I
……………………………………………………………………..
Kyela
Kufuatia adha ya usafiri wa majini
inayowakabili wakazi waishio katika fukwe za Ziwa Nyasa, Mamlaka ya
Bandari Tanzania kupitia kituo chake cha Kyela ipo mbioni kujenga meli
ya abiria na mizigo ili kuwahudumia wakazi hao.
Hayo yaliwekwa bayana na Mkuu wa
Bandari ya Kyela, Bw. Percival Ntetema wakati timu wakaguzi wa miradi ya
maendeleo kutoka Ofisi ya Tume ya Mipango ilipotembelea na kukagua
bandari za Itungi na Kiwira zilizopo wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya.
Bw. Ntetema alisema kuwa Mamlaka
imeshakamilisha mchakato wa manunuzi na tayari imempata mkandarasi M/S
Songoro Marine Transport Ltd kwa ajili ya ujenzi wa meli yenye uwezo wa
kubeba jumla ya tani 200 za mizigo na abiria 200.
“Mamlaka ipo kwenye hatua za
mwisho za kuandaa mkataba unaotarajiwa kutiwa saini mwezi ujao na kazi
itaanza mwanzoni mwa mwaka ujao,” alisema.
Bw. Ntetema aliongeza kuwa mpaka
sasa Bandari ya Kyela imeshaanza maandalizi ya kuvuta umeme
uliofadhiliwa na Wakala wa Umeme Vijijini pamoja na kuaanza kwa kujenga
matishari mawili ili yaweze kurahisisha utoaji wa huduma mara meli hiyo
itakapoanza kazi mwishoni mwa mwaka ujao.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo,
kiongozi wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais,
Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri aliupongeza uongozi wa Mamlaka
kwa hatua yake hiyo kwani itaongeza tija ya shughuli za kiuchumi katika
kanda hiyo ya Ziwa Nyasa.
“Ninaupongeza uongozi wa Mamlaka
ya Bandari kwa kuanza mchakato huu utakaofungulia fursa za kiuchumi na
maendeleo kwenye ukanda huu, hivyo kuunga mkono jitihada za serikali za
kupunguza vikwazo mbalimbali vinavorudisha kasi ya kusaka kupunguza
umaskini nchini,” alisema.
Bibi Mwanri aliongeza kuwa
kukamilika kwa mradi huo kutatoa fursa za kuhudumia shehena na abiria
kutoka mikoa ya Mbeya, Njombe, na Ruvuma. Pamoja na kuhudumia nchi za
jirani ikiwemo Malawi, Msumbiji na Zambia.
Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo
wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016) bandari ni mojawapo ya
vipaumbele vitano vya kimkakati vyenye lengo la kufungulia fursa za
ukuaji uchumi wa nchi ili kuweka misingi wa uchumi kwa watu walio
wengi.
Vipaumbele vingine ni Kilimo
ambapo lengo kuu likiwa ni kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya
kilimo ili kujitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada ya kuuza nje ya
nchi; Maendeleo ya viwanda: Msisitizo umewekwa katika kuvutia,
kuanzishwa na kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana
nchini (kama vile viwanda vya nguo, mbolea, saruji, makaa ya mawe, chuma
na bidhaa za chuma) na pia sekta ya madini kwa lengo la kuongeza mapato
ya Serikali.
Pamoja na kipaumbele cha Maendeleo
ya rasilimali watu na ujuzi: Mpango unahimiza kuwekeza katika elimu
(hasa katika elimu ya juu na vyuo vya ufundi) na huduma za afya
(kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma) katika kujenga nguvu kazi
itakayotuletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii; na Utalii, Biashara, na
huduma za Fedha ambapo jitihada zimewekwa kwenye uendelezaji uwezo wa
kuuza katika masoko ya ndani na nje, kuongeza idadi ya watalii na
matumizi yao wawapo nchini, na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha.
No comments:
Post a Comment