Tuesday, November 25, 2014

DC, Gambo awataka wauzguzi kukomesha vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua



Kumekucha Blog

Korogwe, MKUU wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo, amewataka wauguzi Wilayani humo kutoa elimu kwa wazazi majumbani kujifungulia katika vituo vya afya lengo likiwa ni kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Akifungua kongamano la Chama Cha Wauguzi Tanzania (TAMA) jana Wilayani humo, Gambo alisema kuongezeka kwa vifo vya mama na mtoto ni kutokana na wazazi wengi kutokuwa na elimu ya kuhudhuria vituo vya afya kutambua mwenendo wa mtoto tumboni.

Alisema hali hiyo imekuwa ikiwalazimu kujifungulia katika sehemu ambazo sio za kutolea huduma na hivyo kuwataka kutoa elimu nyumba kwa nyumba jambo ambalo litasaidia kuwa na ada ya kuhudhuria vituo vya afya kila baada ya muda.

“Nashukuru kwa kupata nafasi hii adhimu ya kuzungumza nanyi natambua kuwa ni watu muhimu sana hasa suala zima la vifo vya mama na mtoto-----tutambue kuwa muko na nafasi ya kuelimisha jamii” alisema Gambo

“Wilayani kwetu hapa munatambua kuwa vifo vya mama na mtoto vimepungua kiasi ila tusibweteke kwani kuna kundi kubwa halina elimu ya kuhudhuria vituo vya afya wakati wa ujauzito na mwisho hujifungulia sehemu zisizo salama” alisema

Gambo aliwataka wauguzi hao kuwa na mkakati wa kupita nyumba kwa nyumba kutoa elimu hiyo kwa wanawake  ili wakati wa ujauzito kuwa na utaratibu wa kuhudhuria vituo vya afya na madhara ya kujifungulia sehemu ambazo sio za kutolea huduma.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mkunga na mwalimu chuo kikuu cha Canada, Angella Spencer, aliwataka wauguzi kuwa na kauli nzuri kwa wajawazito hasa wakati wa kujifungua.

Alisema wauguzi wako na nafasi kubwa ya kumfanya mzazi kujifungua kwa hali ya furaha baada ya kupata faraja na hivyo kuwataka kuzitumilia nafasi zao lengo likiwa ni kuwaweza wazazi katika mazingira ya  kujifungua salama.

“Ili kutokomeza vifo vya mama na mtoto kwanza ni muuguzi kuhakikisha anampokea mzazi kwa furaha-----hii itamfanya kujisikia furaha hadi muda wa kujifungua” alisema Spencer

Alisema kama wauguzi wataifuata taaluma yao ni wazi kuwa vifo vya watoto wakati wa kujifungua vitapungua Tanzania sambamba na utoaji wa elimu ya kila mjamzito kuhudhuria kituo cha afya kwa utaratibu.

                                                Mwisho

No comments:

Post a Comment