Friday, November 14, 2014

Kamanda wa polisi Mkoani Tanga akiwaonyesha waandishi wa habari magunia ya madawa ya kulevya

POLISI kituo kikuu cha Chumbageni Mkoani Tanga, inamshikilia Hajji Hamis (27) mwenyeji wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kupatikana na madawa ya kulevya aina ya  mirungi kilo 116 akiwa ameyaficha katika magunia ya mkaa wakati akisafirisha kwenda Dar es Saalam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, kamanda wa polisi Mkoani Tanga, Fresser Kashai, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 8 usiku katika kizuizi cha polisi Mazinde Wilayani Korogwe.

Alisema polisi wakati inafanya ukaguzi wa gari pamoja na kujua ilichobebea iliweka mashaka baada ya kusikia harufu ambayo ni tofauti na hivyo kutambua mbali ya mkaa kiko kitu ambacho gari hilo limebeba.

Alisema ililazimika kuteremsha gunia moja baada ya jengine na kadri walivyokuwa wanashusha ndivyo harufu inavyoongezeka na ikaweza kugundua magunia matatu yenye mirungi ambayo ilikuwa ikisafirishwa kwenda Dar es Salaam.

“Kwa sasa si rahisi kwa watu kusafirisha na kupitisha madawa ya kulevya katika mpaka wetu kwani polisi wako na utaalamu wa kutambua hasa madawa ya kulevya----mara nyingi tumekuwa tukiyakamata” alisema akiongeza

“Na zaidi tumekuwa tukitumia mbwa wenye utaalamu wa kutambua madawa ya kulevya na vitu kama mabomu hata kama yamefichwa wapi mbwa atatambua” alisema Kashai

Kamanda Kashai alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na mtuhumiwa mara baada ya kukamilika atafikishwa mahamakani kujibu tuhuma zinazomkabili ikiwa na pamoja kupewa adhabu na kuwa fundisho kwa wengine.

Katika tukio jengine, Polisi Wilayani Korogwe Tarafa ya Magoma  inawatafuta watu watano kwa tuhuma za mauaji ya kijana mmoja wakimtuhumu kuiba Mbuzi  katika zizi karibu na nyumba yao.

Alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 6 usiku wakati kijana huyo akiwa anapita karibu na zizi la mbuzi na ndipo mtu mmoja alipopiga kelele za mwizi na majirani kutoka na kumpiga hadi kufa papo hapo.

Alisema uchunguzi wa awali wa kipolisi wa tukio hilo umebaini kuwa kija huyo alieuwawa hakuwa mwizi bali alikuwa mpita njia na taarifa za majirani ni kuwa kulikuwa na visa vya mipaka ya mashamba.

Alisema kwa mujibu wa majirani ni kuwa kijana huyo alikuwa na ugomvi wa mara kwa mara na majirani wa shamba lake na wameshawahi kupelekana katika vyombo vya sheria.

“Uchunguzi wa kipolisi umebaini kuwa kulikuwa na visa vya kugombea mipaka katika konde zao----kifo hiki ni kutekeleza dhamira yao ila taarifa ni kuwa watu watano ndio waliohusika na tukio hilo na tutawatia mbaroni” alisema Kashai

Alisema polisi inaendelea kuwatafuta watu hao na kuwahakikishia ndugu wa marehemu kuwa itawatia mbaroni na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili kuwa fundisho la watu kujichukulia sheria ikononi

No comments:

Post a Comment