Friday, November 28, 2014

Majeruhi wa ajali ya Costa watoa ushuhuda

Kumekucha Blog
Muheza, MAJERUHI wa ajali iliyohusisha basi dogo la abiria  na lori kijiji cha Mkanyageni Wilayani Muheza Mkoani Tanga, wamedai uzembe wa dereva wa lori imekuwa chanzo cha vifo hivyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wodini jana, majeruhi hao walisema dereva wa lori huenda alikuwa na usingizi au kulewa baada ya gari lake kushindwa kulimudu na  kulifuata basi hilo upande wake likiwa mwendo kasi.

Walisema lori hilo lililokuwa likiendeshwa  na Benjamin Abeid lilikuwa mwendo kasi jambo ambalo dereva alishindwa kulimudu na hivyo kuifuata costa na kulisukumiza porini na watu 11 kufa papo hapo.

“Nilikuwa naenda kumsalimia wifi yangu Kwafungo na kukaa nyuma ya dereva---wakati lori linakuja naliona na dereva wa basi alijitahidi kulikwepa lakini mwisho wake likatugonga  uso kwa uso” alisema Mwajuma Kassongo

“Kwa mwendo ambao alikuwa anakuja ni wazi alikuwa amelewa au lundo la usingizi kwani alitoka upande wake na kuja upande tulio na jitihada za dereva watu zimepunguza wingi wa vifo kwani tungemalizika sote” alisema Kassongo

Akiwashauri askari wa usalama barabani, Kassongo amewataka kuwa na utaratibu wa kuwapima madereva  kama wametumia vilevi na kutoruhusiwa kuendesha gari na hivyo kusaidia kupunguza ajali na vifo.

Kwa upande wake Heri Phillimon akievunjika mguu, alisema ajali hiyo imemuweka kilema cha maaisha  huku akiwa anategemewa na familia yake na hivyo kushindwa la kufanya baada ya kutoka hospitali.

Alisema wakati wa ajali hiyo ambayo aliwashuhudia abiria  wenzake wakikata roho na baada ya kupasuka sehemu za vichwa na kukatika mikono amedai katika maisha yake hatoweza kuisahau siku hiyo.

“Ajali hii ni mbaya sana na sitoweza kuisahau kwani nimewashuhudia wenzangu wakikata roho machoni mwangu----kila mtu atakufa lakini vifo vyengine vinahuzunisha na kuogopesha” alisema Phillimon

Alivitaka vyombo vya sheria kulichunguza tukio hilo na kuweza kuchukuliwa hatua na mhusika kuwa fundisho kwa wengine na kuvitaka vyombo vya usalama barabarani kuzidisha ukaguzi wa magari na madereva.

                                               Mwisho

No comments:

Post a Comment