Monday, November 17, 2014

Bodaboda amkanyaga ajuza Pongwe

Salim Mohammed, Mwananchi

Tanga,JESHI la Polisi kituo kikuu cha Chumbageni Tanga kinamshikilia dereva wa bodaboda, Moris Daffa (49) mkazi wa Pongwe kwa tuhuma kuendesha pikipiki mwendo kasi na kumgonga mtembea kwa miguu, Florida Msanga(70) na kufa papo hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, kaimu kamanda wa polisi Mkoani Tanga, Juma Ndaki, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 11 jioni baada ya ajuza huyo kuvuka barabara na kukumbana na dereva wa  bodaboda na kumgonga na kufa papo hapo.

Alisema bibi huyo alikuwa anavuka barabara kukimbilia mifugo yake mbuzi na kondoo na kutokea na dereva wa bodaboda akiwa mwendo kasi na hivyo kumsababishia kifo.

“Kwa sasa tunasema kuwa tunamshikilia dereva na pikipiki yake wakati uchunguzi unaendelea----tutaoa taarifa hapo baadae na kuwaiteni na kuwapa taarifa kamili” alisema Ndaki na kuongeza

“Yule bibi alikuwa anakatisha barabara kuifukuzia mifugo yake na mara akatokea dereva wa bodaboda na kumsomba mzimamzima na kufariki papo hapo” alisema Ndaki

Alisema wakati wa kutokea ajali hiyo dereva wa pikipiki alijaribu kukimbia lakini wapita njia wakiwemo abiria wa mabasi ya Wilayani waliweza kumfukuza na kumkamata na ndipo polisi ilipotaarifiwa na kufika muda huo huo.

Akizungumzia suala zima la usalama wa barabani, kaimu kamanda amewataka watumiaji wa vyombo vya moto kufuata sheria pamoja na kuacha kutembea mwendo kasi jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wao na watembea kwa miguu.

Alisema polisi itafanya msako wa kuwabaini madereva feki wakiwemo wasio na leseni za udereva pamoja na kuvamia maegesho ya bodaboda na hivyo kuwataka wanaoendesha vyombo hivyo wasio na leseni kuacha kufanya hivyo.

Alisema msako huo utakuwa endelevu ikiwa ni kuwabaini watu wasio na sifa za udereva kuwafikisha mahakamani baada ya matukio mengi ya ajali kuongezeka na chanzo kikiwa ni uzembe wa madereva.

                                           Mwisho

No comments:

Post a Comment