Kumekucha Blog
Korogwe, WAZAZI na walezi wenye watoto
wametakiwa kuwapa malezi mazuri watoto wao na kuwapeleka shule ili kuweza
kupata elimu na kuwa msaada katika
maisha yao ya baadae.
Akizungumza na wazazi na walezi wakati wa mahafali ya 14
shule ya awali ya Hill View Korogwe, Padri wa Parokia ya Korogwe, Joseph
Sekija, alisema kuna baadhi ya wazazi wanashindwa kutambua kuwa elimu ndio
msingi wa maisha ya kila mtu.
Alisema kuna wimbi la watoto mitaani wakiwa wamezagaa na chanzo
ni wazazi kutowapa matunzo na kuwapeleka shule na hivyo kujingiza katika
magenge ya wabwiaji unga na waporaji wa wizi wa mifukoni.
“Leo toka nifike hapa nimekuwa na bumbuwazi na kushindwa
kupata majibu---sijaona shule ya awali kufanya mahafali kama haya---watoto
wamependeza na huu ni mfano kwa shule nyengine za awali” alisema Sekija
“Kwa vile hapa wapo wazazi na walezi ni nafasi ya kukumbusha
na kupelekeana salamu kwa ambao hawapo---tutambue kuwa elimu ndio msingi wa
mambo yote hivyo kila mmoja wetu kumpeleka mtoto wake shule kwa wakati na
kufuatilia maendeleo shuleni” alisema
Aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanafuatilia maendeleo
ya watoto wao shuleni na kuacha kusubiria ripoti za mwisho wa mwaka jambo
ambalo linaweza kuchangia kuwa na matokeo mabaya.
Akizungumza katika mahafali hayo, Mkurugenzi wa shule hiyo ya
awali, Silvester Mgoma, amewataka walimu kuzidisha bidii darasani lengo likiwa
ni kuibua vipaji na kuweza kutoa vijana wenye akili.
Alisema walimu wako na mchango mkubwa kwa kushirikiana na
wazazi katika kuwajenga katika misingi ya maadili ya kiroho na hivyo kuwataka
kushirikiana ili kuibua vijana wenye vipaji.
“Mimi nasaha yangu kwenu wazazi na walimu ni kudumisha
ushirikiano na mahusiano mema ili kuwajenga watoto wetu katika maadili mema ya
kiroho shuleni na majumbani” alisema Mgoma
Alisema endapo kutakuwepo mahusiano mema ya pande mbili hizo ni wazi kuwa Taifa litakuwa
na vijana wenye elimu na vipaji na kuondokana na tatizo la uhaba wa fani ikiwemo ya sayansi.
No comments:
Post a Comment