu haraka na kutazama juu ya kaburi hilo.
Nilijuta!
DUH! JAMAA KAFUMWA NA NANI
TENA? HAYA ITKUWAJE JAMANI! HUU NI MKASA MWINGINE TENA!
HEBU TUKUTANE TENA KESHO
TUONE NINI KITATOKEA.
No comments:
Post a Comment