Kumekucha Blog, Tanga
Tanga, POLISI kituo kikuu cha Chumbageni Tanga
inawashikilia watu watu kwa tuhuma za kupatikana na noti bandia za Kimarekani
Dola 11,200 wakati wakiwa katika harakati za kuzibadilisha kwa wabadilishaji wa
pesa za mikononi kituo kikuu cha mabasi Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana,
kamanda wa polisi Mkoani Tanga, Freisser Kashai, alisema tukio hilo lilitokea
juzi saa 5 asubuhi eneo la kituo cha mabasi yaendayo Mombasa nchini Kenya.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwani, Julias Kanza(30), Kenedy
Binagi(35) na Saddy Muha (33) wote wakiwa ni wakazi wa Ubungo jijini Dar es
Salaam na kudai kuwa walikiri kufanya biashara ya pesa za bandia kwa muda
mrefu.
Alisema wakati wakiwa katika harakati za kubadilisha pesa
hizo mmoja wa watu wanaobadilisha aliweza kutilia shaka pesa hizo hasa kikiwa
ni kiwango kikubwa kwa pesa za mikononi na hivyo kupiga simu polisi kwa kutarifu
juu ya pesa hizo.
“Mmoja wa kijana wanaobadilisha pesa pale kituo cha mabasi
yaendayo Mombasa alizitilia shaka kwani
kwanza nikiwango kikubwa na pili pesa ya kubadilishana ilikuwa ndogo sana”
alisema na kuongeza
“Dola za kimarekani elfu kumi na moja sio kiwango kidogo kwa
pesa za kubadilisha juu juu tena kituo
cha mabasi----ile yatosha kwa yoyote kutilia shaka na ndio maana mmoja wa
wafanyabiashara alishtuka na kupiga simu polisi” alisema kamanda Kashai
Kamanda alisema mahojiano ya awali na watuhumiwa hao wamekiri
kufanya biashara hiyo haramu ya kubadilisha pesa za bandia na wamekuwa
wakitumia vituo vya mabasi na mipaka ya
nchi jirani ukiwemo mpaka wa Horohoro.
Alisema uchunguzi utakapokamilika watuhumiwa hao watafikishwa
mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili ili kuwa fundisho kwa watu wengine
wenye tabia kama hiyo.
Akizungumzia wafanyabiashara kuzitumia taasisi za fedha
yakiwemo mabenki katika kubadilisha na kuweka pesa zao ili kuepusha utapeli na
wizi, Kashai alisema wizi huo utakoma.
Alisema matapeli wengi wamekuwa wakitumia mwanya huo baada ya
kuona wafanyabiashara na matajiri wamekuwa wakibadilisjha pesa kienyeji na
hivyo kuwa rahisi kutekeleza vitendo vya
kitapeli.
“ Watu wengi hawatumii mabenki na taasisi za fedha katika
kubadilisha na kuweka pesa zao na hivyo matepeli kuutumia mwanya huo kutekeleza
unyang’anyi” alisema Kashai
Alisema ili kuweza kutokomeza na kuziba mianya ya kitapeli
amewataka kuyatumia mabenki katika kupadilisha na kuweka ili kuepusha utapeli
na kuweza kuwa na uhakika wa kufanya biashara zao.
No comments:
Post a Comment