Watumiaji
wengi wa huduma ya simu za mkononi wamekuwa wakilalamikia wizi wa pesa
unaofanywa na baadhi ya makampuni hayo, leo katika kikao cha Bunge
Dodoma Serikali imesema inatambua kuhusu wizi unaofanywa na baadhi ya
makampuni ya simu za mkononi na kutoa tamko namna ambavyo imejipanga
kukabiliana na wizi wa aina hiyo.
Akitoa tamko hilo Naibu Waziri wa
Mawasiliano Sayansi na Teknolojia January Makamba amesema Serikali
itaanzisha kituo maalum cha kushughulikia malalamiko hayo CCC,
kitakachokuwa kinasimamiwa na TCRA.
Akiuliza swali kuhusiana na jinsi Serikali ilivyojipanga kukabiliana na wizi huo Mbunge wa Konde Khatib Said Haji amesema; “…
Wizi huu unaofanywa na makampuni ya simu si wizi mkubwa kama ule wa
ESCROW.. ni wizi mdogo mdogo unaowaibia Watanzania elfu tano elfu tatu
lakini kwa ujumla wake, Mpemba aliyeko Konde akiibiwa elfu tatu,
Mnyamwezi wa Tabora elfu mbili, Ukizijumlisha ni mamilioni ya shilingi
wanaibiwa Watanzania… Leo watu hao elfu tatu elfu mbili unawaambia
wapeleke malalamiko yao, gharama hiyo umeikadiriaje hata mtu huyo akadai
malalamiko ya elfu tatu..”
“.. Hivi
serikali yenu makini imekuwa wapi muda wote mpaka kukiri kama Watanzania
wamekuwa wakiibiwa na bila wenyewe kujijua?, na bado hamna hatua
mlizozichukua, ni nani aliyeko nyuma ya pazia hili la kuibia Watanzania
na ninyi mkaridhia ama ni yale yaliyosemwa kama CCM ina fund katika wizi
huu..?”- Khatib Said Haji.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia January Makamba amesema; “…Napenda
nikiri tatizo la wizi au dhuluma kwa wateja lipo na ndio lililopelekea
tukaweka hizi kanuni ambazo zinaweka adhabu na hatua za kuchukua katika
kuchukua katika kudhibiti wizi huo.. Licha ya utaratibu wa kawaida wa
kulalamika katika makampuni ya simu, kwa sababu moja ya matakwa ya
sheria ni kwamba kampuni za simu zinapaswa kuweka utaratibu wa kuhudumia
watekja wake, lakini tumebaini kwamba utaratibu huo una matatizo,
unaweza ukapiga simu muda mrefu isipokelewe, unaweza kuambiwa usubiri
na wakati unasubiri kulalamika pia unakatwa..
Kwa hiyo
Serikali inafahamu hilo, pamoja na hatua tulizozichukua ni kuweka ule
mtambo wa kufuatilia mawasiliano ambao moja ya kazi yake sio kufuatilia
tu mapato lakini ubora wa mawasiliano.. Kwa kutambua kuwa makampuni ya
simu haya wakati mwingine yanachelewa wakati mwigine yanapuuza wateja,
kituo hiki ambacho tunakianzisha namba zake zitasambazwa kila mtu
atakuwa nayo, kwa hiyo huna haja kusafiri kufuatilia shilingi elfu mbili
elfu tatu elfu tano. Kutakuwa na namba ambayo ni bure kupiga..”- January Makamba.
“ Kila
utakapopiga kulalamika utapewa namba maalum ya lalamiko lako, na
lisiposhughulikiwa hata kitengo cha kampuni ya simu kutoshughulikia
lalamiko lako na yenyewe itakuwa sababu ya makampuni hayo kuadhibiwa..”- January Makamba.
No comments:
Post a Comment